RA Achunguzwe!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,462
39,928
Raia Mwema
Lula wa Ndali Mwananzela

Nilikaa pembeni nikisikiliza kwa makini maelezo ya Mbunge wa Igunga Mhe. Rostam Aziz (CCM) akielezea na kufafanua msimamo wake kuhusu hatua ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Tanzania kukana mchango wake na kumruka kufuatia kushiriki kwake kwenye hafla ya uzizundi wa albamu ya kwaya ya “Amkeni” usharika wa Kinondoni. Bw. Rostam alishiriki katika siku kuu hiyo jumapili ile iliyopita ya tarehe sita ambapo yeye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.

Maelezo yake kwa waandishi wa habari yamenifanya niamini kuwa Bw. Rostam anapaswa kuchunguzwa na vyombo vyetu vya usalama ili kuondoa utata wowote wa mambo ambayo anayafanya ambayo kwa kuyaangalia (kama nitakavyoonesha) siyo tu yanaweza kusababisha vurugu isiyo ya lazima, lakini kwa hakika yanachezea utawala wetu wa demokrasia, misingi ya haki, na michakato ya kidemokrasia nchini.

Sitopenda kurudia kile alichosema kwani aliyoyasema siku ile Jumapili na aliyoyarudia jumapili hii kwa waandishi wa habari yote yanaweza kusikika vizuri kwenye tovuti ya http://www.klhnews.com. Hata hivyo yatosha kusema kuwa majibu ya Rostam baada ya KKKT na Mch. Mtikila na wenzake kuanzisha kelele za kutaka arudishe fedha alizotoa pale Kinondoni kumenifanya niamini pasipo shaka kabisa kuwa Bw. Rostam ni mwanasiasa mjanja, mwenye dalili ya vitendo vya rangi ya majivu majivu, na ambaye endapo ataendelea kuonewa haya atakuwa anaweka mchakato wa kisiasa na demokrasia nchini kuwa matatani.

Kwa wale wanaokumbuka Aprili 16 (siku mbili tu baada ya Rostam kumpatia fedha Mtikila) niliandika makala kwenye gazeti hili iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Sipendi Rostam Azizi atikise kiberiti Bungeni”. Wiki ile inayofuata mwandishi mmoja alijitokeza na kumtetea Rostam na kujaribu kuchambua hoja zangu, jaribio ambalo wiki moja baadaye niliweza kulionesha udhaifu wake na mwandishi “wetu” yule kutokomea bila kujibu.

Katika makala hiyo ya kwanza niliandika hivi kuhusu Mhe. Rostam Aziz “Kama wananchi wengine Rostam ana haki ya kujitetea na mahali ambapo anaweza kujitetea pasipo shaka sana ni hapo bungeni kwani huku uraiani haina kinga ya kusema awezacho. Kama kweli Rostam anaamini hakutendewa haki na ya kuwa amebebeshwa mzigo usio kuwa wa kwake kwa yeye kuchutuma na kuendelea kuubeba si tu anajidhihakisha lakini anafanya watu waamini kuwa yaliyosemwa juu yake ni kweli.”

Nikaongeza na kusema hivi, “Rostam ni mwana CCM, hajanyamazishwa wala kukatazwa kusema. Kama hatopewa nafasi bungeni anavyo vyombo vyake vya habari na anao waandishi wake wa kumpamba, awatumie ili siri itoke. Hata hivyo akumbuke kuwa “wewe ukijua hili, wenzio wanajua lile”

Na mwisho nikagongelea msumari kwa kuhitimisha kwa wito huu “Ninampa changamoto asimame aseme, vinginevyo na anyamaze! Kama amezoea kutisha wana CCM wenzake, aendelee kufanya hivyo hivyo lakini asifanye kama walivyofanya mafisadi wa EPA ambao wameliteka Taifa huku sisi wenyewe tukiwa hatuna uwezo wa kufanya lolote. Sitaki Rostam kwa maneno yake na yeye aliteke Taifa, kwani hatuwezi kutekwa mara mbili!”

Baada ya mwandishi yule kunijibu, niliandika makala ya pili ambayo ilikuwa na kichwa cha habari “Rostam: Mtu mzima hatishiwi nyau” na kimsingi niliendeleza nilichoandika kwenye makala ya kwanza. Mwishoni mwa makala hayo nilisema hili lifuatalo “Kwa upande wangu narudia nililosema kama analo lake la kusema na anafikiri ameonewa asimame ajitetee; wenye kutikisika watatikisika na Tanzania haitotishika. Wale walio mabua ya mitete ambao wanatetemeka akikohoa na kukosa pumzi akipita waende kupanga foleni na kumlilia asiseme.
Mimi nasema Rostam anatikisia kiberiti ambacho akikiwasha vitakavyoungua ni yeye na nguo zake na za marafiki zake. Sisi wengine tutakaa pembeni kuwachora wanavyoumana na kutafunana kama mchwa. Kama haamini na asubiri.”

Ndugu zangu Rostam siku ya Jumapili amejaribu kukiwasha kiberiti na walioshtuka kwa mlio wake wameruka pembeni kwa woga. Amejaribu kutikisa na kutuma ujumbe kwa wabaya wake, lakini kama nilivyosema akikiwasha “vitakavyoungua ni yeye na nguo zake na za marafiki zake.” Huu ni wakati wa kuonesha kuwa alichokifanya siku ya jumapili ni kuthibitisha kuwa anayo nguvu ya pekee katika Tanzania, nguvu ambayo inampa aina fulani ya kiburi na uwezo fulani wa kibabe. Kiburi kwamba anauwezo wa kuamuru mvua inyeshe ikanyesha na jua kuwaka likawaka. Tuanze pole pole kumchambua.

