Rais Magufuli malizia kiporo cha Mwalimu

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
Kutafakari mambo kwa yakini na umakini kuna raha yake, moja ikiwa kuupa ubongo changamoto mpya hivyo kufanya kazi kwa kiwango cha juu kuliko kilichozoeleka. Hili hurahisisha ugunduzi mpya, utatuzi tofauti wa mikwamo na ukomavu wa fikra.

Kutafakari ndiko kumefanya wanazuoni mahiri tena maarufu kuyang’amua mambo mengi ambayo hayakuwa katika mazingira yao wala vizazi walivyoishi havikuyaishi lakini yamekuwa muhimu miaka mingi baada ya kufa kwao kimwili.

Hata kizazi kilichopo, kile kinachothamini ukuu wa fikra kwa wingi wake ndani ya jamii zilizoendelea kina gunduzi (innovations) nyingi, changanuzi za nadharia, tafiti na vinginevyo ambavyo vitakuja kutumiwa kwa uaminifu, weledi na mafanikio miaka mingi ya vizazi vijavyo.

Tukiacha hayo, fikra moto na uwezo wa kusoma katikati ya mistari ndivyo vinafanya kuihoji nadharia ya kujenga taifa kupitia siasa za Bara la Afrika, na kutoa jibu rahisi kueleweka kwa mtu aitwaye wa kawaida.

Ujenzi wa taifa kwa muktadha tofauti unaelezeka kwa upana na urefu usiokutanika, kwa maana kwamba tafsiri ni nyingi tofauti zenye malengo dhahiri na siri kukidhi mazingira na watu husika. Ukiachilia mbali maana zenye malengo ya kimaslahi yanayofanya ujenzi uitwao wa taifa kukosa ukomo, ujenzi mahiri wa taifa ni ule timilifu ndani ya muda unaotokana na kukamilika kwa utekelezaji wa mipango, malengo na matakwa ya wananchi kwa ujumla wao.

Ujenzi wa taifa ni ukamilifu wa ahadi za wajenzi wakuu, viongozi na serikali wanazoziongoza kwa kipindi husika. Ujenzi wa taifa ni ule unaokamilika, wenye mafanikio yanayoakisiwa katika maisha ya kila siku ya mwananchi; si ule unaoendelea kila mwaka bila kikomo!

Nchini Tanzania dhana ya ujenzi wa taifa imekuwa ikisikika tangu Uhuru hadi sasa ambapo baadhi ya wanasiasa wanajinadi kuendelea kujenga nchi licha ya msingi wa taifa kusemwa ulishajengwa kwa ukamilifu na Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere enzi za uongozi wake.

Hapa ndipo naweka hoja mezani kwamba; kama Hayati Nyerere alifanikiwa kujenga na kukamilisha msingi imara wa taifa katika kipindi chake cha uongozi, kwanini sehemu ya ujenzi iliyobaki haikamiliki, haimaliziwi na muda unazidi kwenda!

Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli nahisi anayo fursa ya kuibeba changamoto hii na kujipa kila sababu ya kuingia kwenye historia kuu ya nchi kwa kuifanyia mambo muhimu na makubwa Tanzania likiwemo hili la kumalizia ujenzi wa taifa unaoendelea zaidi ya nusu karne sasa.

Rais Magufuli ambaye kwa bahati nzuri amepata kuwa waziri wa ujenzi naamini anajua gharama za ujenzi zinavyoongezeka maradufu pale ujenzi unapochelewa kukamilishwa ndani ya wakati uliopangwa.

Binafsi najua Rais anao uwezo wa kufanya mambo mengi kwa nchi yatakayokamilisha rasmi ujenzi wa taifa kwa kuzitimiza ahadi za viongozi na serikali tangu awamu ya kwanza hadi hii ya tano ya uongozi wa Tanzania ili serikali zijazo zikose kisingizio cha kudai zinajenga nchi hivyo kukwepa kuwapa wananchi maendeleo. Huko tuendako tungependa tusisikie hadithi zisizoisha za ujenzi bali ukarabati na uboreshaji kwa kuwa hayo ndiyo maendeleo.

Mungu mwenyewe aliujenga ulimwengu kwa maana ya kuuumba pamoja na viumbe wote ndani yake kwa siku sita, na akapata muda wa kupumzika; iweje nchi yenye watu wengi wenye kila aina ya uwezo na maarifa wakiwemo wasomi nguli iendelee kujengwa tu bila kukamilika au kujua lini ujenzi unamalizika!

Hata maisha yanajengwa kwa wakati, yanatimia kwa miaka na kutamatishwa kwa kifo hapa duniani sembuse ujenzi wa nchi ulio ndani ya uwezo wa wananchi na viongozi wao kupitia mipango mahsusi ya maendeleo!

Bahati nyingine nzuri Tanzania imeongozwa na chama kimoja tangu uhuru, yaani TANU iliyobadilika na kuwa Chama Cha Mapinduzi-CCM hivyo kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi kuwa rahisi zaidi kwa kuwa msimamizi mkuu wa ujenzi ni yule yule. Itakuwa heshima kubwa kama ujenzi ulioanzishwa na chama tawala utakamilishwa nacho chini yake Rais Magufuli mwenye nia ya dhati ya kuibadilisha nchi kuifanya ijitegemee kupitia uchumi wa viwanda.

Kama Rais Magufuli na serikali yake wameweza kumaliza tatizo lililoonwa sugu la madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini kwa kuwashirikisha wananchi na kuwashawishi wadau mbalimbali pasi shurti, suala la kumalizia ujenzi wa taifa linawezekana kupitia utekelezaji wa miradi inayosuasua, ahadi na mipango ya serikali zilizotangulia.

Kwa mfano; ujenzi wa eneo mojawapo la mbele unaweza kukamilika mapema zaidi kwa kukamilisha miradi yote ya umeme na kulipa uwezo zaidi Shirika la Umeme (ugavi ukiwemo) Tanesco ili Tanzania iondokane na tatizo sugu la kukatika ovyo umeme na kuwezesha nchi kuwa na nishati ya kutosha na ya uhakika itakayowezesha uchumi tarajiwa wa viwanda.

Ujenzi wa taifa usiokamilika una athari nyingi. Ndiyo unafanya watumishi wa umma kuendekeza urasimu, kufanya kazi kwa mazoea, kupalilia rushwa na u-hewa hewa mwingi unaogharimu mabilioni ya shilingi za kodi za wananchi, achilia mbali migogoro mingi ya kujitakia.

Hebu fikiri mzee mstaafu serikalini anapolazimika kufuatilia majibu ya barua ya madai yake stahiki kwa zaidi ya mwaka mmoja halafu ofisini yuko mtumishi wa umma anayelipwa mshahara kwa kazi ya kumhudumia kwa wakati mwananchi kama huyu mstaafu! Kuendelea kwa ujenzi ndiko kunafanya kuandika tu barua ya majibu iliyofika ofisini, kazi isiyozidi dakika 10 eti kugharimu miezi kadhaa ya kufuatilia!

Nashawishika kwamba serikali hii haitaacha mambo yaende kimazoea zoea mbele ya macho yake.

Najishawishi kwamba Rais Magufuli atamalizia ujenzi wa taifa wenye msingi uliokamilishwa kitambo na hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Watanzania wamejibana kwa zaidi ya miaka 50 ili ujenzi wa taifa wanaoambiwa na viongozi wao ufanikiwe. Nafasi kubwa na uwezo vipo mikononi mwake Rais Magufuli kukamilisha ujenzi huu wa muda mrefu ili hatimaye Watanzania waanze kula matunda ya kujitolea, kujitoa kwao, kujibana na kufunga mikanda wakati wote ujenzi unapotajwa kuendelea.

Inawezekana.


Chanzo: Rai
 
Back
Top Bottom