Rais Magufuli aweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki ya reli ya kisasa

Tanzania Railways Corp

JF-Expert Member
Mar 23, 2018
251
595
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mahandaki manne ya reli ya kisasa – SGR Kilosa mkoani Morogoro, Juni 29, 2020.

Mahandaki 4 yenye jumla ya urefu wa Kilometa 2.7 yanajengwa katika Mradi wa SGR kipande cha Morogoro – Makutupora katika eneo la Kilosa ambapo handaki refu zaidi lenye urefu wa Kilometa 1.031 tayari limekamilika sambamba na mahandaki mengine matatu ambayo yote kwa pamoja yataunganishwa na madaraja ili kuepusha athari za mafuriko ya mto mkondoa.
“Ujenzi wa Mahandaki manne ambayo yote kwa pamoja yatakuwa na urefu wa Kilometa 2.7 pamoja na daraja la mita 500 litakalounganisha Mahandaki haya” alisema Mhe. Magufuli

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Isack Kamwelwe, Waziri wa Nishati Mhe. Medard Kalemani, Mkuu wa Jeshi la Polisi Simon Sirro, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Bilnith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanar, Wakuu wa Wilaya mkoani Morogoro, viongozi wa Dini na Chama cha Mapinduzi – CCM pamoja na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Prof. John Wajanga Kondoro na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa.

Rais Magufuli amefurahishwa na kazi zinazoendelea na amewapongeza wakandarasi na Shirika kwa kuendelea kusimamia mradi huo kwa ufanisi pia Mhe. Rais amewataka wananchi wa Kilosa kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi huo mkubwa. Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa jitihada hizi za utekelezaji wa miradi mikubwa ni za watanzania kwani wameweza kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kutumia fedha zao wenyewe
“Sikutegemea kama siku moja Tanzania tutakuwa na Mahandaki kama haya na Mahandaki yenyewe yajengwe na fedha za watanzania masikini, leo mimi mwenyewe nimekuwa shahidi wa mafanikio haya makubwa yaliyopatikana, ninamshukuru sana Mungu” alisema Rais Magufuli

“Wakati ninapanga kujenga reli, watu wengi hawakuamini, ni kipindi ambacho treni ya kwenda Moshi na Arusha ilikuwa imekufa, treni za kwenda Tabora na Kigoma zilikuwa zinasuasua lakini pia ni kipindi ambacho hapa Kilosa njia ya reli ilikuwa inajifunga kutokana na mafuriko, kwa mazingira hayo wapo walioniona ninaota mchana lakini nilimuamini Mungu na watanzania masikini” aliongeza Rais Magufuli

Katika kuhakikisha treni za umeme zinafanya kazi kiufanisi pindi mradi utakapoanza Waziri wa Nishati Mhe. Medard Kalemani amewahakikishia wananchi wa Kilosa na watanzania kwa ujumla kuwa serikali inatekeleza Miradi ya uzalishaji umeme ikiwemo Mradi mkubwa wa Bwawa la Mwl. Nyerere ili umeme uwepo kwa uhakika na kuwezesha treni kutoa huduma kwa ufanisi pindi mradi utakapokamilika.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa mradi unaendelea vizuri huku watanzania wakiendelea kunufaika na mradi huo kwa kupata kipato na kuongeza pato la taifa kupitia kodi wanazolipa wakandarasi
“Mpaka sasa hivi Wakandarasi kwa maana kuna wengine wanaleta nyama, sukari, maziwa mpaka sasa hivi pesa ambayo imerudi nchini ukiacha kodi ni Dola Milioni 576 hiyo ni pesa ambayo imeenda kwa watanzania wenzetu” alisema Kadogosa

Katika taarifa yake Ndugu Kadogosa meongeza kuwa “Reli yetu ya zamani imepita kandokando ya mto umbali wa Kilometa 120, hivyo kila mwaka tunatumia fedha nyingi za watanzania kurudishia reli iliyochukuliwa na maji, kwahiyo (ujenzi wa Mahandaki) huu ni muarobaini kwamba hatutakuwa na tatizo na reli yetu ya kisasa katika mto Mkondoa”

Katika kuelekea kipindi cha uchaguzi Mheshimiwa Rais Magufuli amewaomba watanzania kuendelea kutunza amani iliyopo ili kuwezesha shughuli za kimaendeleo kufanyika na kusaidia kukuza pato la taifa kwani endapo hakutakuwa na amani nchi haitaweza kutekelea miradi ya kimaendeleo kama huu wa ujenzi wa reli ya kisasa.
13%20(1).jpeg
3%20(2).jpeg
14.jpeg
6%20(2).jpeg
2%20(3).jpeg
 
Back
Top Bottom