Rais Magufuli hakuvunja Katiba kuwateua Prof. Kabudi na Mpango kuwa Mawaziri kabla ya kumuapisha Waziri Mkuu. Zitto ndiye alifaulu kupotosha umma

Mdanganywa

JF-Expert Member
Jun 15, 2009
620
500
_ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _
TITLE: KATIBA HAIMLAZIMISHI RAIS KUSHAURIWA
ANALYST: JOSEPH MAGATA
Cell: +255 75 4710684
DATE: December 16, 2020
NEWSPAPER: RAIA MWEMA, pg. 19
_ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _
Tarehe 12/11/2020 Rais John Magufuli alimteua Kassim Majaliwa kuwa waziri mkuu. Tarehe 13/11/2020 akamteua Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Palamaganda Kabudi kuwa waziri wa Mambo ya nje.

Tarehe 15/11/2020 Kassim Majaliwa, Palamaganda Kabudi na Philip Mpango wakaapa kiapo cha majukumu yao.

Dakika chache baada ya kiapo mitandao ikaibua hoja kwamba Kabudi na Mpango ni mawaziri batili kwa sababu ibara ya 55(1) inamtaka Rais kuteua mawaziri baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

Kigezo ni kwamba tarehe 13/11/2020 walipoteuliwa mawaziri hao Kassim Majaliwa hakuwa na madaraka ya uwaziri mkuu maana ibara ya 51(1) ya katiba inasema madaraka hayo aliyaanza alipoapa tarehe 15/11/2020.

Hoja hii ni ngumu kwa asiyefahamu miundo ya serikali za hapa duniani. Novemba 4, 2020 yaani siku nane kabla ya uteuzi wa waziri mkuu nilieleza miundo hiyo kwenye gazeti hili (uk. 9) na leo tena narudia kwa kifupi.

Muundo wa kwanza ni wa Uingereza unaoitwa "parliamentary" au "Westminster" ulianzia England mwaka 1689.

Katika muundo huu mawaziri wote ni wabunge na kuwemo kwao bungeni kunalazimisha wawe na waziri mkuu.

Muundo wa pili unaitwa "presidential" ulianzia Marekani mwaka 1789. Katika muundo huu wa "kimarekani" rais anachaguliwa na watu lakini mawaziri hawamo bungeni, hivyo hakuna waziri mkuu.

Muundo mwingine ulioanzia Ufaransa mwaka 1958 ambao waziri mkuu anatokea chama chenye wabunge wengi. Je, waziri mkuu akitoka chama tofauti na rais inakuwaje? Jibu ni refu kidogo.

Kwa historia ya Ulaya chama kinapopata wabunge wengi maana yake taifa limekituma kikaisimamie ilani kiliyoinadi. Hivyo madaraka ya serikali yanatoka kwenye bunge tofauti na Marekani ambako yanatoka kwa rais.

Rais wa Ufaransa akikosa wabunge wengi maana yake bunge linasimamia ilani tofauti na yake. Hivyo rais huyo hawezi tena kuendesha serikali anageuka kuwa kama mfalme au malkia wa Uingereza.

Kinyume chake waziri mkuu sasa ndiye anayeendesha serikali na muundo huo unakuwa ni wa "Westminster".

Mwaka 1986 Jacques Chirac na chama chake walipata wabunge wengi. Francois Mitterrand aliyeshinda urais wa Ufaransa akaacha kuendesha serikali, Jacques Chirac akawa waziri mkuu akaendesha serikali.

Kitendo hiki cha waziri mkuu wa Ufaransa kumzidi rais madaraka kinaitwa "cohabitation" na kilitokea tena kwa mawaziri wakuu Edouard Balladur (1993-1995), Lionel Jospin (1997-2002).

Hii ndiyo sababu ya rais wa Ufaransa kushauriwa na waziri mkuu kwani inapotokea hali hii ("cohabitation") rais anachokosa si tu mamlaka ya kuteua mawaziri bali hata kutenda lolote bila ruhusa ya waziri mkuu.

Rais akipata wabunge wengi anabaki na madaraka hivyo anaamua kazi za kumpa waziri mkuu au ikibidi hampi kabisa maana wako chama kimoja. Hapo muundo unakuwa wa "kimarekani" yaani "presidential".

