Prof. Lumumba: Wekeza ktk Waalimu, Wekeza Kesho

8691jakigili

Senior Member
Mar 30, 2012
179
67
Akihutubia Chama cha Waalimu Kenya (KNUT) amejadili mambo mazito kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwa waalimu. Ustawi wa sekta zote hutengemea ni jinsi gani nchi imewekeza kwa waalimu. Sekta za kilimo na afya haziwezi kuboreshwa kama jitihada za makusudi kabisa hazijafanyika katika sekta ya elimu.

Katika hotuba hiyo, ameelezea historia ya elimu katika Kenya, akilinganisha hali ya waalimu kipindi nchi ilipopata uhuru na sasa. Waalimu nyakati hizo waliheshimika sana kuliko sasa. MC analipwa vizuri kuliko mwalimu sasa. Anatamani kuona siku moja mwalimu akilipwa vizuri kuliko mwanasiasa. Alitolea mfano nchi ya Finland ambayo mwalimu ana mshahara mnono kuliko mwanasiasa.

Nimevutiwa mno na hotuba yake. Aligusia Mpango wa Maendeleo wa 2030 (miaka 16 tangu sasa) akisema kwamba anawasiwasi mkubwa kuwepo kwa dhamira ya dhati ya utekelezaji wake. Iwapo tangu uhuru hadi sasa ni miaka 50 imepita na suala la elimu ndio liko hivi, ni miujiza gani itafanyika ndani ya miaka 16 ijayo?

Kenya inajivuna kwa kujilinganisha na nchi za A. Mashariki. Akasema, kufanya hivyo ni sawa na mbilikimo kujilinganisha na mbilikimo wenzake, kwa kuwazidi kidogo urefu, bali ni vema Kenya ikajilinganisha na mataifa makubwa kiuchumi.

Aidha, msomi huyo alitumia mifano mingi ili kufikisha ujumbe wake. Kwa mfano, alisema wanasiasa wanatoa ahadi za maji yenye ujazo wa ziwa kwa waalimu, wakati kwa sasa mwalimu anahaja ya bilauri la maji. Akasema, "Maji hayo mengi ya ziwa [2030] yatakuwa na faida gani kwa mwalimu huyu anayekufa kwa kukosa bilauri moja tu la maji? Aliongeza kusema, "Utamwaahidije mwenye njaa kiwanda cha mikate wakati anakufa akihitaji kipande cha mkate? Hicho kiwanda cha mikate kitakuwa na faida gani atakapokuwa amekwisha kufariki dunia [mwalimu huyu]?"

Mwisho amesisitiza umuhimu wa waalimu kufanyakazi ili kuibadilisha Kenya. "Mwalimu, utakumbukwa kwa lipi mara baada ya kufariki dunia? Ni vema Wakenya wakakukumbuka wakiwa na wahandisi wao, madaktari, n.k. sio wahandisi wa kichina na kutibiwa nje ya nchi."

Source: The Citizen TV (Tafsiri isiyo rasmi ya kipande cha hotuba yake ni yangu mimi).
 
Back
Top Bottom