Rais Magufuli: Hakuna lockdown Tanzania! Mwanangu amepona COVID-19 kwa kujifukiza (Mei 17, 2020)

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,746
11,877
Mhe. Rais Magufuli anatarajiwa kutuma salaam kwa Taifa leo Mei 17, 2020.

Hotuba yake inaaminika itajaa mambo mazito.

Kaa standby kwenye media zote na mitandao ya kijamii muda si mrefu ujao.

Inatarajiwa kuanzia mida ya saa sita na nusu mchana (12:30PM) ndipo atakuwa mubashara.

======




AE76E92B-10D7-43FB-8358-0F81848DEC22.jpeg


‪RAIS AMETOA SALAAM BAADA YA KUSHIRIKI KATIKA IBADA YA KANISA LA KKKT USHARIKA WA CHATO‬

Raisi Magufuli akiwa katika kanisa la KKKT Chato amepata nafasi ya kuzungumza mbapo ameongea mambo mbalimbali,

Katika hotuba hiyo Raisi ameanza kwa kumshukuru Mungu na viongozi wa dini wote nchini. Raisi magufuli amesema “Waimbaji wameimba hapa kwamba bila mungu huwezi kuongoza, bila kumtanguliza mungu huwezi ukafanya chochote. Kwahiyo napenda niwashukuru Watanzania wote, Viongozi wa dini mbalimbali ambao wameshiriki kuliombea taifa hili"

"Na ndio maana siku za nyuma wakati ugonjwa huu umeingia niliwaomba ndugu zangu watanzania angalau tutumie siku tatu za kuomba kwelikweli. Ninawashukuru sana kwa sababu wote tuliomba tulifunga na Mungu amejibu na Mungu ametusikia”

“Ndugu zangu mifano mingi imetolewa, hata katika mahubili yako leo Baba Mchungaji katika injili na katika matendo ya mitume umeeleza ni namna gani watu walivyoweza kumtegemea Mungu walivyoweza kufanikiwa”

“Yule kipofu alimlilia yesu, Mwana wa Daudi nirehemu, Yesu ambaye ni mtoto wa Mungu ambaye naye pia ni Mungu alimponya. Wakati wa dhoruba kula baharini wanafunzi walivyokuwa wamelala wakaona mtumbwi unataka kuzama walipiga kelele” Katika maandiko pia sehemu zingine Yesu aliwakemea kwanza mitume kwa kuwa na Imani ndogo na baadaye akaikemea pepo na mambo yakawa shwari kwahiyo sisi katika kipindi chochote kigumu cha aina yoyote tukimtanguliza Mungu tutafanikiwa”

“Kwahiyo ninawashukuru sana ndugu zangu, ninawashukuru sana Wachungaji, Masheikh, Mapadri, Maaskofu kila mmoja katika eneo lake ambao tulimtanguliza Mungu na Mungu ametusaidia sana”.

“Ndugu zangu katika mapambano ya aina yoyote ni vita. Ugonjwa huu wa Corona hauna tofauti na vita nyingine. Nilikwisha eleza na wataalamu pia wameahaeleza ni namna gani nzuri ya kuweza kupambana na ugonjwa huu hata Baba Mchungaji umezieleza mbinu zote”.

“Ni kweli sikutoa amri ya lockdown ya kuwafungia watu majumbani, ulikuwa ni utumwa wa ajabu. Imagine wewe Lyabange ufungiwe saa nyingine hata usionane na Mme wako Iseme au na watoto wako. Sisi hapa huwa tunaondoka asubuhi kwenda kuchukua chakula, ukachume viazi, maharage yako, uende ziwani ukavue hivyo vyote vingekuwa vimezuiliwa tungekuwa tuko wapi sisi Watanzania miliono 60?"

"Huruhusiwi kwenda sokoni, na saa nyingine unaruhusiwa kutoka kidogo tu, halafu usiku usitoke kana kwamba Corona inatembea usiku tu. Hebu tujiulize sisi Watanzania tuna miradi mingi tumeweka katika nchi yetu, Hiyo miradi yote ingekuwa imesimama."

