Raia mwema anapoamua kutafuta haki na Paradiso iliyopotea

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,009
NASAHA ZA MIHANGWA

Nakala chapishi
Mtumie mwenzio

Raia mwema anapoamua kutafuta haki na Paradiso iliyopotea

Joseph Mihangwa Oktoba 31, 2007
Raia Mwema

NI Rais wa Marekani, hayati Abraham Lincoln aliyesema; “unaweza kuwadanganya baadhi ya watu wakati wote. Unaweza kuwadanganya watu wote wakati mwingine. Huwezi kuwadanganya watu wote wakati wote”.

Naye mwanamapinduzi wa Kisoshalisti, V.I. Lenin anakita kwa kusema; “ukweli ni thabiti”.

Oktoba 14, mwaka huu, Watanzania waliadhimisha miaka minane ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa staili mbalimbali yakiwemo makongamano, mijadala ya vikundi pamoja na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru.

Katika matukio yote hayo, mada kuu ya mrejeo iliyotawala ilikuwa ni juu ya demokrasia na utawala kwa misingi ya mtazamo wa Baba wa Taifa na utekelezaji wake, chini ya awamu nne za Serikali kuanzia mwaka 1985 hadi sasa.

Karibu wasomi wote na vigogo kadhaa wa chama tawala (CCM) na Serikali waliyatumia maadhimisho hayo kuinyooshea kidole Serikali kwa maovu yaliyokithiri nchini yakiwemo rushwa, ubadhirifu, ufisadi, ukoloni mamboleo na uwekezaji usiojali maslahi ya taifa.

Kuna tuhuma kede kede za mambo haya dhidi ya Serikali ya awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi iliyofuta Azimio la Arusha na kuweka Azimio la Zanzibar mwaka 1992, na sera za “Ruksa” kwa kila kitu zilizoendelezwa na awamu zilizofuatia.

Wapo pia wanaoona kuwa udhaifu ulianza na Serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin William Mkapa, aliyeuza maadili ya taifa kwa sera za utandawazi, ubinafsishaji na uwekezaji usiojali. Alikuwa kipenzi cha wawekezaji kutoka nje.

Lakini wapo pia wanaoanza kukata tamaa na Serikali ya awamu ya nne ambayo wengi waliamini kwamba ingerejesha nidhamu na uadilifu katika uongozi kama ilivyokuwa enzi za usawa chini ya Serikali ya awamu ya kwanza iliyowakilisha ahadi (commitment), dhamira, ushupavu, matumaini na matarajio, sio tu kwa Watanzania, Afrika na Waafrika, bali pia kwa wanyonge wote wa dunia hii wanaoonewa na kunyanyaswa. Tanzania ilikuwa Paradiso, kitovu cha fikra na harakati za ukombozi barani Afrika na Dunia ya Tatu kwa ujumla.

Kuzuka kwa wimbi la kuinyooshea kidole Serikali juu ya rushwa, na ufisadi, lililoibuka na kuzidi kukomaa hivi karibuni ni kilelezo tosha kwamba Paradiso imepotea. Mtindo wa raia wema kuzomea viongozi wa Serikali wanapowatembelea, uliozuka hivi karibuni, ni dalili za wao kuanza kukosa imani kwa viongozi wao, na kwamba njia za kuitafuta haki kwao zimegonga mwamba, kwa maana hawasikilizwi na hawana wa kuwasemea.

Hii inathibitishwa na ukweli kwamba licha ya raia wema hao kuweka wazi maovu ya viongozi wao ili waweze kuwajibika, Serikali imetetea maovu hata yaliyo wazi. Inaendelea kuwabeba hata wasiobebeka.

Hatuna sababu ya kuyataja yote hapa, lakini itoshe kusema tu kwamba rushwa, dhuluma, ufisadi na uwekezaji usiojali maslahi ya taifa umo mbioni kuliangamiza taifa hili.

Yaliyosemwa na wengi wakati wa maadhimisho ya siku ya Baba wa Taifa, yanaonyesha kuwa hali si shwari ndani ya Serikali ya awamu ya nne ambayo pia inaonekana kubeba mzigo wa dhambi za awamu mbili ziliyoitangulia. Hata Kada Mkuu wa CCM, mhimili na mshauri mkuu wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye hapo nyuma amejaribu, bila mafanikio, kutetea vitendo vya ufisadi ndani ya Chama na Serikali ili kuficha aibu, safari hii mzimu wa Mwalimu Nyerere ulimshukia, akaamua kutoboa ukweli.

Kingunge, katika hatua inayoonekana kukumbuka wosia wa Mwalimu kwamba, “afichaye ugonjwa kilio kitamuumbua”, huenda yeye pamoja na viongozi wengine wameanza kugundua ukweli kuwa “hawawezi kuwadanganya watu wote wakati wote”, kwa sababu “ukweli”, kwa mujibu wa V.I. Lenin, ni thabiti.

Kwa mara ya kwanza kabisa Kingunge amenukuliwa akikikosoa Chama na Serikali, akisema “CCM imejisahau, wana CCM wamepotoka; sasa wanashangilia rushwa na dhuluma”. Siku za nyuma asingeweza kutamka hayo na akadumu.

Akiwaumbua viongozi wenzake Kingunge alisema; “Tuna viongozi wanaopenda dhuluma. Hivi sasa viongozi wengi wanaweka mbele maslahi binafsi na kusahau ya taifa.” Imekuaje mzee Kingunge aanze kujichoma kisu tumboni? Ni kujiepusha na ghadhabu ya umma inayonyemelea? Huenda amesoma maandiko ukutani?

Mzee Mwinyi, Rais wa awamu ya pili, ambaye Serikali yake inatuhumiwa kuwa chanzo cha kukomaa kwa rushwa, kifo cha Azimio la Arusha na ubinafsishaji usiojali, kwa upande wake amejitetea akisema; “Kukosolewa ni moja ya changamoto zinazoikabili Serikali. Inapaswa izikubali hoja za msingi. Tuhuma zisipuuzwe, wanaozitoa wana akili kwa kufanya hivyo na hivyo Serikali ichukue tahadhari.”

Mwinyi akijisafisha aliendelea kusema; “Sijawahi kula rushwa; haikuwepo wakati wa utumishi wetu tangu miaka ya 1960… kulikuwa na usawa na woga wa kutenda kinyume na taratibu za kazi na haki.”

Katika hatua ya kuonyesha kukerwa na hali ya sasa, Mwinyi aliendelea kusema; “Watu wengine leo wamekuwa na tamaa, wanakiuka maadili ya kazi na hata utu...”

Kuhusu Azimio la Arusha, anasema; “Mimi sikuua Azimio la Arusha kwa kuanzisha Azimio la Zanzibar. Kilichofanyika ni kulegeza masharti yake tu kwa kuwa utekelezaji wake ulikuwa mgumu.”

Ni wakati wa utawala wa Mwinyi na wa Mkapa (awamu ya tatu) ubinafsishaji ulipotekelezwa kwa nguvu zote bila kujali “mihimili mikuu ya uchumi wa nchi” iliyotetewa na Azimio la Arusha, kiasi kwamba leo raia mwema ni omba omba kwa “wawekezaji” ndani ya nchi yake. Hana kauli kiuchumi na kisiasa.

Kuna wakati Mwalimu akiwa hai alionya juu ya uwezekano wa kubinafsisha hata magereza na wafungwa kama viongozi watabeza uzalendo.

Pengine ni kwa sababu hii mwandishi mahiri hapa nchini, Jenerali Ulimwengu alikuwa na kila sababu ya kudai kuwa; “Tanzania na Afrika nzima inazidi kuwa koloni la weupe kuliko ilivyokuwa wakati wa ukoloni. Siku hizi viongozi hakuna, hawa ni watawala”.

Jenerali Ulimwengu amebainisha kwa uhakika kuwa; “Uongozi siku hizi umegeuka kuwa bidhaa inayonunuliwa. Wananchi tupo sokoni tunauzwa. Mtu anakupigia hesabu ya kuchukua Ikulu au jimbo (la ubunge) ili kutawala kwa dola bilioni kadhaa... Fedha inanunua nchi”.

Si hayo tu, hivi leo fedha inanunua madaraka na madaraka yananunua fedha. Matajiri wa leo ndio hao hao viongozi wa nchi na wapambe wao. Na hii inaleta kile ambacho Profesa Issa Shivji amekiita “mpasuko mkubwa katika jamii ambao umewagawa wananchi katika makundi ya walalahoi na walalaheri”. Walalaheri wamenyakua Paradiso ya walalahoi.

Nini matokeo ya rushwa na ujenzi wa matabaka nchini?

Jenerali Ulimwengu anajibu: “Migogoro mingi Afrika husababishwa na rushwa iliyokithiri katika serikali na katika jamii kwa ujumla, na ndiyo maana wananchi hujiingiza katika mapigano ili kutetea haki yao na kuondokana na umasikini”.

Jenerali Ulimwengu alibainisha, kwa kushangiliwa, aliposema; “wachochezi wa vita ya baadaye ni (hawa) mafisadi wa leo….ukoloni unarudi haraka kuliko ilivyokuwa kabla ya uhuru… misaada ya wahisani itaifikisha nchi mahali pa kushindwa kuwa na sera zake na kuzitekeleza”.

Wakati wasomi na vigogo wakiiweka wazi mianya ya rushwa na ufisadi unakoipeleka nchi, Rais Kikwete, kwa upande wake, alikuwa akitoa wito kwa Watanzania, wakati wa sherehe za kuzima Mwenge huko Arusha, wasiwasikilize wanasiasa wanaohubiri vurugu katika kuleta mabadiliko nchini, na wakati huo huo akakiri kuwa “rushwa inaweza kukwamisha maendeleo ya kiuchumi na Serikali yake”.

Siku chache kabla ya sherehe za kuzima Mwenge, Rais Kikwete aliwakemea raia wema na wanasiasa wanaodiriki kuwasuta wala rushwa na mafisadi akisema; “huwezi kuwa wewe ni mpelelezi, mwendesha mashitaka na hakimu”, katika utawala wa sheria.

Utawala wa sheria unasema kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria. Je, ni vigogo wangapi wamefikishwa mbele ya sheria ukilinganisha na maelfu ya watu wadogo wenye rushwa ndogo ndogo? Wadogo hukamatwa kwa tuhuma za rushwa, lakini wakubwa hawakamatwi; bali huundiwa tume zinazotumia mamilioni ya fedha za wavuja jasho.

Ni viongozi wetu hao hao ambao wakati mmoja wanapofurahi hutupa ujasiri kuwasuta mafisadi; lakini ni hao hao wakati mwingine wanaokemea raia wema wanapofanya hivyo.

Ni Rais Mkapa, ambaye katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Januari 31, 2005, aliyetutia mori dhidi ya rushwa aliposema; “mtu anayekosa uaminifu sehemu ya kazi ni kusutwa, si wa kufichwa; ni wa kufichuliwa. Na uhalali wa raia wema kufanya hivyo ni kuwa, tabia za watu hao hazikubaliki; maana huo sio Utanzania.”

Lakini ni mheshimiwa Mkapa huyo huyo ambaye baadaye aliwaita watu wenye kuhoji katika kutafuta ukweli kuwa ni “wavivu wa kufikiri, wenye wivu usio wa kimaendeleo”. Ni Serikali ya mheshimiwa Mkapa iliyowaambia wananchi “wale majani” lakini utapanyaji wa rasilimali za taifa utaendelea.

Ni Rais Kikwete aliyetuagiza kuwaumbua wabadhirifu miongoni mwetu katika hotuba yake ya kwanza Bungeni aliposema; “…kadhalika hatuna budi kuchukua hatua thabiti za kuzuia watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha na kujilimbikizia mali.

Jambo hili linakera sana watu kuona mtu ambaye hana chochote, lakini miezi michache tu baada ya kuwa mbunge au waziri, katibu mkuu wa wizara, ana majumba ya kifahari, madaladala, teksi bubu, anaishi maisha ya kifahari na kadhalika”.

Kwa nia njema kabisa, Rais Kikwete alisema; “Raia wema wanayo haki ya kuhoji, na wanayo haki ya kupata majibu… Serikali ya awamu ya nne haina budi ichukie tabia hiyo na kila mmoja wetu awe askari wa kupambana na hiyo rushwa”.

Sasa, inakuaje leo raia wema wanaohoji vitendo vya rushwa na ufisadi waitwe “wapelelezi, waendesha mashitaka na mahakimu” wanaokwenda kinyume na misingi ya utawala wa sheria? Kitu gani kimebadili mtizamo huo wa Rais kwa kuuonea haya ufisadi?

Kuwaziba midomo raia wema kunaweza kusababisha wachoshwe na maovu yanayotendwa na viongozi wao, wakajenga chuki kwa Serikali wakasema “lolote na liwe”.

Ni mambo haya haya yaliyozaa mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 dhidi ya Serikali ya Mfalme Louis XVI. Jenerali Ulimwengu hakukosea aliposema, “wachochezi wa vita ya baadaye ni (hawa) mafisadi wa leo”. Wachochezi wa vita si hawa raia wema wanaotafuta haki yao na Paradiso yao waliyopokonywa na mafisadi.

Ni vyema mamlaka ya nchi ikawaacha watu waseme, wajadili na kutoa maoni yao kwa uhuru ili kufafanua ni nani yupo kwa ajili ya kutumikia watu, na nani yupo kwa ajili ya kutumikiwa na kuwanyonya wengine.

Vyombo vya serikali vitapwaya iwapo viongozi wakuu wa serikali na vyombo vyake watajiona wana kinga au nguvu turufu ya kutoguswa katika nchi inayopaswa kuheshimu utawala wa sheria.

Kama wananchi watanyimwa kutumia haki yao ya kuhoji juu ya matendo na tabia ya viongozi wao, basi tusitegemee kupata uongozi bora na makini katika nchi. Badala yake tutaendelea kuongozwa na watu wanafiki, waongo, mafisadi waliojijengea ngome bandia kwa jina la “Chama” na utawala wa sheria.

Viongozi ni watu wa kuingia na kutoka; hawawezi kuwa hati miliki ya uzalendo. Mfalme Louis XVI wa Ufaransa alizoea kujitapa akisema; “mimi ndimi taifa na taifa ndilo mimi”, lakini alipokufa taifa halikufa naye. Watu na taifa walibaki, na wapo mpaka leo.

Yaliyodhihirisha wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka minane ya kifo cha Baba wa Taifa ni sehemu tu ya hisia pana za Watanzania enzi hizi za demokrasia na utawala wa sheria.

Yanathibitisha, vilevile, usemi wa Rais Lincoln kwamba uongo una mwisho, na huenda kwamba uozo wa rushwa na ufisadi hausikii ubani; maana nyingine sikio la kufa halina dawa.

Tukimwacha V.I Lenin, anayetuasa kwamba “ukweli ni thabiti”, tuna Shabaan Robert wa mazingira ya enzi zetu akituasa akisema:

Kweli itashinda, namna tunavyoishi, Kweli haihofu tisho, wala nguvu ya majeshi, La uongo lina mwisho, kweli kitu cha aushi, Kweli itashinda kesho, kama leo haitoshi.
 
Back
Top Bottom