Kuitisha waandishi wa habari anaowataka.
Sijui ina ukweli gani habari kuwa Bw. Rostam alitoa mwaliko kwa waandishi anaowataka yeye ndio waende kumsikiliza. Kwamba, vyombo vya habari havikuwa huru kupeleka mwandishi wanayemtaka na badala yake majina yaliyopendekezwa ndiyo walitakiwa kwenda huko. Kwa kuangalia kwa haraka ni baadhi ya wahariri waandamizi ndio walialikwa kwenda kumsikiliza. Binafsi napinga kabisa mtindo wa viongozi kuchagua ni waandishi gani waende kumsikiliza au vyombo gani vya habari viende.

Mtindo huu umetumiwa hata na Rais mwenyewe wakati fulani ambapo anaamua ni waandishi wa vyeo gani waende kumsikiliza. Inasikitisha kuwa waandishi wetu na hasa wahariri wanakubaliana na upuuzi huu. Nimetumia neno upuuzi nikimaanisha hivyo. Jukumu mojawapo la vyombo vya habari na waandishi hasa linapokuja suala la utawala bora ni wao kuwa kiungo cha habari kati ya watawala na watawaliwa. Katika kufanya hivyo vyombo vya habari vinatakiwa kuwa huru kufanya kazi yake pasipo kuingiliwa na watawala.

Mtawala anapokuja na kusema “nina jambo la kusema kwa wananchi, na ningependa x,y waje kunisikiliza na kuwaambia wananchi” mara moja kengele za tahadhari hazina budi kulia. Jukumu la mtawala au kiongozi ni kusema lini, wapi na nani ana la kusema na ni jukumu la waandishi wa habari kuona umuhimu wa kuripoti jambo hilo na kuamua nani anafaa kwenda kusikiliza.

Hivyo, kitendo cha Rostam kuitisha waandishi anaowataka yeye (aidha moja kwa moja au kwa kuashiria chombo kingine) ni kumpa nguvu ambayo haistahili na kwa hakika ni kucompromise suala zima la kuripoti tukio lake. Yeye mwenyewe akiwa ni mmiliki wa vyombo vya habari, ni wazi kuwa ana ushawishi wa aina yake katika vyombo hivyo. Ni vizuri kuanzia sasa vyombo vyetu vya habari (kupitia Baraza la Wahariri au chombo kingine kinachowaunganisha) kuchukua msimamo wa pamoja wa kukataa kugawanywa na watawala na kuhakikisha kuwa wao wanabakia na uamuzi wa mwisho wa nani aende kuripoti kuhusu nini. Kiongozi asiyekubali hilo basi vyombo vyote vimgomee (ukiondoa vile vyake).

Ni kwa misingi gani Rostam alichagua waandishi waliokuja kuripoti habari zake? Je alitumia ushawishi wowote wa ahadi au vitisho kupata waandishi anaowataka yeye?

Rostam na Mtikila
Mojawapo ya mambo ambayo yalifunua sura ya Rostam ni urafiki wake na Mch. Christopher Mtikila. Wengi wetu tumekuwa tukiona mara nyingi jinsi Mch. Mtikila amekuwa akimshambulia Rostam katika mambo mbalimbali. Kumbe kwa mujibu wa Rostam hawa jamaa wawili wanafahamiana kwa ukaribu na urafiki wa kiasi cha kupeana/kukopeshana fedha! Unapofikia mahali unampa mtu fedha lazima kuna kiwango cha kuaminiana na ukaribu. Sidhani kama mtu yeyote ambaye anakutuhumu hadharani akija na kukuomba fedha utampa. Isipokuwa kama na wewe una kitu unakipata toka kwa mtu huyo.

Kwa watu ambao tumekuwa tukifuatilia suala la Rostam na Mtikila kuna baadhi ya matukio ambayo hayana budi kuonesha ni jinsi gani hawa jamaa wawili kama siyo ni wazugaji wa kimataifa basi wote wawili wamekula njama ya kuihadaa Tanzania kwa malengo ya kusaidiana. Nikumbushe matukio machache tu:

Kwanza, tarehe 16/9/2005 Mchg. Mtikila alitoa madai mazito sana kumhusu Rostam na Kikwete. Madai hayo ambayo yalinukuliwa na vyombo mbalimbali hasa wakati wa mchakato wa uchaguzi Mkuu. Katika madai hayo Mch. Mtikila alisema kwamba anazo taarifa kuwa Serikali ya Iran imekuwa ikimtumia Bw. Rostam fedha nyingi ambazo zilitumika katika kampeni ya mgombea wa CCM Bw. Jakaya Kikwete. Mch. Mtikila alisema kuwa Wairan wamekuwa wakimtumia Rostam kwa sababu ya nasaba yake na ya kuwa wana maslahi fulani kama Kikwete angechaguliwa. Madai haya ya Rostam pamoja na uzito wake hayakuchunguzwa na vyombo vyetu vya sheria na usalama.

Sasa kwa watu wengine hili wanaweza wasiwe wameliona. Wiki moja kabla ya mkutano huu na waandishi wa habari (yaani tarehe 9), Kampuni ya Kagoda Agriculture ilisajiliwa na siku iliyofuata (jumamosi) ikawa tayari imepata mikataba mikubwa kutoka Benki Kuu. Je, yawezekana fedha ambazo Mch. Mtikila alikuwa anazizungumzia wiki moja baadaye hazikutoka Irani bali Benki Kuu? Yawezekana kuwa sababu kina Rostam na Kikwete hawakumshtaki Mtikila ni kwa sababu ingejulikana hakuna cha fedha za Irani bali kukombwa kwa fedha toka Benki Kuu?

Pili, Kumbukumbu yangu ni nzuri kwani hayo hayakuwa madai ya pekee dhidi ya Rostam na Kikwete kupokea fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kampeni zake. Mwezi wa Aprili mwaka huo huo gazeti la African Confidential liliandika taarifa kuwa Bw. Rostam alipokea shilingi Bilioni mbili (vijisenti mara mbili!) kutoka Oman kwa ajili ya kampeni zao. Licha ya vitisho vya mgombea wa CCM Bw. Kikwete kuwa atafungua mashtaka dhidi ya gazeti hilo, hakufanya hivyo kwani gazeti hilo lilimuambia atangulie kwenda mahakamani kwani ushahidi upo na ni mkubwa. Siyo Kikwete wala Rostam aliyefungua mashtaka. Kwa maneno mengine walikubali jambo hilo.

Kitendo cha vyombo vyetu vya usalama kutokufuatilia habari nyeti kama hizi au hata kuomba ushirikiano kutoka kwa Mtikila na gazeti la African Confidential kumethibitisha ni kwanini wengine wamekuwa wakipiga kelele juu ya kulega lega kwa usalama wetu wa Taifa.
Kama Kikwete alipokea mabilioni ya shilingi kutoka nje ya nchi ili afanikiwe kuwa Rais, alifanya hivyo kwa misingi gani? Hao waliomtaka aingia kwa “udi na uvumba”, kwa “mbinde na kwa pinde” walikuwa na maslahi gani?

Anaposema yeye msafi, Rostam anajilinganisha na nani, Kikwete?

Tarehe 17 Machi mwaka huu Mch. Mtikila tena akaja na madai mazito juu ya Rostam. Safari hii akagusa eneo nyeti sana nalo linahusu Uraia wa Rostam. Mchg. Mtikila akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake alisema hivi “Licha ya kuwa Bw. Rostam ni rafiki yangu, siwezi kumtetea yeye kuliko nchi yangu? ushahidi wa kuwa yeye sio Mtanzania ninao, maana najua mpaka hospitali aliyozaliwa na mpaka sasa, wazazi wake wako Iran”. Rostam alipoulizwa na mojawapo ya vyombo vya habari siku hiyo hiyo hakukanusha wala kusema lolote isipokuwa kusema “Wanasema mimi siyo raia...asante sana...asante sana”.

Sasa hilo linaweza lisiguse fikra zako ndugu msomaji hadi pale mwezi mmoja baadaye, yaani tarehe 14 Aprili mwaka huu ambapo kwa maelezo ya Rostam ndiyo siku ambayo yeye alimpatia Mch. Mtikila kiasi cha Shs. Milioni 3. Kwanini Rostam alimpatia fedha Mch. Mtikila mtu ambaye amemtuhumu kuwa si raia mwezi mmoja kabla yake? Katika mazungumzo yake juzi alimuelezea Mtikila kwa maneno makali akidai kuwa maneno yake (Mtikila) yamejaa “kinyaa, chuki, ubaguzi, na yananuka ufisadi”. Alipompa milioni 3 alikuwa hajui hayo yote? Au ni kitu gani kilikuwa kinawaunganisha?
Katika haya yote tuliyaona tunaweza kuona kitu kimoja ambacho kwa wale wenye kumbukumbu nzuri watakigundua. Sijui kama umewahi kuiona picha ya “urafiki wenye mashaka”. Katika picha hii wanyama mbalimbali wamechorwa wakiwa kwenye tafrija nyikani, na wanyama ambao ni mahasimu wakiwa karibu karibu, hivyo simba na swala wako pamoja, chui na mbuzi wako pamoja wanasherehekea. Katika hayo yote wote wanaangaliana kwa mashaka kwa maana huwezi kujua ni lini nani atamgeuka nani.

Rostam na Waandishi wa habari.
Mojawapo ya vitu ambavyo vimemfanya Rostam kuonekana ana malengo ambayo yanamfanya aonekana ni mmoja wa watu wenye urafiki wenye mashaka ni jinsi gani amekuwa akihusiana na waandishi wa habari. Kuna madai mengi ambayo ni yeye pekee anaweza kuyathibitisha ya jinsi gani anaweza kumlipa mtu kwa sababu fulani, hata kama mtu huyo ni adui au rafiki yake. Alipoamua kuingia kwenye biashara ya magazeti kuna madai mengi sana ya jinsi gani amekuwa akishawishi uandishi wa magazeti yenye hisa zake hususan kuhusu habari zake.

Kama nilivyoonesha hapo juu jinsi wito wake ulivyotolewa kwa vyombo vya habari kumekuwa kama mtu mwenye ubia wa aina ya pekee. Swali langu kwa Mhe. Aziz ni hili, kama kweli yeye ni mtu msafi kama alivyodai, na kwa vile inaonekana amekuwa akitoa misaada ya fedha kwa watu mbalimbali wakiwamo mahasimu wake; je yuko tayari kutaja majina ya waandishi wa habari ambao amewapa fedha ambazo si mikopo kama fadhila yake na watu hao wameendelea kumuandika vibaya? Kwa maneno mengine, waandishi wanafiki ambao wameandika habari za madai ya ufisadi dhidi yake licha ya kupewa fedha na Bw. Rostam? Je kuna waandishi ambao wamelipwa na Bw. Rostam na ambao hawajawahi kuandika habari zozote mbaya dhidi yake? Tukisema huo unaodaiwa kuwa ni mtindo wake ni ishara ya vitendo vya kifisadi atakataa?