Japo muundo huu ni wa "kifaransa" kiukweli ni muundo unaogeukageuka yaani leo unakuwa wa "kimarekani" kesho unakuwa wa "Westminster" kadiri rais anavyokosa au kupata wabunge wengi.

Kwa kuwa tunachambua tofauti ya rais na waziri mkuu sasa tuone tofauti za miundo hii duniani.

Katika muundo wa "Westminster" kiongozi wa serikali yaani waziri mkuu lazima yumo bungeni na ni mbunge wakati katika muundo wa "kimarekani" kiongozi wa serikali ni rais na hayumo bungeni.

Asili ya muundo wa "Westminster" bungeni ni mahali pa kujibizana na serikali yaani "parle" hivyo pakaitwa "parliament". Kwa muundo wa "kimarekani" bungeni ni mahali pa kutunga sheria hivyo pakaitwa "legislature".

Hivyo, katika muundo wa "Westminster" bungeni kuna kipindi cha maswali kwa mawaziri, katika muundo wa "kimarekani" kipindi hicho hakipo wala hakihitajiki, rais hayumo bungeni.

Katika muundo wa "Westminster" kikao cha baraza la mawaziri kipo kinaongozwa na waziri mkuu. Katika muundo wa "kimarekani" kikao cha baraza si cha lazima tena hakimo kabisa kwenye katiba ya Marekani.

Katika muundo wa "Westminster" mawaziri huwajibika kwa pamoja bungeni yaani "collective responsibility". Katika muundo wa "kimarekani" kila waziri anawajibika kwa rais tu, hakuna waziri yoyote bungeni.

Katika muundo wa "Westminster" bunge linaweza kupiga kura ya kutoiamini serikali yaani kutomuamini waziri mkuu. Katika muundo wa "kimarekani" bunge haliwezi kumuondoa rais kwa kutokumuamini.

Katika muundo wa "kimarekani" mke wa rais amezoea kuitwa "first lady". Dunia bado inasubiri mwanamke atawale Marekani tupate jina la mume wa rais. Katika muundo wa "Westminster" mke wa waziri mkuu haitwi "first lady" na mume wa waziri mkuu haitwi chochote.

Tumeiona miundo hii miwili kwa kiasi cha kutosha. Je, Tanzania ina muundo gani? Tanzania muundo wetu ni wa "kifaransa" hivyo madaraka ya Rais yanageuzwageuzwa na idadi ya wabunge anaowapata bungeni.

Rais wetu akikosa wabunge wengi madaraka yanahamia kwa waziri mkuu. Yakishahamia huko muundo huo unakuwa ni wa "Westminster", hivyo rais atalazimika kumsikiliza waziri mkuu kwa chochote.

Rais wa Tanzania akipata wabunge wengi muundo unamrudishia madaraka unakuwa ni wa "kimarekani" yaani "presidential".

Marais wote wa Tanzania wamepata wabunge wengi tangu enzi za TANU hadi CCM. Hatujawahi kupata rais aliyemwachia waziri mkuu serikali kwa kukosa wabunge wengi kama wale marais wa Ufaransa.

Maana yake ni kwamba matukio ya muundo wa "kimarekani" yametutawala kwa miaka yote, hivyo ni vizuri tuyachambue tuone yalivyoyazidi yale ya muundo wa "Westminster".

Kipindi maswali kwa waziri mkuu kila wiki bungeni, ambacho ni cha muundo wa "Westminster" hakikuwa cha lazima na uthibitisho ni kwamba kimekuja juzijuzi tu baada ya Pius Msekwa kustaafu uspika mwaka 2005.

Hata huko Uingereza kilipoanzia kipindi hiki, waziri mkuu anayeulizwa maswali kila wiki ni kiongozi wa serikali, wakati hapa Tanzania kiongozi wa serikali ni rais na hayumo bungeni kama mwenzake wa Marekani.

Katiba ya Marekani haina neno "parliament" wakati ina neno "Legislature" lililotokea mara 23. Kwenye Katiba yetu Tanzania neno "Legislature" limetokea mara nne tu wakati neno "parliament" limetokea mara 313.

Tarehe 09/12/1961 Maria Nyerere hakuwa "first lady" kwa sababu Tanganyika ilipojitawala Julius Nyerere, alikuwa ni waziri mkuu kwa muundo kwa "Westminster".

