Rais Magufuli ajitafakari upya, yeye ni zao la demokrasia

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Tamko la rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kueleza kuwa shughuli za kisiasa ziendelee wakati wa uchaguzi mkuu ujao na siyo sasa, limenishtua sana. Darubini yetu inajikita katika kuangalia kauli hiyo ya rais na kumshauri.
Takribani mwezi mmoja uliopita shughuli za kisiasa zimekuwa zinapigwa vita sana na jeshi la Polisi. Bila shaka watu wenye weledi tayari walianza kuhoji kulikoni Jeshi la Polisi limekuwa “serious” sana kutoa mazuio ya shughuli za kisiasa?

Hata shughuli za kisiasa zinazofanyika ndani ya kumbi (indoor) nazo zikaanza kuzuiliwa! Hii ikashangaza wengi. Chama cha ACT kilipokutana ndani ya hoteli moja jijini Dar Es Salaam ili kujadili bajeti pamoja na wanachama na wapenzi wake au wananchi, hoteli ile ikazungukwa tangu asubuhi hadi jioni.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF – Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa katika ziara visiwani Zanzibar – msafara wake ukapigwa marufuku kutembea na watu wanaomuunga mkono.

Umoja wa Vijana wa CHADEMA wasomao vyuo Vikuu (CHASO) ulipokuwa unafanya mahafali zake ndani ya kumbi za hoteli, ukazuiliwa huko Kilimanjaro, Dodoma n.k. Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA alipokuwa anatembelea wananchi kwenye vijiwe vya kahawa jijini Mwanza, akafuatwa na polisi na kuzuiwa.

Matukio yote hayo na mengine mengi viliwafanya wachunguzi na wadadisi wa mambo waanze kutafakari ikiwa hatua zote hizo zinafanyika bila kuwepo na maelekezo kutoka juu. Wakati tafakuri inaendelea ndipo Rais amejitokeza mwenyewe hadharani na kutamka kuwa hataki kukwamishwa na ni lazima “wanasiasa waache kuzunguka zunguka huku na kule kupinga juhudi zake” (maneno yangu).

Yaani Rais anaupasha umma kuwa wapo watu wamekuwa wakizunguka huku na kule kumpinga na kwa tafsiri ya maneno hayo, watu hao ni vyama vya siasa vya upinzani.

Ukilitafakari zaidi tamko la rais unagundua kuwa mkuu wa nchi anataka shughuli za kisiasa zifanywe pale tu ambapo mhusika (kiongozi au mwanasiasa anatokea), na si hivyo tu – hata kama anatokea mahali hapo lazima awe ni kiongozi wa kuchaguliwa na wananchi wa eneo hilo na kwa hiyo mipaka ya shughuli zake iwe kwenye maeneo hayo.

Tamko hili la rais lina maana pana zaidi, kwamba ikiwa mbunge wa chama “A” anataka kufanya shughuli za kisiasa katika jimbo la mbunge wa chama “B”, atazuiliwa – hata kama shughuli anazokwenda kuzifanya ni kueneza sera na itikadi ya chama chake kwa mujibu wa sheria.

Zuio hili la rais lina maana nyingine pia, kwamba ikiwa kiongozi wa kitaifa wa chama “A” anataka kufanya shughuli za kisiasa katika jimbo ambalo linaongozwa na chama “B”, hataruhusiwa, na ikiwa kiongozi wa kitaifa wa chama “A” atataka kufanya shughuli za siasa katika jimbo ambalo linaongozwa na chama “A” atazuiliwa pia huwenda hadi pale itokeapo kuwa kiongozi husika wa kitaifa naye anatokea kwenye jimbo hilohilo na kwa hiyo hatakuwa na uwezo wa kufanya shughuli za kisiasa kwenye jimbo hilo hadi pale mbunge wake (wa chama chake) na ambaye ni mbunge wa jimbo hilo, atoe taarifa polisi na ndipo amkaribishe kiongozi wake wa kitaifa kufanya shuguli za kisiasa.

