Rafiki niliyemuamini akanipora mchumba, Mungu akanilipia! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Rafiki niliyemuamini akanipora mchumba, Mungu akanilipia!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by vukani, Jul 16, 2012.

 1. vukani

  vukani JF-Expert Member

  #1
  Jul 16, 2012
  Joined: Dec 30, 2009
  Messages: 245
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  Alipofika hapa Arusha kwa mara ya kwanza ni mimi niliyempokea, nakumbuka ilikuwani mwaka 2000. Alikuwa ndio amemaliza chuo cha ualimu huko Ndala Tabora na alipangiwa kuja kufanya kazi hapa Arusha. Akiwa ni mzaliwa wa huko Old Moshi mkoani Kilimanjaro, hakuwa na ndugu wala jamaa hapa Arusha, hivyo akiwa kama mwalimu mwenzangu nilimpokea na kukaa naye kama mdogo wangu. Hata hivyo uamuzi wa kumkaribisha binti huyu nyumbani ulifurahiwa na mpenzi wangu ambaye ni mchaga wa Marangu na alimuona yule binti kama dada yake na mimi kuanzia siku hiyo tukawa tunaitana wifi na binti huyo.

  Kwa kuwa nilikuwa na ugeni pale nyumbani ilibidi wakati mwingine niwe naenda kulala kwa mpenzi wangu kwa sababu pale nyumbani nafasi ilikuwa ni ndogo, kwani kutokana na mishahara ya waalimu kuwa midogo na kodi za nyumba hapa Arusha kuwa juu sikuwa na uwezo wa kulipia vyumba viwili. Tulikuwa na kawaida ya kutoka jioni mara kwa mara mimi na mpenzi wangu kwenda kula nyama choma, nililazimika kumchukua wifi yangu na kutoka naye ili asijisikie mpweke.

  Nakumbuka siku moja, wifi yangu huyo aliniuliza kama nina muda gani tangu niwe na uhusiano na kaka yake, nilimjibu kuwa tuna miaka minne tangu tuwe wachumba. Huku akionekana kushangaa alisema "Miaka minne hamfungi tu ndoa mnangoja nini?"

  "Sijui kaka yako, kila nikimwambia tufunge ndoa anadai eti hajajiandaa, mpaka akamilishe mambo fulani"
  "Mimi siwezi, miaka minne mko wachumba tu! Si umzalie mtoto labda ndio atachukua uamuzi? Alishauri wifi yangu,

  "Siko tayari kulazimisha kuolewa kwa kumbebea mwanaume mimba kisa nataka kuolewa, kama anasubiri mpaka nibebe mimba, basi atasubiri sana," nilimjibu

  "Wifi wanaume wa siku hizi mwEnzangu, wagumu kweli kuoa, usipowabebea mimba basi utabaki hapo, utashangaa kesho unasikia ana mtoto kwingine au anaoa mwanamke mwingine kisa kamjaza mimba" Alisema wifi yangu


  "Wifi kama imepangwa tuoane tutaoana lakini kama haijapangwa basi labda ni mipango ya mungu," nilimjibu.
  Kuanzia siku hiyo nikashangaa kukawa na ukaribu sana kati mpenzi wangu na huyo wifi yangu, mara nyingi ilikuwa mpenzi wangu akija anatumia muda mwingi akiongea na huyo wifi yangu tena wakati mwingine wakiongea kikwao yaani kichaga, hata hivyo sikujali sana kwani nilikuwa namuamini sana mpenzi wangu.
  Nilikaa na binti yule kwa takribani miezi sita na ndipo akapata chumba na kuhama. Nilifurahi sana kwa binti huyo kuhama kwani nilijua kuwa sasa nitapata wasaa wa kujivinjari na mpenzi wangu, lakini mambo yalkuwa ni kinyume, kwani mpenzi wangu alibadilika na alikuwa haonekani kwangu kama ilivyokuwa kawaida yake, na nilipokuwa nikimuuliza alikuwa akisingizia kuwa yuko bize sana.

  Mpenzi wangu alikuwa ni mtumishi wa Benki na ni kweli kuna wakati huwa anakuwa bize, lakini sio kwa kipindi kile. Kwa hiyo kitendo cha mpenzi wangu kuwa bize katika kipindi kile kilinishangaza sana, hata hivyo hakupunguza upendo wake kwangu, aliendelea kunipenda na kunihudumia kama kawaida na tena aliongeza upendo sana kwangu kiasi kwamba sikuweza kumtilia mashaka kuwa huenda amepata mpenzi mwingine.

  Siku moja majira ya jioni nikiwa ndio nimerudi kutoka kazini nilipokea simu kutoka Singida kuwa mama yangu ni mgonjwa na kama nikimkuta hai ni bahati. Miaka mitatu iliyopita ndio nilimpoteza baba yangu kutokana na ugonjwa wa Kansa na sasa ni mama yangu sijui amepatwa na nini masikini. Kwa kuwa nilikuwa ni katikati ya mwezi na sikuwa na akiba ya kutosha nyumbani nilikata shauri kumpigia simu mpenzi wangu ili anipe msaada wa kifedha ili siku inayofuata nisafiri kwenda nyumbani kumuona mama yangu ambaye mpaka wakati huo sikujua kama yuko hai au ameshafariki, lakini nilipompiga simu mpenzi wangu, simu yake ilikuwa imezimwa. Huku nikiwa nimechanganyikiwa niliamua kwenda kazini kwake na nilipofika nikaambiwa ametoka.

  Ilibidi niende nyumbani kwake maeneo ya Kaloleni na nilipofika huko napo sikumkuta. Nilikaa pale nje nikiwa nimechanganyikiwa kabisa nisijue cha kufanya, niliamua kumpigia simu yule wifi yangu niliyempokea na kukaa naye pale kwangu, siku hiyo ya ijumaa hakuja kazini alituma ujumbe kuwa anaumwa na asingeweza kuja kazini, na yeye nilipopiga simu iliita sana bila kupokelewa, na nilipojaribu kupiga tena simu ilikuwa imezimwa, niliamua kwenda nyumbani kwake maeneo ya Sanawari, na nilipofika nilikuta mlango wake umefungwa lakini nilisikia sauti ya redio ikiimba nyimbo za dini. Niliona viatu vinavyofanana kabisa na vya mpenzi wangu pale nje, nilihisi labda atakuwa ameamua kumtembelea dada yake. Nilibisha hodi mara kadhaa, mara mlango ukafunguliwa, yule wifi yangu aliponiona alistuka sana na akafunga mlango haraka na kuniambia nisubiri. Mara alitoka na kufunga mlango kwa nje na huku akiwa amekunja sura akaniuliza nina shida gani, nilishangaa jinsi alivyoonekana kukerwa na ujio wangu, nilimuuliza kama anaendeleaje na kuumwa

  "Yaani umetoka kwako kuja kutaka kujua tu kama ninaendeleaje, si ungepiga tu simu, sasa usumbufu wote wa nini?"

  Nilimjibu kuwa nilipiga simu sana lakini haikupokelewa, nikadhani labda amezidiwa. Kama nikutaka kujua hali yangu, basi mimi ni mzima wa afya, samahani nina mgeni ananisubiri ndani, alisema vile na kugeuka kuelekea ndani. Nilishangazwa na majibu yale, lakini nilijua labda ni kwa kuwa anaumwa, unajua sisi wanawake tuna vipindi tunakuwa na visirani kutokana na matatizo yetu mzunguko wa mwezi. "Samahani Gau, nina matatizo na ndio nikaja kukuona, nimepigiwa simu kutoka nyumbani mama yangu ni mgonjwa mahututi, naomba kama una akiba ya shilingi elfu hamsini unisaidie kisha nitakurudishia, nimejaribu kumpigia simu kaka yako lakini simu yake imezimwa" nilimwambia.. Aligeuka kwa dharau na kuniambia, "hivi kumbe hukuja kuniona bali umeletwa na shida zako, kama ni pesa sina mtafute sijui mpenzi wako au mume mtarajiwa akusaidie" alisema vile na kuondoka zake akiniacha pale nje.

  Nilisimama pale nje kwa nukta kadhaa nikiwa nimeduwaa, nilikuwa siamini kile kilichotokea, ama kweli fanya wema wende zako usingoje shukurani walisema waswahili, nilikaa na binti huyu kwa upendo. Miezi yote sita niliyokaa naye hakuwa akipokea mshahara kutokana na kuwa nje ya bajeti ya mshahara, nilimsaidia kwa kila kitu na hata alipopata malimbikizo ya mshahara alitaka kunirudishia kiasi cha fedha nilizokuwa nikimpa lakini nilikataa na ndipo akamudu kutafuta chumba na kuhama, sasa leo nakuja kumuomba anikopeshe pesa kidogo ananijibu kama anamjibu mtu asiyemfahamu!

  Niliondoka nikiwa nimechanganyikiwa, kwanza nilijiuliza juu ya vile viatu vinavyofanana na vya mpenzi wangu nilivyovikuta pale nje kwa yule binti, halafu kile kitendo cha kustuka aliponiona, na mbona alitoka na kufunga mlango kwa nje, au alikuwa hataki nimuone huyo mgeni wake, atakuwa ni nani? Nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu. Niliamua kumpigia simu rafiki wa mpenzi wangu wanaefanya nae kazi, alinielekeza mahali alipo, alikuwa kwenye Baa na rafiki zake wakinywa pombe na nyama choma, nilipofika alinikaribisha na kuniagizia bia, lakini nilikataa na sikupoteza muda nilimsimulia matatizo niliyo nayo, na yeye alijaribu kumpigia simu mpenzi wangu lakini simu yake haikupatikana. Alinipa kiasi cha shilingi laki moja na kuniambia atamalizana na mpenzi wangu.

  Nilikwenda kutoa taarifa kwa mwalimu mkuu na alinipa ruhusa ya siku tatu. Siku iliyofuata niliondoka asubuhi na mapema kwenda singida na hata asubuhi wakati naondoka nilipojaribu kumpigia simu mpenzi wangu simu yake haikupatikana vile vile. Nilipofika nilikuta watu ni wengi pale nyumbani, nikajua kuwa, mama yangu ameshafariki. Ni kweli alikuwa amefariki siku ile ile niliyopigiwa simu, na kilichomuua ni shinikizo la damu. Tumezaliwa watoto watano wanaume wanne na mimi mwanamke peke yangu, na ni wa mwisho kuzaliwa, tangu baba afariki kaka zangu wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara wakigombea urithi wa mali alizoacha baba ambazo ni nyumba mbili na mifugo kadhaa, yaani ng'ombe, mbuzi, na kondoo.

  Ugomvi huo ndio chanzo cha mama kupata shinikizo la damu na kufariki kutokana na ugomvi wa kaka zangu usioisha kutokana na kugombea mali za mzee. Katika familia yetu mimi peke yangu ndiye niliyebahatika kuendelea na masomo hadi kuwa mwalimu lakini kaka zangu walikataa kusoma na kukimbilia kuwa wachuuzi wa biashara ndogo ndogo. Tulimzika mama na baadae ndugu wa baba waliweka kikao na kupitisha uamuzi kuwa mifugo igawanywe na kisha nyumba ziuzwe na kila mtoto apewe chake ili kukata mzizi wa fitina.

  Kila kitu kilifanyika kama maamuzi ya baraza la wazee walivyoamua, nilikabidhiwa ng'ombe zangu kumi na mbuzi nane na kondoo sita na nyumba ziliwekwa chini ya wazee wa familia ili zitakapouzwa kila mtu apate mgao wake, huo ndio ukawa mwanzo wa familia kusambaratika. Nilikabidhi ile mifugo kwa mjomba wangu kaka yake mama na kuondoka kurudi Arusha kuendelea na kazi. Kipindi chote nilipokuwa msibani Singida nilijitahidi kumtafuta mpenzi wangu lakini simu yake hauikupatikana. Niliripoti kazini na kupokelewa na walimu wenzangu, na kuanza kazi, sikumkuta yule wifi yangu kazini niliambiwa kuwa aliaga kwenda kwao Moshi kuhudhuria matatizo ya kifamilia. Baadae nilianza kusikia minong'ono kwa kaenda kwao kumtambulisha mchumba wake, sikufuatilia habari hizo, niliendelena na kazi zangu. Siku iliyofuata nilipokwenda nyumbani kwa mpenzi wangu niliambiwa kuwa amesafiri kaenda kwao Moshi.

  Siku tatu baadae nikiwa nyumbani kwangu uani nimetulia nikiwa bado nina majonzi ya kufiwa na mama yangu, mchumba wangu alikuja kwangu lakini hali aliyokuja nayo ilinishtua, hakuwa mchangamfu kama nilivyomzoea. Nilimkaribisha ndani, alisita kidogo kisha akaingia ndani, kabla hajakaa alianza kunishambulia kwa maneno makali eti nimemdhalilisha sana kwa marafiki zake kwa kitendo changu cha kukopa pesa kwa rafiki yake badala ya kumtafuta, aliongea kwa sauti ya juu na hakunipa nafasi ya kujieleza. Aliniambia kuwa kuanzia wakati huo mimi na yeye tusijuane niende kwa huyo huyo aliyenipa nauli ya kwenda Singida. Aliondoka bila ya kunisikiliza na kutoweka. Nililia sana kwa uchungu. "Sijui nina mkosi gani mie," nilijisemea.

  Niliamua kumtafuta rafiki yake aliyenipa nauli ya kwenda nyumbani, Singida, nilimpata na baada ya kumweleza yaliyonipata, alishanga sana na alipompigia simu ili kujua sababu ya kuninyanyasa alimjibu kuwa hayamuhusu na kukata simu. Yule shemeji aliniambia kuwa nirudi nyumbani na atajaribu kutusuluhisha. Yule wifi yangu alirudi kutoka kwao, na kuripoti kazini, lakini hakunichangamkia wala kunipa pole, nilishangaa sana, kwani sikuwahi kugombana naye. Nilikuwa sina mawasiliano na mpenzi wangu kabisa na hata namba yake ilikuwa haipatikani, baadae nilikuja kugundua kuwa amebadilisha namba, hiyo ni baada ya kumpigia rafiki yake mmoja na ndio akaniambia kuwa amebadilisha namba.

  Siku moja jumamosi nikiwa zangu sokoni nilikokwenda kununua mahitaji nilikutana na mpangaji mwenzie na mpenzi wangu tulisalimiana, na kuanza kupiga stori za hapa na pale, aliniuliza kwa nini sionekani tena pale kwa mpenzi wangu, sikutaka kumweleza juu ya tofauti zetu, nilijua tu kuwa lile lilikuwa ni tatizo la kawaida ambalo lingeisha, kwani kutofautiana kwa watu wawili wapendanao ni jambo la kawaida tu. Nilimjibu kwa kifupi tu kuwa niko bize na masomo, nilimdanganya kuwa ninasoma chuo kikuu huria. Alionekana kutoridhika na jibu langu, nilimuaga na kuanza kuondoka, lakini wakati naondoka, aliniita kwa nyuma "Eliza" nilisimama ili kumsikiliza. "Nina mazungumzo na wewe unaweza kunipa nafasi tukae mahali tuongee kidogo, ni kwa faida yako" aliniambia kwa kuonesha msisitizo. Nilimkubalia, tukasogea hadi kwenye baa moja iliyokuwa jirani, aliniomba niagize kinywaji, nikaagiza maji na yeye akaagiza soda. "Hivi ni kweli umeachana na mpenzi wako" Alianza mazungumzo kwa kuniuliza swali. Nilishikwa na mshangao, kwa swali lile, nikamuuliza sababu ya kuniuliza lile swali.

  Mbona tunamuona yule binti uliyekuwa ukija naye pale kwa mpenzi wako, ndiye ameshikana uchumba na mpenzi wako na hivi karibuni alipekeka posa huko uchagani, Hayo maneno ya mwisho niliyasikia kama mwangwi, na mwili wote umekufa ganzi, nilibaki kimya kwa nukta kadhaa, nilibabaika kidogo… Yule mwanamke alionekana kushangaa, ina maana ulikuwa hujui? Nilimjibu kuwa nilikuwa sijui, nilimshukuru na kuondoka zangu kuelekea nyumbani, nilipofika niliweka mizigo yangu ndani, nikatoka kuelelekea kwa yule binti Sanawari, nilipofika niliingia ndani moja kwa moja bila kubisha hodi, nilibaki nimesimama huku nikitetemeka, nilimkuta mpenzi wangu na yule binti wakilishana chakula kwa mahaba….

  Sikuamini macho yangu, na hata wao walibaki wameduwaa, niliondoka mahali pale bila kusema lolote, hata majirani ambao walikuwa uani wakati huo walijua kuwa kuna jambo kwani niliwapita bila kuwasemesha na niliondoka bila kuwaaga. Nilikwenda kwa mwalimu mwenzangu mmoja ambaye ni rafiki yangu, na kumweleza kila kitu. Kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba kumbe kipindi kile niliposafiri kwenda kumzika mama yangu ndio akachukua likizo ya wiki moja kwa madai kuwa amepata mchumba lakini alikuwa akitamba kuwa atatushangaza pale kazini. Hakuna aliyejali maneno yake.

  Siku iliyofuata nilifika kazini na niliamua kuchukua likizo ya wiki mbili ili kupumzisha akili kwani nilihisi kuchanganyikiwa, nilimueleza mwalimu mkuu kila kitu naye alitaka kutukutanisha ili kujaribu kuondoa tofauti zetu lakini nilikataa, na alikubali kunipa likizo. Nilikaa nyumbani siku zote nilikuwa nilishinda ndani nikilia. Kwa muda mfupi nilikonda sana. Kumbe huku nyuma wakati nikiwa likizo yule binti aliomba uhamisho wa haraka na kwa kutumia pesa alifanikiwa kuhamishiwa shule nyingine. Baada ya wiki mbili nilirudi kazini, lakini nilikuwa na aibu sana kwa kuhisi kufedheheka, ilikuwa hata waalimu wenzagu wakicheka nahisi wananicheka mimi, pale nilipokuwa nikikaa napo mambo yaligeuka, baadhi ya wapangaji wenzangu ambao tulikuwa hatuelewani walitumia nafasi hiyo kunikejeli na kunisengenya waziwazi, nilikosa amani.

  Niliamua kuhama, na baada ya wiki mbili nilihamia maeneo ya Sakina. Miezi mitatu baadae nakumbuka ilikuwa ni mwanzoni kwa mwaka 2001 yule mchumba wangu alifunga ndoa na yule binti, tena ilikuwa ni ndoa kubwa hasa iliyosheheni mbwembwe kibao. Siku hiyo niliamua kwenda Moshi kwa mwanafunzi mwenzangu niliyesoma naye chuo. Siku zilipita na maisha yaliendelea, niliamua kusahau yote na kikubwa zaidi niliwasamehe yule mchumba wangu na yule binti, nikaendelea na maisha kama kawida.
  Mungu huwa analipa hapa hapa duniani, kwani miaka mitano baadae nilipata taarifa kuwa aliyekuwa mchumba wangu amelazwa katika Hospitali ya Mount Meru na hali yake ni mbaya sana. Aliyenipa taarifa hizo hakuniambia kuwa anaumwa ugonjwa gani. Sikwenda kumuona wala sikujishughulisha kufuatilia habari zake, niliendelea na maisha yangu kama kawaida. Wiki mbili baadae nilikutana na rafikiye na alishtuka sana kuniona kwani tulipoteana kwa muda mrefu sana takribani miaka mitano kwani nilihama katika shule ile siku nyingi nikapangiwa kufundisha shule iliyoko jirani na ninapoishi kwa hiyo kuja maeneo ya katikati ya mji ilikuwa ni mara chache sana.

  Yule rafiki wa aliyekuwa mpenzi wangu aliniomba tutafute mahali tukae ili tuongee kwani alikuwa akinitafuta kwa siku nyingi sana. Tulisogea katika Baa iliyoko jirani na tulipofika pale yule bwana aliniomba niagize kinywaji, niliagiza maji ya kunywa. Yule bwana akaniomba niende Hospitalini nikamuone mpenzi wangu wa zamani kwani hali yake ni mbaya na amekuwa akinitajataja sana kuwa anahitaji kuniona kabla hajafa ili aniombe radhi, nilishangaa sana, aniombe radhi kwa lipi? Mbona mimi nilishamsamehe siku nyingi.

  Nilikataa kwenda kumuona, lakini baada ya rafikiye huyo kunibembeleza sana nilikata shauri niende kumuona, ili kuondoa lawama. Nakumbuka ilikuwa ni siku ya ijumaa, rafiki wa mpenzi wangu alinifuata shuleni mida ya jioni akiwa na gari lake na tukaondoka na kwenda Mount Meru hospitali kumuona yule bwana. Tulipofika, tulielekea wodini moja kwa moja, kwa jinsi tulivyokuwa tukitembea kuelekea wodini na ndivyo mapigo ya moyo wagu yalivyozidi kuongezeka, nilikuwa napumua haraka haraka kama vile nilikuwa nakimbia mpaka shemeji angu akawa na wasi wasi.

  "Vipi shemeji, unayo matatizo ya moyo?" aliniuliza….
  "Hapana sina kabisa? Nilimjibu kwa sauti ya kutetemeka. Tulipo karibia Wodi aliyolazwa yule mpenzi wangu wazamani yule shemeji yangu aliniomba tupumzike pale nje kwanza kabla ya kuingia wodini, lengo lake ilikuwa ni kunipa nafasi nipumue na ku relax kidogo. Tulipoingia wodini niliwakuta ndugu zake wengi, nadhani walikuwa wanafahamu ujio wangu kwani walisogea pembeni na kunipa nafasi ili niweze kumuona mgonjwa.

  Nilisogea pale kitandani alipo, alikuwa amekonda sana kiasi kwamba hata ile sura yake niliyoizoea ilikuwa imetoweka, alinikazia macho kwa nukta kadhaa bila kusema neno, ndugu zake waliniambia kuwa alikuwa amekata kauli tangu jana. Alinionesha ishara niiname kama vile alitaka kuniambia kitu, nilijongea karibu na yeye na kuinama, alinishika mkono kwa nukta kadhaa kisha akaongea kwa sauti ya chini sana,,, "Naomba unisamehe mpenzi wangu, nisamehe ili nikapumzike kwa amani"

  Nilijikuta machozi yakinitoka na nilishindwa kusema kitu chochote nikabaki nikiwa nimemtumbulia macho..
  "Nilishakusamehe mpenzi wangu, najua sio wewe bali ni shetani ndiye aliyesababisha yale yaliyotokea yatokee" Nilimwambia. Tuliangaliana, nikamuona akitokwa na machozi, namimi sikuweza kujizuia nilijikuta nikilia nilitoa leso yangu na kujifuta machozi na kisha kumfuta na yeye. Niliondoka pale na yule shemeji yangu, aliyenipeleka pale. Njiani alinisimulia mkasa uliompata mpenzi wangu yule wa zamani mpaka kuwa katika hali ile. Kumbe yule mpenzi wangu wa zamani alihamishiwa Moshi, kwa hiyo ikabidi yeye na yule mkewe aliyenisaliti wahamie moshi. Miaka miwili baadae mkewe akiwa ni mjamzito wa miezi mitatu yule bwana akapata mkasa wa upotevu wa mamilioni ya pesa katika kitengo chake na yeye kama mkuu wa kitengo hicho na wenzake wakawekwa ndani. Kutokana na mshituko wa mumewe kuwekwa ndani, yule mkewe akapoteza ujauzito.

  Baadae walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka, lakini walinyimwa dhamana kutokana na unyeti wa mashitaka yao. Inasemekana wakati mumewe akiwa bado yuko ndani, yule mkewe akawa anachapa umalaya akitembea na wanaume mbali mbali wakiwamo marafiki wa mume wake. Ilichukua mwaka mmoja yule bwana kuachiwa kwa kufutiwa mashitaka kwa kuwa hakuhusika na ule upotevu. Alipotoka ndugu zake walimshauri amuache yule mwanamke kwa kuwa alikuwa na tabia mbaya za umalaya na alikuwa amemdhalilisha kwa ,marafiki zake, lakini yule bwana hakusikia aliwapuuza nduguzake na kumtetea mkewe kuwa hakuwa Malaya bali wanamsingizia.

  Baadae yule mwanamke alipata ujauzito tena, lakini ujauzito huo ulikuwa na complicationa nyingi, na kumfanya kudhoofu sana, baadae ujauzito ule ulitoka tena na kuanzia hapo akawa ni mgonjwa wa kitandani, na alipopelekwa hospitali alikutwa na TB. Hali ilizidi kuwa mbaya, mume alikuwa hana kazi na mke ndio alikuwa ni mgonjwa. Pamoja na juhudi za kumtibu mkewe kwa kushirikiana na ndugu zake lakini haikusaidia kwani alifariki. Kutokana na kifo cha mkewe, yule bwana alipata mshtuko na hivyo kulazwa hospitali kwa matibabu, hata hivyo hali yake haikuonekana kutengemaa, ikabidi ndugu zake waishio Arusha wamchukue na kumhamishia Arusha kwa ajili ya kumhudumia. Baada ya vipimo ilionekana kuwa yule bwana alikuwa ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi. Naambiwa kuwa kila siku alikuwa akinitaja taja na alikuwa anataka nitafutwe ili aniombe radhi kwani alinikosea sana.Ukweli ni kwamba mimi nilikwisha wasamehe wote na nilishasahau.

  Yule rafikiye alinifikisha nyumbani kwangu, na tulipeana namba za simu na akaondoka zake. Siku iliyofuata yaani jumamosi, alifajiri alinipigia simu na kunijulisha kuwa yule bwana amefariki alifajiri ile na mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Moshi kwa mazishi inafanyika kwa kaka yake mkubwa maeneo Njiro. Nilikwenda Njiro na kuungana na ndugu wa marehemu. Nilikuwa ni miongoni watu waliosafiri kwenda Moshi kwa mazishi na ndugu wa marehemu walikuwa karibu na mimi utadhani nilikuwa ni mke wa marehemu.

  Tulimzika mpenzi wangu wa zamani na kisha kurejea Arusha siku hiyo hiyo. Maisha yanaendelea kama kawaida na nimeshasahau, ila tukio hili limenifundisha jambo, kuwa kama ukiona jambo haliwi kama unavyotaka au ulivyotarajia, huna haja ya kulazimisha, kwani huenda kuna kitu unaepushwa nacho. Namshukuru mungu kwa yote, kwani yeye ndiye mchungaji wangu. Ninaumia sana mpaka sasa nimetimiza miaka 41, lakini sijabahatika kupata mtu wa kunioa achilia mbali kupata mtoto, nimefikia mahali natamani sana kuwa na mtoto lakini nitamzaa na nani? Wanaume walivyojaa ulaghai. Ingawa nimebahatika kujenga nyumba yangu huko maeneo ya Kwa Moromboo baada ya kupata fedha za mgao wa mauzo ya nyumba zetu za urithi, lakini nahisi nina deni kubwa sana, nahitaji sana kuwa na mtoto.  ANGALIZO:

  Huu ni mkasa wa kweli, na unamuhusu mtu ninayefahamiana naye anayepatikana pande za Arusha, majina ya wahusika sio ya kweli na pia majina ya maeneo nimeyabadilisha ili kuepusha usumbufu kwa wahusika.
   
 2. kapistrano

  kapistrano JF-Expert Member

  #2
  Jul 16, 2012
  Joined: Apr 2, 2012
  Messages: 1,204
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 135
  Nitasoma usiku then nitachangia
   
 3. stroke

  stroke JF-Expert Member

  #3
  Jul 16, 2012
  Joined: Feb 17, 2012
  Messages: 13,394
  Likes Received: 6,578
  Trophy Points: 280
  Eric shigongo
   
 4. mkonowapaka

  mkonowapaka JF-Expert Member

  #4
  Jul 16, 2012
  Joined: Feb 19, 2010
  Messages: 1,483
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 145
  heeeeeeeeeee gazeti kumbe..kwa heri
   
 5. MadameX

  MadameX JF-Expert Member

  #5
  Jul 16, 2012
  Joined: Dec 27, 2009
  Messages: 7,847
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  Duuh hii ndefu inashinda Mtambuzi...nitarudi baadae
   
 6. L

  Luluka JF-Expert Member

  #6
  Jul 16, 2012
  Joined: Oct 6, 2011
  Messages: 628
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  Dah!very sad story!!hiyo ndo mitihani ya maisha!
   
 7. mdoe

  mdoe JF-Expert Member

  #7
  Jul 16, 2012
  Joined: Feb 4, 2009
  Messages: 436
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Duuuh! Darasa la ukweli! Thanx!
   
 8. Kimbweka

  Kimbweka JF-Expert Member

  #8
  Jul 16, 2012
  Joined: Jul 16, 2009
  Messages: 8,608
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 145
  Pole sana na inasikitisha sana,
  Piga magoti muombe MUNGU ukiamini, atakupa mume.....
   
 9. vukani

  vukani JF-Expert Member

  #9
  Jul 16, 2012
  Joined: Dec 30, 2009
  Messages: 245
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  Unaweza kusoma hata kesho
   
 10. vukani

  vukani JF-Expert Member

  #10
  Jul 16, 2012
  Joined: Dec 30, 2009
  Messages: 245
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  Inaelimisha kwa kweli hasa kwa sisi vijana
   
 11. BADILI TABIA

  BADILI TABIA JF-Expert Member

  #11
  Jul 16, 2012
  Joined: Jun 13, 2011
  Messages: 30,874
  Likes Received: 6,228
  Trophy Points: 280
  ndo maana inatakiwa kuwa na mipaka kati ya uhusiano/mawasiliano ya mpenzi na mashosti.....
  Wanawake wengi wanalisahau hili....
   
 12. LD

  LD JF-Expert Member

  #12
  Jul 16, 2012
  Joined: Aug 19, 2010
  Messages: 3,021
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Nimejitahidi kusoma mwanzo mpaka mwisho, nimejifunza kitu. Tuwe tunafikiri kabla ya kuamua na kutenda kwa kweli. Mahusiano haya bwana.....khaaaaaaaa
   
 13. Anselm

  Anselm JF-Expert Member

  #13
  Jul 16, 2012
  Joined: Nov 16, 2010
  Messages: 1,705
  Likes Received: 42
  Trophy Points: 145
  Ni ndefu lkn very interesting,jamani haya mambo ni changamoto haswa
   
 14. cacico

  cacico JF-Expert Member

  #14
  Jul 16, 2012
  Joined: Mar 27, 2012
  Messages: 8,392
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  eish, felt like crying! so touching.
   
 15. Crucial Man

  Crucial Man JF-Expert Member

  #15
  Jul 16, 2012
  Joined: Jan 11, 2011
  Messages: 3,277
  Likes Received: 470
  Trophy Points: 180
  Kama ni true story inauma sana.
   
 16. Rose1980

  Rose1980 JF-Expert Member

  #16
  Jul 16, 2012
  Joined: May 10, 2010
  Messages: 5,701
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 0
  zaa wewe
  tafuta mwanaume mkapime mzae ubaki na mtoto sio lazima uolewe
  ukisubiri uolewe ndo uzae utakawia sana thou mungu hapendi kuzaa nje ya ndoa
   
 17. fazaa

  fazaa JF-Expert Member

  #17
  Jul 16, 2012
  Joined: May 20, 2009
  Messages: 2,986
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Aaa kisa hichi kizuri sana yani mpaa nimesoma nakukimaliza.
   
 18. Graph Theory

  Graph Theory JF-Expert Member

  #18
  Jul 16, 2012
  Joined: Jul 2, 2011
  Messages: 3,809
  Likes Received: 1,129
  Trophy Points: 280
  Ujumbe mwanana huu.
   
 19. J

  Jalem JF-Expert Member

  #19
  Jul 16, 2012
  Joined: Nov 29, 2011
  Messages: 218
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  Mimi nachangaia muda huu kwani nimesoma habari yt,
  nashauri post yk isiwe Mungu amekulipia ila Mungu awasamehe, kwanza kwangu nauchukulia mkasa huu kama shule na dira ya maisha, huyu dada Mungu anampenda sana asife moyo atapata mume mwenye upendo wa kweli kabisa, pia haraka haina baraka ina laana na balaa, huyo dada ajipange, na aendelee kumuomba Mungu ampe amani ya kweli na subira itokayo mkononi mwa Mungu mwenyewe,
  Pia kulipiza si sawa, kwake yeye kuwa kimya imemsaidia kwani kama angemfatilia sana labda na yy angeangukia kwenye ukimwi.
  Mungu wangu akubariki dada;Eliza' utapata mwana mwema utakaye pewa na mume mwema.
  Be Blessed
   
 20. TabletFellow

  TabletFellow JF-Expert Member

  #20
  Jul 16, 2012
  Joined: May 17, 2011
  Messages: 928
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  hata kama ni yakutunga bado habari hii ni swnsitive sana

  fundisho kwetu
   
Loading...