Prof Ndulu asema amepania kurejesha imani ya umma kwa BoT

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,791
288,003
Posted Date::3/6/2008
Prof Ndulu asema amepania kurejesha imani ya umma kwa BoT

Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi

WATANZANIA wameanza kupata matumaini kuona mabilioni yao yaliyoibwa katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), yanarudi.

Tayari Sh50 bilioni kati ya zaidi ya Sh133 bilioni ambazo ziliibwa na mafisadi, zimeanza kurejeshwa, hii inatia moyo, lakini jambo moja kubwa hadi sasa bado linabaki kuhusu hatma ya taswira ya BoT kwa umma.

Ni dhahiri taswira ya BoT, imechafuka kutokana na tuhuma hizo za EPA na nyingine kuhusu ufisadi ikiwemo ujenzi wa majengo pacha ya ghorofa 18 ya benki hiyo.

BoT ambayo ni taasisi nyeti na iliyokuwa na heshima kubwa, katika kipindi cha uongozi wa Gavana Daud Ballali, imekuwa na ikitajwa tajwa katika ufisadi.

Ukitaja BoT kwa sasa akili na fikra za Watanzania walio wengi, zinagonga kwamba ni kichaka cha ufisadi nchini huku ikishindwa kusimamia mambo ya msingi kama kudhibiti uchumi na kuangalia ukuaji wake.

Tuhuma hizo za ufisadi katika EPA na majengo pacha ambazo hadi sasa gharama zake ni tata, zinaonyesha kazi kubwa iliyopo kwa Profesa Benno Ndulu, ambaye ni Gavana aliyechukua nafasi ya Ballali, ambaye hadi sasa aliko ni kitendawili.

Hata hivyo, Profesa Ndulu mtu ambaye anaonekana kuwa makini na muwazi na mfano bora wa kuigwa katika kuzingatia utawala bora wa utoaji taarifa muhimu, kwa wakati na asiye mrasimu, anakiri changamoto hiyo akisema taswira ya BoT imechafuka.

Profesa Ndulu, Gavana ambaye anaonekana kuifungua BoT na kuitoa katika kile kinachoonekana kama moja ya 'zoo', anasema jambo kubwa ni kuhakikisha taswira njema na imani ya wananchi kwa BoT, inarudi.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya siku chache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo mapema Januari, Profesa Ndulu anasema BoT itarejesha heshima yake.

Ndulu ambaye aliingia katika nafasi hiyo baada ya Rais Jakaya Kikwete, kusitisha uteuzi wa Ballali katika nafasi hiyo, anasema BoT ni taasisi ya umma hivyo lazima umma ujenge imani nayo.

"Jambo kubwa ni kuhakikisha imani na taswira ya BoT kwa umma inarejea, nitahakikisha hilo linafanyika," anasema Ndulu.

Kwa msisitizo, Profesa Ndulu anasema njia ya kurejesha hali hiyo ni kuendesha benki kwa uwazi bila kuficha mambo.

Anasema kuendesha benki huku mambo mengi yakifanyika kwa siri, kunachangia mianya ya rushwa na ufisadi katika benki.

"Kila kitu kitaendeshwa kwa uwazi, hakuna jambo litakalofichwa, kuficha mambo wakati mwingine kunachangia mianya ya rushwa na ufisadi," anasema Profesa Ndulu.

Anasema jambo analo amini ni kwamba kuendesha taasisi kubwa kama hiyo kwa siri kunachangia kuwepo mianya ya rushwa.

Profesa Ndulu anasema kwa msisitizo kwamba katika kuonyesha uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa BoT, atakuwa na mikutano na waandishi wa habari kila baada ya miezi mitatu.

"Tutakuwa tukifanya mikutano na waandishi mara kwa mara ili kuondoa utata, hivyo mtapata fursa ya kuuliza maswali mengi tu," anasema.

Kuhusu namna BoT itakavyosaidia kurejesha fedha za umma zilizoibwa katika EPA, anasema chini ya uongozi wake atatoa taarifa zote muhimu kuhusu makampuni na watu ambao walionekana kujipatia fedha hizo.

"Lakini si unajua hili liko chini ya Kamati ya Rais, sisi tunachofanya ni kutoa taarifa zote kwa kamati hiyo," anasema Profesa Ndulu na kuongeza:

"Kujua ni kiasi gani cha fedha kimerejeshwa hadi sasa, ni suala la Task Force ya Rais, (Timu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete), wao wanajua ndiyo wanachunguza na kuchukua hatua za kisheria."

Kuhusu Richmond na mapendekezo ya Kamati ya Bunge kutaka BoT ichunguze jinsi Sh 5bilioni za ziada zilivyoplipwa katika mkataba wa Richmond/Dowans, anasema hilo litafanyiwa kazi bila woga na mapandekezo yatapelekwa kwa Tume ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Anasema baada ya bodi kukaa na kufanya maamuzi taarifa husika zitapelekwa katika mtiririko husika ambao ni Tume hiyo ya Waziri Mkuu.

Kamati ya Bunge katika mapendekezo yake ambayo yameridhiwa na bunge, limemtaka Gavana na Bodi ya Benki hiyo ichunguze jinsi fedha hizo Sh5 bilioni zilivyolipwa nje ya utaratibu.

Pendekezo hilo la Kamati ya Bunge, lipo bayana kwamba taratibu za malipo ya madai ya mkataba wa umeme wa dharura zilifanywa kupitia Barua ya Dhamana ya Benki ya dola za Marekani 30,696,598 milioni iliyofunguliwa kati ya Tanesco na Benki ya CRDB Desemba 27, 2006.

Kamati hiyo ilithibitisha kwamba, hadi kufikia Juni 19, 2007 malipo yaliyolipwa na BoT yalifikia dola za Marekani 35,561,598 kiasi ambacho ni zaidi ya Barua ya Dhamana ya Benki kwa dola 4,565,000 milioni (Sh5.7 bilioni).

Hiyo ilitia shaka kwamba ni kwa vipi BoT iliidhinisha malipo hayo nje ya Barua ya Dhamana ya Benki iliyofunguliwa kati ya Tanesco, CRDB na Dowans Holdings S.A?

Kutokana na hali hiyo, kamati ilipendekeza kuwa Gavana wa Benki Kuu pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wachunguze kwa makini uhalali wa malipo hayo na kuhakikisha kwamba udhaifu wa namna hiyo hautokei tena. Profesa Ndulu anasema hakuna kitu kitakachofichwa kila kuhusu fedha hizo.

Kuhusu mabadiliko ya wakurugenzi ambayo ameyafanya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kumng'oa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DPA) Amatus Liyumba, anasema yamekuwa na lengo la kuleta tija ndani ya BoT. Liyumba ni mmoja wa vigogo wa BoT ambaye alikuwa maarufu katika uongozi wa Gavana Ballali.

Anasema mabadiliko hayo yamegusa matawi yote ya BoT isipokuwa Mwanza na pia yamegusa baadhi ya kurugenzi za Makao Makuu.

Profesa Ndulu anasisitiza kwamba, lengo la mabadiliko hayo ni kuwapandisha vijana wenye uwezo ambao walikuwa chini. Gavana huyo anasema vijana wanapaswa kupandishwa vyeo kama wanafanyakazi kwa bidii.

Akisisitiza hilo, anasema amelenga kuleta uwiano wa rika katika utendaji ndani ya BoT ili kuongeza tija.

Miongoni mwa mambo ambayo Profesa Ndulu, amekwishafanya hadi sasa ni pamoja na kupangua safu ya wakurugenzi na kung'oa vigogo ambao walitamba wakati wa Ballali kutoka matawi yote, isipokuwa Mwanza.

Huo ndio masimamo wa Gavana Profesa Ndulu, swali ni je, ataweza?
 
Ndulu alikuwa board member wakati mipesa inatoka, I dont expect anything from him...
 
Masatu unakumbuka baadhi ya member humu JF walimshabikia sana Ndulu....Mbona hukuweka hii kauli mapema soon after uteuzi wake? au sikuiona?...

Kimsingi as long as Mafisadi NETWORK yao ni Kali, basi kazi tunayo...ILA TUSICHOKE KUPAMBANA NAO HAWA MAFISADI CLUB...
 
Yaani kama mnafanana mawazo, lakini sawa tu..
Nilijiuliza huyu naye mnamwita mwandishi wa habari au... ama kweli uandshi basi shughuli..!

Huu ni wakati wa habari za namna hii kweli tena huku basi... waandike hukohuko kwao...chcheem

Ndulu ni kampuni hiyohiyo... hana lolote jipya..!
 
Hivi nyie waandishi wa habari, saa nyingine muwe makini
nani kakwambia kwamba watanzania wamepata matumiaini kuhusu EPA wakati unaona wanatufanya kama wajinga

Pili una uhakika kuwa Bilion 50 zimerudishwa? Je unaweza kuweka evidence ya kurudishwa kwa hizo pesa!!

Mafisadi ndo wana imani, ila Watanzania bado hata kidogo hatuna imani na tume yenye mafisadi kama Mwanyika Hosea. Hawa ni Wezi wakubwa na ni waongo, kwahiyo kulidanganya Taifa kwao ni kawaida, kwani wamekuwa wakisema uongo mara kibao tu na Mabosi wao (Mafisadi pia) wanakubali tu
Hivyo usishangae huu ni uongo wa kuendela kuzitafuna kijanja

Hatuna imani hata kidogo, tusisemeane bila kuwa na vigezo vya kutosha, kwa sababu watanzania wengi wamelalamikia hiyo kauli ya huyo Fisadi Mkullo

Ahsante sana Baba H. Mpaka sasa hivi hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kama pesa hizi bilioni 50 zimepokelewa. Tumeomba majina ya waliorudisha na kiasi walichorudisha lakini hadi hii leo bado ni siri kali, pia tumeomba kujua je, pesa hizo zililipwa kwa cash, cheque, money order or bank to bank transfer n.k. lakini hili nalo pia bado ni siri kali. Tumeomba pia kujua bank account number na jina la bank ambako fedha hizi zimehifadhiwa ili tupate ushahidi toka benki hiyo kwamba wamepokea kiasi hicho cha bilioni 50 lakini hili nalo ni siri kali! Waandishi kuweni makini mnapoandika habari hasa hizi za ufisadi.
 
Back
Top Bottom