Rostam naUshirika Usio Mtakatifu
Wakati anazungumza na waandishi wa habari aliowaita Bw. Rostam alisema yafuatayo baada ya kutangaza kuwa maneno ya Mtikila ni “kinyaa, yananuka harufu ya chuki, wivu, ubaguzi, unafiki na ufisadi” Bw. Rostam aliendelea na kusema hivi “huu ni mwendelezo tu wa kampeni chafu unaoendeshwa na watu wachache ambao ni maarufu na ni wazito katika jamii yetu waliojiunga pamoja katika ushirika usio mtakatifu. Ambao kwa kutaka kutimiza malengo yao wameamua wanaoyajua wao wenyewe wameamua kuchafua majina, heshima, na hadhi za baadhi yetu.

Katika kikundi hicho wapo ambao hawaridhiki na nafasi za uongozi walizonazo, ambao wamejenga chuki kwa kudhani na kujiaminisha kuwa labda mimi nilihusika kuwazuilia kujichukulia fursa za ufahali na haki inayostahiki vyeo vyao...wapo ambao uwezo wa maarifa yao umewapeleka kutomudu ushindani wa kibiashara na badala yake wamejianimisha labda baadhi yetu ndio sababu ya kutofanikiwa kwao, na wapo ambao wamejiingiza katika kikundi hicho kwa sababu ya wivu. Mawazo yote hayo si sahihi, na yanaelekea kunipa uwezo ambao sina.”

Swali ambalo mimi ninalo kwa Mhe. Rostam na ambalo wenye uwezo wakuchunguza wachunguze ni kuwa Bw. Rostam anawajua hawa watu kiasi kwamba ameweza kujua wako katika makundi gani. Je yuko tayari kuwataja watu hawa ambao yeye amewaita ni “maarufu na wazito katika jamii yetu?” Maana kama hawa watu wapo na wanaendeleza hizi kampeni za kuchafuana naamini Watanzania wangependa kuwajua ni kina nani? Vinginevyo kuna mtu amhoji Bw. Rostam ili tuweze kujua ni kina nani chanzo cha kuchafuana kunakoendelea. Vinginevyo, tutaweza vipi kumuamini Bw. Rostam kwa maneno yake hayo?

Umiliki wake wa Richmond


Kati ya majibu ya kijanja ambayo nimewahi kuyasikia ni pale alipoulizwa kuhusu kuhusishwa kwake na Richmond. Mhe. Aziz hakukana kumiliki au kuhusika katika kumiliki kampuni ya Richmond. Alichofanya Bw. Rostam ni kuelekeza utetezi wake kwenye ripoti ya Kamati Teule ya Mhe. Mwakyembe. Alichosema ni kuwa Kamati Teule haikusema yeye ni mmiliki na hivyo basi ina maana hamiliki au kuhusika katika umiliki wake. Huu ni mtitiririko mbovu wa ujengaji hoja (illogical flow of an argument). Kwa vile Kamati Teule haikusema anamiliki RDC, haina maana hamiliki. Binafsi ningependa kumsikia yeye Rostam akisema kuwa hakuhusika katika umiliki wake na hakuwa na maslahi yoyote yale. Hadi hivi sasa yeye hajakana.

Taifa linahitaji kujua ni nani aliyekuwa mmiliki wa RDC tangu mwanzoni?

Mwisho
Ndugu zangu, naweza kuendelea kusema mengi. Lakini kati ya mambo ambayo yamedhihirika katika jambo hili na ambalo inaonesha ipo haja ya Rostam kuchunguzwa na vyombo husika ni kuwa, kwanza, Uhusiano wake na Mtikila na habari ambazo Mtikila amekuwa akitoa zinaonesha kuwa chanzo kikubwa ni yeye mwenyewe Rostam. Kuna mambo ambayo yamekuwa yakifanywa na kusemwa na Mtikila ambayo kama siyo Rostam chanzo chake basi ni mtu wa karibu wa Rostam. Hilo la pili naliondolea uwezekano mkubwa kwani kama Rostam anataka kuwa mkweli angesema ni mara ngapi nyingine pasipo risiti ambapo amewahi kumpa Mtikila fedha kwa kiwango chochote kile kwa shughuli nyingine? Je amewahi kumlipa Mtikila kuhusiana na kesi zozote ambazo Mtikila amekuwa akifungua aidha dhidi ya serikali au dhidi ya mambo mbalimbali likiwamo mojawapo ya magazeti maarufu nchini?

Hivyo mtu mwenye ujasiri na chombo chenye ujasiri hakina budi kuanzisha uchunguzi kwanza kujua ushiriki wake katika kupata fedha kutoka nje ya nchi wakati wa kampeni za mgombea wa CCM Kikwete mwaka 2005, na vipi kuhusu fedha ambazo imedaiwa na gazeti mashuhuri la African Confidential, fedha za Shs. Bilioni mbili toka Omani kumsaidia Kikwete. Na zaidi ipo haja ya kufanya uchunguzi wa mahusiano ya watu hawa wawili isije kuwa wote wawili wanachotufanyia ni uzugaji wa daraja la kwanza kwani kama wana urafiki basi ni urafiki gani huo na kama ni uadui ni uadui wa aina gani huu.

Vinginevyo hawa wawili yawezekana kuwa ni watu ambao wanaweza kutuletea matatizo makubwa huko mbeleni kama hakuna mtu atakayewafunga breki. Binafsi, simuamini hata mmoja wao kwani nilichoona ni dalili ya unafiki wa mchungaji na mwanasiasa!
 
NI jambo la bahati mbaya sana kwamba, ninalazimika kujenga hoja yangu leo nikianza kwa kumjadili mtu badala ya kuanza na mada au kuzungumzia jambo ninalotaka kuliandikia; Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Kama hiyo haitoshi, jambo baya ni kwamba, nimeingia katika mkumbo wa kumjadili mtu yule yule ambaye ni hivi majuzi tu ametunyoshea kidole Watanzania ambao kwa muda mrefu sasa, tumenaswa katika mtego wa kujadili watu badala ya kujizatiti kwenye hoja za msingi zilizo na tija.

Hata hivyo, kwa sababu ya mwelekeo wa mambo ulivyo kisiasa hapa nchini hivi sasa, nimelazimika kwenda kinyume cha mtazamo huo, na kwa mara nyingine tena, nimeamua kuanzisha mjadala wangu huu leo kwa kumwangalia mtu ambaye kwa sasa amekuwa katikati ya mada za kisiasa.

Huyu si mwingine, bali ni Rostam Abdulrasul Aziz, Mbunge wa Igunga na mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nje ya sifa hizo rasmi za Rostam, huyu bwana yeye ni mmoja wa wana mikakati ya siri na ya wazi ya ushindi wa wagombea mmoja mmoja ndani ya chama hicho tawala kwa miaka mingi sasa.

Nimeamua kumjadili Rostam kwa sababu kadhaa, lakini kubwa ikiwa ni matukio ya kisiasa na kijamii ambayo yametokea hapa nchini katika siku za hivi karibuni, ambayo kwa bahati mbaya au nzuri, yote hayo yanatokea yakizingira jina la mwanasiasa na mfanyabiashara huyo.

Hali ya sasa ya mambo inayozingira jina la Rostam, inatokana na ugeni wake rasmi na matamshi aliyoyatoa wakati alipoalikwa katika Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kinondoni zaidi ya wiki moja iliyopita.

Napenda kuamini kwa dhati kwamba, uamuzi wa Rostam kukubali mwaliko wa kwenda KKKT siku hiyo, na kisha kuzungumza maneno yale mazito kuhusu masuala yanayohusu mmomonyoko wa maadili na akagusia juu juu kuhusu kushamiri kwa tuhuma za ufisadi na aina mpya ya siasa za kuzushia vifo, uchawi wa kisasa, haukuwa ni wa bahati mbaya hata kidogo.

Kama hiyo haitoshi, imani yangu inanifanya niendelee kuamini pia kwamba, uamuzi wa Rostam kuitikia wito wa kwenda kanisani, tena akiwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu ya kwaya ya Amkeni na kisha kutoa hotuba ya namna ile aliyoitoa mbele ya waumini na wanahabari, halikuwa ni tukio la bahati mbaya.

Kwa Rostam ninayemfahamu, tukio zima ukianzia la ugeni rasmi wake, hotuba na matukio yaliyofuata baada ya kazi hiyo, ni mambo ambayo yalikuwa yakitarajiwa.

Hapa inapaswa ieleweke kwamba, Rostam alikubali mwaliko katika kanisa hilo akijua fika kwamba, mmoja wa wazee wa kanisa alilokuwa akienda, alikuwa ni mwana Tabora mwenzake na jemedari wa mapambano yanayowaumiza yeye na wanasiasa wenzake wengine kadhaa, Spika wa Bunge, Samuel Tegeza Sitta.

Kwa hakika Rostam alikwenda pale akijua kwamba hakuwa mgeni katika kanisa lile, kwani ilikuwa ni miaka miwili na ushei imepita tangu alipofika pale akiwa amepewa baraka za kufanya hivyo na Sitta, ambaye zama hizo walikuwa wanasiasa maswahiba wawili wa kundi moja maarufu la mtandao, na wana Tabora waliokuwa na mshikamano wa kipekee katika mkoa wao.

Kwa sababu hiyo basi, Rostam alijua fika kwamba, uamuzi wake wa kwenda kanisani, safari hii akipewa baraka na viongozi na wazee wengine wa kanisa na si Sitta tena, ulikuwa ni ushindi wa kisiasa dhidi ya mwana Tabora mwenzake huyo, ambaye hakuna shaka kwamba, tangu ilipoanza vita dhidi ya ufisadi miezi kadhaa iliyopita, wanasiasa hawa wawili wamevunja upacha wao wa kisiasa.

Kutokana na hilo basi, sitashangazwa nikidokezwa kwamba, Sitta aliposikia Rostam amekuwa mgeni rasmi na akatoa hotuba ile aliyoitoa katika kanisa ambalo yeye ni mzee wa kanisa, alitaharuki.

Kutaharuki kwa Sitta katika suala hili, kunaweza kukawa kulichangiwa na mambo kadha wa kadha. Mosi, miongoni mwa mengi likiwa ni kupigwa kumbo la kisiasa, katika kiota chake mwenyewe na kwa namna ambayo chimbuko la pigo hilo ni yeye mwenyewe.

Upo uwezekano mwingine pia kwamba, Sitta alitaharuki baada ya kubaini kwamba, kanisa analoabudu akiwa mzee wa kanisa, ndilo ambalo Rostam aliligeuza kuwa kituo kikuu cha safari yake ya kuweka sawa mambo, hasa baada ya kukabiliwa na shinikizo zito dhidi yake kwa miezi kadhaa sasa. Ni mapema mno kusema kwa uhakika iwapo alikuwa sahihi kuchukua uamuzi huo au alikosea.

Kwa hakika katika mkumbo huo huo wa taharuki aliyokabiliana nayo Sitta, wanaweza kujumuishwa pia wanaharakati wengine waliojipa dhamana ya kupambana kufa na kupona kuukabili ufisadi.

Kwa watu wa kundi hili, sababu za kutaharuki huko ni za wazi, kwa kuwa ni dhahiri sasa kanisa lilianza kutoa dalili za kuwa mwokozi wa mtu ambaye mwelekeo wa mambo yake katika kipindi cha miezi michache, alishikwa kwa kiwango cha kushindwa kupumua.

