Profesa Shivji: Umma una haki kuwajua warejesha fedha BoT

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Profesa Shivji: Umma una haki kuwajua warejesha fedha BoT

Aristariko Konga Machi 12, 2008
Raia Mwema

Wiki iliyopita Profesa Issa Shivji alitoa maoni yake kuhusu timu inayochunguza ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na utendaji wake. Pamoja na maswali na majibu, Mwandishi Wetu ARISTARIKO KONGA anapitia sehemu ya wasifu wake pia.

Raia Mwema: Hivi karibuni serikali ilitangaza kwamba zaidi ya shilingi bilioni 50 zilizochukuliwa kwa ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zimerejeshwa. Lakini cha kushangaza majina ya wahusika hayatajwi. Una maoni gani kuhusu suala hili?

Profrsa Shivji: Inashangaza, ingawa tulitarajia. Nionavyo, sisi bado hatujajenga hulka ya kutofautisha kati ya mambo ambayo ni ya binafsi, ya siri, na mambo ambayo ni ya umma, yanayohusu umma kwa jumla yake.

Hizi ni fedha za umma wa Tanzania, si za Serikali wala BoT au za wafadhili. Umma wa Tanzania una haki ya kujua kila kitu, kila hatua, kinachochukuliwa kuwarudishia fedha zao. Sasa, kwa nini, tusiambiwe, nani karudisha, alitumia taratibu gani na njia zipi za kurudishia. Je, alihojiwa? Je, alijieleza jinsi alivyozipata? Je, kwa nini ameamua kuzirudisha? Je, aliandikisha maelezo Polisi? Yaani jambo hili ni siri kwa wenye mali wenyewe? Inanishangaza.

Raia Mwema: Inafahamika kwamba wafanyakazi wa BoT ambao wamebainika kuhusika na fedha hizo za EPA wameachishwa kazi, lakini hawa wanaorejesha fedha hizi huenda wasichukuliwe hatua. Je, unadhani kuna haki ya kisheria inayofuatwa hapa?

Profrsa Shivji: Ni wazi kwamba kila mtu ambaye anashukiwa kuwa mhalifu lazima achukuliwe hatua za kisheria, hasa wale waliobeba dhamana kubwa ya kitaifa.

Kuna mantiki gani machinga kufungwa jela kwa sababu ameiba soda wakati ShaglaBagla wala asihojiwe wakati ameiba mabilioni na baada ya kuiba tena ameenda likizo Dubai?

Raia Mwema: Je, Profesa Shivji unadhani Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Edward Hosea wanafaa kuwamo katika timu ya uchunguzi wa ufisadi wa fedha za EPA?

Profrsa Shivji: Nisingependa kuanza kuchambua watu, na uwezo wao na utaalam wao au kuhoji uamuzi wa Rais wa kuwatuma hawa na si wengine. Busara za Rais na sifa za hao waheshimiwa zitaonekana kama kweli kazi yao itazaa matunda.

Kama shughuli waliyopewa na Rais kwa niaba ya Watanzania haitatekelezwa ipasavyo, basi watakuwa wamejihukumu wenyewe. Isipokuwa niseme tu kwamba sina shaka juu ya utalaamu wao.

Lakini unapotumwa kutekeleza kazi nzito kama hiyo, suala si utaalamu tu; bali unahitaji uadilifu, ukweli, ujasiri na, zaidi ya yote, unahitaji kuwa na uchungu na nchi yako na upendo kwa watu wako.

Kama huna sifa hizi, utaalamu wako, pamoja na digrii zako tatu au nne au rungu lako, hauna maana wala, angalau kwangu, haunitishi wala kunitetemesha.

Raia Mwema: Je, unadhani ni jitihada gani zifanywe ili kuzipata fedha zote shilingi bilioni 133 za EPA zilizoingia katika mifuko ya mafisadi?

Profrsa Shivji: Kwa kweli, jitihada zote lazima zifanywe. Lakini suala si tu kurudisha fedha. Ni tukio lenyewe ambalo linahitaji kuchambuliwa kwa karibu sana.

Suala muhimu la kujiuliza si jinsi gani tutarudisha fedha zetu? Suala ni: Jinsi gani, na kwa nini, fedha hizi zikapokonywa kutoka Hazina ya Nchi? Hakuna mtu alivunja Benki; hakuna mtu au kikundi kilichomshinikiza au kumuua Gavana ili awapatie ufunguo wa strong room.

