13 January 2010
Mimi ni m-Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa.
Sizuiwi na yeyote au chama chochote katika kutoa hoja na misimamo yangu. Wala sina sababu ya kumbembeleza au kumwogopa yeyote. Siwanii cheo kutoka kwa chama chochote, kwani si mwanachama na sitaki uanachama.
Kwa hali inavyokwenda, namwona Rais Kikwete ndiye amekomaa kisiasa kuliko wengi, na anafaa kuendelea kuwa rais.
JK Anajiamini, anatoa fursa kwa wapinzani
Profesa Joseph L. Mbele
BAADA ya makala yangu ya wiki iliyopita, kuhusu safari za Rais Kikwete nchi za Nje, ambayo imezua mjadala mkubwa, nimeamua kuongelea suala la Rais Kikwete na wapinzani. Nimeamua kuongelea suala hili kwa vile Rais Kikwete ameleta picha tofauti na ilivyozoeleka katika miaka ya karibuni Tanzania, chini ya utawala wa CCM.
Ninavyokumbuka, suala la uhusiano wa Rais Kikwete na wapinzani lilijitokeza kwa namna ya pekee siku Kikwete alipoapishwa kuwa rais wa Tanzania.
Sikuwepo uwanjani, lakini nilipata taarifa katika mitandao ya mawasiliano. Kitu cha pekee ni namna Kikwete alivyowaongelea wapinzani katika hotuba yake, baada ya yeye kuibuka mshindi katika kampeni ya kugombea urais. Aliwashukuru wapinzani kwa changamoto waliyotoa katika kampeni za uchaguzi, akisema kuwa changamoto yao iliiboresha kampeni.
Kauli hii ilinigusa. Kwanza, haikuwa tabia ya CCM kuutambua mchango wa wapinzani. Hatua aliyochukua Kikwete siku hiyo ni tofauti na jadi ya CCM. Kwa miaka mingi, CCM ilikuwa inawaona wapinzani kama maadui wa Taifa. Hali hii ilidhihirika zaidi katika Awamu ya Tatu ya uongozi Tanzania.
Wapinzani walikumbwa na hujuma nyingi zilizofanywa na vyombo vya dola, ambayo vilikiuka wajibu wake kama vyombo vya Taifa, vikawa vinafanya umachinga kwa CCM. Hayo yalibainishwa na taasisi huru za ndani na nje ya nchi, wakati wa uchunguzi wa vurugu zilizotokea Visiwani. Tanzania ilifedheheka kimataifa.
Pili, kauli ya Kikwete siku ile ilikuwa ni ishara ya busara na uungwana. Kiongozi anapaswa awe mwenye kuwajali na kuwaheshimu watu anaowangoza, wakiwemo wapinzani. Mtu anayejiamini, haogopi kuwapa sifa wengine. Ni ishara ya kujiamini, na kukomaa katika falsafa na saikolojia ya uongozi.
Kiongozi wa nchi anapowachukulia wapinzani kama afanyavyo Rais Kikwete anathibitisha kuelewa kuwa yeye ni kiongozi wa wote. Tumeshawaona wengine nchini mwetu ambao wanafanya vingine. Tumeshawaona ambao, siku ya kuapishwa, wanaendelea kuwabeza washindani wao, kama vile bado wako kwenye kampeni. Pengine sio sahihi kusema kuwa hao ni viongozi. Uongozi wa kweli si wa mbwembwe wala mabavu, bali unatokana na tabia njema. Unatokana na tabia inayowafanya watu wamkubali huyu mtu kwa hiari yao kuwa ni kiongozi.
Kama nilivyosema, alivyofanya Kikwete siku alipoapishwa ni tofauti na jadi ya CCM ya kuwabeza, kuwahujumu na kuwashambulia wapinzani. Napenda kurudi nyuma na kukumbushia kuwa jadi hii Mwalimu Nyerere alikuwa anajitahidi kuwakanya CCM waiache. Kwa mfano, wakati wanachama wa vyama vya upinzani walipokuwa wanasukuma magari ya viongozi wao kwa shangwe, na vyombo vya dola, kwa kutekeleza matakwa ya CCM, vikawa vinawazuia, Mwalimu Nyerere aliingilia kati na kusema watu waachwe na uhuru wao wa kusukuma hayo magari. Hivi ndivyo CCM ilivyokuwa, kwamba ilibidi Mwalimu awaelimishe jambo la wazi kama hilo, linalohusu uhuru na haki ya binadamu.
Baada ya kuingia madarakani, Rais Kikwete ameendelea kwenda njia tofauti na ilivyozoeleka, katika mahusiano yake na wapinzani. Amekuwa akiwashirikisha wapinzani katika shughuli za kiTaifa. iwe ni kuwakaribisha wageni wa nchi za nje Ikulu, au kuwa katika tume muhimu za kiTaifa. Vile vile, katika ziara zake za nchi za nje, Rais Kikwete anawajumuisha wapinzani. Hii haikuwa jadi ya CCM. Awamu ya Tatu, kwa mfano, sikuwahi kusikia wapinzani wamekaribishwa Ikulu.
Binafsi, nayatilia maanani hayo yote, hata kama baadhi yanaonekana madogo. Kwa ujumla wake, yanaonyesha kuwa Rais Kikwete ana moyo na mwelekeo tofauti na ule wa zamani. Kuwajumlisha wapinzani katika tume kama ile ya kuchunguza mikataba au tuhuma za kashfa ni ishara ya kuwa Rais Kikwete anatambua kuwa suala la maslahi ya Taifa ni suala la wote, si la chama tawala tu. Suala la kusafiri na wapinzani nje ya nchi linaweza kuonekana dogo, lakini mimi naliona kubwa. Nazingatia kuwa kusafiri ni fursa ya kujifunza na kupanua akili. Kusafiri ni kuelimika. Tangu enzi za mababu na mabibi, ilifahamika hivyo, hata wakatuachia methali: tembea uone. Kwa kuwajumuisha wapinzani katika misafara ya nje, Rais Kikwete anawapa fursa ya kujiimarisha kielimu na kimtazamo. Angekuwa mtu asiyejiamini, angeogopa kuwa wapinzani wakiimarika watakuja kuwa tishio kwenye kampeni za uchaguzi.
Jukumu nililojipa katika kuandika makala hii ni kuibua mjadala, na nategemea mjadala utakuwepo. Ninafahamu kuwa Rais Kikwete, kama kiongozi mwingine yeyote, hawezi kumridhisha kila mtu. Ninahisi kuwa hata haya niliyosema huenda watu wengine ndani ya CCM hawayapendi. Nafahamu kuwa katika uongozi wake kuna mapungufu, kama ilivyo katika uongozi wowote. Lakini mimi kama Mtanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa naona msimamo wa Rais Kikwete kuhusiana na suala la wapinzani ni mzuri na unastahili kutajwa kama nilivyofanya. Kwa namna fulani, kama nilivyodokeza, anayofanya Rais Kikwete ni mwendelezo way ale aliyoyawazia Mwalimu Nyerere, alipokuwa anawakingia kifua wapinzani.
–
Joseph L. Mbele
English Department
St. Olaf College
Northfield, MN 55057
Phone: (507) 786 3439
CHANZO: kwanzajamii.com