Rais Magufuli, kiongozi wa watu au mtawala muimla anayejificha kwenye maendeleo ya vitu?

mtapa wilson

Member
Jan 2, 2014
10
13
Novemba 2019, Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ametimiza miaka minne tangu alipoapishwa rasmi kwa mujibu wa katiba kuwa Rais wa nchi hii.

Ndani ya uongozi wake tangu ameingia madarakani amejipambanua kama kiongozi wa wanyonge kwa kupambana na rushwa kila mahali katika taasisi ya serikali.

Mara kadhaa ameonekana hadharani akichukua hatua za moja kwa moja dhidi ya watendaji pamoja na wateule wake wanaodaiwa kushindwa kwendana na kasi yake.

Rais Magufuli ameshatumbua wateuzi wake wengi wakiwemo mawaziri, wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na mikoa, makatibu tawala wilaya na mikoa, wakuu wa taasisi za ulinzi na usalama pamoja na kupangua safu za uongozi serikalini kwa kuhamisha watendaji na wateuzi wake hawa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Hii yote akilenga kuchagiza kuongeza kile alichokiita kuwa ni uwajibikaji serikalini huku akisisitiza kuwa suala la mabadiliko kwake litaendelea kuwepo bila kujali wakati gani ilimradi tu maendeleo ya wananchi yapatikane.

Ndani ya miaka minne, utawala wa Rais Magufuli umejikita zaidi kujenga miundombinu ya kuuchumi mikubwa kama vile ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege unaolenga kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Pamoja na masuala yote hayo, utawala wa Rais Magufuli umejitia dosari kwa kwa kushindwa kusimamia misingi ya utawala bora inayofuata misingi ya sheria.

Ndani ya miaka minne ya Rais Magufuli, zimeanzishwa sheria nyingi kandamizi dhidi ya vyombo vya habari ikiwemo sheria ya huduma za vyombo vya habari (2016), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Takwimu Mwaka 2015 (Marekebisho ya Mwaka 2018), Sheria ya Vyama vya Siasa 1995 ( Marekebisho ya Mwaka 2019), Mabadiliko ya Mwaka 2019 ya Sheria ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (Sura ya 56).

Sheria zote hizo zimetajwa kuminya uhuru wa wanahabari, wanasiasa wa upinzani pamoja na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya haki za binadamu wakiwemo wakuu na viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayokosoa utawala wa Rais Magufuli.

Hivi karibuni mashirika mawili ya Amnesty International na Human Rights Watch yalitoa ripoti zake mbili ambazo yametaja visa kadhaa vya ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo kuminywa kwa uhuru wa kujieleza, kujumuika na kutoa maoni.

Ripoti hizo mbili zilieleza namna wakosoaji wa utawala wa Rais Magufuli unavyowakandamiza wanahabari, wanasiasa wa upinzani na watetezi wa haki za binadamu ikiwemo taasisi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwa kuwekea vikwazo watendaji wake wakuu.

Mathalani; wapo wanahabari na wanaharakati wa mashirika mbalimbali waliotuhumiwa na kuhojiwa juu ya uraia wao. Wapo wengine wamenyang'anywa hati zao za kusafiria. Hii ikiwa ni mwendelezo wa kuminya haki za binadamu-haki ya kutembea.

Ndani ya miaka hii minne tumeshuhudia nchi ikiingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa kukiwa na hila za wazi kabisa.

Wagombea wa vyama vya upinzani wakiondolewa kwa sababu ambazo hazikuwahi kutajwa miaka yote ya uchaguzi. Mfano; chama cha mgombea hakijasajiliwa kwa kwakuwa tu mgombea aliandika kifupi cha jina la chama chake.

Mwenendo wa siasa za Tanzania, ambayo imetajwa kama kisiwa cha amani na nchi yenye demokrasia ya kweli kwa miaka mingi, sasa uko njia panda chini ya utawala wa Rais Magufuli.

Wapo wanaomuunga mkono wakidai analeta maendeleo. Lakini wapo wanaomkosoa kwa kumuita mtawala muimla anayeminya wakosoaji wake.

Hali hii inaacha maswali mengi ikiwemo; Je, Rais Magufuli ni kiongozi wa watu au ni mtawala muimla anayejificha kwenye maendeleo ya vitu?

Makala hii ilichapishwa katika mitandao ya runinga ya mtandaoni ya Watetezi TV inayomilikiwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) mnamo Novemba 10, 2019. Makala hii ni maoni binafsi ya mwandishi na wala sio msimamo wa chombo cha habari.
images%20(22).jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom