Rais Magufuli na dhana ya watumishi wa umma

MsemajiUkweli

JF-Expert Member
Jul 5, 2012
13,172
23,975
Kama kuna mwaka ambao watumishi wa umma hawatausahau, basi ni 2016 ambao Serikali ya Awamu ya Tano umeutumia kufanya mabadiliko, ambayo yametingisha wafanyakazi wa serikalini na kuwaweka roho juu wakati wote.

Hayo yametokea wakati Serikali ya Rais John Magufuli ikiwa imepania kuwezesha kila mwananchi kunufaika na matunda ya rasilimali za nchi kwa kudhibiti ufujaji wa fedha za umma, kuondoa posho za vikao, kudhibiti safari za nje na ndani, kuondoa wafanyakazi hewa na kupiga marufuku mikutano ya kikazi kufanyika hotelini.

Makali hayo yaliambatana na kupunguza mishahara ya watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma hadi chini ya Sh15 milioni, kusaka watumishi wasio na sifa kwa kuhakiki vyeti, kutimua wafanyakazi wazembe na wasiowajibika na kufukuza kazi waliobainika au kutuhumiwa kuhusika au kufanikisha ufisadi.

Kuanzia Rais, mawaziri hadi wakuu wa wilaya, neno “utumbuaji” lilitamba mwaka huu, huku watumishi wa umma wakisali wasikutane nalo. Wapo waliotimuliwa, kusimamishwa kazi, kufikishwa mahakamani, na wengine kujikuta wakilala mahabusu.

Kwa ujumla ulikuwa mwaka wa mchakamchaka na hofu kwa watumishi wa umma wakati Rais na Serikali yake “wakiinyoosha nchi”. “Nadhani wafanyakazi walio sekta binafsi wana amani, huku kwetu hali ni mbaya. Tunaishi roho juu, tena kwa kuwindana. Mtu anasubiri ukosee kidogo apate sababu ya kukutimua,” alisema mfanyakazi mmoja wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Mfanyakazi huyo alisema huu ni mwaka ambao wafanyakazi wa Serikali wamekuwa katika wakati mgumu kutokana na hofu ya kufukuzwa kazi endapo watakwenda kinyume na maagizo ya viongozi wao.

Mfanyakazi mwingine aliyeomba jina lake lisitajwe kwa hofu ya kutumbuliwa, alisema hata viongozi wao maofisini wamekuwa na wakati mgumu. “Hali ilikuwa ya wasiwasi kiasi kwamba hujui ufanye nini,” alisema mtumishi huyo wa taasisi ya Serikali ambaye ni karani.

“Mabosi wanahaha. Hawajui leo itakuwa zamu ya nani; hali imekuwa ngumu kwa sababu vile vihela vya posho za vikao vilivyokuwa vinasaidia kusukuma maisha, sasa havipatikani; yaani unashindwa kujipanga.”

Lakini mwalimu wa shule moja ya Serikali mkoani Mbeya alisema idara zinazohusika na walimu zimeboresha utendaji kwa sababu matatizo ya walimu yanasikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka tofauti na zamani.

Alisema kumekuwa na uwajibikaji na kila mwalimu sasa anatimiza wajibu wake awapo kazini. Hata hivyo, alibainisha kwamba ufanisi huo unatokana na hofu ya walimu kufukuzwa kazi. “Kuhusu Serikali hii, ninafanya kazi kwa amani kwa asilimia 50 na nina hofu pia kwa asilimia 50. Hofu yangu ni kufukuzwa kazi nikifanya kosa au hata kwa makosa,” alisema.

Wafanyakazi hewa
Dalili za mwaka 2016 kuwa wa kubanana zilionekana mapema baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango na baadaye kukutana na makatibu wakuu, manaibu wao, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na kutoa picha halisi ya “Serikali ya Magufuli”.

Rais alianza kutekeleza mpango wake wa kampeni ya kuwaondoa watumishi hewa serikalini, akiagiza wakuu wote wa mikoa kufanya uhakiki wa watumishi wao.

Alisema baadhi ya watumishi walikuwa wakipokea mshahara zaidi ya mmoja kutokana na kunufaika na majina ya watu waliokufa. Wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru, Rais Magufuli alisema idadi ya wafanyakazi hewa imefikia 19,000. Alisisitiza kwamba bado wanaendelea kuwasaka na kuwaondoa kwenye malipo ya mishahara.

Uhakiki wa wafanyakazi hewa, pia ulilenga kubaini wanufaika wa mishahara hiyo na kuwachukulia hatua, baadhi wameshafikishwa mahakamani.

Uondoaji posho
Jambo jingine lililotikisa wafanyakazi wa sekta ya umma ni uamuzi wa Serikali kubana matumizi. Uamuzi huo unagusa sehemu kama safari za nje zisizo za lazima, posho za vikao vya ndani, semina za mara kwa mara, mikutano yote ya ndani kutofanyika hotelini, kufutwa kwa baadhi ya sherehe za maadhimisho ya kitaifa.

