Rais hapatikani kwa tukio la uchaguzi, anaandaliwa tangu shuleni

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,214
3,587
Matukio mengi makubwa yaliyowahitukia, ama katika maisha ya mtu wa kawaida au katika maisha ya ziada ya mtu mwenye historia, yametukia katika muda usio muafaka wa maisha yake.

Kwa mfano, kanuni ya jumla ya sheria ya mvutano (Universal Law of Gravitation) ilizaliwa kwenye akili ya Isaac Newton katika muda ambao tufaa (apple) lilidondokea kichwani mwake alipokuwa amejipumzisha chini ya mti wa mtufaa. Inawezekana, kama tufaa hilo lisingedondokea kichwani mwa Newton siku ile, tusinge, hadi sasa, fahamu kuhusu sheria hii muhimu ya asili ambayo baada ya pale imebadilisha kabisa mfumo wa Fizikia.

Sambamba, kama Archimedes hasingeoga kwenye beseni kubwa la kuogea bafuni (tub) siku hiyo ya tukio, ambapo aligundua duniani kanuni yake maarufu isemayo “The upward buoyant force that is exerted on a body immersed in a fluid, whether fully or partially submerged, is equal to the weight of the fluid that the body displaces.” Ambayo hii ndiyo ilitumika kugundua meli, tusingejuwa kuhusu kanuni hii adhimu ya asili ambayo ni sheria ya msingi ya Fizikia kwa wahandisi wa vimiminika tangia hapo.

Maandalizi ya rais tangu akiwa mdogo, yanaanza pasipo yeye kujuwa kama anaandaliwa na anapokengeuka katikati ya safari ya kuandaliwa basi anaondolewa kwenye orodha na safari ya maandalizi inaendelea na waliobaki kwenye orodha au wapya wanaoingizwa kwenye orodha. Huo ndiyo mfumo unaoendesha dunia na kanuni ya urithi (succession formula).

Fihavango G.M, (2017) katika kitabu chake “Tumpate wapi mtu kama huyu? Uongozi, Uadilifu, Uwajibikaji. Dai la uadilifu na uongozi wa karne ya 21” anasema ifuatavyo: “Mtu anayefaa kuwa kiongozi ni yule aliye tayari kuishi bila kuwa kiongozi na aliye tayari kuachia uongozi.”

Ujio wa rais Magufuli ulichanganya nchi kwanza na baadaye dunia kwamba je, ni huyu kweli alikuwa ameandaliwa au MUNGU aliamua kupindua meza tu?
Utendaji wake uliegemea uchumi zaidi ya siasa (demokrasia), akijitahidi kutengeneza utajiri wa kitaasisi badala ya mtu (individual) ili kuuishi msingi wa Azimio la Arusha wa kuweka milki ya mali kwenye mikono ya umma badala ya mtu mmoja. Hii ni tofauti na nchi za Ulaya ambako kanuni na sera nyingi za uchumi za nchi maskini zinaanzia huko ndipo huletwa kwa nchi maskini baada ya kuthibitika kwa waliozitengeneza (wazungu) kwamba ni vitanzi tosha vya chumi za nchi maskini. Sera hizi zinafanikiwa kwao lakini kwenye nchi maskini hazizai matunda tarajali.

Nchini Uingereza kwa mfano, inakisiwa kuwa watu takriban 5 katika idadi yote ya watu wake wanamiliki uchumi wa asilimia 20 ya watu wote wa nchi hiyo (lakini wanafuata sheria zote za nchi ikiwamo kulipa kodi za serikali, na nchi masikini zinapoomba misaada, basi misaada hiyo hutoka kwenye mifuko ya matajiri hawa na kupita mikononi mwa serikali zao ndipo inaziendea nchi masikini zilizoomba misaada hiyo). Marekani yenyewe katika nchi zote za dunia inamiliki pato la wastani wa asilimia 14 ya mapato yote ya dunia nzima ikiwa na takriban zaidi ya dola za Marekani trilioni 30 kwa mwaka kama pato ghafi lake lote la ndani (GDP); huku katika nchi zingine ili mtu aweze kupata mkate wa siku analazimika kuuza mwili wake au kumiliki bunduki au afanye ufisadi ndiyo mkono uweze kwenda kinywani.

Mgawanyo huu usio sawia wa rasilimali za dunia na keki ya taifa hauwezi kufanya dunia ikawa salama hata siku moja na ukizingatia kuwa ulimbikizaji huo wa rasilimali na mapato baina ya wanadamu na mataifa umewezeshwa na urari mbovu wa biashara kati ya mataifa ya dunia; ambao umelalamikiwa kwa miongo mingi pasina kupatikana dhamira ya kuondokana nayo. Kukosekana upendo, kutokujaliana na kutokuchukuliana mizigo baina ya mataifa ya dunia kumefanya sehemu za dunia ambazo hazikubarikiwa na rasilimali za kutosha kufanyika maficho ya wahalifu wa kimataifa wakiwemo maghaidi ambao huendesha shughuli zao haramu za kiuhalifu katika mataifa yenye rasilimali za kutosha na ziada na kurudi kufichama kwenye mataifa yao yasiyo na rasilimali za kutosha.

Zipo nchi duniani ambazo zimejitawala kabisa lakini bajeti zao hadi leo zinategemea mapato yatokanayo na uhalifu (ughaidi na mihadarati). Mhe. rais JPM alipopambana na uoza wa jamii na kudhamiria kuleta neema ichukuwe nafasi ya mateso, ilitupasa kumuunga mkono kwa asilimia 100. Uswisi ile, inaishi kwa biashara ya chokoleti, haina utajiri wa rasilimali, ardhi (ni milima mitupu) wala idadi kubwa ya watu wanaotakiwa kujituma kufanya kazi kama Tanzania. Ethiopia ile, inajiendesha kwa biashara ya safari za anga ikimiliki ndege kubwa zipatazo 47 na leo Ethiopia ndiyo hub ya dunia kutokea na kuingia Afrika, lakini pia inamiliki meli kubwa kubwa pasina kuwa na bandari/bahari. Watanzania tumekosea wapi? Kwanini hatukutumia fursa ile ya Mhe. rais JPM kujisahihisha? Wuololoo Nyasaye wuorwa!

Laiti Mhe. rais JPM angekuwa ni Mobutu Tseseseko, Bouekassa, Iddi Amin, Omar Al Bashir, Omar Bongo, Denis Sassou Nguesso, Pierre Nkurunziza wapinzani wake wangemfananisha na malaika? Wapinzani wake walitaka Tanzania ifanane na Comoro inayoongoza kwa idadi kubwa ya mapinduzi ya serikali ya kumwaga damu na yasiyo ya kumwaga damu yapatayo 20 tangu uhuru wake mwaka 1975? Rais wa zamani wa Nigeria jenerali Olusegun Aremu Okikiola Mathew Obasanjo aliwahi kukaririwa katika moja ya hotuba zake akitoa takwimu kuwa ndani ya miaka 50 bara la Afrika limeshuhudia mapinduzi ya kijeshi 186 na migogoro mikubwa 26 yenye kutumia rasilimali nyingi na muda mwingi wa utatuzi wake, idadi hiyo imeishapanda na kuzidi.

Aidha inakadiriwa kuwa migogoro ya kisiasa ya bara la Afrika, inachukuwa asilimia 60 ya kazi zote za baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Wazungu ni wepesi kujifunza na kubadilika kuliko Waafrika, huenda huko tuendako kama Waafrika tusipobadilika basi labda baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litabadilika na kuwa ICC ya UN likishughulika kwa asilimia 100 (siyo 60 tena) na bara la Afrika tu kwa sababu Wazungu wanatambua umuhimu wa amani na utangamano kuliko sisi Waafrika. Mfumo wa demokrasia tunayotumia Afrika nayo pia kama bidhaa iliingizwa Afrika kutoka kwa Wazungu (haijatengenezwa Afrika).

Wenzetu Wazungu wameendelea kuitekeleza kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa sana, yaani demokrasia haipewi nafasi kuzuia fursa ya kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa. Viongozi wa kiroho kesheni mkiomba msije mkaingia majaribuni (mtegoni mwa wanasiasa wa wastani wanaohamasisha umma kukaidi hata taarifa za kitaalam za kijasusi ambazo zinatahadharisha kuhusu viashiria vya amani na usalama kuvunjika kwenye harakati za kisiasa) maana mna kiapo cha kuombea taifa na serikali halali iliyopo madarakani kwa mujibu wa katiba, hata kwenye liturgia zenu mmetuandikia sala ya kuombea nchi na serikali.

Duniani viongozi walio wengi wanachagua kufanana kwa utendaji wa wastani au chini ya wastani, msingi wa chaguo hili ukiwa ni ama uoga wa kulaumiwa kwa hatua zao wanazochukuwa katika utendaji wao au kuelemewa na nguvu za tabia zao za asili za kuendekeza tamaa ya ulimbikizaji mali kwa ziada na kujikuta wakitanguliza maslahi-binafsi yao dhidi ya yale ya umma wakingali katika dhamana za madaraka yao rasmi. Ni wachache sana wanaochagua kuongozwa na nguvu za ujasiri, uthubutu, ubunifu, ibada na uzalendo wa kutanguliza maslahi ya umma na kujikuta wakijipambanua kwa utendaji makini wenye matokeo chanya dhidi ya wenzao hao huku wakijipatia kibali ndani ya nyoyo za watu duniani kama siyo nchini kwao tu.

Kuwaiga hawa kwa tamaa ya kutaka sifa wanazojipatia kuna gharama zake ambazo kwanza lazima kuzikokotoa na kufanya tathmini makini, aidha wapo waliotamani mbinu hii na kufanya uamuzi wa kurejea madarakani au kujiongezea muda wa uongozi na kujikuta wakijiingiza katika migogoro ya gharama kubwa kisiasa kwa sababu tayari maisha yao ya awali walipoanza uongozi hayakuwa na ushuhuda mzuri hivyo wanastuka kujikuta tayari waliishahukumiwa na historia zao wenyewe (judged by their own history). Mhe. Rais Dkt. Magufuli utendaji wake makini na wa matokeo chanya yenye mguso umemtengenezea mtaji mkubwa wa watu duniani (social capital). MUNGU atusamehe kwa kusema tulipotakiwa kunyamaza na kunyamaza tulipotakiwa kusema.

majwalaoriko@yahoo.co.uk

 

Similar Discussions

Back
Top Bottom