RAI: Hamkani! Haya ndiyo madhara ya kumdharau Nyerere

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Na Emmanuel J. Shilatu



BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuja na falsafa yake kuhusu dhana ya maendeleo. Kwa kutumia hekima, busara na kwa kinywa chake mwenyewe, Mwalimu Nyerere alisema "ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora"

Naam, huu ni unabii wa aina yake ambapo kauli hii ni zaidi ya falsafa inayowezwa kufanywa kama imani ya kutuponya na kutuokoa kutoka katika hili dimbwi la umaskini. Jambo la kushangaza ni kuwa Watanzania tunazidi kuwa maskini licha ya kujaaliwa mambo yote ya msingi na muhimu. Inakuwaje maendeleo hakuna kwa maana ya watu ni maskini, wakati vitu hivyo vyote tunavyo?

Kama ni suala la ardhi, tunalo eneo kubwa tu lenye ukubwa wa zaidi ya kilometa za mraba 940,000. Ardhi yetu imejawa na rutuba ya kutosha, ardhi yetu imesheheni madini na vitu vya thamani, ardhi yetu hii hii imesheheni vyanzo vya maji (mito, maziwa, bahari n.k) na pia ardhi yetu hii imebarikiwa kuwa na mbuga za wanyama na mioto ya asili (misitu) ya kutosha tu. Hivyo ardhi si tatizo kabisa.

Pia katika suala la watu nalo pia hatujambo. Ni takribani miaka 50 sasa tangu tupate uhuru wetu lakini leo hii tupo karibu Watanzania milioni 45. Kati ya Watanzania hao, tuna wasomi wa kutosha, tuna wataalamu na mabingwa wa kila idara ama nyanja, tuna vijana (nguvu kazi ya taifa) ya kutosha. Hivyo uwepo wa watu kama nguvu kazi ya taifa ama wajasiriamali pia si tatizo.

Suala la siasa safi napo hali si mbaya. Uhalisia wa uwepo wa siasa safi upo ila, isipokuwa kuna baadhi ya viongozi ‘sisimizi' ambao wanajaribu kulivuruga hili. Licha ya uwepo wa mfumo wa vyama vingi, ikumbukwe tangu TANU na ASP hadi hii leo Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chama tawala, kimeendelea na ujenzi imara si tu wa maendeleo bali pia hali nzima ya uhakikishaji wa uwepo wa demokrasia nzuri inayoleta amani na utulivu ambayo ndio nguzo yetu ya kimaendeleo.

Siasa na demokrasia yetu ni ile inayofuata mfumo wa nyama vingi. Uwepo huu wa vyama vingi umesababisha vyama baina ya vyama ama viongozi baina ya viongozi kusiginana ambapo kila mtu ama kila chama huvutia upande wake. Hapa ndipo kwenye tatizo sugu linalotuweka njia panda huku tukiendelea kutafunwa na mdudu ‘umasikini'.

Nao "uongozi bora" hali si shwari. Hali hii si kwa upande wa chama {yaani CCM} bali ni kwa upande wa baadhi ya viongozi wetu. Uongozi una miiko na si lelemama, kama baadhi yao wanavyojifikiri. Uongozi bora msingi wake ni utawala wa kisheria ambao ni nguzo ya uwepo wa utawala bora.

Tatizo linalotukumba ni uwepo wa laana inayotumaliza kutokana na kuiasi falsafa ya Baba yetu, Mwalimu Nyerere kwa kupuuzia dhana ya uwepo wa siasa safi na uongozi bora. Hatuwezi kuendelea kwa kuendesha ushabiki upofu ama siasa za maji taka, yaani siasa chafu za kuchafuana na kupakana matope kila kukicha.

Mbaya zaidi ni hayo madudu yamekuwa yakifanyika chini ya mwamvuli "unafki". Kwa tafsiri ya haraka haraka neno unafki unaweza ukasema ni undumila kuwili wa kujivika sura mbili tofauti kwa nyakati moja lakini kwa mahali tofauti tofauti kulingana na muktadha husika. Lengo kuu la kufanya hivyo ni kutaka kuharibu uhalisia kwa njia ya mficho na wakati huo huo mtu huyo huyo aonekane mwema machoni.

Hali hii ya baadhi ya watu kuwa wanafki haikuanza leo wala jana. Historia inatudhihirishia hilo kuwa hali ya baadhi ya watu kuutumia mwamvuli huu wa unafki na kuamua kuwa wanafki, haikuanza leo, wala jana kwani ulikuwapo tangu enzi za utawala wa kwanza wa Mwalimu Nyerere hadi hii leo katika utawala wa awamu ya nne yake Dk. Kikwete na utaendelea kuwepo. Utofauti wa unafki upo kwenye ukomavu wake.

Tuweke kumbukumbu zetu sawa. Mwalimu Julius Nyerere wakati akiwa madarakani alimwagiwa lawama na tuhuma lukuki kwani wapo waliosema Mwalimu haambiliki na wengine wakadai anaendesha nchi kwa "remote" akiwa Butiama (kijijini kwao). Lakini mara baada ya kung'atuka kwa hiari Urais ndipo sifa za kinafki zilianza kummiminikia huku tukianza kumuita "Baba wa Taifa". Mara baada umauti kumkuta ndipo unafki ulizidi kwake na leo hii kila kitu kibaya kinachotokea tunasema laiti Mwalimu Nyerere angekuwepo haya yote yasingetokea. Lakini angali hai ama madarakani hatukuyatambua haya zaidi ya kuuendekekeza unafki.

Ama Alhaji Hassan Mwinyi wakati akiwa Rais wa awamu ya pili walimwita mbinafsi, muuzaji nchi kutokana na ubinafsishaji lakini leo hii ni mstaafu wanaanza kummwagia sifa teletele na hata kumwita "Mzee wetu" huku wakijivunia kuchota hekima na busara kutoka kwake lakini angali madarakani hatukuliona hilo. Huu ni unafki mtupu.

Pia Benjamin Mkapa alidhihakiwa kweli kweli wakati wa uongozi wake hadi kufikia hatua ya kumwita ‘ukapa' badala ya Mkapa kutoka katika neno la ‘ukata'.

Lakini leo hii kila anapokatiza ni shangwe, kofi, vifijo, na vigelegele na tukisema afadhali ya Mkapa kuliko wote na wengineo tumewaona wakimpa hata tuzo ya heshima. Jamani! Kama huu si unafki, basi tuuiteje?

Na bila shaka haya marashi ya kinafki yalioanza kupulizwa tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza hautaiacha awamu hii ya nne. Leo hii Rais Kikwete anatukanwa vibaya mno kwani kila mtu anayejisikia kumuongea vibaya anafanya hivyo. Lakini subiria akitoka madarakani, hizo sifa atakazo mwagiwa, usizipimie kabisa!. Rais Kikwete awe sawa kimkao na marashi haya ya kinafki.

Unafki niliouzungumzia ni sehemu ya khulka ya kawaida kabisa kwa asilimia kubwa ya watu kutokupenda kuzungumzia mazuri ya mtu akiwa hai wanasubiria mpaka awe amefariki ndipo wamzungumzie kwa mema; Ama wale walio katika uongozi huwa hawasifiwi kwa kile wanachokifanya mpaka wamalize muda wao wa uongozi ndipo sifa kedekede huanza kumiminika. Yote hayo ni sehemu ya unafki wetu sie tusio na shukrani. Hilo ni kundi mojawapo tu la unafki, unaofanywa na wanafki waliokubuhu.

Kundi lingine la wanafki ni lile ambalo wanatambua mambo yalivyo ama uhalisia wa mambo ulivyo lakini wanaamua kuupindishia kwa maksudi, ilimradi uonekane ni uongo. Watu wa sampuli hii ni wale ambao wanalikubali tukio fulani, lililofanywa na mtu ama kikundi cha watu fulani pasipo kutia shaka wala alama ya kuuliza kitu.

Lakini inapotekea kuwa tukio lile lile ama hali ile ile ikafanywa mtu mwingine ama kundi la watu wengine walio na mitazamo tofauti dhidi yao, huanza kutia shaka, fitna kuwaghubika, hujawa na maswali mengi ya kipuuzi ambayo majibu yake wanayo.

Mathalani, mwaka 1977 kulianzishwa operesheni kali ya kuwasaka wanaosadikiwa walikuwa ni wauaji na wachawi ambapo watu kadhaa walikamatwa, wakawekwa ndani na kupewa mateso makali, yaliyosababisha vifo vya baadhi ya watu. Operesheni hiyo iliyoendeshwa katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga ilisadikiwa kufanywa na maofisa wa kiserikali.

Makosa hayo yaliyofanywa na baadhi ya maofisa wa Kiserikali yalisababisha mabosi wao ama wakubwa wao kimadaraka ambao ni Mzee Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Peter Said Sioverwa (kwa sasa ni Marehemu) aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais usalama wa Taifa; bila ya kuwasahau waliokuwa Wakuu wa Mikoa wa Mwanza na Shinyanga Mzee Peter Kisumo na Marco Mabawa (Marehemu) walijiuzulu kutokana na vitendo vya kikatili vilivyofanywa na maafisa wa Serikali waliokuwa chini yao.

Hapa Mzee Mwinyi aliamua kuwajibika kwa niaba ya makosa yaliyofanywa na maofisa wa ngazi ya chini yake. Yaani makosa wafanye watu wengine ama maofisa wa ngazi ya chini lakini mkubwa wao (Mzee Mwinyi) anaamua kubeba msalaba wao, kwa niaba yao. Kitendo hicho kinajulikana kama kuchukua wajibu wa kisiasa yaani "political responsibility" kwa lugha ya kitaalamu na kisomi zaidi.

Kutoka awamu ya kwanza mpaka awamu ya nne, tunashuhudia hali ile ile ikijitokeza kwa kiongozi mwingine. Ilikuwaje? Wakati awamu ya nne inaingia madarakani, Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) walitangaza hatari ya Taifa kuingia gizani kutokana na ukame uliosababisha vina vya maji yanayozalisha umeme kupungua sana, hivyo jitihada za haraka na za lazima zilihitajika.

Serikali waliisikia taarifa hiyo na ikaiamuru wahusika ama wataalamu wa wizara ya nishati na madini washirikiane na Tanesco katika kutafuta kampuni itakayozalisha umeme wa dharura katika kipindi hicho kigumu.

Hatimaye kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond ilipatikana ambayo baada ya muda mfupi tu ilionekana kuwa na uwezo duni wa kiutendaji na pia hawakuwa na mtaji wa kutosha.

Hali hiyo ya makosa hayo kufanywa na wataalamu wa Tanesco na Wizara yalisababisha wakubwa wao kimadaraka ambao ni Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu na Mawaziri wengine wawili ambao ni Ibrahimu Msabaha na Nazir Karamagi kuamua kujiuzulu kutokana na uzembe uliofanywa na maafisa wao wa chini.

Lowassa hakujiuzulu kwa sababu yeye ndiye aliyehusika katika hili au eti alikuwa na maslahi yake binafsi bali Edward Lowaassa aliamua kubeba msalaba kwa kuchukua dhamana ya kuwajibika kisiasa "political responsibility" kwa kuiokoa serikali isiendelee kusurubiwa na Wabunge kwa maslahi ya Serikali ya awamu ya nne na chama chake CCM.

Jionee unafki wa watu ulivyo. Tukio ni lile lile na hali ni ile ile ambapo lilitokea kwa Mzee Mwinyi lakini leo hii limetokea kwa Lowassa, kwa Mzee Mwinyi hakukuwa na maneno lakini kwa Lowassa kuna maneno tele. Mzee Mwinyi alichukua hatua gani na Lowassa naye alichukua hatua ipi? Wanaopindisha uhalisia huu, kwanini wasiitwe wanafki?

Lowassa aliamua kuwajibika kwa misingi ile ile ya kuchukua dhamana ya kisiasa (Political responsibility). Inakuwaje kwake inakuwa nongwa kwa kitendo chake cha kuamua kuwajibika?