Wakati hatua hizo zikisababisha hali ngumu kwa watumishi wa umma, sekta binafsi ilijikuta ikiathirika kutokana na mzunguko wa fedha kudorora. Biashara ya hoteli ilidorora kutokana na Serikali ambayo ni mteja mkuu kuamua kufanyika shughuli zake kwenye majengo yake.

Baadhi ya kampuni zimepunguza wafanyakazi, baadhi ya hoteli kufungwa na nyingine kubadilishwa matumizi.

Akifafanua juu ya kupotea kwa fedha kwenye mzunguko, aliyekuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema hilo linasababishwa na Serikali kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama vile ununuzi wa ndege na ujenzi wa reli. Hata hivyo, alisisitiza kwamba matokeo ya uwekezaji unaofanywa na Serikali yataonekana baadaye.

Ubanaji matumizi pia ulihusu safari za nje ambao uliathiri mifuko ya wafanyakazi wengi na safari za ndani. Kwa mwaka 2014/15 jumla ya Sh3.2 zilitazamiwa kutumiwa kwa safari, kiwango ambacho ni takriban nusu ya mishahara ya wafanyakazi wote.

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na Serikali mwaka 2015, posho za safari ya mfanyakazi wa ngazi ya kati, ilipanda kutoka Sh65,000 hadi Sh100,000 kwa safari za ndani, wakati za wakurugenzi na maofisa waandamizi ziliongezeka kutoka Sh80,000 hadi Sh120,000 kwa siku.

Kwa safari za nje, posho za wafanyakazi wa ngazi ya umeneja zilikuwa dola 365 za Marekani kwa siku (takriban Sh700,000), wakati wakurugenzi walikuwa wakilipwa dola 420 (takriban Sh850,000) kwa siku.

Mbali ya posho hizo za kujikimu, safari za watumishi wa umma huambatana na marupurupu mengine kama malipo ya usafiri wa ndani wa eneo analoenda, fedha za njiani, dharura na matumizi mengine. Ni dhahiri safari ya siku 10 kwa mtumishi huyo wa umma ingeweza kumfanya aishi bila ya wasiwasi kwa miezi miwili.

Wafanyakazi waliojaribu kusafiri bila kibali na kubainika kuchukuliwa hatua. Mfano ulianzia kwa watumishi wanne wa Takukuru ambao walisafiri nje ya nchi bila kibali kutoka Ikulu. Hata hivyo, wamerudishwa kazini.

Utumbuaji majipu
Suala jingine lililotingisha wafanyakazi kwa mwaka mzima ni “utumbuaji wa majipu” ambao uligeuka msamiati maarufu kwa Rais Magufuli, mawaziri wake, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

Uteuzi wa viongozi wengi ulitenguliwa baada ya kutuhumiwa kwa uzembe, ufisadi au makosa mengine ya uwajibikaji. Majina yaliyoongoza ni kama Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Anne Kilango (aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga), na Dk Edward Hoseah (aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru). Orodha hiyo pia ilijumuisha watu kama makamishna, watendaji wakuu wa taasisi za Serikali, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na watumishi wengine wa umma.

Bosi wa zamani Tucta afurahia
Pamoja na hatua hizo kufanya watumishi wa umma kuwekwa kwenye hali ya hofu, aliyekuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholas Mgaya amesema Serikali imechelewa kutekeleza hayo kwa kuwa ndiyo yaliyokuwa kilio chao cha muda mrefu.

Alisema anafurahi kuona mabadiliko anayofanya Rais Magufuli hasa kuondoa wafanyakazi hewa kwa sababu wakati watu wakihangaika na ajira, wengine walikuwa wanapokea mishahara miwili.

“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kuyachukua yale ambayo tumekuwa tukiyasema. Suala la kuondoa wafanyakazi hewa tunaliafiki kwa sababu rasilimali za Taifa zinawamufaisha wachache bila kufanya kazi wakati wapo vijana wengi wasio na ajira,” alisema.

Hata hivyo, Mgaya ameshauri Serikali kutengeneze mfumo ambao utafanya kazi hata akiwa hayupo. Alisema kinachofanyika sasa ni jitihada binafsi za Rais, kwa hiyo kuna haja ya kuwa na sheria au mfumo utakaosimamia sekta ya umma.

Akizungumzia mchakamchaka wa mwaka huu, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema watumishi wengi wameshtushwa na kasi ya Rais Magufuli kwa sababu hawakuzoea uwajibikaji ambao anataka. Alisema mtumishi wa umma lazima abanwe na kusimamiwa ili atimize majukumu yake.

Alisema wengi walizoea kutumia muda wa kazi kufanya mambo yao binafsi. “Kasi yake imekuwa ya hali ya juu kama alivyoahidi wakati wa kampeni na ndiyo ambayo wananchi tunataka. Watumishi wazembe wataona wanabanwa, kweli lazima wabanwe kama wameshindwa kujisimamia,” alisema.

Pia, ameshauri kuwa Katiba Mpya ndiyo itakayobadilisha baadhi ya mambo ambayo hatuyahitaji kwa sasa na kuingiza yale yanayohitajika. Alisema Katiba bora ndiyo inayoimarisha utumishi wa umma.

Lakini Profesa Abdallah Safari amepinga utawala wa Rais Magufuli akisema, “Ninachotaka kuona ni sheria na Katiba kufuatwa. Yeye (Rais Magufuli) aliapa kuilinda katiba, ninataka kuona anasimamia kiapo chake,” alisema Profesa Safari ambaye ni mwanasheria na makamu mwenyekiti wa Chadema na kuongeza kuwa Rais ana haki ya kuchagua watu wa kufanya nao kazi, lakini afuate taratibu
CHANZO: Gazeti la Mwananchi.
 
Bila kusahau anomalies kama za kutumbua jipu na kulirudisha!
Inconsistency is a great door for the change and for the progression! Never hesitate to be inconsistent!―Mehmet Murat ildan
 
..unajua Mwalimu Nyerere alipopunguza mishahara alianza na wa kwake.

..naunga mkono Raisi kupunguza mishahara mikubwa ambayo hailingani na hali halisi ya uchumi na kijamii hapa Tz.

..lakini ni vizuri Raisi pia akaonyesha mfano kwa kupunguza mshahara wake na zaidi kupunguza gharama za kumhudumia. Na hili linahitaji Raisi kuwa muwazi.

..waziri lukuvi alipata kusema gharama za kumtunza Raisi wa Tz ni sawa na bajeti ya mikoa mitano.
 
..unajua Mwalimu Nyerere alipopunguza mishahara alianza na wa kwake.

..naunga mkono Raisi kupunguza mishahara mikubwa ambayo hailingani na hali halisi ya uchumi na kijamii hapa Tz.

..lakini ni vizuri Raisi pia akaonyesha mfano kwa kupunguza mshahara wake na zaidi kupunguza gharama za kumhudumia. Na hili linahitaji Raisi kuwa muwazi.

..waziri lukuvi alipata kusema gharama za kumtunza Raisi wa Tz ni sawa na bajeti ya mikoa mitano.
Nadhani hoja zako zilishajibiwa kwa kiasi kikubwa.

Pitia thread hii;
Rais Magufuli akifuta kitengo cha lishe cha Rais na Dawati la wageni Ikulu

Pia Thread hii;
Msamaha wa kodi ya kiinua mgongo kwa Rais, Makamu wa Rais, Mawaziri,Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wafutwa
 

..hoja yangu siyo Raisi kulipa kodi.

..hoja yangu ni mshahara na marupurupu yake kupunguza ili iendane na hali halisi ya kiuchumi na kijamii.

..Mh.Lukuvi alidai gharama za kumtunza Raisi wa Tz ni sawa na bajeti ya mikoa mitano. Tuanzie hali.
 
Mwaka unaisha, najiandaa kuandika makala yangu, kuelezea jinsi gani JPM amesimamia alichowaahidi kwa watanzania
 
..hoja yangu siyo Raisi kulipa kodi.

..hoja yangu ni mshahara na marupurupu yake kupunguza ili iendane na hali halisi ya kiuchumi na kijamii.

..Mh.Lukuvi alidai gharama za kumtunza Raisi wa Tz ni sawa na bajeti ya mikoa mitano. Tuanzie hali.
Rais Magufuli alisema mshahara wake ni shilingi milioni 9.5. Kama huo mshahara ni mkubwa kulingana na hali halisi, huo ni mjadala mwingine.

Sielewi maana ya dhana inayosema kumtunda Rais wa Tanzania ni sawa na bajeti ya mikoa mitano. Mikoa gani hiyo kwa sababu kila mkoa unatofautiana katika bajeti. Hata hivyo kuna matumizi mengine hayaepukiki kutokana na mazingira.
 
Rais Magufuli alisema mshahara wake ni shilingi milioni 9.5. Kama huo mshahara ni mkubwa kulingana na hali halisi, huo ni mjadala mwingine.

Sielewi maana ya dhana inayosema kumtunda Rais wa Tanzania ni sawa na bajeti ya mikoa mitano. Mikoa gani hiyo kwa sababu kila mkoa unatofautiana katika bajeti. Hata hivyo kuna matumizi mengine hayaepukiki kutokana na mazingira.

..Raisi analipwa milioni 9.5 kwa mwezi lakini ana uwezo wa kuwapa Bakwata briefcase iliyojaa fedha?

..suala hili linahitaji chombo huru kuchunguza mshahara wa kweli wa Raisi pamoja na marupurupu yake.
 
bila shaka mshahara wa rais ni tofauti na gharama za kumtunza rais. gharama ni kubwa kwa mujibu wa Lukuvi na hii ndiyo hoja. swali ni je, hizo gharama ni zipi na je, zinaweza kupunguzwa?
 
Back
Top Bottom