Prof Mwakyusa awaponza watumishi Mbeya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Prof Mwakyusa awaponza watumishi Mbeya

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, Jan 29, 2010.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Jan 29, 2010
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,606
  Likes Received: 5,781
  Trophy Points: 280
  [​IMG]Ni wale waliofichua kero zao kwake
  [​IMG]Mkurugenzi awataka wajieleze

  HOFU imetanda kwa baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela waliotoa kero zao kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Prof David Mwakyusa alipotembelea hospitali hiyo mapema mwezi huu.

  Ni wazi sasa kwamba ziara hiyo ya Prof. Mwakyusa wilayani Kyela, Januari 4, mwaka huu, imewaweka katika wakati mgumu baadhi ya wafanyakazi wake kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo pamoja na mkoa dhidi yao.

  Ziara ya Prof Mwakyusa wilayani humo inaonekana ilikuwa mahsusi kwa ajili ya kujionea hali halisi ya Hospitali ya Wilaya hiyo yenye kukabiliwa na matatizo makubwa katika utoaji huduma, na alipofika hospitalini hapo alipata fursa ya kuzungumza na kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi na uongozi wa hospitali hiyo.

  [​IMG]
  Prof David Mwakyusa

  Lakini katika hali ya kushangaza, mara baada ya Waziri huyo kuondoka wilayani humo, baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo walijikuta katika wakati mgumu na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na hatua yao ya kumweleza waziri wao kuhusu kero mbalimbali zinazowakabili hospitalini hapo.

  Baadhi ya wafanyakazi hao tayari wameandikiwa barua wakitakiwa wajieleze kutokana na hatua yao ya kuwasilisha kero zao kwa waziri, na siku chache baadaye wakaandikiwa barua za kuwahamisha kwenda wilaya zingine mkoani humo.

  Taarifa za ndani ya mkutano wa Waziri Mwakyusa na wafanyakazi pamoja na uongozi wa hospitali hiyo, zinabainisha kuwa hatua ya wafanyakazi hao kuwasilisha kero zao, tofauti na zile alizosomewa na uongozi wa hospitali hiyo, ilitokana na waziri mwenyewe kutoa fursa kwa wafanyakazi kuuliza maswali pamoja na kutoa kero zao.

  Miongoni mwa kero zilizowasilishwa na wafanyakazi baada ya kupewa nafasi hiyo na Waziri ni pamoja na uongozi wa hospitali hiyo kuongoza kwa ubaguzi wakitoa mfano wa nafasi za watumishi kuhudhuria semina mbalimbali kwamba hutolewa kwa upendeleo.

  Wafanyakazi hao vile vile waliwasilisha kilio chao cha siku nyingi kwa watumishi kutolipwa pesa zao za saa za ziada na likizo, kutolipwa posho za sare, upungufu wa watumishi, vifaa pamoja na madawa katika hospitali hiyo.

  Mmoja wa viongozi hospitalini hapo, ambaye hata hivyo aliomba kutotajwa jina lake gazetini, anabainisha kuwa kuanikwa kwa kero hizo kulikofanywa na wafanyakazi hao hakukuwafurahisha wakubwa kutokana na ukweli kwamba takribani asilimia 70 ya kero hizo zinasababishwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

  Kwa miaka kadhaa sasa hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na kero nyingi ambazo zimechangia kuzorota kwa huduma za afya wilayani humo na kuwalazimisha wananchi kukimbilia Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana.

  Miongoni mwa wafanyakazi walioumia kutokana na ziara hiyo ya Waziri Mwakyusa ni pamoja na Afisa Muuguzi, Maxmin Ngelesha kutokana na hatua yake ya kumsomea waziri kero zao siku hiyo walizoziorodhesha kwa maandishi.

  Tayari Afisa Muuguzi huyo amepewa barua inayomtaka kujieleza ndani ya siku 14 kutokana na hatua yake ya kusoma taarifa kwa waziri wakati uongozi wa hospitali, kupitia mganga mkuu wa hospitali, ulikuwa umesoma na kuwasilisha taarifa nyingine kwa waziri huyo.

  Katika barua yake kwenda kwa mmoja wa wafanyakazi hao yenye kumbukumbu namba KDC/CM/1.VOL.111/5 ya Januari 8, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mhando Senyagwa anabainisha kuwa kitendo cha wafanyakazi hao ni uvunjaji wa protoko, kuwasilisha taarifa ya kero kwa waziri tofauti na ile iliyowasilishwa na uongozi wa hospitali.

  Ni katika barua hiyo ambapo Mkurugenzi Mtendaji huyo anamwagiza mfanyakazi huyo kuwasilisha utetezi wake kwa maandishi kwa nini hatua kali za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, zisichukuliwe dhidi yake kwa kutokuwa ‘mwadilifu’ kwa viongozi wake wa kazi.

  Sehemu ya barua ya Mkurugenzi Mtendaji huyo inasomeka hivi:
  “Nimesikitishwa sana kupata taarifa ikihusu wewe kama mtumishi wa umma kukosa maadili ya kiutumishi mahali pa kazi. Ushahidi wa kimaandishi nilionao ni kwamba Waziri wa Afya Mh. David Mwakyusa tarehe 04/01/2010 alipofanya ziara hapa wilayani na kufanya mazungumzo na uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela na watumishi wa idara kwa ujumla.

  “Aidha, katika mazungumzo hayo, uongozi wa Hospitali ulisoma taarifa kwa Waziri ikihusu uendeshaji na utoaji wa huduma ya afya wilayani. Baada ya taarifa hiyo kusomwa wewe binafsi ulimwomba Waziri akuruhusu umsomee taarifa tofauti na ile iliyoandaliwa kiidara ukidai kuwa taarifa hiyo ilikuwa imeandaliwa na watumishi wa hospitali na kwamba ulimwomba Waziri kumsomea kwa niaba ya watumishi wenzio.”
  Barua hiyo (nakala tunayo) inaeleza kuwa kitendo cha kumsomea waziri taarifa nyingine tofauti na ile ya idara imesababisha madhara ambayo ni pamoja na kuonyesha dharau kwa mkuu wake wa idara na mwajiri wake kwa kutoa taarifa kwa kiongozi wa kitaifa bila kupata kibali.

  Mkurugenzi huyo katika barua yake hiyo anayaorodhesha madhara mengine kuwa ni pamoja na kusababisha taarifa hizo mbili kuwa na migongano; kwani imeonyesha kuwa na lengo la kuchonganisha uongozi wa hospitali na mwajiri kwa waziri na pia imewagawa watumishi wa idara ya afya katika makundi mawili na kusababisha hali ya mtafaruku wa mgongano kifikra na kiutendaji.
  Senyagwa anahitimisha barua yake kwa kuagiza:
  “Kutokana na maelezo hayo hapo juu, nakutaka utoe maelezo ya kimaandishi kwa nini hatua kali za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, zisichukuliwe dhidi yako kwa kutokuwa mwadilifu kwa viongozi wako wa kazi kiasi cha kusababisha hali ya kukosekana kwa amani katika eneo la kazi.”
  Lakini ndani ya siku kumi tangu kutakiwa kujieleza, uongozi wa Mkoa wa Mbeya ukamhamisha Afisa Muuguzi huyo, Ngelesha kupitia barua kumb. Na. DC.251/277/011/25 ya Januari 18, 2010 iliyosainiwa na Moses Chitama kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya.

  Sehemu ya utangulizi wa barua hiyo inasomeka:
  “Ninapenda kukufahamisha kuwa chini ya kanuni za utumishi wa umma, Tangazo la Serikali Na. 168 la mwaka 2003, ikisomeka pamoja na barua kumb. Na. C/CB.271/431/01/J/144 ya tarehe 27 Agosti, 2007, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya ameamua uhamishiwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mkoa wa Mbeya.”
  Kwa mujibu wa Chitama, barua hiyo ya uhamisho inafuta barua nyingine ya Januari 4, 2010 yenye kumb. Na DC.251/227/01/119 ambayo haieleweki kama ni ile ya Mkurugenzi au ni nyingine.

  Kinachotatiza zaidi wafuatiliaji wa masuala ya wilaya hiyo ni hatua ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwabana watumishi hao ambao walitumia haki yao ya kikatiba kufichua uozo uliopo hospitalini hapo pamoja na uongozi mzima wa halmashauri ya wilaya hiyo.

  Ushahidi wa mazingira unathibitisha uongozi wa wilaya hiyo pamoja na mkoa kutoikubali ziara ya Waziri Mwakyusa hospitalini hapo kutokana na ukweli kuwa ilitawaliwa na mizengwe.

  Miongoni mwa mazingira yenye utata yaliyoigubika ziara hiyo ni hatua ya viongozi wa Halmashauri hiyo kutoambatana na waziri kuitembelea hospitali hiyo huku Mkurugenzi akidaiwa kutoa udhuru wa kuitwa na Mkuu wa Mkoa.

  Mbali ya kumkwepa Waziri, hata pale Mkurugenzi huyo alipotakiwa na Mbunge wa Jimbo la Kyela, Dk Harrison Mwakyembe waende pamoja kusikiliza matatizo yanayowakabili wafanyakazi wake hospitalini hapo kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi, alikwepa akisingizia kuwemo kwenye ziara ya kuhimiza Kilimo Kwanza.

  Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na Raia Mwema wanahoji sababu za Mkurugenzi huyo kukwepa kuwasikiliza wakati matatizo mengi yanasababishwa na ofisi yake, pamoja na mantiki ya kutosikiliza matatizo ya hospitali ambayo ni ya kiutendaji zaidi kwake kwa kisingizio cha ziara ambayo ni ya kisiasa zaidi.

  Prof Mwakyusa sio waziri pekee aliyeonja joto ya jiwe kwa kutembelea wilaya hiyo ya Kyela. Wapo pia Prof Mark Mwandosya ambaye alizuiwa kuendesha harambee aliyoalikwa na kikundi cha kina mama wauza mchele mjini Kyela; hatua iliyowaingiza kina mama hao kwenye hasara kubwa ya zaidi ya shilingi milioni mbili ambayo hadi leo hawajafidiwa na uongozi wa wilaya hiyo uliozuia harambee yao.

  Waziri mwingine ni wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliyetembelea wilaya mwaka jana kwa ajili ya kuonana na wafanyakazi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira kwa lengo la kuwaelezea kuhusu ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwa yakiwakabili pamoja na mgodi wenyewe.

  Wote, Waziri Ngeleja na Mwakyusa walijikuta wakiishia kuwa wageni wa Mbunge wa jimbo hilo, Dk Mwakyembe huku viongozi wa wilaya kila mmoja akitoa udhuru wake kuwakwepa.
   
Loading...