"Tunajenga reli kwa mabilioni ya fedha, Makandarasi kutoka Nje wale wote tungewazuia vijana wasipate kazi tungekuwa wapi?"

"Tunajenga Mradi wa umeme, thamani yake ni Zaidi ya Trilioni saba zimechukuliwa na Watanzania kwenda kuinvest pale kusudi tuwe na umeme, leo wale wote tungekuwa tumewasimamisha, vijana wale wote tungekuwa tumewasimamisha; tunajenga barabara zote zingekuwa zimesimama."

"Hapo tunajenga meli kwenye ziwa Viktoria na juzi mmeona Injini zimekuja kutoka Korea, zote zile zingekuwa tumesimamisha na injini zisingekuja."

“Kila mmoja afikirie katika maeneo yake tungekuwa wapi? Ndio maana nilimuomba sana Mungu na nawashukuru sana viongozi wa dini zote nikasema hapana, hakuna kujifungia ndani kwa sababu huu utakuwa ugonjwa mkubwa Zaidi kuliko Corona”

"Lakini watu ukishawafungia ndani utawalisha chakula? Watafanyaje? Sitaki kueleza matatizo wanayoyapata katika maeneo mengine nyinyi wenyewe mnajua lakini sisi tumeamua kwenda hivi."

"Tuliamua tumtangulize Mungu, tulianza na Mungu na tutamaliza na Mungu. Na katika hali halisi Mungu amesikia sala zenu kwa taarifa za leo nilizoletewa na naomba niwaeleze kidogo nilizoandika hapa."

"Wagonjwa wamepungua san ahata katika hospitali zetu; Mfano Hospitali ya Amana ya Dar es Salaam ilikuwa inalaza watu 198, leo walikuwepo watu 12 tu."

- Hospitali ya Mloganzila ilikuwa inalaza watu 30 leo wamebaki 6

- Pale kibaha palikuwa pana kituo kinaitwa Rulanzi huwa wanalazwa pale Zaidi ya watu 50 leo walikuwa wamebaki 22 na hawa 22 sio kwamba wamezidiwa wako kama sisi ila tu ado wanaonesha positive.

- Kwenye hospitali ya Agha Khani nako wamepungua wamebaki watu 31,
- Hindu Mandal wamebaki 16,
- Ragent Hospital wamebaki 17,
- TMJ wamebaki 7,
- Labinisia kule Tegeta wamebaki watu 14

"kwahiyo, unaweza kuona trend ya majibu ya Bwana Mungu wetu yalivyofanya kazi".

"Lakini pia hata katika mikoa, Arusha wana vituo vitatu.
- Mshono kina wagonjwa 11,
- Longido jina la kituo linaitwa Nyorendeke hakuna mgonjwa hata mmoja.
- Karatu kuna kituo kinaitwa Dofu hakina mgonjwa.

"Mwanza hapa wana vituo jumla kumi, vinane ni kutoka Halmashauri zifuatazo;

- Busweru wana wagonjwa wawili
- Misungwi wana wagonjw wawili wote wana hali nzuri
- Ukerewe kuna kituo kinaitwa Nyakatunguru hakuna hata mgonjwa mmoja
- Nagu kuna kituo kinaitwa John Mongela hakuna mgonjwa
- Jiji la Mwanza kituo cha Mkuyuni hakuna mgonjwa
- Buchosa kituo cha Nyamunge hakuna mgonjwa
- Sengerema hakuna mgonjwa
- Kwimba hakuna Mgonjwa
- Hospitali mbili za Bugando na seketule Wagonjwa ni wawili hao wana uhitaji wa kuangaliwa kwa sababu pia wana magonjwa mengine.

"Lakini Dodoma kuna vituo vinne mjini viko viwili vina wagonjwa wawili kwa vyote wanahitaji uangalizi na karibu na pia wanamagonjwa mengine, wawili walikuwa wagonjwa Zaidi ya arobaini na kitu wengine wote wamerudi nyumbani."

- Kongwa hakuna mgonjwa
- Kondoa tuna kituo kinaitwa Baleko hakuna mgonjwa. Na kadhalika na kadhalika

"Kwahiyo, Mungu amejibu maombi yenu, Mungu amejibu maombi yetu, na Mungu ashukuriwe sana kwa kutusikiliza. Kwa mwendo huu nataka niendelee kuwasisitiza muendelee kuchukua tahadhari, tuendelee kumuomba. Na tahadhari hizi ambazo tumeendelea luzichukua tuendelee nazo".

"Na kwa trend hii ninavyoiona hapa, kama wiki hii tunayoianza kesho itaendelea hivi nimepanga kufungua Vyuo ili wanafunzi wetu waendelee kusoma. Lakini nimepanga pia sisi kama taifa kuruhusu michezo iendelee kwa sababu michezo ni sehemu moja ya burudani kwa Watanzania".

"Lakini pia, mpaka ninavozungumza hapa kuna Mashirika ya ndege sitaki kuyataja hapa yameshabook watalii, wengine mpaka mwezi wa nane ndege zimejaa kwa ajili ya kuja Tanzania kuanza kutalii".

"Wanakuja kwa sababu wanaujua ukweli, wanakuja kwa sababu Tanzania ni pazuri. Na mimi nimeshatoa maagizo kwa Waziri wa Maliasili pamoja na Waziri wa Uchukuzi waruhusu hizo ndege ziingie na wala hawatawawekea karantini. Akishafika hapa akapimwa Tmperatute akakutwa temperature iko kawaida hana dalili za Corona, aende akaangalie wanyama akakoronaizi huko akaende vizuri".

"Hatuwezi sisi kama taifa huru tukakubali Corona itawale. Mungu wetu atatawala lakini Corona haitatawala".

"Tumekuwa na magonjwa mengi, magonjwa kama Ukimwi nayo ni Virus, Surua ni Virus na kadhalika, lakini hatujakubali yakatawala".

"Uchumi wetu ni namba moja kwanza, tukiufanya uchumi wetu ukalala hata mishahara hatutalipa, hata sadaka tutakosa au uongo baba? Leo pasingekuwa na misa hapa sadaka ingepatikana? Hamna! Toleo la kumi kwa Bwana wetu Mungu tusingetoa. Kwa hiyo, maisha lazima yaende. Lakini nitoe wito kwa Watanzania, pamekuwa na maneno mengi ya kuongezwa ongezwa na kutiwa chumvi. Narudia hofu ni ugonjwa mkubwa kuliko ugonjwa wa Corona".

"Inawezekana watu wamepoteza maisha kwa sababu ya hofu au kudanganywa. Yuko rafiki yangu mmoja Injinia, na nataka niutoe mfano wa kweli alipata strock nyumbani, akabebwa akapelekwa Muhimbili pale Jakaya Kikwete akiwa amepata Strock, kuharusi"

"Amekaa pale baada ya siku mbili tatu akiendelea kutibiwa wakampima Corona wakasema ana Corona, Wakamtoa pale Muhimbili Jakaya Kikwete Centre kwamba huyu ana Corona anapelekwa Amana".

"Amepelekwa pale Amana, akalazwa kwenye kitanda watu wanamuogopa ana Corona. Baadaye ndugu zake wakasemakuwa hapa kama bado amechelewa kushughulikiwa hivi tumchukue. Wakampeleka kwenye hospitali ya Agha Khan, na kule kwa sababu alikuwa ameshaambiwa ana Corona akatafutiwa chumba kimoja akaambiwa atoe advance kwanza miliono 6".

"Wakachangishana wakatoa hizo miliono 6, wakachukua tena vipimo walivyoenda kumpima wakamkuta hana Corona, ndipo wakamuhamisha, wakamuhamishia kwenye wodi ya kawaida. Sasa hivi ameshapona yuko nyumbani anazungumza",

"Kwahiyo unaweza ukaona ni kwa namna gani wengine wamepoteza kwa sababu ya kufikia Corona, Corona Corona. Wapo Wauguzi na Madaktari walikuwa wanafanya Muhimbili na kadhalika kwenye siku za mwanzo walikutana na wagonjwa kuwahudumia. Wakaenda wakafungiwa kwamba lazima wakae siku 14 walikuwa Madaktari 60 pamoja na Manesi'.

"Sasa ukishakuwa Daktari ni kwa namna gani utaacha kukutana na mgonjwa was Corona?"

"Nilipokutana na hizi habari nikasema wafungulie kwa sababu kukuitana na Wagonjwa wa Corona ndio wajibu wao. Wanaendelea na kutoa huduma. Kwa hiyo katika mipango hii ya kupambana na Corona kuna mambo mengi yameingizwa ya hovyo humu ndani."

"Wapo watu wamekuwa wakifariki kwa ugonjwa mwingine, kwanza wanang’ang’ania kumpima. Huyo ameshafariki unampima umfanye nini? Nguvu za kupima wanazo lakini za kumhudumia mpaka afariki hawana. Na akipima kila kitu kinaandikwa Corona. Na wanamzuia asiende kuzikwa na ndugu zake. Sasa kama umempima unaogopaje kuwaruhusu ndugu zake wakamzike mahali walipo. N mbinu za ajabu, za hovyo."

"Kwa hiyo nitoe wito kwa Madaktari kwa sababu najua watanisikia na Wizara ya Afya mtu atakapofariki kw ugonjwa wowote hata kama ni kwa Corona afikishwe na aheshimiwe kwa maziko ya kawaida kutokana na heshima ya uanadamu Corona sio Ebola!! Mbona wa Ukimwi hatuwatengi? Nao tuwatupe hukohuko. Mnona wa TB hatufanyi hivyo? Mbona wa Surua hatufanyi hivyo nao ni virus?"

Ni muelekeo tu wa hovyo ambapo saa nyingine watu wetu tumekuwa tukidanganywa. Mimi napozungumza hapa nina Mtoto wangu alipata Corona, Mtoto wa kuzaa mimi!! Amejifungia kwenye chumba akaanza kujitibu akajifukizia, akanywa malimao na tangawizi, amepona yuko mzima sasa anapiga push up.

"Huu ndio ukweli siwezi nikasema uongo mbele ya madhabahu hapa kwa sababu ninamuheshimu Mungu wangu, Na nampenda Mungu wangu nampenda Yesu wangu siku zote. Kwa sababu wanaweza kufikiri labda mimi hili halijanipata, mtoto wangu wa kuzaa".

"Kwa hiyo ugonjwa huu utasambaa lakini baadaye utaisha. Lakini kama ehee!!, unajua kuna mambo mengine ya ajabu, unakuta Dereva anazuiliwa sijui kwenda wapi. Wewe atoke Dar es Salaam atembee mpaka huko Kilomita elfu moja na kitu, hajaanguka mule kwenye gari anajiendesha vizuri unajua ehee!!"

"Na ndio maana ndugu zangu mimi sikufunga mipaka niliheshimu majirani zangu tumezungukwa nan chi karibu nane ukizifungia maana yake umezinyima uchumi wao. Kuna baadhi ya nchi zinategemea vyakula vya Tanzania, mahindi mchele, nyama kwa sababu sisi tunaongoza kuwa na Ng’ombe wengi, maziwa. Ukiwafungia wale wasipelekewe kule kwanza umewadumaza uchumi wale waliokitengeneza hicho kitu lakini umewanyima pia vyakula watu wanaokuzunguka katika nchi hii."

"Juzi juzi nilikuwa nazungumza na Rais wa Uganda, tulikuwa na upungufu sisi wa sukari karibu tani 40 elfu kwa sababu ya mvua zilizonyeshwa mashamba ya miwa ya viwanda vyetu yakawa yamezama kwenye maji kwahiyo yasingeweza kutengeneza sukari lakini uzalishaji wa sukari Uganda ukawa mzuri. Nimezungumza na Mzee wetu Mzee Museven akasema wala usihangaike tutakuuzia tani 26,000/="

"Ameshatuuzia na tani zimeshaana kuja hapa kwahiyo wala hakuna upungufu wa sukari lakini kwa wanaoficha ni wanafiki na watu wabaya. Wanaficha sio kwa sababu sukari haipo, sukari ipo. Sasa mipaka tungekuwa tumeifunga tungepata hiyo sukari kutoka Uganda? Imekuja kwa meli kutoka Jinja na Rais akaweka watu pale wakatueskot mpaka Mwanza, imeanza kuingia."

"Lakini nyingine imepitia bandandari ya Dar es Salaam Zaidi ya Tani elfu kumi, ni kwa sababu biashara lazima iende. Na ndio maana nimekuwa nikisisitiza ndugu zangu Watanzania, ndugu zangu waumini magonjwa yamekuwepo; ukoma ulikuwepo, wengine walikuwa wanaambiwa na Yesu nenda kanawe kwenye mto anatoka kule ametakasika."

"Wapo wengine waliponywa kumi mmoja akarudi kushukuru, tisa hawakurudi Yesu akawauliza na wale kenda wako wapi? Kwahiyo, katika Yesu kila kitu kinawezekana Leo tumeambiwa hapa Petro alifungwa na Erodi akafungwa minyororo na Maaskari wanamlinda lakini alitoka. Mahubiri yako wazi."

"Kitabu hiki kitakatifu kina yote/ tukiyafata tutashinda na ndio maana Baba Mchungaji wewe hujafunga hili kanisa. Baba Askofu Shoo umfikishie salamu zangu na Baba Askofu wa jimbo hili … Mshahara atapata mshahara wake mbinguni. Kwa kazi kubwa anayoifanya"

“Tutumie mvua hizi za mwisho zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwetu, kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili baadaye wenzetu watakapofunguliwa tuwauzie chakula, endeleeni kuchapa kazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu uchunguzi uliofanyika katika Maabara ya Taifa, Mhe. Rais Magufuli amesema tume iliyoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu imefanya kazi nzuri na matokeo ya uchunguzi wake yatatangazwa na Waziri mwenyewe.

Mchungaji wa KKKT Usharika wa Chato Thomas Paschal Kangeizi amemshukuru Mhe. Rais Magufulu kwa kuungana nao katika Ibada, kuruhusu Makanisa kufanya Ibada na amemuahidi kuwa Wataendelea kumuombea ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ulinzi wa Mwenyezi Mungu.

Katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamechangia shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa jipya la KKKT Chato na amechangia shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kwaya 3 zilizoimba katika Ibada hiyo.

======

TAARIFA YA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Mei, 2020 ameungana na Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Chato Mkoani Geita kusali Ibada ya Jumapili iliyoongozwa na Mchungaji Thomas Paschal Kangeizi.

Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru Waumini wa KKKT Usharika wa Chato kwa kumkaribisha kusali Ibada ya Jumapili pamoja nao, na pia amemshukuru Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Fredrick Shoo na Askofu wa Jimbo la Kusini C (Biharamulo) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Askofu Abednego Keshomshahara kwa kuwaruhusu Waumini kuendelea na Ibada huku wakichukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote wa Dini hapa nchini ambao wamemtanguliza Mwenyezi Mungu na kuwaongoza Waumini kumuomba Mungu aepushe janga la ugonjwa wa Corona na pia kwa kumuombea na kumtia moyo katika kipindi hiki kigumu ambapo dunia inapita katika janga la ugonjwa huo.

Mhe. Rais Magufuli amesema hakutoa amri ya kuwafungia ndani wananchi (lockdown) wala kufunga mipaka kwa sababu ingeleta madhara makubwa katika shughuli za uzalishaji mali, utekelezaji wa miradi, ajira za watu na pia upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo chakula hali ambayo ingesababisha madhara makubwa zaidi.

Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa anamuamini Mungu aliyehai na ndio maana aliamua kumtanguliza Mungu katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona kwa maombi ya siku 3 na sasa amewasihi viongozi wa Dini na Watanzania wote kwa ujumla kutumia siku 3 za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ijayo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa hivi sasa maambukizi ya ugonjwa Corona yameanza kupungua.

Ametoa takwimu za mpaka leo tarehe 17 Mei, 2020 kuwa Hospitali ya Amana (Dar es Salaam) iliyokuwa na wagonjwa 198 imebakiwa na mgonjwa 12, Hospitali ya Mloganzila iliyokuwa na wagonjwa 30 imebakiwa na wagonjwa 6, Kituo cha Lulanzi (Kibaha) kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 50 wamebaki 22, Agha Khan wamebaki wagonjwa 31, Hindu Mandal 16, Regency wamebaki 17, TMJ 7, Rabinisia 14, Moshono (Arusha) 11, Longido 0, Karatu 0, Buswelu 2, Misungwi 2, Ukerewe 0, Magu 0, Mkuyuni 0, Nyahunge 0, Sengerema 0, Kwimba 0, Bugando na Sekou Toure 2, Dodoma 2 (kutoka zaidi ya 40), Kongwa 0, Kondoa 0 nakadhalika. Na kwamba wagonjwa wengi wana hali nzuri.

“Mimi namwamini Mungu na Mungu amejibu maombi yetu, tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutusikiliza na tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu wa Corona” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amesema endapo hali ya ugonjwa wa Corona itaendelea hivi Serikali inafikiria kufungua vyuo ili wanafunzi warudi vyuoni kuendelea na masomo na pia michezo itaruhusiwa kuendelea kufanyika hapa nchini.

Amebainisha kuwa kuna idadi kubwa ya watalii wanaotaka kuja hapa nchini na ambao tayari wameonyesha nia ya kukata tiketi za kuja, hivyo ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka zingine zinazohusika kutowazuia watalii na ndege zinazotaka kuleta wageni hapa nchini.

Amesisitiza kuwa viongozi na Watanzania wote wasiwe na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa Corona kiasi cha kusababisha matatizo mengine ikiwemo kutowahudumia ipasavyo wagonjwa mbalimbali ambao baadhi wanaambiwa wana Corona ilihali hawajaambukizwa ugonjwa huo, ama kuwazuia watoa huduma wakiwemo Madaktari na Wauguzi wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa Corona.

Amesema “wapo watu ambao wanaambiwa wana Corona lakini wakipimwa tena wanakutwa hawana” na amewataka viongozi waache kuwazuia watu kuzika kwa heshima marehemu wao kama ambavyo wanawazika watu waliokufa kwa magonjwa mengine yakiwemo ukimwi, kifua kikuu na surua.

“Hata mimi mtoto wangu alipata Corona lakini amepona, alikuwa anakula limau, tangawizi, anajifukiza mpaka amepona, kwa hiyo ugonjwa huu utasambaa na utakwisha, hatuwezi kufunga mipaka, sisi Tanzania tukifunga mipaka nchi zinazotuzunguka watapata shida, hata sasa tulipata tatizo la upungufu wa sukari, nimezungumza na Rais wa Uganda Mhe. Museveni na zimekuja tani 26,000 kwa meli hadi Mwanza, na tani nyingine 10,000 zimekuja kupitia bandari ya Dar es Salaam, tungefunga mipaka ingekuwaje?” amesema Mhe. Rais Magufuli

Amesisitiza kuwa Watanzania waendelee kuchapa kazi hasa kuzalisha chakula kwa wingi kwa kuwa majirani ambao wamefunga mipaka na wamewafungia watu wao (lockdown), pindi watakapofungua watahitaji chakula na watakuja Tanzania.

“Tutumie mvua hizi za mwisho zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwetu, kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili baadaye wenzetu watakapofunguliwa tuwauzie chakula, endeleeni kuchapa kazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu uchunguzi uliofanyika katika Maabara ya Taifa, Mhe. Rais Magufuli amesema tume iliyoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu imefanya kazi nzuri na matokeo ya uchunguzi wake yatatangazwa na Waziri mwenyewe.

Mchungaji wa KKKT Usharika wa Chato Thomas Paschal Kangeizi amemshukuru Mhe. Rais Magufulu kwa kuungana nao katika Ibada, kuruhusu Makanisa kufanya Ibada na amemuahidi kuwa Wataendelea kumuombea ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ulinzi wa Mwenyezi Mungu.

Katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamechangia shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa jipya la KKKT Chato na amechangia shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kwaya 3 zilizoimba katika Ibada hiyo.



Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato

17 Mei, 2020




1.jpg
2.jpg
3.jpg


.
 
56 Reactions
Reply
Back
Top Bottom