Wapo wanaomlaumu Lowassa kutokana na ufuatiliaji wa ukaribu katika mchakato huu. Watu hawa wanasahau ya kwamba kwanza, Lowassa alikuwa ndio mtendaji mkuu wa Serikali (Waziri Mkuu) akimsaidia Rais katika kipindi hicho. Pili; inawezekana Lowassa alitambua umuhimu wa umeme kijamii na kiuchumi kwa watu na kwa Taifa. Jiulize, endapo nchi ingeingia gizani, huyo anayemsaidia Rais asingeonekana mzembe kwa kutokuchukua hatua za kuinusuru hali ile?

Pia kuna kundi jingine wanalomtuhumu Lowassa kuwa alikuwa na maslahi binafsi dhidi ya kampuni hiyo. Mbaya zaidi ni kuwa hawa wanaoshabikia hili ni mabingwa wa sheria ambao sasa wameivamia siasa, wengineo walishawahi kuongoza mhimili mmojawapo wa dola na hivyo wanazijua vyema sheria zilivyo. Kwanini hawampeleki mahakamani kama kweli wana uhakika na tuhuma zao? Wanamtuhumu (ili waonekane wema), lakini wanashindwa kwenda kwenye vyombo vya sheria, tuwaeleweje? Kama huu si unafki, ni kitu gani haswaa?

Hakika, tuhuma hizi za baadhi ya watu kujigeuza mahakama kwa kumwita mtu au watu wezi pasipo mahakama kuhukumu, zinaelekea kuchochewa zaidi na unafki wao.

Hila, roho mbaya, tamaa za fisi za uchu wa madaraka na mali huwafikisha kwenye upindishaji wa mambo kwa maksudi ilimradi ukweli uonekane ni uongo, kwa kuwaamisha watu uongo wao pasipo kujua kuwa umma wanaujua uongo wao.

Wanauendekeza unafki wao pasipo kujua kuwa unafki wao ndio unaoliangamiza Taifa letu. Unafki wao umeleta chuki iliyozaa makundi baina ya wanasiasa; unafki wao unasababisha baadhi yao kuutafuta utukufu binafsi na si tena utumishi kwa umma; unafki wao umezaa u"bize" wa majungu, fitna, usaliti; unafki wao umeleta uadui unaosababisha viongozi kwa viongozi kutokushirikiana. Pasipo nguvu ya umoja, maendeleo yatatoka wapi?

Leo hii tumefika kwenye hatua ambayo waziri hana ushirikiano na naibu wake; katibu mkuu hawapeani hata salaam na naibu wake. Watu wanaishi kwa mtindo wa nikanyage bahati mbaya, nikulipue maksudi.

Matokeo ya hayo ni kila upande kutokuona mwenzake anapata kile anachokiita sifa kwa jamii. Huyu ataleta mradi bora wa maendeleo kwa jamii, mpinzani wake ataukwamisha; yule atatoa hoja yenye tija, mwenzake ataupinga. Mathalani walipinga mitambo ya Dowans isinunuliwe kwa kuwa ina harufu ya ufisadi na pia ni mitambo chakavu, lakini leo hii tunawasikia Wamarekani wakiinunua na kukiri ni mipya na watatuuzia umeme. Unaona mambo hayo, badala ya kuwa na mitambo yetu wenyewe, tunaishia kuwa Taifa la kuuziwa umeme. Kisa? Unafki wao! Umaskini utatuachia kweli?

Leo wataunda tume kuchunguza, kesho tutalipa faini ya mamilioni ya pesa kutokana na madudu yaliyofanywa na tume hiyo. Haya ni matokeo ya unafki wao; watakubaliana hili ila kwenye mkataba utaandikwa kile. Kwa mwendo huu, tutaacha kuwa maskini? Kisa, unafki wao ambao unazidi kuliangamiza Taifa!

Ipo mifano mingi tu ya kuelezea jinsi gani unafki unaofanywa, unavyotuletea umaskini. Laiti kama unafki ungelikuwa ni pesa, basi watu wangekuwa matajiri. Kwani leo hii baadhi ya watu wameigeuza nchi hii kuwa kama Taifa la Makambare. Si Baba, Mama wala mtoto wote ni wanafiki watupu. Tuukatae unafki huu!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom