Rais Magufuli: Hakuna Lockdown kwa Dar wala Tanzania, NEVER! Tusiwatishe watanzania, hofu ni ugonjwa mkubwa kuliko Corona

idawa

JF-Expert Member
Jan 20, 2012
23,464
2,000
Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Magufuli anatarajiwa kuzungumza mubashara na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu ugonjwa wa Corona kutokea Chato saa 9:45 alasiri leo tarehe 22.4.2020


--

HOTUBA YA RAIS MAGUFULI (KWA UFUPI)

Rais ameshauri tuendelee kutumia njia za asili kama kujifukizia ili kupunguza corona.

Watanzania tuendelee kuchukua hatua za tahadhari, ugonjwa huu wa COVID-19 upo na ni hatari

Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuilinda nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya COVID-19, nimekubaliana na hatua mnazoendelea kuzichukua katika kipindi hiki”-

Nawapongeza viongozi wa Dini na watanzania kwa ujumla kwa kuitikia wito wa kuliombea taifa kwa siku 3 dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, nina amini Mungu wetu ni wahuruma atatusikiliza na siku moja tutalishinda hili gonjwa.

Nawashukuru kwa kuja kunipa 'briefing' za jinsi tunavyoendelea kupambana. Nimekubaliana na hatua mnazoendelea kuzichukua katika kipindi hiki - Napenda kushukuru Watanzania ambao kwa nyakati za maombi tulizotangaza kwa siku 3, wote walishiriki

Nawapongeza Madaktari, Manesi na Wahudumu wote wa sekta ya afya nchini ambao kila mmoja katika maeneo yao ya kazi wameendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa mbalimbali na wagonjwa wa COVID-19.

endeleani na moyo huo wa uzalendo, mnafanya kazi ya Mungu ya kuwahudumia Watanzania, msivunjike moyo, Serikali ninayoiongoza ipo pamoja nanyi, ninatambua kazi kubwa mnayoifanya.

Natoa wito kwa watanzania kupuuza taarifa za upotoshaji zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii na watu kutoka nje ya Tanzania kuhusu ugonjwa wa COVID-19”

Tujaribu kutumia njia nyingine za asili kama kujifukiza. Kujifukiza ni scientific kwa kuwa mvuke wa maji, maji yanakuwa vapour yakiwa 100 degree centigrade ambazo zinatosha kumyeyusha hata #CoronaVirus

Wizara ya Afya waeleze namna gani kujifukiza kunakinga dhidi ya #COVID19. Njia za kutumia hata kuchanganya na muarobaini na vitunguu swaumu zitumike

Dar es Salaam ina wagonjwa wengi kwasababu ni ‘great city’ ambayo lazima iwe na wagonjwa wengi. Nimeteua Katibu Mkuu mpya ili takwimu za wagonjwa wanaopona ziwe zinatangazwa ili wananchi wawe na confidence

Lakini pia taarifa zetu ziendane na ukweli hasa katika watu wanaopona. Nina taarifa kwamba mpaka leo tulikuwa na wagonjwa 284, lakini naambiwa karibu 100 ya wagonjwa walishapona. Hizi takwimu za wagonjwa wanaopona nazo zitangazwe ili kuwaondolea hofu wananchi.

Hakuna haja ya kumuweka mtu Magufuli Hostel sijui siku 20, wakati unamuona kabisa hana tatizo - Kumuweka ‘isolation’ mtu ambaye ni mzima unapoteza resources zetu

Kila mwezi tunalipa Bilioni 700 kwa madeni ambayo karibu Bilioni 200 inaenda World Bank. Sasa kwasababu wao wameguswa na ugonjwa huu hasa World Bank watusamehe madeni hata kwa percentage ili hela zitumike kupambana na Corona

Tumesikia kwenye vyombo vya habari maeneo fulani, hata hizi mask zimetolewa kwenye nchi fulani wamezikuta na corona. Vyombo vya ulinzi na usalama waanze kushughulikia vitu vya msaada visije leta madhara. Ukiletewa mask lazima ujue imetoka wapi

Nawapongeza Watanzania walioanza kushona mask zao wenyewe. Shona mask zako zitumie. Usisubiri za kuletewa ambazo hata huwezi kujua aliyekuletea ana misingi gani

Rais Magufuli: Hii fumigation iliyokuwa inafanyika Dar ni upuuzi mtupu kwasababu kwa watalaamu wote wanajua #CoronaVirus hawezi kufa kwa Chlorine. Virus yule ni futa, linapasuka ama kwa kutumia sabuni au kwa kutumia alcohol au joto kubwa, maji moto au mvuke

Hakuna fumigation yoyote inayoweza kuua #Corona na hili Watanzania lazima tuambizane ukweli. Kama pangekuwa panafanyika fumigation na #CoronaVirus wanakufa, basi nchi zilizoendelea zisingeshindwa kutengeneza fumigation na kumwagia nchi yote

Kumekuwa na papara kutoka kwa watu wetu wenyewe. Wizara ya Afya nimeambiwa siku za nyuma walitoa amri ya kufanya fumigation. Mabasi yanatoka wapi yanafanyiwa fumigation yaende wapi yanafanyiwa fumigation. Nililiona hili sana Dar na Mwanza.

Nimewaita ninyi vyombo vya Ulinzi na Usalama mfanye uchunguzi hata kwenye hizo fumigation, nani alitoa maagizo?. Lakini pia uchunguzi mfanye katika 'testing kits' na hizo barakoa zinazotoka nje. Jiridhisheni kama ni salama kwa Watanzania.


----- HABARI KUTOKA IKULU-----
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 22 Aprili, 2020 amezungumza na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwa Chato Mkoani Geita kuhusu hali ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Watanzania kwa kuitikia wito wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona, na kwa kushiriki katika siku 3 za kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa huo.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Madaktari na Wauguzi walio mstari wa mbele katika kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Corona na ametoa wito kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha inachukua tahadhari za kutosha kwa misaada ya vifaa vya uchunguzi wa Corona na vifaa vya kujikinga kuambukizwa au kuambukiza (barakoa) hasa baada ya baadhi yake kuhofiwa kusababisha maambukizi ya ugonjwa huo.

Pia ametoa wito kwa wenye viwanda hapa nchini kuzalisha barakoa kwa ajili ya Watanzania na vifaa vingine vya kukabiliana na ugonjwa huo yakiwemo mavazi ya watoa huduma na mashine za kupumulia kwa wagonjwa badala ya kutegemea vifaa hivyo kutoka nje ya nchi pekee.

Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi kujihadhari na baadhi ya njia zinazotumika kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwemo kupulizia mitaa na majengo kwa kutumia kemikali zisizokuwa na uwezo wa kuua virusi vya Corona kama ilivyofanyika kwa baadhi ya Mikoa hapa nchini, na badala yake amewataka viongozi hao kusisitiza njia za uhakika za kujikinga na ugonjwa huo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haitawafungia wananchi majumbani (lockdown) wala kulifunga Jiji la Dar es Salaam ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kuwakumba wananchi na kuathiri uchumi wa nchi, na ametaka Watanzania kuondoa hofu, kuendelea kuchukua tahadhari huku wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa.

“Tuwaondoe hofu wananchi, sio ugonjwa huu pekee unaosababisha vifo kwa wananchi, na sio kila anayepoteza maisha hivi sasa basi amekufa kwa Corona, nimejulishwa takwimu za mpaka jana idadi ya walioambukizwa ni 284 na kati yao takribani 100 wamepona, tuwaambie wananchi kuhusu taarifa hizi badala ya kuwaacha wanajawa na hofu hali inayoleta madhara zaidi” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Amewataka Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaosababisha hofu kwa wananchi na kusambaza taarifa zisizo sahihi wakiwemo Wanasiasa ambao amewaonya kuacha kutafuta umaarufu wa kisiasa kupitia janga hili, na badala yake Watanzania wote waungane kupambana nalo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi zote za Afrika kuungana kuziomba taasisi za kifedha za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia ambazo zimetangaza kusaidia Mataifa ya Afrika, kutoa msamaha wa madeni badala ya kutaka kukopesha mikopo mingine ilihali nchi hizo zinakabiliwa na madeni ya mikopo ya zamani.

