PSRS: Majibu ya Maswali na Hoja za wadau, Desemba 2014/Januari 2015

Status
Not open for further replies.

Maxence Melo

JF Founder
Feb 10, 2006
4,196
13,186
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, inapenda kuwashukuru wadau na wananchi wote waliotuandikia maoni pamoja na kuuliza maswali mbalimbali kwa kipindi chote cha mwezi Juni, Julai na Agosti, 2015.

Tunapenda kuwajulisha wale wote waliotuandikia maoni na maswali na hawajafungua baruapepe (Emails) na kurasa za Facebook wazifungue kwa kuwa kila swali limejibiwa na kutumwa katika anwani husika na baadae kuyaunganisha maswali na maoni yanayofanana na kuyatolea majibu ya jumla kwa faida ya wasomaji wetu wengine ili kuendelea kuelimishana kuhusu masuala ya uendeshaji wa mchakato wa ajira Serikalini.

Swali la 1; Habari Sekretarieti ya Ajira. Mimi ni muhitimu wa chuo mwaka 2013,nataka kujua taratibu za jumla za kujiunga na mfumo mpya wa kutuma maombi kwa njia ya mtandao. Na je, ninaweza kujiunga na mfumo huo mpya kwa sasa katika "recruitment portal". Na je naweza kuomba nafasi za kazi zitakapotangazwa au mpaka nijisajili na mfumo huo mpya kwanza? Ahsanteni.

Jibu: Tunashukuru kwa maswali yako, Sekretarieti ya Ajira imeanzisha utaratibu kwa waombaji wote wa maombi ya kazi kutumia mfumo wa kuwasilisha maombi ya kazi kwa njia ya mtandao katika ‘Recruitment Portal', Unaweza kujiunga na mfumo huu wakati wowote kuanzia sasa maana huwezi kuwasilisha maombi yako ya kazi bila kujiunga na mfumo huo, utaratibu wa kujiunga unapaswa uwe tayari unayo barua pepe kisha fungua portal ya ajira yaani portal.ajira.go.tz ili ujisajili na kuingiza taarifa zako za kitaaluma na nyinginezo. Aidha, unashauriwa kufungua Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz ili kuweza kusoma na kufahamu hatua kwa hatua namna ya kujisajili kwa kuwa maelekezo yametolewa kwa mapana na marefu ili kupata muongozo mzima utakaokuwezesha kutambua namna ya kujisajili katika mfumo huo kwa urahisi.

Swali la 2; Mimi ni muhitimu wa kidato cha nne niko mkoani Arusha nimetafuta ajira kwa muda mrefu na sijafanikiwa, ninaomba kazi ya kufanya usafi katika ofisi zenu ama bungeni dodoma, nikafanye usafi huko ndani naombeni mnisaidie tu kazi.

Jibu: Tunashukuru kwa kuonyesha nia ya kufanya kazi serikalini, kwa kuwa umefika kidato cha nne na hukuendelea zaidi ya hapo tunakushauri ukiona kazi za msaidizi wa ofisi (Office Assistant) imetangazwa katika Halmashauri mbalimbali nchini jaribu kutuma maombi huko ukiambatanisha na barua ya maombi ya kazi, wasifu wako (CV) na nakala ya cheti ya kidato cha nne kwa kuwa kada hiyo inahitaji watu wenye elimu ya kidato cha nne ambacho ndio kiwango cha elimu ulichofikia. Mfano pamoja na majukumu mengine ya kada hiyo ya msaidizi wa ofisi sifa za kuajiriwa kwa muombaji anapaswa kuwa wahiitimu wa kidato cha nne waliofaulu vizuri katika masomo ya Kiingereza, Kiswahili na Hisabati.

Swali la 3; Kwanza napenda kuwapongeza kwa kurahisisha njia ya utumaji maombi ya nafasi za kazi kwa njia ya mtandao. Naomba kufahamishwa iwapo ninakidhi vigezo vyote vya nafasi ya kazi ninaweza kuapply nafasi za kazi kwa vyeti original bila certification ya TCU ambayo imechelewa kutoka. Nina vyeti original A-Level, O-level vya Tanzania isipokuwa cheti cha degree nje ya Tanzania. Nina uhakika mpaka wakati wa mahojiano (interview) hiyo certifcation itakuwa tayari hivyo nitaiwasilisha siku ya mahojiano (interview) kama nitakuwa nimeitwa kwa ajili ya usaili.

Jibu: Tunashukuru kwa pongezi zako, utaratibu kwa mwombaji kazi aliyesoma nje ya nchi lazima vyeti/ cheti chake kipate uthibitisho kutoka mamlaka zinazohusika kama Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Hivyo ni vyema kama ulipeleka cheti chako cha chuo TCU ukasubiri kabla ya kufanya maombi maana hutaweza kuchaguliwa ili kuja kufanya usaili kwa kuwa utakuwa ujatimiza vigezo vya nafasi husika endapo utakuwa huna hiyo barua ya uthibitisho kutoka mamlaka husika. Aidha, unaweza kuanza kuingiza taarifa zako nyinginezo kwenye mfumo wakati ukisubiria cheti chako cha uthibitisho kutoka TCU.

Swali la 4; Kila siku mnatangaza nafasi za kazi, lakini mbona kilimo na mifugo mmetusahau?

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako. Ni kweli kila wakati tunatangaza nafasi mbalimbali za kazi ila ni vyema ukafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira ni chombo kilichokabidhiwa dhamana ya kutangaza na kuendesha mchakato wa ajira Serikalini kwa niaba ya waajiri mbalimbali. Hivyo nafasi za kazi za kilimo na mifugo zitatangazwa na Sekretarieti ya Ajira mara baada ya kupokea vibali vya ajira vya kada hizo na sio kwamba tumewasahau bali mchakato wa ajirs serikalini una taratibu zake.

Swali la 5; Mimi ni muhitimu wa masuala ya Supplies au Procurement je mtatangaza lini nafasi za kazi kwa kada hii?

Jibu: Matangazo ya kazi kwa kada uliyoitaja kwa wiki mbili zilizopiya yalikuwa hewani huenda hujaangalia vizuri katika matangazo yaliyopo, kwa kuwa kuna nafasi za kazi kwa kada hizo za Supplies Assistant na Assistant Procurement Officer ambazo zimetangazwa kwenye portal ya Sekretarieti ya Ajira tangu tarehe 31 Julai, 2015.

Swali la 6; Mimi ni muhitimu wa fani ya plumbing installation bt tangu nianze kuandika maombi ya kazi sijawai kuitwa kwenye usaili jamani watanzania wenzangu naomba msaada wenu ninafanya kibarua apa ndanda kama fundi na mwalimu nilipata cheti cha katika chuo cha ualimu wa ufundi morogoro teacher training collerge nina level iii katika plumbing.

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako. Pole kwa kutuma maombi mara kwa mara na kushindwa kuitwa kwenye usaili. Tatizo la kutokuitwa linategemea mambo mengi huenda barua zako za maombi zilikuwa hazitufikii kutokana na kukosewa anwani, au ulikuwa ukituma nje ya wakati (baada ya kupita deadline) au kutokana na kukosekana kwa baadhi ya nyaraka muhimu katika maombi yako kunaweza kuwa sababu ya kutokuitwa. Mfano katika maombi yako kukikosekana nakala ya cheti ya kidato cha nne, au barua ya maombi ya kazi husika, wasifu wako nk. ila tunapenda kukujulisha kuwa hivi sasa Sekretarieti ya Ajira imeboresha mfumo wa uwasilishaji wa maombi ambapo mwombaji anatakiwa kutuma maombi ya kazi kwa njia ya mtandao baada ya kujisajili na ukishatuma baada ya maombi yako kupokelewa mwombaji anapata ujumbe wa barua pepe kuwa maombi yake yamepokelewa.

