RAI: Bunge limekuwa ni kichaka cha ufisadi; Bungeni haukuanza leo, upo mtindo " nipe nikupe" | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

RAI: Bunge limekuwa ni kichaka cha ufisadi; Bungeni haukuanza leo, upo mtindo " nipe nikupe"

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Aug 4, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Aug 4, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Alhamisi, Agosti 02, 2012 12:12

  Na Mwandishi Wetu


  *Ufisadi bungeni haukuanza leo, upo siku nyingi
  *Serikali imeshindwa kudhibiti fedha chafu nchini
  *Mfumo wa uchaguzi, "wengi wape"
  *Uteuzi na utendaji kazi wa mawaziri

  UFISADI bungeni umekuwapo kwa siku nyingi, hasa baada ya kurejesha mfumo wa vyama vingi, imeelezwa.

  Uchunguzi wa Rai unaonyesha kwamba umekuwapo mtindo wa "Nipe nikupe" na Wabunge wengi wamekiri kuwa wanalijua hilo, hasa tangu kuwapo kwa ushindani wa vyama vingi.

  Baadhi ya Wabunge na waliokuwa Wabunge, wanazinyooshea vidole Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali za Mitaa na Nishati na Madini, kuwa zimekuwa zikifanya kazi kwa kulindana.

  Aidha, imeelezwa pia kwamba mfumo wa uchaguzi wa "wengi wape" unachangia kuendeleza vitendo vya rushwa.

  Vile vile wanasema Serikali imeshindwa kuthibiti fedha chafu, sio tu zinavuruga jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei nchini, bali pia zimekuwa chanzo cha ufisadi ambao umejikita bungeni.

  Kamati nyingine za Bunge ambazo zinatajwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi ni Kamati ya Afya na Huduma za Jamii, ambayo inaongozwa na Margreth Sitta na Kamati ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Zitto Kabwe. Kamati nyingine ni ile ya Ardhi na Maliasili ambayo inaongozwa na James Lembeli.

  Kuna madai dhidi ya wenyeviti na wajumbe wa kamati hizo, kwamba kuna mgongano wa kimaslahi, ambapo wahusika wanafanya biashara na makampuni ya umma. Hivyo ni wazi kwamba kuna kulindana kwa mtindo wa "funika kombe mwanaharamu apite".

  Kwa mfano, inasemekana kwamba Kamati ya Afya na Huduma ya Jamii, ilinyamazia ubadhirifu mkubwa wa Bohari Kuu ya Madawa (MSD), ambapo

  James Lembeli anadaiwa kuwa ana maslahi binafsi kwenye Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA).

  Baadhi ya wabunge wanasema kwamba tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, ushindani kati na baina ya vyama, umechochea watu wenye nia mbaya ndani na nje ya Bunge, kujitafutia njia za kutimiza malengo na maslahi binafsi.

  Walio nje ya Bunge, hasa katika Idara za Serikali na sekta binafsi, wanatumia njia chafu za kujihami na kuendeleza malengo binafsi-kutafuta fedha kwa ajili ya gharama za kampeni za uchaguzi wa majimbo na chaguzi ndani ya vyama.

  Shughuli ya kutafuta uongozi ina gharama zake. Wabunge licha ya matakwa binafsi ya kuwa na maisha bora, mahitaji yao ni makubwa, hasa kwa kuzingatia mazoea ya kutumia fedha kwa karibu kila jambo.

  Wabunge wanatarajiwa kutoa michango majimboni mwao kwa miradi ya maendeleo, miradi ya chama na miradi ya kijamii kama harusi, vilio, miradi ya makanisa na misikiti.

  Tanzania inatumia mfumo wa ‘wengi wape' ambapo mgombea aliyeteuliwa na chama chake, anapaswa kugharamia karibu sehemu yote ya kampeni za uchaguzi katika jimbo lake. Kukusanya fedha kwa ajili ya kampeni na mikakati ya kutafuta fedha baada ya uchaguzi.

  Wanaogombea ubunge majimboni na wale wa viti maalumu, wote wanahitaji fedha. Swali kubwa ni je, fedha hizo wanazipataje?

