Rais Magufuli alivyotimiza ahadi alizotoa bungeni

elivina shambuni

JF-Expert Member
May 31, 2018
461
295
Kampeni za urais mwaka 2015, na wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 2015. Rais alihutubia Bunge kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 91 ibara ndogo ya kwanza, inayomtaka Rais aliyechaguliwa kufungua rasmi Bunge hilo.

Akihutubia bunge hilo, Rais Magufuli aliwaambia wabunge kuwa wananchi waliwachagua wakiwa na matarajio makubwa; na watawapima kwa namna watakavyokidhi kiu na matarajio yao. “Wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi cha Awamu ya Tano ambapo matarajio yao ni makubwa sana, sote tuliahidi kuwatumikia na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji.

“Mimi na Mheshimiwa Samia (Suluhu Hassan), Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na kuhakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida,” alisema Rais Magufuli. Akutana na watendaji Ni dhahiri uchapakazi wa Rais Magufuli, umeonesha mabadiliko makubwa ya kiutendaji, tumeshuhudia Rais akifanya mikutano mbalimbali na viongozi kuanzia ngazi ya mawaziri hadi watendaji wa kata Tanzania Bara na kuzungumza nao masuala mbalimbali ya kiuongozi, ikiwemo wajibu wao kwa wananchi.

Mkutano kati ya Rais na watendaji wa kata ni mwendelezo wa mikutano yake na watendaji wa serikali, wakiwemo wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa wilaya, makatibu tawala ya wilaya na makatibu watendaji wa tarafa.

Akizungumza na makatibu watendaji wa tarafa, Rais Magufuli alisema “Ninyi ni wawakilishi wangu ngazi ya kata, tunapozungumza mafanikio ya Serikali, ninyi ndio wasimamizi wa mwanzo wa mafanikio hayo.” Hatua ya Rais kuwaita watendaji hao wa tarafa kutoka Tanzania Bara na kuzungumza nao, ni kitendo kinachoonesha jinsi anavyowajali viongozi wote kuanzia ngazi ya chini hadi juu. Usimamizi rasilimali za umma Katika Bunge hilo, Rais pia aliahidi kusimamia matumizi ya mali za umma na rasilimali za Taifa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali zetu zinatumika kwa matumizi kwa manufaa ya umma na si kwa manufaa ya mtu binafsi.

Aidha, kuhakikisha kuwa ugawaji wa rasilimali hizo, unafanyika kwa haki. Katika siku za mwanzo za utawala wake, Rais Magufuli alianza kwa kufanya ufuatiliaji wa rasilimali zetu, ambapo aliunda kamati maalumu ya kuchunguza mchanga na madini yalikuwa yanasafirishwa nje ya nchi.


Kamati hiyo ilinainisha upotevu mkubwa wa mapato na rasilimali za nchi, ambapo nchi ilikuwa inapoteza Sh bilioni 829.4 hadi Sh trilioni 1.439 kwa kusafirisha mchanga (makinikia) nje ya nchi. Ili kuhakikisha anazuia upotevu huo, kamati ilitoa mapendekezo kadhaa ambayo Rais aliyakubali. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni usitishwaji wa usafirishaji wa mchanga huo hadi mrabaha stahiki utakapolipwa, na kujengwa kwa vinu vya kuchakata madini yote ili yaweze kufahamika na kutozwa kodi.

Aidha, Rais aliwaagiza wakuu wa mikoa inayozalisha madini, kuanzisha masoko ya madini ili kudhibiti utoroshaji na uuzaji holela wa madini. Hadi sasa baadhi ya masoko yamekwishaanzishwa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Dar es Salaam, Mtwara, Manyara, Morogoro, Kagera na Arusha.

Kwa upande wa wilaya, masoko hayo yamefunguliwa Simanjiro na Chunya. Ufunguzi wa masoko hayo umeleta neema, si kwa serikali tu, bali hata kwa wauzaji wa madini hayo, ambao walikuwa wakiyauza kwa kudhulumiwa na wanunuzi wakubwa. Kwa Serikali na nchi kwa ujumla, masoko haya yameongeza Pato la Taifa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la upatikanaji wa madini. Ukusanyaji wa mapato Eneo lingine ambalo Rais Magufuli aliahidi kulishughulikia ni kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Katika kutimiza ahadi yake, kwa upande wa kusimamia mapato tumeshuhudia Rais akifanya mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Rais pia alizindua Kituo Kikuu cha Taifa cha Kuhifadhi Mifumo ya Ukusanyaji wa Mapato kwa njia ya Elektroniki, ambapo makusanyo ya mwezi Septemba 2019 yalikuwa Sh trilioni 1.7 sawa na asilimia 97.20, kiasi ambacho hakijawahi kukusanywa na mamlaka hiyo tangu kuanzishwa kwake Julai 1, 1996.

Ni dhamira ya TRA kukusanya mapato kwa utaratibu rahisi na wa wazi ;na walipakodi watapata urahisi wa kupata huduma zinazotolewa kwa wakati. Kituo hicho ni ushirikiano wa pamoja baina ya TRA na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), ambacho kimeundwa ili kusaidia kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato ya serikali zote mbili. Akizindua kituo hicho, Rais Magufuli alizitaka taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali, kampuni na benki kujisajili katika kituo hicho ili kuweza kukusanya kodi kwa ufanisi.

Mapambano rushwa, ufisadi Katika kuhakikisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inakuwa kinara wa utawala bora, Rais Magufuli aliahidi kupambana na rushwa na ufisadi. Awali akihutubia Bunge la kwanza, Rais aliwaambia wabunge kuwa mojawapo ya maeneo yaliyolalamikiwa na wananchi wakati wa kipindi cha kampeni ni rushwa, ambapo sehemu nyingi wananchi walisema kuwa rushwa ni mojawapo ya kero kubwa wanazokumbana nazo.

Baadhi ya mafanikio ya mapambano ya vita dhidi ya rushwa ni kuanzishwa kwa ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hadi ngazi za wilaya. Pia serikali hii inajipambanua kwa uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa umma, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa utoaji wa elimu kwa umma kuhusu rushwa na madhara yake.

Katika mkutano wa 32 wa Wakuu wa Nchi za Afrika (AU), uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwaka 2017, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika ufuatiliaji na utekelezaji wa mapambano dhidi ya rushwa.

Taasisi ya Transparency International imesifu juhudi za Rais Magufuli na kuitaja Tanzania kuwa ni nchi ya pili kwa kupunguza rushwa na kufanikiwa kuifanyia kazi mianya mingi ya rushwa. Hivi karibuni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athuman alisema kuwa utafiti uliofanywa na taasisi za kimataifa za Transparency International na Afro Barometer, unaoitwa Global Corruption Barometer Africa 2019, unaonesha kuwa Tanzania ni ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika katika kipengele cha juhudi za serikali katika kupambana na rushwa kwa mwaka 2019.

Kero ya migogoro ya ardhi Kuhusu kero ya migogoro ya ardhi, Serikali ya Awamu ya Tano imefuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 ambayo yamepoteza sifa na kuyagawa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji, na misitu 7 yenye ukubwa wa ekari 46,715 kurudi kwa wananchi.

Hatua hii ilifuatiwa na kubaini uwepo wa vijiji 975 vyenye migogoro, ambapo iliamuliwa kuwa vijiji 920 vibaki ndani ya hifadhi na mipaka irejerewe upya na kupatiwa vibali vya ardhi vya kijiji. Pia serikali iliridhia kumega misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na mifugo.

Sera ya elimu bure Ahadi nyingine ambayo Rais Magufuli ameitimiza ni katika Sekta ya Elimu, ambapo katika elimu aliahidi kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Kutokana na utekelezaji wa ahadi hiyo, kumekuwa na mwamko mkubwa wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule, ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza. Idadi ya wanafunzi hao imefikia 1,670,919 mwaka 2019 kutoka 896,584 mwaka 2016.

Kwa upande wa shule za sekondari, idadi ya wanafunzi walioandikishwa kwa mwaka 2019 ni 710,436 kutoka wanafunzi 238,365 walioandikishwa mwaka 2016 wakati sera ya elimu bure ilipoanza kutekelezwa nchini. Katika sekta ya elimu, pia tumeshuhudia maboresho mbalimbali ambapo vifaa vya kufundishia na kujifunzia vimeongezwa, michango isiyo ya lazima imeondolewa, madawati yameongezwa na nyumba nyingi za walimu zimejengwa.

Uboreshaji huduma za afya Katika eneo la afya, dhamira ya Rais Magufuli ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umaskini, amelipa msukumo wenye tija ili kuwa na wananchi wenye afya bora. Tumeshuhudia uboreshaji wa sekta hii ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya, kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Lengo likiwa ni kuwaondolea usumbufu wananchi na kutolazimika kupeleka watu kutibiwa nje ya nchi.
 
Hongera Magufuli kwa kujali Watanzania Endelea kuchapa kazi

Tunaanza kuonja matunda yako ya uongozi

Sasa nasafiri kuanzia mjini hadi kijijini kwetu ni lami tupu,na umeme kila kona
 
Back
Top Bottom