Tunashauri kwa mwombaji yeyote kabla ya kutuma maombi kuhakikisha amesoma tangazo la kazi vizuri na kuhakikisha unaambatanisha vyeti vyote vinavyotakiwa na kujitahidi kutuma maombi yako ndani ya muda ulioainishwa kwenye tangazo husika na pia kabla ya kutuma hakikisha kazi unayoomba inaendana na kiwango chako cha elimu ulichosomea.

Swali la 7; Mimi nimehitimu masomo yangu ngazi ya diploma katika chuo kikuu sokoine mwaka huu mwezi wa saba na nina matokeo yangu ya semester tatu maana masomo yangu yalikuwa na semester nne, nimeona matangazo ya ajira je naweza kutuma kwa kutumia matokeo yangu ambayo ninayo naomba msaada dafadhali kwa ufafanuz zaidi.

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako. Ufafanuzi ni kwamba huwezi kutuma maombi ya kazi kwa matokeo uliyonayo ya semester tatu, Ni vyema usubiri umalize masomo yako ndio unaweza kuomba kazi katika Utumishi wa Umma ukiwa tayari umeshapata cheti/vyeti vya taaluma uliyosomea. Maana hatupokei matokeo ya mihula ni cheti cha mwisho kinachoonyesha umehitimu ngazi gani ya taaluma na fani uliyomaliza, kwa kuwa matangazo ya kazi hutoka mara kwa mara ni vyema ukavuta subira ila wakati huo ukajisajili katika Recruitment Portal ya Ajira na kuweka wasifu wako (CV), vyeti vya taaluma za awali ili pindi utakapopata cheti na tangazo la kazi kutolewa unaweka tu barua yako ya maombi ya kazi na cheti.

Swali la 8: Jamani mnatuumiza sana tunatoka familia masikini mnapotuita kwenye usaili halafu ajira hatupati isitoshe tumetoka mbali mikoani nauli kubwa tunafika Dar es Salaam hatuna hata ndugu tunagharamika pesa nyingi tunaumia sana nasi ni watanzania mtujali sana.

Jibu: Hoja yako imepokelewa, lakini tunapenda kukufahamisha kuwa kwa changamoto unayoizungumzia ni kweli na ndio maana Sekretarieti ya Ajira ina utaratibu wa kufanya usaili katika kanda mbalimbali hasa pale tunaapoona waombaji kazi ni wengi ili kuwapunguzia gharama pamoja na kuepusha usumbufu kwa waombaji kazi walioko mbali na Dar es salaam.

Tatizo la waombaji wengi hupenda kutoa anwani ya Dar es Salaam wakiamini wakisema wanatoka Dar es Salaam watapata ajira kwa urahisi ilihali wanaishi mikoani na utaratibu wa kuwapangia vituo vya usaili ni anwani zenu huwa zinatumika kuna wakati unakuta mtu kwao ni Kigoma kwa mfano ila kwenye maombi kaonyesha Dar es Salaam itabidi aje kufanya usaili huku wakati walioonyesha anwani za Kigoma wamefanyia hukohuko au wakati mwingine wamefanyia kanda ya karibu na mkoa husika.

Usaili umekuwa ukifanyika kikanda katika mikoa mbalimbali isipokuwa kwa baadhi ya kada ambazo usaili wake hufanyika makao makuu Dar es salaam. Mfano mzuri ni kada ya Wakaguzi ambao usaili wake wa mchujo uliofanyika mwezi Julai ulifanyika katika kanda saba.Kanda hizo zilikuwa Dar es Salaam (Kwa mikoa ya Mashariki), Mbeya (kwa miko ya Nyanda za juu kusini), Iringa (kwa mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma), Arusha (Kwa mikoa ya Kaskazini), Dodoma (kwa mikoa ya Kanda ya Kati), Mwanza (kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa) na kanda ya saba ilikuwa Tabora kwa mikoa ya kanda ya Magharibi.

Swali la 9: Nilituma maombi ya kazi kwa kada ya afya wizarani nilitaka kujua kama jina langu lipo ili niende kwenye usaili.

Jibu: Kada zinazohusiana na afya hazikutangazwa na Sekretarieti ya Ajira, tunakushauri uende au uwasilishe swali lako wizara husika watakupa majibu sahihi zaidi.

Swali la 10: Mimi nimetuma maombi ya kazi ya cooperative officer grade II ya tar 15/6 na sijaona tukiitwa kwenye interview au wameitwa sijaona? Naomba majibu tafadhali.

Jibu: Usaili kwa ajili ya Maafisa Ushirika na kada nyinginezo zilizokuwepo kwenye tangazo hilo la mwezi Juni mwaka huu waombaji kazi waliotimiza vigezo wanatarajiwa kuitwa kwenye usaili hivi karibuni na majina yao yamewekwa kwenye tovuti ya Sekretarieti ya ajira, hivyo unashauriwa kujenga mtandao wa mawasiliano na wenzio mliomaliza pamoja ili wakiona tangazo hilo waweze kukujulisha na pia kuendelea kutembelea tovuti yetu mara kwa mara ili uweze kuona tangazo hilo la kuitwa kwenye usaili pindi litakapotolewa.

Swali la 11; Habari za kazi poleni na majukumu. Mimi ni mwajiriwa katika wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia na watoto. Niliajiriwa tangu Novemba, 2010. kama Tabibu Msaidizi. Swali langu ni juu ya upandishwaji wa madaraja. kinachoniuma ni kwamba wenzangu wote nilioajiriwa nao tayari wameshapandishwa madaraja tangu mwaka juzi na waliobaki wamepandishwa mwaka jana na walioajiriwa awamu iliyofuata pia wameshapandishwa madaraja. lakini kinachoniuma mie ni kwamba sijapandishwa daraja mpaka sasa. Je, unanisaidiaje katika hili ndugu yangu? Tafadhali naomba msaada wako.

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako. Tunapenda kukufahamisha kuwa suala la upandishwaji madaraja si jukumu la Sekretarieti ya Ajira, jambo hili ni kati ya mwajiri na mwajiriwa, Sekretarieti ya Ajira inahusika na uendeshaji wa mchakato wa ajira serikalini kwa niaba ya waajiri, hivyo ni vizuri kufuatilia swala lako idara ya Utawala na Rasilimali Watu hapo ulipo na kumuuliza Afisa Utumishi anayehusika katika kituo chako cha kazi.

Swali la 12; Mimi ni muhitimu wa masuala ya kilimo na mifugo nimesoma katika chuo kwa kupitia mfumo wa vyeta njombe .Naomba ajira katika utumishi wa umma.

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako, tunapenda kukufahamisha kuwa ajira katika Utumishi wa Umma hutangazwa kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz au portal.ajira.go.tz hivyo tunakushauri utembelee tovuti hiyo mara kwa mara ili ajira zinapotangazwa zinazohusiana na taaluma yako uweze kutuma maombi kwa njia ya mtandao.

Swali la 13; Mimi ni miongoni mwa watu waliofanikiwa kwenye usaili la tangazo la tarehe 18/6/2015, shida yangu niliandika anuani ambayo ilishafungiwa ni anuani ya shule ya msingi ya kijiji chetu, sasa barua ya kuripoti kazini sitaipata, naombeni msaada wenu na hata ikiwezekana niifate huko Dar es salaam. asante.

Jibu: Tunapokungeza kwa kufaulu usaili na kupangiwa kituo cha kazi. Kutokana na changamoto uliyoieleza kwenye swali lako tunakukaribisha ofisi za Sekretarieti ya Ajira ili uweze kupatiwa nakala ya barua yako ila unatakiwa kuja na uthibitisho wa vitambulisho kuonyesha kweli wewe ndiye muhusika wa nafasi hiyo.

Swali la 14; Habari za kazi Sekretarieti ya Ajira. Napenda kujua mimi ambaye nimehitimu chuo muda mrefu, je, naweza kujiunga na mfumo mpya, katika recruitment portal yenu na taratibu zake kwa ujumla zikoje?. Na je, siwezi kuomba nafasi za kazi zitakapotangazwa mpaka nijisajili na mfumo huo mpya? Ahsanteni.

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako. Aidha, tunakupongeza kwa ufahamu wako juu ya kuanzishwa kwa mfumo mpya wa utumaji wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao. Utaratibu wa mfumo huo unapaswa uwe tayari unayo barua pepe kisha fungua portal ya ajira yaani portal.ajira.go.tz ili ujisajili na kuingiza taarifa zako za kitaaluma na nyinginezo. Lakini pia tunakushauri ufungue Tovuti ya Sekretarieti ya ajira ambayo ni www.ajira.go.tz utakuta muongozo wa namna ya kujisajili na mfumo huo umefafanuliwa kwa kirefu hatua kwa hatua.

Swali la 15; Nawapongeza kwa utendaji kazi wenu, angalau sasa mnapunguza Urasimu wa kuajiri, zamani anaeajiriwa ni mwenye refa (wanaita) endeleeni kuboresha utoaji wenu wa huduma maana sasa walau na sisi tusiojua mtu huko serikalini tumeanza kupata kazi kupitia Sekretarieti ya Ajira.

Jibu: Tumezipokea pongezi zako na Sekretarieti ya Ajira inaahidi kuendelea kutatua changamoto na kuboresha uendeshaji wa mchakato wa ajira Serikalini kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu.

Swali la 16; Naomba kuuliza ni kwanini zinapotangazwa nafasi za kazi ni lazima kutoa angalizo kuwa transcript, statement of result havikubaliki? what are the essence of it while others ndo tumemaliza mwaka huu tuna transcript tu kwasababu vyeti havijatoka sasa hamuoni ni wakati wa kuondoa hiki kigezo kwa wanaomaliza mwaka ambao vyeti havijatoka? kwani kuendelea kuviweka ni kuivunja katiba chini ya IBARA YA 22 NA 23 YA CAP 2 RE:2002 OF 1977. naomba majibu juu ya hili. kwani wengine tuna vigezo vya kufanya kazi kwa mfano mie nina diploma ya sheria na GPA ya 4.3 but nimekaa tu mtaani nataka kulitumikia taifa ila kuna masharti magumu.

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako, ni kweli kwamba statement of Results, Testimonials,Partial transcripts and results slips havikubaliwi/haviruhusiwi kwa kuwa nyaraka hizo sio vyeti halisi na zinakuwa hazina matokeo kamili kutoka chuo ambacho mhitimu amesomea. Ni vizuri ukafahamu kuwa mwombaji anapofaulu na kupangiwa kituo cha kazi anapaswa kuripoti kwa mwajiri wake akiwa na vyeti halisi. Ukisoma vizuri ibara ya katiba ya 22(2) utagundua kuwa inasisitiza masharti ya usawa ndio maana kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo tunawataka waombaji wote wa ajira Serikalini wakidhi vigezo vinavyoainishwa katika tangazo husika.


Transcript huwa zinaruhusiwa kwa wale waombaji ambao wamemaliza mwaka huo na vyeti bado havijatoka kwa kuwa tunafahamu kuwa baadhi ya vyuo vyeti halisi hutoka mwaka mmoja baada ya kuhitimu. Ila kwa wahitimu waliomaliza vyuo zaidi ya mwaka mmoja uliopita wanapaswa kuambatanisha vyeti vya elimu ya juu kwa kuwa tayari vyuo wanakuwa wameshatoa vyeti hivyo. Hivyo endapo nawe umemaliza hivi sasa na kuna nafasi ya kazi imetangazwa na una Trascript kwa kuwa cheti hakijatoka unaweza kuwasilisha maombi yako,endapo utakuwa umedanganya kuwa vyeti havijatoka tutakugundua maana tuna utaratibu wa kuwasiliana na mamlaka husika kabla ya kuita waombaji waliofaulu kwenye usaili.

Swali la 17; Mmekuwa mkituambia wasailiwa wanaofanya usaili na kufaulu na kutopangiwa vituo vya kazi kutokana na nafasi za kazi kuwa chache ukilinganisha na waliofaulu huwa wanawekwa kwenye Kanzidata, Sasa swali langu nitawezaje kujua kama jina langu lipo kwenye kanzidata au halipo?

Jibu: Sekretarieti ya Ajira ina utaratibu wa kutunza kanzidata ya wasailiwa waliofanya usaili lakini hawakupangiwa vituo vya kazi kutokana na nafasi kuwa chache. Aidha, wakati nafasi za kazi zinapopatikana kwa kada husika wasailiwa waliohifadhiwa kwenye kanzidata hupangwa kulingana na ufaulu wa alama. Unapaswa kufahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira haina utaratibu wa kuwapa taarifa wasailiwa walioko kwenye kanzidata kwa kuwa ni mali ya Serikali na upangaji unategemea upatikanaji wa nafasi husika na pia Kanzidata inahifadhiwa kwa muda kati ya miazi sita (6) hadi miezi nane kutegemeana na nafasi husika.
Hivyo muda wa kuhifadhiwa ukipita na hakuna nafasi ya kazi iliyojitokeza kanzidata hiyo matumizi yake husitishwa na kuandaliwa mpya baada ya usaili mwingine. Kwa hali hiyo endapo ulikuwa miongoni mwa waliofanya vizuri na kuhifadhiwa na nafasi ya kazi ikajitokeza utapangiwa kituo cha kazi na kujulishwa kuwa umepata fursa ya ajira ufuate barua yako katika anwani uliyokuwa umetoa endapo anwani husika hutumii waweza kufuata nakala ya barua katika ofisi zetu.


Swali la 18; Nashukuru sana ofisi yenu kwa utendaji kazi wake na uwazi katika utendaji wa mchakato wa ajira, nashukuru nilipewa barua ya kupangiwa kituo cha kazi baada ya kukaa wiki mbili bila kufika kwenye anuani yangu ya posta.

Jibu: Tunashukuru kwa pongezi hizo na tunakupongeza kwa kufaulu na kupangiwa kituo cha kazi, tunakutakia utendaji kazi mwema na wenye kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuweza kuleta kuleta tija katika Taifa.

Swali la 19; Jamani nadhani kuna ulazima wa kupunguza miaka ya uzoefu kazini kama kweli tuna nia ya kusaidia vijana tunaotoka vyuoni bila uzoefu kazini, hivi Sekretarieti ya Ajira hamuoni umuhimu wa kafanya hivyo?

Jibu: Tunakushukuru kwa swali lako. Katika Utumishi wa Umma matangazo ya kazi yanayotolewa uzoefu unakuwepo kwa kazi ambazo zinaanzia ngazi ya uandamizi (Senior Position) lakini nafasi nyinginezo za maafisa wa kawaida sifa za kuingilia ni kiwango cha elimu kilichowekwa endapo ni diploma ama shahada ya kwanza kulingana na nafasi ya kazi iliyotangazwa pasipo kuhitajika uzoefu.

Endapo umekuwa ukifuatilia matangazo mengi yanayotolewa na Sekretarieti ya Ajira na kusoma sifa zinazotakiwa kwa kila nafasi ya kazi utapata uelewa mzuri wa haya tunayokueleza. Changamoto hujitokeza pale muhitimu anapomaliza tu chuo na kutaka kuomba nafasi ya juu mfano Afisa Utumishi Mkuu badala ya kuomba Afisa Utumishi daraja II ambayo ndio ngazi ya kuingilia kazini, endapo utaomba ngazi ya juu ni lazima uwe na uzoefu kuanzia miaka mitatu (3) na nafasi nyingine uzoefu huhitajika hadi miaka kumi (10) kulingana na majukumu ya nafasi husika.

Swali la 20; Nyie watu wa Utumishi mimi naomba kuwauliza hivi kweli mtu wa degree anahitajika serikalini, Na kama ndiyo ni kwanini msiache michujo maana it is not fair kabisa kwani Mimi nakaribia miaka 35 ambayo ndo mwisho wa kuomba kazi serikalini. Je, mnataka nife bado naomba kazi au nifanyeje mitihani maana najibu vizuri tuu why sichaguliwi?

Jibu: Tunashukuru kwa swali lako. Ni vyema ukafahamu kuwa kupata kazi serikalini ni hatua ndio maana ina mchakato wake hivyo mchujo nayo ni sehemu ya mchakato husika, na sio kweli kila kada mara zote wanapoitwa kwenye usaili huanza na usaili wa mchujo, Usaili wa mchujo huwa unalazimika kufanyika pale ambapo idadi ya waombaji waliokidhi vigezo vya kazi husika ni wengi kulinganisha na nafasi za kazi zilitongazwa, Ikitokea hali hiyo Sekretarieti ya Ajira hulazimika kufanya usaili wa aina mbili au zaidi Mfano usaili wa mchujo, usaili wa mahojiano na wa vitendo ili kupata idadi ya watu ambayo wataweza kushindania nafasi zilizopo kwa uwiano unaohitajika.

Aidha ni vizuri ukafahamu kuwa kwa mujibu wa sera ya Menejimenti ya Ajira ya mwaka 1998 pamoja na marekebisho yake ya 2008, Ajira katika utumishi wa Umma hupatikana kwa ushindani na sifa.

Unashauriwa kujiandaa vyema kwa ajili ya usaili maana ajira ni chache na kila muhitimu ana sifa kulingana na wewe au kukuzidi hivyo kitakachokupa wewe ajira ni maandalizi yako kwa ujumla. Aidha, ni vyema kutokata tamaa na kuendelea kuomba kazi pindi kazi zinapotangazwa na ni vizuri ukafahamu kuwa mwisho wa kuomba kazi serikalini ni miaka 45 na sio 35 kama ulivyodai.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

24 Agosti, 2015.

Kwa mawasiliano zaidi +255687 624975, facebook page 'Sekretarietiajira', Barua pepe: gcu@ajira.go.tz au kupitia portal ya ajira sehemu iliyoandikwa feedback.
 
Mie huwa nakwazika saana na hili...WALE WALIOAJIRIWA,KUSTAAFU AU KUFUKUZWA KAZ HAWAPASWI OMBA....SASA SIE AMBAO TUMEAJIRIWA NA SERIKALI HAWAONI KUWA WATUNYIMA FURSA ZINGINE??
 
Zile ajira za SSRA ndo zmechinjiwa baharin, interview toka mwez wa saba mpka leo hakuna majibu..
 
Nimejifunza kitu ambacho ckukijua na hata ckujua kama ni muhimu kujua... Asante sana.
 
Mie huwa nakwazika saana na hili...WALE WALIOAJIRIWA,KUSTAAFU AU KUFUKUZWA KAZ HAWAPASWI OMBA....SASA SIE AMBAO TUMEAJIRIWA NA SERIKALI HAWAONI KUWA WATUNYIMA FURSA ZINGINE??

Huoni kuwa ni kuwazibia fursa ambao hawajaajiriwa?
 
1.swali langu kwa PSRS ni kwa nini mchakato wenu wa usahili unachukua muda mrefu sana kuanzia mnapo tangaza mmbaka kuwapangia vituo vya kazi?
 
1.swali langu kwa PSRS ni kwa nini mchakato wenu wa usahili unachukua muda mrefu sana kuanzia mnapo tangaza mmbaka kuwapangia vituo vya kazi?

swali la msingi sana hili,,yani mtu unaomba kazi mpaka majina yakija kutoka ushasahau km uliomba yani
 
Mnaposema hand delivery ya application letters hairuhusiwi mnamaanisha hata hand delivery ya EMS au inakuaje?
msaada please
 
Vipi kuhusu vyuo vikuu vizembe, ambayo, kushindwa kutoka vyeti kwa baadhi ya wahitimu kwa muda husika?? Na je tutor taarifa au introduction letter inatosha!
 
Mimi ni mmoja wa walioomba kazi kwa kupitia mfumo wa elektroniki. Nimeitwa kwenye usaili na wakatuambia kuwa majibu yatatoka baada ya wiki mbili. Ila sasa unaenda wiki ya nne hakuna majibu yoyote.

Naomba ufafanuzi, tafadhali...
 
Status
Not open for further replies.
9 Reactions
Reply
Back
Top Bottom