Tarehe 09/12/1962, Maria Nyerere alianza kuwa "first lady" kwa sababu Julius Nyerere alianza kwa Rais wa Tanganyika yenye vyama vingi lakini mwenye wabunge wengi wa TANU bungeni.

Kikubwa hapa ni kwamba hata usipoujua muundo wa "kimarekani" basi hata neno "first lady" tu linatosha kukuonyesha tulivyomezwa na muundo wa "kimarekani" kuliko wa "Westminster".

Tofauti ya msingi kabisa ni madaraka ya mkuu wa nchi. Muundo wa "Westminster" unamlazimisha sana mkuu wa nchi kushauriwa. Muundo wa "kimarekani" yaani "presidential" haumlazimishi rais kushauriwa.

Hivyo, katika muundo wa "Westminster" kiongozi wa nchi asipoomba ushauri anaweza kusababisha mgogoro mkubwa nchini. Katika muundo wa "kimarekani" si kosa hata kidogo rais asipoomba ushauri.

Kwenye katiba yetu neno "kushauri" au "kushauriana" limo kwenye ibara 16 zifuatazo 44, 37(1), 37(5), 44(2), 54(5), 55(1), 55(2), 59(3), 61(2), 61(3), 109(2), 109(9), 109(11), 118(5), 129(3), 130(1)(g).

Je hitaji la rais kushauriwa lina uzito gani kama limo kwenye kikatiba kama hivi?

Maana ya "kushauri" au "kushauriwa" ni kujulishwa maoni ya anayekushauri. Kikitokea chochote kinacholazimisha rais akubali ushauri basi huo hauwi tena ushauri bali ni amri kwa huyo rais.

Rais yoyote wa muundo wa "kimarekani" ndiye mbeba lawama kwa lolote linaloiharibu au kuifedhehesha au kuiumbua nchi. Hivyo rais huyo anaweza kutofuata ibara zote zinazomuelekeza kushauriwa.

Mfano ni marais wa Marekani wasivyoifuata ibara ya II(2)(2). Ibara hii inasema rais akimteua jaji wa mahakama ya juu kabisa inayoitwa "Supreme Court" lazima kwanza apate ushauri wa bunge kubwa linaloitwa seneti.

Hata hivyo kitabu cha "Encyclopedia Britannica" toleo la mwaka 2012 kinaonyesha kuwa marais wa Marekani huwa wanateua tu majaji bila kuomba ushauri wa hiyo seneti.

Je, marais hawa wamevunja katiba ya Marekani kwa kuipuuza seneti? Hapana, hawajaipuuza seneti.

Jibu ni kwamba binadamu akiamua asishauriwe hakuna tena duniani wa kumlazimisha kushauriwa, yaani ana "sovereignty" ya kukataa au kukubali kushauriwa.

Hata mahakama zinatumia sana uhuru wa kutofuata ushauri. Maneno ya kilatini yaani "amicus curiae" humaanisha mabingwa wa sheria wanaomshauri jaji kabla hajahukumu kesi.

Hata hivyo majaji hawalazimiki kufuata ushauri wa hawa "amicus curiae", tena kesi nyingi za hapa Tanzania, hawa "amicus curiae" huwa hawaitwi kabisa mahakamani.

Tumeona rais wa Marekani asivyoipelekea seneti jina la jaji aliyemteua kinyume na katiba inavyosema, wakati seneti hiyohiyo ndiyo humhukumu rais mvunja katiba, yaani "impeachment".

Hivyo, Rais wa Tanzania anaweza asihitaji ushauri wowote kama wasivyohitaji wenzake wa Marekani. Anaweza asiombe kabisa ushauri wa waziri mkuu anapoteua mawaziri.

Hata zile ibara 16 zenye neno "ushauri" haipo hata moja inayosema lazima rais akubali "ushauri". Hata akishauriwa anaweza kuukataa huo ushauri. Ukiweza kumkatalia mtu ushauri unaweza hata kutomuomba kabisa.

Wala katiba haijafanya tendo la "kumshauri" rais lionekane hadharani linapotendeka. Sasa mtu baki utashutumuje kutoshauriwa wakati hujawahi kuona waziri mkuu yeyote akimshauri rais?

Tume ya Kuajiri ya Mahakama hushauriana na Rais akitaka kumteua jaji wa Mahakama Kuu. Kushauriana huko kuhusu jaji mteule ni kwa mujibu wa ibara ya 109(2) ya katiba yetu.

Sasa Rais wa Tanzania akiteua jaji utashutumuje kuwa hakushauriana na tume hii wakati kushauriana kwenyewe hakufanyiki hadharani?

Hata kama kumshauri rais kungefanyika hadharani, mbona seneti ya Marekani ni kikao cha hadharani na bado marais wa Marekani hawapeleki jina la jaji mteule kwenye hiyo seneti.

Rais hapewi mamlaka na washauri unaowajua na usiowajua. Rais anapewa mamlaka na wananchi yaani ilani ya uchaguzi ya wabunge wengi. Binadamu unaweza usihitaji ushauri wa yeyote duniani kutekeleza mamlaka yako.

Rais wa Tanzania atanyimwa mamlaka siku atakapokosa wabunge wengi, ndipo waziri mkuu ataendesha serikali yaani "cohabitation". Hapo ndipo rais atalazimika kufuata ushauri wa kila aliyeandikwa kwenye zile ibara 16 za katiba.

Hivyo Profesa Palamaganda Kabudi na Phillip Mpango ni mawaziri halali, waliteuliwa tarehe 13/11/2020 kihalali.
_ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _ _

Authored by
Joseph Magata,
Cell: 075-4710684
Email: josephmagata@yahoo.com
 

mnengene

JF-Expert Member
Nov 21, 2011
2,162
2,000
Katiba ipo clear kabisa inaelekeza Rais atateua mawaziri baada ya kushauriana na waziri mkuu. Hata kama ukweli kushauriana huko hakufanyiki hadharani jinsi uteuzi ulivyofanyika hakukuwa na ushauriano wowote.

Kiukweli Rais amevunja katiba mawaziri Kabudi na mipango ni mawaziri feki nachelea huko baadae watu wakaja kuchallenge uwaziri wao ikaamuliwa waliteuliwa kimakosa hivyo maamuzi yao waliyoyafanya wakiwa mawaziri ni null and void.
 

CAPO DELGADO

JF-Expert Member
Aug 31, 2020
1,135
2,000
Hongera Mwandishi kwa Makala NZURI SANA KWENYE GAZETI PENDWA LA RAIA MWEMA.

Umeandika makala nzuri mno na uchambuzi yakinifu.

Tulitamani kuona kuwa Rais AKIMUAPISHA KWANZA Waziri Mkuu BAADA ya KIAPO cha Waziri Mkuu, NDIPO wangeshauriana na Rais KUTEUA MAWAZIRI.

Magufuli anadharau sana.
ANADHARAU NA KUSIGINA KATIBA WAZI WAZI.
 

DOMBWELA

JF-Expert Member
Jan 18, 2014
655
1,000
"Rais yoyote wa muundo wa "Kimarekani" ndiye mbeba lawama kwa lolote linaloiharibu au kuifedhehesha au kuiumbua nchi."

Kama ni hivyo ilikuwaje kwenye kashfa ya Richmond aliwajibishwa Waziri Mkuu Edward Lowassa badala ya Mh. Rais Kikwete?
 

Mdanganywa

JF-Expert Member
Jun 15, 2009
620
500
Lowasa hajawahi kuwajibishwa, alijiuzulu.

"Rais yoyote wa muundo wa "kimarekani" ndiye mbeba lawama kwa lolote linaloiharibu au kuifedhehesha au kuiumbua nchi." Kama ni hivyo ilikuwa je kwenye kashifa Richmond aliwajibishwa Waziri Mkuu Edward Lwossa badala ya Mhe Rais Kikwete?.
 

Gwappo Mwakatobe

JF-Expert Member
Nov 22, 2019
360
500
Rais anashauriwa kisheria na hata bila sheria. Lakini pia kisheria halazimiki kufuata au kupokea ushauri. Sheria inampa uhuru na mamlaka ya kufanya maamuzi yake mwenyewe pasipo kuathiri sheria zingine.

La sivyo atakuwa kama robot akiendeshwa na matakwa au maamuzi ya washauri. Hatuna budi tuwe na rais mwenye hekima na uwezo wa kuchuja na kupima kila anachoambiwa.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom