Rais Magufuli amekosea kuteua wapinzani bila kufanya "A" au "B"

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
Na. M. M. Mwanakijiji

Baba wa Taifa aliwahi kuja na msemo wa “Tanzania ni ya Watanzania, na Watanzania ni wote”. Msemo huu miaka ya mwisho ya sitini ulikuwa unamanisha hasa kuwa kila Mtanzania bila kujali nafasi, kabila, rangi, mahali anakotoka n.k ana haki na wajibu sawa wa kushiriki katika ujenzi wa taifa lake. Dhana hii ya Mwalimu hatimaye imekuwa ni sehemu ya Katiba yetu ya Muungano ambapo inasema wazi kuwa kila Mtanzania ana haki na wajibu wa kushiriki hadi ukomo wa mipaka yake katika ujenzi wa taifa lake.

Ni kwa misingi hiyo basi Rais Magufuli kama mtendaji mkuu wa serikali yetu ana haki na uwezo wa kumuita Mtanzania yeyote kushiriki katika ujenzi wa taifa lake bila kujali mtu huyo anatoka wapi, kabila gani, rangi gani au ni wa chama gani. Hata hivyo, haki na uwezo huu haumpi Rais mamlaka kama ya mfalme ambapo neno na agizo lake peke yake linatosha kufanya lolote, popote, kwa yeyote na wakati wowote. Mamlaka ya aina hii ambayo ni kamili (absolute power) yako katika mikono ya wafalme ambao wana madaraka yote (absolute monarchs).

Uamuzi wa Rais Magufuli kumteua Prof. Kitila Mkumbo na kumpa nafasi katika Serikali yake kama vile ulivyo uamuzi wa kumteua Bi. Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro unaonekana kwa namna fulani kuwa ni kama wa mfalme ambaye ameamua tu kwa vile yeye ni mfalme basi anamteua huyu au yule katika baraza lake la kifalme (at the king’s court).

Bahati mbaya (kwa Magufuli) ni kuwa yeye ni Rais katika nchi ya kijamhuri ambayo imeweka taratibu mbalimbali za kiutawala kwa mujibu wa Katiba. Mojawapo ya taratibu hizo ni kuwa viongozi wetu wa kisiasa watatokana na vyama vya siasa. Yeye mwenyewe Magufuli aliingia madarakani akiwa ni mgombea aliyesimamishwa na chama chake (CCM) na hivyo basi anatii takwa hilo la Kikatiba. Leo hii akiamua kuachana na CCM, akasema kwa mfano anajitoa kwenye chama chama cha Mapinduzi basi atapoteza nafasi yake ya Urais – ama sivyo atasababisha mgogoro wa Kikatiba kama ule uliotokea Malawi lakini kwa nchi yetu utakuwa ni Rais sana kutatuliwa.

Nimesema hapo juu kuwa Rais ana haki na uwezo wa kumteua Mtanzania yeyote yule na kumuita kwenye utumishi wa umma. Nimesema pia mfumo wetu unatambua uwepo wa vyama vya kisiasa na viongozi wetu wa kisiasa wanatokana na vyama hivyo. Ni kwa misingi hiyo, sioni ni kwa namna gani Rais anaweza kuteua mtu wa chama kingine cha kisiasa ambacho kwanza, hakikuwa sehemu ya umoja wa kisiasa na chama tawala (chama cha Rais) au hakikuwa kimemuunga mkono na hivyo kikitarajia kushirikishwa katika serikali.

Namna pekee ya kuhalalisha maamuzi hayo ya Rais ni kusema “Rais kasema” au kusema kuwa “huwezi kumkatalia” na kwa namna nyingine ni kuitikia wito wa kulitumikia taifa. Kitila na Mghwira wote ni viongozi ndani ya vyama vyao hivyo kuwateua kiholela ni kutumia madaraka ya uteuzi vibaya na kutokujali matokeo ya tendo hilo (ignoring the implication of such an act).

Ni kwa sababu hiyo nipendekeze kwamba Rais hapaswi na siyo hekima kufanya uteuzi wa watu kutoka vyama vya upinzani bila kwanza kufanya mambo yafuatayo:

A: Kufanya mazungumzo na chama husika kwanza - Mfano wa Anna Mgwira ni mfano mzuri sana. Yeye ni Mwenyekiti wa chama cha ACT na hivyo ni kiongozi wa chama chake kama alivyo Magufuli kwa CCM. Sasa kama Rais alikuwa anaona anamhitaji sana mama huyo kwa ajili ya nafasi yoyote serikalini utaratibu mzuri ulipaswa kuwa ni kuanzisha mazungumzo ya kisiasa (political consultation) kati ya chama cha Rais (CCM) na chama cha ACT-Wazalendo ili kuona ni jinsi gani chama hicho kitamuachilia mwenyekiti wake na maana ya uamuzi huo kwa kazi za mama Mghwira.

Mama huyo leo hii akitaka kufanya kazi za ACT-Wazalendo ataweza kuzifanya akiwa katika nafasi yake ya Mkuu wa Mkoa? Kikiitwa kikao cha chama chake wakati wa kazi wa kawaida ambapo anatarajiwa kuwa ofisini kwake aende? Au kwa vile yeye ni Mwenyekiti anaweza kuitisha kikao cha chama chake Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pale Kilimanjaro kama vile Magufuli anavyoita vikao vya chama chake Ikulu Dar-es-Salaam?

Sasa maswali haya yote siyo swali la mtu mmoja tu; ni suala la mahusiano vyama na vyama. Uzuri wake ni kuwa kama mazungumzo yanafanyika na kunakuwepo na utaratibu unaokubaliwa basi baadhi ya matatizo ambayo ni Rais kuyaona mbeleni yanaweza kuepukika bila kuja kuona kuwa mama Anna ametengenezewa nafasi ya kutenguliwa nafasi yake kwa kosa la kuchanganya siasa na kazi za serikali.

Nje ya hapo, ni muhimu Ikulu imlinde mapema kwa kumueleza kabisa kama inamtaka mama huyo aachie ngazi zote za kisiasa kwenye ACT-Wazalendo au vipi. Haya yote yanapaswa kutatuliwa kabla ya kuteuliwa.

Hili pia upande mwingine linatuonesha tatizo la mfumo wa uongozi wa ACT-Wazalendo. Zitto Kabwe Mbunge wa Kigoma Mjini ndiye anajulikana zaidi kati ya wanachama wa ACT na ndiye kiongozi mkuu wa chama hicho. Hapa panaonesha tatizo la nafasi ya Mwenyekiti na Kiongozi wa Chama nani anatakiwa kuwasiliana na mwenzie.

Mama Anna kama aliulizwa kabla ya jina kutangazwa alipaswa mara moja kuwasiliana na wenzake kabla ya kuitikia wito huo; na kama jina lake alilisikia hewani tu bila kuulizwa – kwani Magufuli ameshawahi kukiri kutumia mbinu hii ya kuwateua watu bila kuwauliza – alipaswa ama kuomba radhi kuchelewa kuitikia wito hadi awasiliane na viongozi wenzake wa chama au kukataa kwa vile chama chake hakikushirikishwa.

Kimsingi, uamuzi wa kumteua mama Mghwira na labda hata Kitila unaelekea kukiletea matatizo chama hicho bila sababu ya msingi kwani kunaweza kutafsiriwa kama njia rahisi ya kukiletea migogoro ya ndani hasa kama chama kitapinga Mwenyekiti wake kuwa Mkuu wa Mkoa na kumtaka ajiuzulu.

B: Kufanya mashauriano na chama chake kuhusu kushirikiana na vyama vingine – Kwa vile Katiba yetu haina mfumo wa kulazimisha vyama kushirikiana katika serikali kama ilivyo kwenye baadhi ya nchi, basi uamuzi huu wa kuhusisha vyama vya upinzani ni uamuzi ambao ni wa mtu mmoja tu. Ni sawasawa na uamuzi wa Kikwete kumteua Mbatia kuwa Mbunge wa kuteuliwa.

Ni vizuri kabisa kama Rais Magufuli anaona kuwa ni wakati muafaka kuwashirikisha wapinzani katika serikali yake – kitu ambacho sidhani kuna Mtanzania anaweza kukipinga – basi la kwanza ni fanya hili liwe sera ya chama tawala kwanza kabla ya teuzi hizi kutangazwa. Sera hiyo yapaswa kuanishwa inawafunga vipi wale wapinzani wanaoteuliwa kushika nafasi mbalimbali na maamuzi hayo yanaishia kwa Rais tu au hata kwa viongozi wengine wenye kuteua wanaruhusiwa au la. Bila kuifanya hili kuwa sera ya kiutawala ya CCM wakati huu basi inaonekana kwa namna fulani ni kujaribu kurusha vipepeo kwenye vichwa vya wapinzani.

Magufuli kama Mwenyekiti wa chama chake alipaswa kuzungumza na chama chake kwanza na kusikiliza maoni ya wenzake kabla wenzake hawajaanza kutetea maamuzi ambayo hawayajui mantiki, mwelekeo au ukomo wake. Hivi leo, Waziri fulani akiamua kumteua Mwenyekiti wa Mkoa wa CHADEMA kuwa mwenyekiti wa bodi ya shirika fulani atakuwa sawa au anaweza kuonekana anafanya kitu kinyume na ‘sera’ fulani ya CCM, sera ambayo haipo? Na akisema anafuata mfano wa Rais si anaweza kurukwa na Rais kwa kufanya kitu ambacho labda ni Rais peke yake alipaswa kukifanya kwa sababu anazozijua yeye?

Hili linanikumbusha lile lililotokea wakati wa mjadala wa Katiba Mpya ambapo Rais Kikwete alijiamulia mwenyewe kuja na mchakato wa kuandika Katiba mpya kitu ambacho hakuwa na uwezo nacho na wala chama chake hakikuwa kimekubali. Tukumbuke kuwa CCM haikuwa na ajenda ya Katiba mpya na wala wakati wa kampeni ya 2010 hakikuahidi jambo lolote la kuhusiana na Katiba mpya hadi usiku ule wa salamu za mwaka mpya ambapo Rais Kikwete aliamua kutangaza “kuanzisha” mchakato wa kuandika Katiba Mpya. Wengi tulipinga wakati ule kwa sababu hizi hizi; haiwezeni Rais akaamua kufanya jambo kubwa kama lile bila kuhusiana na chama chake au kuanzisha mijadala ya ndani ili kufikia makubaliano ya kisiasa (political consensus) ndani ya chama kabla ya kufanya jambo hilo kuwa ni la sera ya kitaifa.

Hivyo basi, changamoto kubwa iliyopo sasa ni jinsi gani ACT-Wazalendo waitikie jambo hili. Tayari Mwenyekiti wao kakubali kuteuliwa, kaapishwa na kapewa na Ilani ya CCM na tumeona amepanda gari lake kwenda kuanza kazi Kilimanjaro. Wao wafanye nini? Binafsi naamini kuwa jambo la busara ni wao wenyewe kuanzisha (initiate) mazungumzo na Rais kama Mwenyekiti wa CCM ili waweze kuelewa yale ambayo yamekubaliwa baina ya Anna Mgwhira na Rais Magufuli na nina uhakika hekima itaamua njia ya “A” ni bora zaidi hata kama imechelewa.

Nje ya hapo, ili kutokujidhoofisha kama chama, ACT-Wazalendo inaweza ikaamua kusitisha (siyo kumvua) uanachama Bi. Mghwira kwa muda wote ambao atakuwa Mkuu wa Mkoa. Hii ni kwa ajili ya kuondoa mgongano wowote ambao unaweza kutokea hasa kwa vile chama bado kinajijenga kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2020. Na kinaweza kuweka taratibu mapema kuwa uamuzi huo ndio utakaofuatwa kwa kiongozi yeyote wa juu wa chama (wa kitaifa au wa mkoa/kanda) ambaye atateuliwa kushika nafasi yoyote na kiongozi yeyote kutoka chama tawala bila kuwa na makubaliano baina vya vyama hivyo kwa mtindo wa “A” nilioanisha hapo juu.

Kwa upande wa CCM nina uhakika chama hicho kitakapokaa katika vikao vyake vya sekretariati n.k basi vinahitaji kuhakikisha vinazungumza na Rais ili kujua mtazamo wake na lengo lake katika mahusiano haya na wao kama chama wana sehemu gani.

Nje ya hapo, uamuzi wa aina hii pia unadhoofisha CCM yenyewe kwa upande mmoja. Nina uhakika kuna watu ndani ya CCM ambao wanaweza kuanza kujiuliza kama kweli ndani ya chama hicho hakuna watu tena ambao wanaweza kuitwa kulitumikia taifa katika nafasi ambazo wamepewa wapinzani. Wanaweza kuhoji kuwa inawezekana Rais Magufuli sasa hana Imani tena na watu ndani ya chama chake? Swali linaweza kuwa kubwa zaidi kama itatokea Magufuli ataamua kujaza nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini (au kama ni wizara mbili mpya – mawaziri) wakatoka nje ya CCM. Suala hili la kiutawala linahusiana na CCM yenyewe kwani ndio chama tawala.

Endapo taratibu nzuri zikafuata na maridhiano ya kisiasa kwa vyama kushirikiana yakafanyika na matokeo ya mashirikiano hayo kueleweka sawia kwa kila mmoja basi Rais Magufuli anaweza kutumia madaraka na mamlaka yake ya kuteua watu mbalimbali katika utumishi wa umma na watu hao wakaitikia na kufanya kazi kwa weledi wote bila kusababisha manung’uniko na minong’ono mingine hasi ya kisiasa ambayo itahoji hekima, nia, lengo na makusudi ya teuzi za namna hiyo.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
Kutoka: zamampya.com
 
MMM umeanza kuguswa panapouma! Taratibu utaanza kubadili kauli na msimamo wako na mwishowe utarudi kwenye msimamo wa jamaa zako wa siku zote hapa JF ambao muda mwingine wameduwaa ulivyobadilika ghafla.

Pamoja na yote mawazo yako ni mazuri hasa kupunguza maumivu na hatari kwa ACT
 
Hekima na busara ni kipaji. Sio kila mtu amejaliwa. Lakini, kwa wale wa Kristo, Maandiko yanashauriwa mtu akipungukiwa hekima aombe.
Tuendelee kumuombea
 
Wameshamtangaza makamu mwenyekiti amekaimu nafasi ya mama. Umeandika vyema....
 
Bottom line ni katiba. Maadam tuna hii katiba ya sasa ambayo kimsingi imemweka rais juu ya mihimili yote ya dola na hata juu ya katiba yenyewe, basi rais yupo sahihi kumteua huyu mama.
 
Good analysis, though, apparently, I'm worried so much about the political relevance of ACT-Wazalendo on the Tanzania's political landscape. The appointment of Prof. Kitila Mkumbo and Ms. Anna Mghwira into various government positions is too controversial to say the least!
 
Nadhani mh.Rais anafanya "Divide and rule" Japo itamletea shida ndani ya chama chake kwa namna moja ama nyingine.
 
Mimi sioni shida as long as hawatamfukuza kama MBWA baadaye
That one can not be guaranteed. Uso wa mwanadamu umeumbwa na haya...siku Mama Yetu atakapolazimika kukataza au kufitini mikutano ya kidemokrasia mkoani Kilimanjaro atatumbuliwa. Hatokuwa tena RC na hatokuwa tena CP wa ACT.
 
Ukiamua seriously kukiita ACT Wazalendo ni opposition party basi lazima kichwani kwako kutakuwa hakupo sawa..

Ni chama kilichoanzishwa kupunguza nguvu kwa wapinzani wa kweli ambao ni Chadema.
Hata Zitto akipewa uwaziri so long as yupo ndani ya hiko chama ni sawa tu.
 
Back
Top Bottom