Kwa maneno mengine, kitendo hicho cha Rostam kilichopewa majina mengi; ‘kujisafisha', kulitumia kanisa vibaya, kuliangukia kanisa, kukimbilia kanisani, kutapatapa, kuonya, kujisalimisha na mengine, kilionekana dhahiri kuwashtua watu mbalimbali, wakiwamo waumini na viongozi wa KKKT.

Ni kwa sababu hiyo basi, Dayosisi ya Mashariki na Pwani ilijikuta ikikabiliwa kwanza na shinikizo la kisaikolojia, na kisha viongozi wake wakajikuta wakilazimika kupambana na ushawishi na shinikizo lililokuwa likitolewa na waumini wake, ambao tunaelezwa baadhi yao walifikia hatua ya kutishia kuondoka.

Kwa kweli katika hali hii ya sasa ya ushindani mkubwa wa makanisa kati ya hayo yanayoendeshwa kisiasa kama KKKT, dhidi ya yale mapya ya kiroho ya akina mama Gertrude Lwakatare, Askofu Zakary Kakobe, manabii na mitume kama Mwingira, Munuo na wengine wengi, ilikuwa ni dhahiri kwamba uongozi wa KKKT uliingiwa hofu ya kuendelea kumeguka kwa kupoteza waumini na viongozi wake wengine kadhaa. Hili limepuuzwa katika mjadala huu.

Mambo haya ukichanganya na shinikizo wanalokabiliwa nalo wabunge kadhaa hivi sasa, wanaoonekana kushabikia ushabiki au ‘mafisadi', kwa kiwango kikubwa yalichangia kuwatikisa askofu Alex Malasusa na Walutheri wenzake kwa kiwango cha kujikuta wakilazimika kuitisha kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi na kutoa tamko la kukana kutambua kile walichokiita usafi wa Rostam.

Walipoona hilo halitoshi, walikwenda mbele zaidi na kutengua hata uhalali wa mwaliko aliopatiwa mwanasiasa huyo katika kanisa hilo, hata baada ya picha za televisheni kuonyesha waziwazi kuwa wakati akizungumza kwenye hafla hiyo, pembeni mwake alikuwapo mchungaji wa usharika, wazee wa kanisa na wanausharika wengine.

Ushahidi huo wa wazi ndiyo ambao ulilifikisha kanisa hilo katika hatua ya tatu ya kuamua kuwachukulia hatua za chinichini baadhi ya viongozi wa kanisa hilo ambao kwa namna moja au nyingine walionekana kushabikia au kuunga mkono kuwapo kwa Rostam katika hafla ile.

Wakati nikiwa miongoni mwa Watanzania waliokuwa wakitafakari mwenendo mzima wa mambo, kwanza kama Mlutheri kiasilia na kisha mwanahabari, nilikataa kujiingiza moja kwa moja katika mkumbo wa kumshambulia yeyote katika hao, awe ni Rostam, waliomwalika, waumini waliokuwa wakimshangilia kwa bashaha alipokuwa akizungumza au uongozi wa Askofu Malasusa uliotoa tamko zito.

Kabla sijafikia hitimisho la tafakuri yangu, akaibuka Rostam, kwanza akizungumza na gazeti hili kuhusu dhamira yake ya kuitisha mkutano na wanahabari na katika kipindi kisichozidi siku tatu tangu atoe ahadi yake hiyo ambayo hajapata kuifanya kabla, akakutana na wanahabari na kueleza kile alichokuwa amekikusudia.

Naweza nikatamka wazi kwamba, uamuzi wa Rostam kuitisha kikao cha wanahabari akiwa ameandaa tamko rasmi linaloeleza maisha yake binafsi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi mara moja akili yangu ilifunguka na kubaini kwamba, mwanamtandao huyu alikuwa ameanza safari tofauti na ile ambayo watu wengi wamekuwa wakifikiri.

Mara moja nilibaini kwamba, Rostam alikuwa ameanza kujiandaa yeye binafsi, watu wake, mtandao wake na chama chake kuelekea katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Maneno aliyotumia kupitia katika tamko lake hilo, akitamba kwamba yeye ni mtu safi, anafanya biashara halali ndani na nje ya nchi, ana rekodi safi isiyo na mawaaa katika maisha yake ya kijamii na kisiasa, ni sehemu ya mambo ambayo yamenithibitishia pasipo shaka kwamba, mwanasiasa huyu ameanzisha rasmi mapambano mapya ya siku zijazo.

Jeuri yake ya kuwataka wanaharakati walio na ushahidi wa wazi dhidi yake katika tuhuma zote zinazomkabili, ziwe zile za EPA, Richmond au Dowans kuchukua mkondo wa kisheria, ni ushahidi wa wazi kwamba, mwanamtandao huyu alikuwa ameshaanza kupanga majeshi tayari kwa ajili ya safari ya kisiasa ya siku zijazo.

Msuli aliojaribu kuutunisha dhidi ya Mchungaji Mtikila na pengine dhidi ya kile alichokiita ushirika usio mtakatifu (unholy alliance) unaoundwa na kundi la watu maarufu na wazito linalochafua watu, ni ushahidi kwamba tayari mwanasiasa huyo pengine na wengine wa kundi lake, walikuwa na orodha ndefu ya mahasimu wao wa kisiasa na kibiashara wakati huu wanapojipanga katika safari yao ya maisha ya kisiasa ya siku zijazo na hususan mwaka 2010.

Kama hiyo haitoshi, hamaki yake ya kuwa na ubavu japo wa kauli uliomwezesha kuzungumzia suala zima linalohusu mmomonyoko wa maadili katika siasa, jamii na biashara katika wakati huu, anapokabiliwa na tuhuma nzito za ufisadi, ni ushahidi kwamba, dhamira ya kujisafisha ilikuwa ni daraja tu la kujijengea usalama katika safari yake hiyo kisiasa.

Watu wanaokumbuka harakati za Rostam na wenzake wa kundi la mtandao, akina Jakaya Kikwete, Edward Lowassa na wengine zilizomhakikishia Rais wa Zanzibar ushindi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, wanaweza wakawa mashahidi leo, wa namna wanasiasa wa kundi lao wanavyojipanga kwa ajili ya siasa za siku zijazo wakati wenzao ndani ya chama chao na wapinzani wakiwa wamelala.

Kama hiyo haitoshi, mbinu za namna hii hii za kuweka mambo sawa walizotumia Rostam na maswahiba wake wa kisiasa mwaka 2002 na kabla ya hapo mwaka 1997, ndizo ambazo ziliwawezesha kumhakikishia ushindi mwanamtandao mwenzao na kijana wao, Emmanuel Nchimbi ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM).

Watanzania na wadadisi wa mambo ya kisiasa tunapaswa kutambua kuwa, ni staili hizi za kuwa tayari kujitosa kupambana na kukabiliana na tufani nzito ndizo zilizowawezesha Rostam na wanamtandao wenzao kumhalalisha Kikwete kuwa ndiye ‘chaguo la Mungu' wakitumia makanisa, likiwamo KKKT kutimiza malengo yao hayo, ambayo leo hakuna shaka kila mtu anapogeuka nyuma na kusoma alama za nyakati anapigwa butwaa.

Si hivyo tu, ni staili hizi za kuwa tayari kutengeneza maadui kwa gharama za ushindi, ndizo ambazo zilitumiwa na Rostam huyo wa leo na maswahiba wake wa mtandao, kuhalalisha uspika wa Sitta bungeni wakati akikabiliana na wanasiasa wazito wa aina ya Pius Msekwa, marehemu Juma Akukweti na Philip Marmo, ambao wote walikuwa na rekodi nzuri za kuongoza Bunge kuliko chaguo lao.

Wakazi wa Mkoa wa Tabora wanaomfahamu Rostam ni mashahidi kwamba, bwana mkubwa huyu ndiye ambaye mwaka jana tu alishirikiana vyema na Sitta, ambaye leo ni mahasimu kisiasa, kuhakikisha wanapanga na kufanikisha ushindi wa ‘mtu wao' katika nafasi ya uenyekiti wa CCM wa mkoa huo, hata kuwa na uwezo wa kumbwaga mkongwe katika kiti hicho, mzee Juma Nkumba.

Ushahidi huo wa kihistoria, unatuelekeza bayana kwamba, Rostam mtu aliyepata kupachikwa jina la ‘King Maker' na wana CCM wenzake kutokana na harakati zake za chinichini, ameamua kujitokeza hadharani na kutuanzishia safari ya kuelekea 2010 kwa staili mpya. Huko ndiko anakojielekeza yeye na anakotaka nasi twende. Tunapaswa kujipanga sawasawa kujinusuru na ajali ya ‘Chaguo la Mungu'.
 
Last edited:
Mkuu Mwanakijiji,

Hata akichunguzwa tutapata nini?au tutategemea nini?tumeshaona majibu ya uchunguzi mengi na nimechoka,tutafute njia nyingine zaidi ya kuchunguzwa..Uzuguaji wa siku hizi umebdailika na unatumia njia ya kamati tu na kuchunguza..

Kwa maoni yangu wa kwanza kuchunguzwa awe mpiganaji mwenzetu tuliyekuwa na shaka naye,Mchungaji mkopaji asiyekula katika kundi lake,mpenda wafadhali,mfitina na wa kupenda kusifiwa.kuna watu walikuwa na Imani na Mchungaji ila sasa wameanza kumnyoshea kidole.Mie nilishaanza kutomwamini toka kipindi kile 2005

 
Hapa nnachokiona ni kwamba,

Chequebook journalism + Ufisadi = Disaster to the audience.

Inaeleweka kwamba kuna waandishi uchwara Tanzania na hawatafika popote.

Raisi nae kaja na neno jipya la "Makanjanja". Sijui anamaanisha nini labda kwamba hawa makanjanja ni wale wenye kufuata maadili ya uandishi.

Uandishi wa habari kwa baadhi yao umejaa maneno ambayo naomba radhi kuyatumia, "cynicism", "bread and circuses ", "political manipulation", "spinning" na kila "element" ya uandishi huo ni "against the ethics and moral responsibility."

Kuhusu neno "read and circuses" inamaanisha kwamba kuwepo mipango mahsusi na shughuli mbalimbali ambazo zina lengo la kumfanya mwananchi awe na furaha na aone kila kitu kinakwenda sawa kwa minajili ya kumzuia mwananchi huyohuyo asione matatizo au asilalamike kiuwazi kuhusu matatizo hayo.

Lakini kupitia JF watu kama RA kuna siku watasimama na kuangalia alama za nyakati.
 
Hakuna hata mmojawao ataguswa au kufanywa chochote....get over it!
 
maandiko yanasema "ni yupi kati yenu ambaye mwanawe akimuomba mkate yeye atampa jiwe au akimuomba samaki yeye atampa nyoka?"

jamani "hii imekula kwetu" jamaa hawezi kuchunguzwa wala kubugudhiwa kwa sababu analindwa na mkubwa ambaye hawezi kuona swahiba wake anapata rabsha ya aina yoyote...kwa kifupi RA anadeka tu hana wasiwasi
 
Yafaa achunguzwe kwani maneno yake ni hatari kwa usalama wa taifa,haiwezekani mtu kama huyu kutoa tuhuma nzito kama hizo halafu aachwe tuu ni kuhatarisha sana mustakabali wa taifa hili.
 
...mmoja wa wazee wa kanisa alilokuwa akienda, alikuwa ni mwana Tabora mwenzake na jemedari wa mapambano yanayowaumiza yeye na wanasiasa wenzake wengine kadhaa, Spika wa Bunge, Samuel Tegeza Sitta.

...alipofika pale akiwa amepewa baraka za kufanya hivyo na Sitta, ambaye zama hizo walikuwa wanasiasa maswahiba wawili wa kundi moja maarufu la mtandao,

..Rostam huyo wa leo na maswahiba wake wa mtandao, kuhalalisha uspika wa Sitta bungeni wakati akikabiliana na wanasiasa wazito wa aina ya Pius Msekwa, marehemu Juma Akukweti na Philip Marmo, ambao wote walikuwa na rekodi nzuri za kuongoza Bunge kuliko chaguo lao.

Sitta unamchukulia kama Mwanamtandao, Jemedari wa Mapambano au Mtu ambae hakufaa kuwa Spika?
 
Yafaa achunguzwe kwani maneno yake ni hatari kwa usalama wa taifa,haiwezekani mtu kama huyu kutoa tuhuma nzito kama hizo halafu aachwe tuu ni kuhatarisha sana mustakabali wa taifa hili.
Ni wa ngapi wamechunguzwa?Je tumepata majibu gani?
 
Ni wa ngapi wamechunguzwa?Je tumepata majibu gani?

Kwa kuwa maneno yake na ujumbe wake ulikuwa mahususi ni jukumu la usalama wa taifa na vyombo vya dola kumchunguza na kuweka rekodi hizi ziwe sahihi.

Ujumbe wake ni kuwa kila atakayejaribu kumsema ama kumfuatilia ajue ......
 
Kwa kuwa maneno yake na ujumbe wake ulikuwa mahususi ni jukumu la usalama wa taifa na vyombo vya dola kumchunguza na kuweka rekodi hizi ziwe sahihi.

Ujumbe wake ni kuwa kila atakayejaribu kumsema ama kumfuatilia ajue ......
Kwanini tusikubali Yaishe?
 
Raia Mwema
Lula wa Ndali Mwananzela

Mchungaji Mtikila alisema kuwa Wairan wamekuwa wakimtumia Rostam kwa sababu ya nasaba yake na ya kuwa wana maslahi fulani kama Kikwete angechaguliwa. Madai haya ya Mtikila pamoja na uzito wake hayakuchunguzwa na vyombo vyetu vya sheria na usalama.

Kitendo cha vyombo vyetu vya usalama kutokufuatilia habari nyeti kama hizi au hata kuomba ushirikiano kutoka kwa Mtikila kumethibitisha ni kwanini wengine wamekuwa wakipiga kelele juu ya kulega lega kwa Usalama wetu wa Taifa.

Umejuaje?

Huwa Usalama wanatoa ripoti za uchunguzi?
 
Kwanini tusikubali Yaishe?


.... Ukienda dukani leo, ukatoa noti ya shs. 10,000 ukiwa na nia ya kununua kitu cha shs. 4600, halafu muuza duka akakurudishia shs. 2400 tu kama chenji; basi kama ni mwenye kujua haki yako, ni lazima utamwomba akurudishie mapungufu katika hiyo chenji. Na kama atakataa, ni lazima utatumia mbinu zote uzijuazo kuhakikisha chenji yako ambayo ni haki yako inarudishwa.


.... Gembe, kwa maoni yangu, kama Taifa naona na ninakubali kuwa tuko short-changed katika mengi, na kama watu tunaoelewa haki yetu na mapungufu yaliyopo, ni muhimu na wajibu kufatilia haki yetu kwa mbinu zote tujuazo. Tusikubali kukata tamaa hata siku moja, chenji yetu ni lazima irudi hata kama muuza duka anajifanya 'bouncer.'


SteveD.
 
Mafanikio hayaji kwa urahisi. Kukata tamaa kupo, kushindwa kupo na kushinda pia kupo. Yote haya yatakabiliwa na sisi wananchi wenyewe, ni kwa mtiririko upi, upana upi, ujasiri upi huenda ndio swali.

Binafsi yangu kila mchango japo mdogo una nafasi yake. Hizi kelele ndogondogo (japo kwa maoni yangu ni kubwa) zipigwazo humu si haba. Kwanza zinatufanya baadhi yetu tujue hatuko peke yetu kwenye simanzi hili, na pili, linatufanya tujaribu kuweka mawazo yetu pamoja na kuona lipi tunaweza kufanya. Ni kwenye mtandao huu huu ndio mambo mengi yameweza kujitokeza na pia wananchi wengi kujua ukweli wa mambo yanayoisibu nchi yao pendwa na tajiri, bali iliyojaa mafisadi.

Kelele za mwizi si haba, na kuna ushahidi wa kutosha tu kwamba kuna mahali pengi zimefanikiwa ama kumkamata mwizi huyo au kujua nani ni mwizi huyo. Kuna pengine imepelekea hata hao wezi kupigwa na kuuwawa. Hivyo japo ni ndogo au hafifu kelele za hapa jamvini, kwa maoni yangu bado ni muhimu na tusizipuuze. Tukumbuke mwanzo wa moto ni cheche.
 
Hapa nnachokiona ni kwamba,

Raisi nae kaja na neno jipya la "Makanjanja". Sijui anamaanisha nini labda kwamba hawa makanjanja ni wale wenye kufuata maadili ya uandishi.

Mkuu KANJANJA maana yake ni kitu cha kufoji au fake au kitu ambacho siyo cha kweli, waandishi makanjanja inamaanisha waandishi fake.

Ni hayo mkuu
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom