Rais Hakainde Hichilema amuapisha askari aliyemtendea wema akiwa gerezani kuwa naibu kamishna wa Magereza

Njia ya Mungu ni fumbo

RAIS HAKAINDE HICHILEMA AMUAPISHA ASKARI ALIYEMTENDEA WEMA AKIWA GEREZANI KUWA NAIBU KAMISHNA WA MAGEREZA. KUNA SOMO LA KUJIFUNZA

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ameteua Bwana Kuyomba Bwalya kuwa Naibu Kamishna Jenerali wa magereza "Zambia Correction Service".

Hichilema aliwekwa 2kizuizini katika mahabusu gerezani chini ya Askari kijana mdogo anayeitwa Bwalya mwaka 2017, ambapo alibambikiwa mashtaka ya uhaini " treason" akituhumiwa kutaka kumuua Rais wa Zambia wakati huo Edgar Lungu.

Kiongozi huyo wa Upinzani wakati huo, alibambikiwa mashtaka ya uhaini kwa kile Jamhuri ilichodai kuwa alikataa kuupisha msafara wa Rais Edgar Lungu ambapo upelelezi ulidai kuwa ulibaini kuwa lengo la Hakainde ilikuwa kumuua Rais Edgar Lungu kwa ajali ya gari.

Hakainde aliachiwa HURU baada ya kusota gerezani kwa takribani miezi minne baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kumfutia mashtaka hayo kutokana na Jamhuri kukosa ushahidi wa kudhibitisha uhaini aliokuwa anatuhumiwa nao.

Wakati Rais Hakainde akimuapisha Bwalya na maafisa wengine juzi Jumatano, Rais alimsifu Bwalya kwa kufanya kazi kwa weledi uliotukuka na kuzingatia Sheria na Katiba licha ya mazingira magumu ya utawala kandamizi na unyanyasaji wa utawala dhalili, dhalimu na katili wa Rais Edgar Lungu.

Rais Hakainde amemuamuru Kamishna Jenerali Fredrick Chilukutu na Naibu Kamishna Jenerali Bwalya wa huduma za kitaifa za kubadili tabia kuyafanyia mageuzi makubwa magereza yote nchini Zambia.

"Kipekee nizungumze na nyinyi ndugu zangu wawili wa huduma za kurekebisha tabia katika magereza yetu" alisema 2Rais Hakainde

“Mimi ni mhitimu wa taasisi hiyo (magereza) na ninajua kabisa kinachoendelea katika taasisi hiyo. Wanapaswa kuwa vituo vya marekebisho ya tabia, kwa sasa sio bali magereza yamegeuka kuwa vituo vya mateso, unyanyasaji, udhalilishaji na mauaji. Mazingira ya magereza ni magumu na mabaya sana kwa sisi mahabusu, kama mahabusu wa zamani natuma ujumbe kwenu kwamba uteuzi wenu haukuwa wa bahati mbaya, niliteua kwa makini sana kwa kuzingatia ndoto na sera yetu ya kuliunganisha na kuliponya Taifa hili na hili nitalisisitiza katika kila sherehe za uapisho kwa wateule wapya ili tuweze kutoka katika siku za kutengwa hadi siku za kujumuishwa lakini zaidi kwako hakikisha unayafanyia mageuzi makubwa sana magereza yetu ili yawe vituo vya kurekebisha tabia na sio vituo vya mateso." Rais Hakainde

"Nawaamuru mkaondoe msongamano katika mahabusu na magereza. Kama mhitimu katika mahabusu na magereza yetu ninafahamu kwamba kila sero " cell" ilijengwa kwa ajili ya kuweka mahabusu 20 pekee lakini kwenye sero ambayo Mimi niliwekwa mahabusu tuliishi watu 170 kwa wakati mmoja, kama una UTU na ubinadamu unaweza kuelewa aina ya mateso Mimi na mahabusu wengine wanayopitia katika Taifa hili. Haiwezekani Wazambia tusishi katika Taifa HURU kwa mateso makali kuliko hata kipindi cha ukoloni kabla ya UHURU sasa huu UHURU utakuwa na faida gani? Hebu fikiri hapa katika hii sero usiku ukiingia kila mtu anataka alale, unalala wapi na vipi, hakuna sehemu ya kulala, hakuna usingizi katika sero zetu, mahabusu wanateseka sana" amehoji Rais Hakainde

"Sikujua kuwa siku moja ningetupwa gerezani na ninyi nyote hapa hakuna anayejua hatima yake, huenda hata wewe kamishna general na Naibu kamishna general kesho mkawa mahabusu je mtajisikiaje kuishi katika sero na magereza zenye mateso makali namna ile?" Anaendelea kuhoji Rais Hakainde

"Bwalya ni kijana mdogo, tulikutana katika hayo mazingira magumu niliyowaeleza. Alikuwa boss wangu. Licha ya Mazingira hayo magumu ya utawala kandamizi wa Rais Edgar Lungu lakini bado alihakikisha anafanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Katiba na kiapo." Ameongeza Rais Hakainde

"Bwalya anafahamu kile ninachokiongelea, na Mimi ninakifahamu kile ninachokisema. Ndiposa nikatazama na kujiuliza huyu kijana mdogo kabisa anawezaje kutenda HAKI na kufikiri sawa sawa katika mazingira ya utawala wa dhuluma na kandamizi namna ile? Bwalya alikuwa boss wangu nilipokuwa nimetupwa mahabusu gerezani. Nilifahamika zaidi kwa sababu wakati mwingine sikukubali baadhi ya amri ambazo niliona zinaenda kinyume na HAKI zangu za binadamu. Lakini huyu kijana alinielewa alijua ipi ni sahihi na ipi sio sahihi. Alikuwa boss wangu na leo anaapishwa na mmoja wa mahabusu wake. Maisha yanabadilika, maisha yanazunguka. Meza imepinduka. Alimalizia Rais Hakainde.

Kuna somo muhimu sana hapa. Jifunze kutenda wema siku zote uwe huna madaraka au una madaraka wewe mtendee wema kila mtu, huwezi jua kesho inaleta nini kupitia wema au ubaya wako.

Usimuonee mtu maana yawezekana hata wafungwa na mahabusu unaowaonea leo huko magerezani kesho mmoja wapo akawa boss wako.

Watu unaowaonea na kuwatesa leo ukiwaona wao sio lolote na sio chochote huenda kesho wakawa ni msaada mkubwa na wewe ukawa miongoni mwa wanaohitaji msaada wao.

Usimdharau mtu yeyote kwa sababu tu ya hali yake ya leo ukilinganisha na hali yako. Heshimu kila mtu maana hujui kesho unayemdharau atakuwa wapi na wewe unayejiona umefika utakuwa wapi.

Tumia madaraka, cheo chako, fedha zako na Elimu yako kuunganisha watu, kusaidia watu, ufanyike furaha na tabasamu katika nyuso za waliopoteza furaha maana kesho ipo na hujui inakuja na maajabu gani.

Ubaya HAUFI na wema HAUFI na kumbuka wema na ubaya vyote ni mbegu ambayo humea kwa wakati muafaka.

Zaidi sana usisahau kuwa kuna kitu kinaitwa Karma! Huyu jamaa huwa hamsahau mtu hata kama itachukua muda gani. What goes around comes around. Ukitenda ubaya UTALIPWA MABAYA na ukitenda wema UTALIPWA MEMA kwa saa, njia na wakati usioutarajia.

Usipande miba katika njia yangu maana huenda kesho ukalazimika kuipita njia yangu ukiwa huna viatu.

Rais Hakainde Hichilema aliapishwa kuwa Rais wa Zambia baada ya kumshinda Rais Edgar Lungu kwa ushindi wa kishindo. Hakainde alichaguliwa kuwa Rais baada ya kugombea mara 5 bila mafanikio. Hapa pia liko somo la kutokukata tamaa, ukishindwa jaribu tena na tena na tena hadi utakapofanikiwa.

Wema unalipa, tenda wema nenda zako
Matatizo ya Nchi za kiafrika ni Yale yale
 
Back
Top Bottom