Amewatakia Waislamu wote mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao unatarajiwa kuanza siku chache zijazo na ametoa wito kwao kutumia mfungo huo kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa wa Corona.

Mapema kabla ya kikao hicho, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Prof. Mabula Daudi Mchembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Prof. Mchembe amechukua nafasi ya Dkt. Zainab Abdi Seraphin Chaula ambaye amehamishwa na kuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano.

Mhe. Rais Magufuli amesema amefanya mabadiliko hayo ili kuongeza kasi ya utendaji katika Wizara ya Afya ikiwemo kukabiliana na ugonjwa wa Corona.


Ikulu 1.jpg
Ikulu 2.jpg

======

HOTUBA YA RAIS (KWA UREFU)

Nawashukuru kwa jinsi ambavyo mmenipa briefing ya hatua mbalimbali za kuhakikisha tunapambna na na huu ugonjwa wa Corona.

Nashukuru kwa hatua za kukabiliana ugonjwa huu mulizonieleza hapa, ambazo ninaamini tukizifuata tutapiga hatua kubwa.

Natoa shukrani kwa wananchi na Watanzania wote ambao kwa nyakati za maombi tulizozitangaza za siku tatu, Watanzania wote – wa makabila yote, wa dini zote na Imani mbalimbali walishiriki. Na mimi nina hakika Mungu wetu ni wa huruma na atatusikiliza na siku moja tutalishinda hili gonjwa.

Lakini pia, napenda kuwapongeza madaktari, manesi na wahudumu katika nchi hii ambao wameendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wengine lakini pia wagonjwa wa Corona. Nawapongeza na waendelee na moyo huu. Wanafanya kazi ya Mungu kuwatumikia Watanzania wenye shida. Serikali ninayoiongoza ipo pamoja nao. Ninatambua kazi zao nzuri wanazozifanya.

Lakini pia, Watanzania tuendelee kuchukuwa hatua za tahadhari. Ugonjwa huu upo lakini tahadhari ni muhimu sana. Tuchukue tahadhari katika maeneo mbalimbali. Yale maisha tunayoishi kwa mazoea tuyabadilishe.

Lakini pia nitoe wito kwa Watanzania na hasa Wizara ya Afya kwa nyakati hizi za vita dhidi ya Corona. Hii ni vita kama vita nyingine. Tusiamini kila kitu tunacholetewa. Tumesikia kwenye vyombo vya habari mbalimbali, maeneo mbalimbali; hata hizi masks zimetolewa katika nchi fulani fulani wamezikuta zina Corona.

Na kuna nchi baadhi wameanza hata ku-question hizi test kits ambazo zinatumika. Na ndiyo maana nimeona nilizungumze hili na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Wizara ya Afya waanze kuvishughulikia hata vitu tunavyopewa kama zawadi ili visije vikatuletea madhara.

Unapotuletea mask za kujikinga puani lazima tufahamu aliyeitengeneza, aliyei-supply, na misingi ya kukuletea; kwasababu tunaweza tukajikuta tunaambukizwa Corona kwa mask za kutoka nje.

Na mimi ningewashauri Watanzania na viwanda vyetu na taasisi zetu mbalimbali tuanze kutengeneza mask, sisi wenyewe hapa. Nawapongeza baadhi ya raia wengine wa Tanzania wanaojishonea wenyewe. Shona masks zako mwenyewe badala ya kutegemea unazouziwa na huwezi kujua misingi ya wale walioziuza wana lengo gani.

Lakini suala lingine, pamekuwa na papara kwa watu wetu. Wizara ya Afya, nimeambiwa siku za nyuma, walitoa amri ya kufanya fumigation. Mabasi yaende wapi, yanafanyiwa fumigation; yaende sokoni, yanafanyiwa fumigation. Na hili Dar es Salaam nililiona sana, na Mwanza nafikiri.

Hakuna fumigation yoyote inayoweza kuua Corona. Na hili Watanzania lazima tuambizane ukweli. Kama inekuwa fumigation inaweza kuua Corona, basi nchi zilizoendelea zisingeshindwa kutengeneza fumigation na kumwagia nchi zao zote hata kwa kutumia ndege, kwasababu wana uwezo. Na wasingekufa kwa njia hiyo.

Hii chlorine fumigation iliyokuwa inafanyika Dar es Salaam ni upuuzi mtupu. Wataalamu wanajua kuwa virus wa Corona huwezi kumuua kwa chlorine.

Virus
yule ni futa. Na futa lile linapasuka aidha kwa kutumia sabuni au kwa kutumia alchohol, pombe – methylated spirit. Ndiyo inaya-disintergrate yale mafuta. Au temperature kubwa – maji ya moto au mvuke. Siyo kwa chlorine fumigations. Chlorine fumigation inaua mende, viroboto vya mbwa, inaua bakteria – haiui virus.

Sasa kuna watu walitangaza sana; inawezekana kwa interest ya kutafuta pesa. Na wengine walitamka hadharani niliwaona, viongozi, wakizungumza: “Tunafanya fumigation kuua Corona”. Ni uongo mtupu. Nililitolea hili maagizo kwa Waziri Mkuu. Nina uhakika suakla la kufanya fumigation halipo tena, unless tunafanya fumigation kuua labda viroboto vya mbwa, bakteria n.k.

Lakini pia lazima tujiulize hizi fumigation ambazo zimekazaniwa sasa hivi. Je, zikiwa zina Corona imewekwa mule ndani na wakapulizia kwenye miji yetu humu ili watu wapate Corona? Maana hata baada ya Dar es Salaam kufanya fumigation, sasa ndiyo na wagonjwa wa Corona wameongezeka.

Ndiyo maana nimewaita ninyi wakuu wa vyombo vya usalama mufanye investigation hata kwenye hizo fumigation zilizokuwa zikifanywa – nani alitoa maagizo, lakini hata hizo test kits na hizo barakoa zetu zinazotoka nje. Ni lazima tujiridhishe zipo salama kwa raia wa Tanzania.

Wapo wengine wanatoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam. Hili haliwezekani. Dar es salaam ndiyo center pekee ambapo collection ya revenue inapatikana kwa wingi katika nchi yetu. Nadhani ni karibu percentage 80. Sasa unapofunga Dar es Salaam ina maana Dar es Salaam wasipelekewe mchele? Ina maana Dar es Salaam wasipelekewe viazi kutoka Mbeya? Ina maana Dar es Salaam watu wasipate ndizi kutoka Bukoba? Ina maana Dar es Salaam wasifanye biashara ya vitenge kupeleka vijijini? Ina maana madereva wa Dar es Salaam wasibebe mafuta kupeleka mikoani? Na Dar es Salaam ndipo bandari ilipo.

Kwahiyo tuendelee kuchukuwa hatua, lakini si kwa ku-lock down Dar es Salaam. Never!

Lakini pia lazima tuelewe Dar es Salaam population yake ni almost milioni sita. Unawafungia ndani watu milioni sita? Na ikitokea Mwanza pia ipo nao unawafungia? Ikitokea Mbeya unawafungia? Tutafungia mikoa mingapi?

Kwa Dar es Salaam, probability ya kuwa na wagonjwa wengi ni kutokana na idadi kubwa ya watu. Tofauti na Mwanza ambayo idadi ni milioni mbili point something, au Lindi.

Sisi sote, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wizara husika, lazima tuchukuwe tahadhari. Lakini pia, taarifa zetu ziendane na ukweli, hasa katika watu wanaopona. Nina taarifa kwamba mpaka leo taarifa ilivyokuwa inatangazwa na Waziri Mkuu, tulikuwa na wagonjwa 284 lakini naambiwa wagonjwa karibu 100 walishapona. Mwanzoni walikuwa 11 lakini wameongezeka, sijui wameongezeka wangapi – sina takwimu kamili. Hizi takwimu za wagonjwa wanaopona nazo zitangazwe ili wananchi muwaondolee hofu ya kwamba ukipata ugonjwa lazima ufe. Sisi si case hiyo hapa.

Kwa taarifa nilizonazo mimi, watu waliokufa kwa Corona ni 10. Sasa si kila anayekufa ni Corona. Hiyo ndiyo perception ambayo imejengeka, ya hovyo, kwa kutumia social media. Na nimegundua hawa wa kwenye social media wengine si Watanzania. Namba zao zipo kwenye nchi nyingine jirani, wanawachafua tu Watanzania. Kila anayekufa, corona! Kila anayekufa, Corona! Ina maana malaria imeacha kuua? Kwa hiyo hii perception iwatoke Watanzania, wasiwe na hofu ya namna hiyo. Hofu zinajengwa na maadui. Kwa makusudi yao.

Kwahiyo nimeteua Katibu Mkuu mpya. Kahakikishe taarifa za wanaopona pia zinatolewa. Sio taarifa za wagonjwa tu. Na hili litasaidia kujenga confidence kwamba waathirika wa ugonjwa huu wanapona, na hata sasa hivi wapo wanaopona.

Suala lingine ni kuhusu hostel za Magufuli ambapo ndiyo tunawaweka wale tunaowapokea, lazima liangaliwe upya. Hakuna sababu ya kumuweka mtu pale siku 14 au 20 wakati unaona kabisa hana tatizo. Wizara ya afya mulitazame hili kwani unaweza kumuacha pale kwa muda mrefu na akaenda mtaani akakutana na maambukizi.

Tu-concetrate na wagonjwa zaidi badala yak u-concetrate na kuwaweka kwenye isolation watu ambao ni wazima. Tunapoteza resources zetu.

Lakini ntoe wito pia kwa financial institutions za kimataifa. Ugonjwa huu umeikumba dunia nzima. Na umekumba pia nchi za Afrika. Uwezo wa nchi za Africa kiuchumi hauwezi kulinganishwa na nchi zilizoendelea.

Ningependa nishauri na kuwaomba vyombo vya kimataifa kama World Bank – Benki ya Dunia. Najua wametoa ofa ya nchi zinazosumbuliwa na Corona kukopa pesa. Ni ofa nzuri lakini ningeiomba taasisi hizi, hasa Benki ya Dunia, badala ya kutoa ofa ya kukopesha tena kwa ajili ya kupambana na Corona, wasamehe madeni waliyozikopesha hizi nchi. Wakisamehe madeni, makusanyo ya hizi nchi yataenda kupambana na Corona.

Sisi Tanzania kila mwezi tunalipa karibu Bilioni 700 kwa madeni yaliyokopwa na nchi kwa institutions mbalimbali za kimataifa. Na karibuni bilioni 200 au 300 zinalipwa Benki ya Dunia. Sasa ni wakati muafaka kwa Benki ya Dunia ambayo imeguswa na ugonjwa huu, na wana nia nzuri ya kutusaidia, katika ugonjwa huu, watusamehe madeni. Hata by percentage.

Hili ni ombi na mimi ningeomba nchi nyingine za Afrika tusimamie katika hili – kuwaomba wakubwa hawa watusamehe madeni haya katika kipindi hiki kigumu cha kupambana na Corona badala ya kutuongezea mzigo mwingine wa kukopa na huku wanataka interest. Basi mkopo huo uwe kwa kusamehe madeni. Hii itakuwa ni gesture nzuri za hizi financial institutions kwa nchi masikini.

Hili la vifo, kwamba kila anayekufa ni Corona, naomba Wizara ya Afya mulifafanue vizuri kwasababu kuna upotoshaji mwingi umekuwa ukifanyika kwa ajili ya kuwatisha wananchi. Na kikubwa ningewaomba Watanzania: Tuiondoe hofu! Hofu ni ugonjwa mkubwa kuliko Corona.

Hofu! Hofu! Hofu! Tuimalize hofu! Na tuendelee kuchapa kazi ili kuimarisha uchumi wetu. Si kila mtu anayekufa sasa ni Corona.

Na mimi niwaombe ndugu zangu wa mitandao, ambao wamekuwa wakitumia mitandao yao vibaya, wajizuie katika kuandika uongo wa masuala ambayo hayapo. Lakini pia niwaombe wananchi muipuuze baadhi ya mitandao inayotia chumvi na kuogopesha Watanzania.

Lakini niviombe vyombo vya ulinzi na usalama. IGP upo hapa. Shughulika nao hao. Hao ni saizi yako. Mushirikiane na TCRA na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika ku-deal na hawa watu ambao Wanaka kupotosha hali halisi.

Lakini pia, niwaombe Watanzania kutumia njia nyingine za asili katika kupambana na magonjwa haya. Na hili ningeomba Wizara ya Afya kulisisitiza. Kama vile kujifukiza. Na hili scientifically lipo very clear; kwasababu vapor (mvuke) wa maji unatoka katika temperature ambayo ni above 100 degree centigrade. Na huyo Corona kwasababu ni futa, atapasuka pasuka kwenye maji. Kwahiyo, it’s a scientific treatment.

Wizara ya afya waendelee kulifafanua ni namna gani suala la kujifukiza linasaidia kupunguza Corona. Kama wale virus wapo kwenye pua au mdomo, watayeyuka tu kwenye above 100 degree centigrade.

Hili ni muhimu. Pamoja na hizo chemical nyingine munazoweka – wengine wanaweka mwarobaini, wengine wanaweka vitunguu nk. Hayo ni mambo muhimu ambayo Watanzania wengine wanapaswa kuhamasishwa katika kupambana na hili gonjwa la Corona.

Lakini pia, niwaombe ndugu zangu wanasiasa. Ugonjwa wa Corona ni ugonjwa ambao umekumba mataifa yote. Ni wakati mzuri sasa kwa Watanzania wote kushikamana. Nawapongeza baadhi ya wanasiasa ambao kwakweli wameonesha moyo wa ushirikiano mkubwa katika kupambana na ugonjwa huu. Sisi wanasiasa wote tusimame katika hilo. Kamwe asitokee mwanasiasa akazungumza haya kwa ajili ya kujingea umaarufu kwa kuzungumza uongo. Hizo ni cheap politics ambazo haziwezi kutuletea faida yoyote katika nchi yetu wakati tupo vitani nawananchi wanapambana na ugonjwa huu kuokoa maisha yao.

Suala la elimu ni muhimu sana. Kila mmoja aendelee kutoa elimu kwa ajili ya watu hawa.

Lakini pia, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu atatusaidia sana. Mwenyezi Mungu yupo pamoja na sisi, hawezi akatuacha. Kwasababu anatupenda.

Lakini tuelewe pia, hata scientifically wanazungumza. Huu ugonjwa, baadaye tutajenga immunity. Wataalamu waendelee kutuelimisha hilo ili kuondoa zile hofu zinazoanza kujitokeza miongoni mwetu, na hasa kwasababu ya uongo mwingi unaotolewa.

Nilishasema taarifa zitakazokuwa zinatolewa na Serikali, zitakuwa zinatolewa na Waziri Mkuu, Waziri wa Afya au Msemaji wa Serikali.

Ningependa pia kuchukuwa nafasi hii kuwatakia kheri ndugu zangu Waislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na Mwenyezi Mungu akazidi kuwabariki katika kipindi hiki cha funga, ambapo huenda siku ya Ijumaa au Jumamosi mwezi unaweza ukaandama.

Ndugu zangu Waislam, katekelezeni moja ya nguzo katika Uislam – kufunga. Na mukaendelee kuliombea taifa hili liweze kuepuka janga hili la Corona. Mimi nina uhakika Mungu atatusaidia sana. Hakuna kinachoshindikana kwa Mungu. Mengine ni majaribu tu ya kupita tu lakini tutashinda!

Kwa ndugu zangu wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, kama nilivyozungumza nanyi na kama mulivyonipa briefing, nimefurahi kwa taarifa zenu na hatua munazozichukuwa. Mumenieleza munaichukulia Corona kama vita. Kapambaneni nayo. Kaokoeni roho za Watanzania.

Kasimamieni hii vita kwa nguvu zote, kwa utaalam wote, ili adui yeyote wa nje asije kutumia ugonjwa wa Corona na kupandikiza.

Na nitoe wito kwa wananchi. Usipewe kitu chochote na mtu ambaye humuamini, ambacho kinaweza kuwa ni chanzo cha kueneza Corona kwa wananchi ambao ni very innocent.

Mimi naamini vita hii tutaishinda kwasababu Mungu yupo na sisi.

Wizara ya Afya, kaendeleeni kushirikiana. Kaendeleeni kuwaelimisha watu.

Nimeamua kufanya mabadiliko kidogo Wizara ya Afya, ili kwenda na kasi ambayo inaiamini inaweza ikazaa matunda. Tusiogopane.

Nilikuwa naelezwa, katika kijiji kimoja kule Dodoma, kwenye jimbo la mtani wangu Spika Ndugai. Mgogo mmoja alitokea Dar es Salaam kwenda kwenye kijiji chake. Alipofika pale akaanza kushambuliwa na Wagogo – watani zangu. Wanasema amewaletea Corona kwa kuwa ametoka Dar es Salaam. Walikuwa wamuue, akakimbilia kwenye hospitali akajifungia humo. Baadaye aliokolewa.

Watu wanafikiri kila anayetoka Dar es Salaam ana Corona. Hii mentality ni lazima tuitoe. Hii mentality ya Watanzania kuwaogopa watu wa Dar es Salaam ni mentality mfu. Na ndio maana ninyi nyote mumetokea Dar es Salaam, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Mmekuja hadi huku Chato na wala sijawafukuza wala kuwaogopa.

Iweje Mgogo amwambie Mgogo mwenzake aliyetoka Dar es Salaam kuwa ameleta Corona?

Corona tutaishinda kwa ushirikiano. Corona tutaishinda kwa kuondoa hofu. Corona tutaishinda kwa kumtanguliza Mungu. Corona tutaishinda kama tulivyoshinda vita vingine.

Mungu vibariki vyombo vya ulinzi na usalama. Mungu wabariki Watanzania. Na Mungu ibariki Afrika kwa ushindi wa kweli dhidi ya ugonjwa huu wa Corona, na tuweze kufika salama.

Ndugu zangu ahsanteni sana. Na ninawashukuru sana wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Na hongera Katibu Mkuu. Nendeni mkachape kazi.

Kama kuna lolote sema tu. Say something, please.

CDF, Venance Mabeyo (kwa niaba ya viongozi waliopo): Haya ni maelekezo. Sisi kama vyombo tunakwenda kuyatekeleza kama ulivyoelekeza. Ahsante sana, Mheshimiwa Rais.

Rais: Ahsante sana. 

digba sowey

JF-Expert Member
Mar 1, 2017
3,612
2,000
Kuna athari kubwa sana kwa mtu akijijengea fikira ya kupinga kila kitu,hebu fikiria kidogo makao makuu ya umoja wa mataifa yako Marekani,unataka kuniambia katibu mkuu wa umoja wa mataifa akitaka kutoa hotuba hadi aende Marekani,hawezi kuwa Tanzania na bado akahutubia mataifa yote?

Chato ni Tanzania,tupunguzeni manunguniko yasiyo tija
(Ikulu Chato). Only in Tanzania.
Sent using Jamii Forums mobile app
 

JokaKuu

Platinum Member
Jul 31, 2006
18,634
2,000
Chato ni kijijini kwa Magufuli.

JK hakuwa kuzungumza toka Msoga.

Mkapa hakuzungumza toka Lupaso.

Mwinyi hakuzungumza toka Zanzibar au Mkuranga.

Mwalimu Nyerere hakuwahi kuzungumza toka Butiama.

Raisi anapaswa kuendesha shughuli zake toka IKULU, na siyo toka ktk nyumba yake binafsi. Serikali siyo KAMPUNI binafsi ya Raisi.
 
Top Bottom