  Fedha rahisi zinapatikana kwa Wabunge kukosa uadilifu na kujihusisha na vitendo vya kifisadi. Makundi mbalimbali yanawalenga Wabunge. wafanyabiashara na mashirika mbalimbali, ambayo yanajihusisha na vitendo vichafu, kama vile mitandao ya wizi wa fedha katika mabenki, fedha za madawa ya kulevya na fedha zinazoibiwa serikalini. Wabunge wanakuwa walengwa kwa sababu hakuna sheria inayothibiti ushawishi (lobbying) kwa Wabunge.

  Watendaji serikalini wanaiba fedha za Serikali na wanafanikiwa kuukwepa mkono wa sheria kwa kuwahonga wajumbe wa kamati za Bunge.

  Kamati ambazo zinatajwa ni zile za Hesabu za Serikali za Mitaa kwa kuwa kweenye Bajeti ya Serikali, fedha nyingi kwa ajili ya huduma za elimu, afya, pembejeo na miradi mingine ya wafadhili, zimeelekezwa kule.

  Inasemekana kwamba halmashauri, zina uwezo mdogo wa kusimamia matumizi ya fedha wanazokusanya na nyingine zinazotolewa na Serikali Kuu. Kinachojitokeza ni kwa watumishi wa Serikali za Mitaa, huanzisha ‘miradi bubu' ili wajichotee fedha za umma kiulaini.

  Kwa upande mwingine, kwanza ni kuwalenga madiwani na kuwaingiza katika mtandao wa ulaji fedha za umma. Madiwani wengi wana kampuni hewa au za ndugu na familia zao ambazo hupewa tenda na halmashauri.

  Inaelezwa kwamba mtindo ulioenea hivi karibuni wa kutengua uchaguzi wa mameya wa majiji na manispaa; pamoja na wenyeviti wa halmashauri mbalimbali, unatokana na msuguano wa viongozi hao na madiwani kunyimwa tenda hizo.

  Tayari Meya wa Halmashauri ya Mwanza (CHADEMA) ameondolewa katika wadhifa wake kwa madai ya mapungufu katika uongozi wake wa jiji la Mwanza. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi (CCM), naye ameondolewa. Pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga Vijijini (CCM) na Halmasahuri ya Kibondo nao wameondolewa.

  Ni wazi kuna mgogoro wa uongozi katika halmashauri nchini, lakini kilicho wazi zaidi ni vita vya ulaji ambavyo vinapiganwa kati na baina ya makundi ya viongozi, ambayo yanahusisha Madiwani na Wabunge pia.

  Uozo uliopo katika Serikali za Mitaa unajulikana sana kwa Wabunge, ambao wanaingia pia kwenye halmashauri kama madiwani.

  Wakati wa mjadala wa ufisadi wa EPA ambao ni bilioni 130, Wabunge wengi walipiga kelele sana. Lakini inapodhihirika kutoka kwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), kwamba kiasi cha fedha zaidi ya trilioni 1 zinaliwa katika Serikali za Mitaa, Wabunge wanaona ni jambo la kawaida!

  Mahusiano ya halmashauri na Bunge yako kati ya halmashauri na Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Serikali za Mitaa na pia na Waziri wa TAMISEMI. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa sasa Mwenyekiti wake, Augustine Mrema, anatoka upande wa upinzani bungeni. Kabla ya hapo Kamati hiyo ilikuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge kutoka chama tawala.

  Mpasha habari wetu anasema wakati Kamati za Hesabu za Serikali za Mitaa katika kipindi cha 2000-2005, kazi kubwa ya kukagua utendaji kazi ilifanyika.

  Inadaiwa kuwa wajumbe walitengeneza pesa nyingi kutoka kwa halmashauri za wilaya na pia kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma kutokana na kuleta bidhaa hewa kwa kushirikiana na watendaji.

  Hata hivyo inadaiwa kwamba mwenyekiti na wajumbe katika kamati hiyo walikuwa na zabuni katika halmashauri za wilaya. Pia kuna tuhuma kwamba walikuwa wanapewa pesa taslimu na watendaji wakuu wa halmashauri.

  Kifuatacho ni kisa kinachoelezea jinsi ufisadi mkubwa ulivyokuwa unafanyika katika Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa.

  Kati ya mwaka 2005-2010, nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ilibadilika ambapo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Mwenyekiti alitoka upande wa upinzani. Dk. Wilbroad Slaa, wakati huo akiwa Mbunge (CHADEMA), alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa na baadaye akateuliwa kuwa Mwenyekiti.

  Lakini suala la ufisadi wa kukubali rushwa, si suala la chama. Ni tabia ya mtu kukosa uadilifu. Majaribu na vishawishi ni vingi hasa kwa viongozi wenye dhamana kutumia nafasi zao za madaraka kujinufaisha kibinafsi.

  Hatari ya tukio hili imetolewa na mpiga filimbi (whistle blower na jina tunalihifadhi), ambaye alikuwa anafanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

  Halmashauri hiyo ilitokea kuwa mojawapo ya halmashauri ambazo utafiti wa mwaka 2008/2009 (Fordia), ulionyesha kwamba rushwa ilikuwa imekithiri.

  Anasema alimwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, akimwelezea kuhusu mtandao wa wizi wa fedha za Halmashauri na kuonyesha jinsi fedha zilivyokuwa zinatafunwa. Badala ya kuchunguza na kuchukua hatua, mwenyekiti na kamati yake wakawasiliana na watendaji wakuu wa Halmashauri na kuwapa taarifa kuhusu habari walizo nazo na matokeo mabaya yanayoweza kuwapata kama Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali itawapatia hati chafu.

  Waliofanya mawasiliano hayo hawakuwa watumishi wa Bunge, bali vijana wa chama, waliotumwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge.

  Watendaji wa Halmashauri ya Muleba waliamua kufunga safari kuja Dar es Salaam kukamilisha makubaliano.

  Wakiongozwa na Mweka Hazina na Mhasibu (majina tunalihifadhi) na walikutana na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, lakini Mwenyekiti alikuwa na wajumbe wa chama chake tu.

  Baada ya majadiliano ambayo yalifanyika nje ya majengo ya Bunge, inadaiwa kiasi kati ya shilingi 36m. na 40m. Walipewa wahusika, ili waweze kuipatia Halmashauri ya Muleba hati safi.

  Hii ni njia ambayo imetumiwa na Wabunge kuficha, kushiriki na kuendeleza ufisadi kwenye halmashauri.

  Pengine jambo lingine ambalo linaleta hali ya mkanganyiko katika Serikali ni suala la uteuzi wa mawaziri kuingilia kazi za makatibu wakuu. Mawaziri wanapoteuliwa kutokana na Wabunge, kunakuwepo na hali ya kutotaka kuangushana kati na baina ya Wabunge wenyewe.

  Na vilevile, mawasiliano yasiyo rasmi yanasaidia kuendesha mambo kienyeji. Vita vya makundi ya kisiasa navyo vinakuwa na nafasi yake katika kuleta utata katika suala zima la nidhamu na uadilifu wa Wabunge kwa ujumla.

  Wakati umefika kwa vyama vyenye Wabunge na Bunge lenyewe kufanya tafakuri ya kurejesha heshima ya Bunge.

   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Aug 4, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145

  Kama kweli Wanaipenda Nchi yao kwanini Wasirudishe NGUZO za VIONGOZI wa SERIKALI?

  Yeah utakuwa na Kampuni lakini kutakuwa na MIPAKA utatakiwa kujiuzulu toka kwenye kampuni yako kama umekuwa

  Mbunge ili kuondoa double-standards; na pia kampuni yako haitapewa GOVERNMENT contracts... kutakuwa na strict

  LAW ukipewa GVT contract ni JELA au KUFILISIWA.
   
 3. manuu

  manuu JF-Expert Member

  #3
  Aug 4, 2012
  Joined: Apr 23, 2009
  Messages: 4,063
  Likes Received: 9,672
  Trophy Points: 280
  Si ndiyo maana mi nishaachaga kupiga kura iwe ya nani,chama gani sipigi kabisa.
  Eti ni haki yangu ya msingi,KUNA HAKI BONGO HAPA?
   
Loading...