Rais Magufuli, Katiba Mpya ni kwa manufaa mapana ya Watanzania wa kizazi hiki na vile vinavyofuata

Freesoule

JF-Expert Member
Jun 18, 2013
269
272
Rais Magufuli, kwa muda mrefu yamekuwepo malalamiko juu ya katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, wala hayakuanza wewe ulipoingia madarakani. Serikali iliyokutangulia ikiongozwa na Raisi Kikwete ilikumbwa na kashifa nyingi za ufisadi, ubadhirifu na rushwa (IPTL, Escrow, Richmond, n.k.) mpaka ikaitwa dhaifu na Raisi mwenyewe kuitwa dhaifu katika bunge la Jamhuri ya Muungano.

Pengine kwa kutambua hilo, Raisi 'dhaifu' Kikwete akaona njia pekee ya kuwapa nafasi kubwa wananchi kuchangia katika maendeleo yao wenyewe, na kuwa na maendeleo endelevu, ni kuurekebisha mkataba kati ya wananchi na viongozi (pengine sahihi zaidi kuwaita "watawala" kwa katiba tuliyo nayo sasa). Mkataba huo unaitwa katiba.

Huyu Rais 'dhaifu' aligundua kuwa kwa miaka yake kumi ya "utawala" wake, hakuweza kutimiza dhamira yake ya "maisha bora kwa kila mtanzania", kwani mpaka anaondoka madarakani zaidi ya 70% ya wananchi walikuwa bado wanaishi chini ya mstari wa umasikini. Pengine aligundua kuwa, umasikini hauondolewi kwa ahadi na kauli mbiu kama "maisha bora kwa kila Mtanzania" au "hapa kazi tu", bali uchumi shirikishi.

Uchumi shirikishi ambao huchukua mawazo na matakwa ya Watanzania milioni 55 kupitia bunge na njia zingine shirikishi, badala ya maamuzi haya kufanywa na mtu mmoja na wapambe wake Ikulu. Ndiyo maana katika rasimu ya katiba mpya iliyopendekezwa na tume ya Jaji mstaafu Warioba wananchi walipendekeza madaraka ya Rais yapunguzwe, ili maamuzi ya maendeleo na uongozi yafanywe na Watanzania walio wengi zaidi. Na inaposomeka Raisi haimaanishi wewe ndugu Magufuli, ukifika muda wewe utaondoka na ofisi ya Raisi itabaki - "nothing personal".

Wananchi wana suluhisho la mustakabali wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ambao umekuwa na matatizo kwa muda mrefu, pengine tokea uundwe. Mapendekezo yao juu ya mustakabali wa muungano yamo kwenye rasimu ya katiba mpya ya Jaji Warioba.

Wananchi wanajua kuwa, ili kuwe na maendeleo endelevu, ni lazima nchi iongozwe kwa mifumo ya uongozi na si onyesho la mtu mmoja ('one-man show') kama ifanyikavyo sasa. Kwa sasa Rais ndiye anayefanya ukaguzi kwenye hospitali ya Muhimbili, Rais ndiye anayefanya ukaguzi bandarini, Rais ndiye anayeongea na wafanyabishara wa kila wilaya Tanzania, Raisi ndiye anayeshughulikia korosho za Lindi na Mtwara, Rais ndiye anayeteua kila mkuu wa mkoa na wilaya, mkurugenzi wa kila wilaya, mawaziri, majaji, CAG, IGP, viongozi waandamizi wa tume "huru" ya uchaguzi, ...., ..., orodha ni ndefu. Uteuzi wa wengi wa hawa unaweza kutenguliwa wakati wowote Rais anapotaka. Wapo kutimiza matakwa ya Raisi, na si mara zote matakwa ya Raisi ni matakwa ya wananchi. Kwa hiyo ni uongozi/utawala wa Mtanzania mmoja aitwaye Raisi, akiwaacha karibia wengine wote milioni 55 kuwa watazamaji.

Mfano mzuri ni huu wa katiba mpya, Watanzania wameweka wazi kupitia tume ya Jaji Warioba kuwa wanataka katiba mpya, hayo ndiyo matakwa ya Watanzania. Ila Mtanzania mmoja mwenye cheo cha Raisi, na kwa sasa akiwa ni ndugu John Pombe Magufuli, anasema Watanzania hawatapata katiba mpya - matakwa yake binafsi.

Mfano mwingine ni katiba ya sasa inaruhusu Watanzania kufanya mikutano ya siasa na kufanya siasa, ila Rais John Pombe Magufuli amekataza hilo, tena kwa neno lake tu. Rais anavunja katiba na sheria. Ndiyo maana mapendekezo ya Watanzania kupitia rasimu ya katiba mpya ya Jaji Warioba ni kuwa madaraka ya ofisi ya Raisi yapunguzwe, yagatuliwe.

Hata ungeweza kuifanya Tanzania iwe Dubai ndani ya miaka yako mitano, ndugu Raisi, huwezi kuwa na uhakika kama maendeleo haya yatadumu, pasipokuwa na katiba inayoyalinda hayo maendeleo. Hiyo ndiyo mantiki ya maendeleo endelevu. Wewe ulipoingia madarakani uliitupilia mbali miradi ya watangulizi wako kama haikuwa na maana yoyote (Rejea Kilimo Kwanza, n.k.). Kwa namna hiyo hiyo huwezi kuwa na uhakika kuwa atakayekuwa Raisi baada yako ataienzi miradi uliyoianzisha, pengine ataitupilia mbali na kumbukumbu yako ikasahaulika milele. Kama isemwavyo, Roma haikujengwa kwa siku moja. Hutaimaliza miradi yote unayoianzisha (kama uliianzisha at all), na kwa katiba tuliyo nayo sasa kumalizika kwake kutategemea 'hisani' ya Raisi atakayefuata. Ndipo hapo viongozi wengine hujitawaza kuwa Maraisi wa milele wakidahani wao ndio pekee wanaoweza kutekeleza miradi ya maendeleo, wanakuwa na hofu kama atakayekuja ataendeleza walichokianzisha (tafakari mfano wa Raisi Paul Kagame wa Rwanda). Wanasahau kuwa suluhisho rahisi ni katiba na sheria zinazolinda maendeleo endelevu, badala ya kuwa na mtu mmoja aitwaye Raisi ambaye huamua kwa utashi wake pekee mustakabali wa dira ya maendeleo ya nchi katika kipindi cha "utawala" wake.

Rejea mifano ya nchi zilioendelea kiuchumi kama Libya, zilipoteleza hazikuinuka tena. Laiti Libya ingekuwa na katiba nzuri, inayowapa wananchi madaraka, ingeinuka hata baada ya Kanali Muamar Gadaffi kuondoka, bila kujalisha aliondoka kwa njia gani.

Kama wewe ni Raisi msikivu, basi wasikilize wananchi. Wananchi, ambao ndio wenye nchi, waliona mkataba kati yao na "watawala" uitwao katiba, haukidhi tena matakwa yao, ambalo ndilo jambo pekee la msingi. Wasikilize. Usikivu wako usiwe ni kutaka kusikia yale unayoyapenda wewe, bali wanayoyapenda wananchi. 'After all', wananchi ndio wenye nchi, si Raisi wala mtu mmoja mmoja au vikundi vya watu wachache. Utaacha alama ya uongozi kwa kuweka vipaumbele katika usahihi wake, la sivyo kumbukumbu ya 'utawala' wako haitakuwa ni ile inayong'ara. Wananchi wamekuonyesha vipaumbele vyao, kimojawapo ni katiba.

Rais Kiwete alikuwa na maono juu ya hili, na wewe kuipuuzilia mbali katiba mpya ni kuyadharau maono yake. Uongozi wako haujapunguza umasikini zaidi ya ule wa kwake, kwa hiyo huwezi kusema yaliyoazishwa katika serikali yake hayakuwa mazuri kama ya serikali yako.

#KatibaMpya
 
Katiba mpya ni kupoteza muda..
Iliyopo inatutosha kwa sasa,

Mh Rais wewe endelea na miradi yenye tija kwa jamii tumecheleweshwa sana..likiwemo hili la katiba sababu lishakula pesa nyingi ya mwananchi bure..
 
Katiba mpya ni kupoteza muda..
Iliyopo inatutosha kwa sasa,

Mh Rais wewe endelea na miradi yenye tija kwa jamii tumecheleweshwa sana..likiwemo hili la katiba sababu lishakula pesa nyingi ya mwananchi bure..

Sema mnachowaza siku zote ni kuona tu ccm inabakia madarakani milele! Hata hiyo miradi mnaijenga kwa lengo la kujipatia tu umaarufu wa kisiasa na ndiyo maana pongezi na utukufu hauishi kana kwamba hela inatoka mfukoni mwa Rais! kumbe ni kodi zetu tunazotozwa kila siku/kila mwezi!

Ccm hamjawahi kuwa na ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa moja ya Taifa kubwa lenye nguvu kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiteknolojia baada ya miaka kadhaa mbele kama walivyofanya China, nk. Hatujaona mkakati wowote ule wenye tija zaidi ya bla bla tu nyingi.
 
Hivi Katiba ya Warioba Ingesaidia lolote katika hayo uliyoorodhesha? Au ni basi tu kuwa na Katiba mpya ?
 
Sema mnachowaza siku zote ni kuona tu ccm inabakia madarakani milele! Hata hiyo miradi mnaijenga kwa lengo la kujipatia tu umaarufu wa kisiasa na ndiyo maana pongezi na utukufu hauishi kana kwamba hela inatoka mfukoni mwa Rais! kumbe ni kodi zetu tunazotozwa kila siku/kila mwezi!

Ccm hamjawahi kuwa na ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa moja ya Taifa kubwa lenye nguvu kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiteknolojia baada ya miaka kadhaa mbele kama walivyofanya China, nk. Hatujaona mkakati wowote ule wenye tija zaidi ya bla bla tu nyingi.
Fedha zilipotea kwa sababu watu wachache ambao hawakutaka maoni ya Watanzania walio wengi yaheshimiwe waliuvuruga mchakato wa kupata katiba mpya. Sadly, Magufuli is orchestrating their position. By his position on this, he is complicit.
 
Back
Top Bottom