Kwa maana hiyo, kuanzia sasa tusitegemee ati chama “A” makao makuu kinaweza kuandika barua kwenda polisi kutoa taarifa ya kufanya shughuli za kisiasa kwenye mikoa “A”, “B”, “C” n.k. Kwa mtindo huo atakayenufaika na zuio la rais ni chama ambacho kina wabunge na madiwani wengi, lakini pia ni chama ambacho kina rais na mawaziri – bahati ya rais itakuwa kwamba, mawaziri wake watakwenda mahali kokote kule kwa niaba ya serikali na chama chake na kufanya shughuli zozote za kisiasa kwa kadri wapendavyo kwa kisingizio cha kwamba wao hawana mipaka na kwamba kila eneo la nchi linahitaji miongozo na huduma za wizara zao.

Zuio la rais lina maana nyingine pana zaidi, kwamba vyama vya siasa havitaruhusiwa kukutana katika mikutano na vikao vya ndani hadi tu pale ambapo polisi wataona umuhimu na kufurahia kusanyiko hilo. Na kwa namna JPM anavyotamka jambo hili, unaona namna alivyo tayari kwa lolote, anasema bila kupepesa macho kuwa aachiwe nchi yake atekeleze ahadi zake na chama chake na ukimuangalia machoni unaona akikuonya kwamba hana mchezo na tena anakuhakikishiakuwa yeye na vyombo vya dola watachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekwamisha juhudi zake, ikiwemo hizi za kuzuia shughuli za kisiasa.

Huko nyuma nimewahi kuandika sana, kuwa ikiwa JPM anao washauri basi wafukuzwe kazi, hakuna wanachomsaidia. Na ama kama wapo, basi kila wakikutana naye wanamsifia, wanapiga makofi – wanachukua posho na mishahara na “kusepa”, hakika wanampeleka rais wetu mpendwa shimoni maana nchi hii kamwe haiwezi kugeuka kuwa jiwe, yaani haiwezi kurudi kule ilikotoka.

Watanzania walio wengi watakubaliana nami kuwa hata juhudi ambazo serikali yake inazichukua leo, msingi wake umetokana na msuguano na mbinyo kutoka kwa vyama vya upinzani dhidi ya CCM.

Kama vyama vya upinzani visingelikuwepo huwenda hata JPM asingelikuwepo madarakani, kuja kwake madarakani kulitokana na hali mbaya ya CCM kisiasa na chama hicho kikaangukia kwake kubahatisha ikiwa kitaweza kubakia salama. Wananchi wameichoka CCM kwa sababu chama hicho kilishindwaa kutimiza wajibu wake, si kwa sababu ya uwepo wa vyama vya upinzani – bali ni kwa sababu ya mivutano ya ndani ya CCM na maslahi binafsi ndani ya chama hicho.

Kama rais wetu ana nia njema na taifa hili akapambane na wanaomkwamisha huko huko ndani ya CCM, maana watu wa namna hiyo hawako upande wa upinzani. Tangu nchi hii ianze, sikuwahi kuona upinzani ukiikwamisha serikali, siyo bungeni na siyo serikalini kwenyewe, wala siyo mahakamani.

Iweje basi mkuu wa nchi ainue rungu la mamlaka yasiyo ya kikatiba wala kisheria na kuliangusha juu ya demokrasia na vyama vya upinzani? Rais atapata nini baada ya hatua hiyo? Rais anategemea kuwa vyama vya upinzani vitakubaliana na hatua yake isiyoungwa mkono kikatiba, kisheria wala kimantiki? Wakati ni kila kitu!

Imechapwa/Darubini ya Mtatiro, Gazeti la Mwananchi 26 Juni 2016
 
  • Thanks
Reactions: BAK
Well said,asiwaige Kagame na Museven kwani wao sio zao la demokrasia!Hakuna kiongozi ambaye ni zao la demokrasia,akaikandamiza na kufanikiwa!
 
13528718_738782559596571_6772389937267433792_n-jpg.361245


#FreeKamandaLissu
 
Ninakupongeza kwa kuweza ku-admit kuwa Magufuli ni zao la demokrasia, maana sidhani Kama Ukawa wenzako wanakubaliana na hilo. Otherwise nakubaliana na wewe kuhusu kupinga kidhibitiwa kwa harakati za wanasiasa wa upinzani (wale walio na dhamira ya dhati, si matepeli kama Lowasa and company waliokuja upinzani kwa personal motives tu).
 
Mkuu Mwanahabari Huru, huyu jamaa hawezi kufuata ushauri wako kwa sababu ni "sikio la kufa"....ila sasa akili itamkaa kwani chama chake kishaanza kukataliwa huko kwao Geita kupitia uchaguzi wa vijiji.
 
Back
Top Bottom