Sasa, kama fedha hizi zimeibwa na wale wenyewe, au marafiki zao, viongozi tuliochagua, au kuwateua, kushika nyadhifa nzito kama hizi, basi, tuna ugonjwa wa hali ya juu katika mfumo wetu wa kisiasa na uchumi. Tuliangalie hili.

Raia Mwema: Timu inayochunguza ufisadi huo imekuwa na ukimya mkubwa. Unadhani ni kwanini inakuwa hivyo?

Profrsa Shivji: Waelimishwe na umma na Rais mwenyewe kwamba wao hawakutumwa na Rais; wao wametumwa na Umma kupitia Rais. Kwa hivyo hawana budi wawajibike kwa umma; wawe wazi kwa umma. Hili si hiari yao; kuwa uwazi kwa umma ni jukumu lao. Kama wanashindwa kwa sababu ya woga, au kwa sababu ya kushinikizwa, basi wamekwisha kupoteza sifa yao muhimu ya kuteuliwa kufanya kazi hiyo. Waachie ngazi...

Raia Mwema: Hivi majina ya wahusika na kampuni zao vikitolewa hadharani pamoja na kiasi cha fedha ambacho kila moja alikichukua na kiasi alichorejesha kutakuwa na mgogoro wa kisheria? Unapendekeza njia gani zifuatwe?

Profrsa Shivji: Kila siku ya Mungu magazeti yanachapisha habari za watu wanaopelekwa mahakamani na wanatajwa hadharani; kesi zao zinasikilizwa hadharani.

Sasa wizi wa kitaifa ndio uwe siri, ili kumlinda nani? Isipokuwa wasihukumiwe kisirisiri. Wapewe haki zao zote za kijitetea na umma pia upewe haki yao ya kusikiliza na kudadisi utetezi wao hadharani.

Raia Mwema: Je, suala la wahusika kuwajibika kulipa fidia linawezekana au adhabu gani inaweza kufaa dhidi yao?

Profrsa Shivji: Ah, ndugu yangu, hata mtoto wa shule ya msingi atakuambia kwamba mwizi lazima aadhibiwe hata kama amerudisha mali aliyoiba.

Raia Mwema: Wengine wanapendekeza kuwa wahusika na kampuni zao wakijulikana basi wananchi wanaweza kuchangia kutoa taarifa za wahusika. Una maoni gani kuhusu hilo?

Profrsa Shivji: Wananchi wakichangia au wasichangie, hilo si hoja. Wezi wa mali zetu wajulikane ili tutambue kwamba tumefanya makosa makubwa kwa kuwapatia watu kama hawa dhamana kubwa za kusimamia hazina ya nchi yetu. Hii itatusaidia, sisi wenyewe umma wa Tanzania kujikosoa. Itatusaidia kujielimisha kwamba kama hatuchagui viongozi waadilifu hatutawapata wateule wao waadilifu.

Raia Mwema: Una maoni gani mengine Profesa?

Profrsa Shivji: Nimetoa maoni ya kutosha. Nawasubiri wananchi wenzangu waseme
 
Siku zote nilikuwa ninadhani kwamba pengine "kama walioiba fedha Bot watazirudisha basi hiyo poa tu na nikawa najiconvice kwamba hiyo ndo busara kwa sababu lengo ni chetu kirudi kwanza " lakini baada ya kusoma maelezo ya shivji hapo juu naona nimeanza kuwa conviced kwamba watajwe majina na sheria ichukue mkondo wake, na hii ni kwa faida ya wananchi wenyewe ili kwamba siku nyingine hawa watu wakiomba kura Wasipewe au wakiteuliwa kushika dhamana yoyote wananchi wawakatae kwa sababu siyo watu waaminifu.
 
Siku zote nilikuwa ninadhani kwamba pengine "kama walioiba fedha Bot watazirudisha basi hiyo poa tu na nikawa najiconvice kwamba hiyo ndo busara kwa sababu lengo ni chetu kirudi kwanza " lakini baada ya kusoma maelezo ya shivji hapo juu naona nimeanza kuwa conviced kwamba watajwe majina na sheria ichukue mkondo wake, na hii ni kwa faida ya wananchi wenyewe ili kwamba siku nyingine hawa watu wakiomba kura Wasipewe au wakiteuliwa kushika dhamana yoyote wananchi wawakatae kwa sababu siyo watu waaminifu.

Hapa ni kuwa pesa zirudi na wao washitakiwe... Mbona kitu rahisi sana hiki kwa Kikwete na Mwanyika kuelewa?
 
Back
Top Bottom