Rais Kikwete: Viongozi wa dini acheni biashara dawa za kulevya

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
Rais Dr.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Mhashamu John Ndimbo, askofu mpya wa Jimbo katoliki Mbinga wakati wa ibada ya kumsimika askofu huyo iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Kilian mjini Mbinga leo.
Rais Jakaya Kikwete amepasua jipu mbele ya viongozi wa dini kwamba kuna baadhi yao wanashiriki biashara haramu ya dawa za kulevya.
Akihutubia waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga jana katika ibada maalum ya kusimikwa Mhashamu Askofu John Ndimbo wa jimbo hilo, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Killian, Rais Kikwete aliwataka viongozi hao kuacha biashara hiyo na badala yake washirikiane na viongozi wa serikali katika kuidhibiti.
Katika ibada hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Kikwete, alisema baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakishiriki kufanya biashara hiyo kwa kuwafanyia mipango vijana ya kuwatafutia hati za kusafiria kwenda nchi za nje kwa shughuli hiyo.
Rais Kikwete aliwataka viongozi hao kukemea biashara hiyo na kujenga uhusiano mzuri na vyombo vya dola ili kuikomesha kwa kuwafichua wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.
” Inasikitisha sana na kutisha; biashara hii haramu sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu, Taifa letu litaharibika tusipokuwa makini katika hili, baadhi yenu tumewakamata,” alisema Kikwete na kuongeza kuwa:
” Kauli zenu kemeeni jambo hili kwa kuelimisha jamii hususani vijana waweze kuepukana na matumizi ya dawa za kulevya.”
Aliyaomba madhehebu ya dini katika mipango yao ya maendeleo yaweke kipaumbele kujenga vyuo vya ufundi stadi ili kuisaidia jamii katika ushindani wa soko la ajira.
Alifafanua kuwa kutokana na wananchi wengi kukabiliwa na tatizo la ajira, ni vyema sasa serikali kwa kushirikiana na madhehebu ya dini kujikita zaidi katika kujenga vyuo hivyo ambavyo vitasaidia kupunguza kero hiyo.
” Kufanikiwa kwa viongozi wa dini katika shughuli za kimaendeleo ni faraja kwa serikali iliyopo madarakani na Watanzania wote kwa ujumla, ” alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki Tanzania, Askofu Yuda Thadei Rwaichi, aliiomba serikali kuwa makini wakati wa kuandaa bajeti ya nchi.
Askofu Rwaichi, alisema bajeti hiyo ni vyema izingatie maendeleo ya Watanzania ambao wengi ni maskini.
Pia aliitaka serikali kudumisha amani na utulivu, kwa kuhakikisha vitendo vya vurugu havipewi nafasi na kwamba kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na serikali na Watanzania wote bila ubaguzi wa rangi, dini au kabila.
Pamoja na mambo mengine, Askofu mpya wa Jimbo la Mbinga, Ndimbo, baada ya kusimikwa alitoa shukurani zake kwa Rais Kikwete na waumini wa jimbo hilo kuwa katika uongozi wake atakuwa bega kwa bega kuhakikisha anashirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo, Askofu Ndimbo, alisema kazi yake kubwa ni ya kuwachunga kondoo wa Mungu (Waumini) na kuwahamasisha waumini wa jimbo hilo kujikita katika kilimo cha kisasa ambacho kitawasaidia kupunguza ukali wa maisha.
CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom