Uchaguzi 2020 Prof. Lipumba akiwa Mwanza: Tunahitaji kuboresha Sekta muhimu za Uchumi na Kilimo

CUF Habari

JF-Expert Member
Dec 12, 2019
239
234
IMG_20201005_210337_352.jpg

TUNAHITAJI KUBORESHA SEKTA MUHIMU ZA UCHUMI NA KILIMO."PROF.LIPUMBA"

MWANZA
Historia ya maendeleo ya uchumi duniani inaonesha kuwa maendeleo ya viwanda hutanguliwa au kuambatana na mapinduzi ya kilimo. Ongezeko la uzalishaji na tija katika Sekta ya Kilimo huongeza upatikanaji wa chakula na kupunguza gharama yake na kuruhusu wananchi kuhama toka vijijini na kwenda mijini kufanya kazi za viwandani. Kilimo kinazalisha malighafi inayotumiwa na viwanda vinavyosindika nafaka, mbegu za mafuta, matunda, nyama na maziwa.

Viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi hutumia malighafi inayozalishwa na Sekta ya Kilimo na ufugaji kama vile pamba na ngozi. Pato la wakulima linapoongezeka linakuza soko la bidhaa za viwandani - nguo na mavazi, viatu, sukari, samani na vifaa vya matumizi ya nyumbani.

Soko kubwa la ndani la bidhaa hizi huwezesha kuanzishwa kwa viwanda vyenye uwezo mkubwa na gharama za wastani za chini na kuvifanya viwanda hivyo kuweza kushindana na bidhaa za kutoka nje, na hata kuweza kuuza nje ya nchi.

Kuongezeka kwa mapato ya wakulima huongeza uwekaji wa akiba ambayo inaweza kutumiwa kuwekeza katika viwanda.

Mauzo ya bidhaa za kilimo nje ya nchi hulipatia taifa fedha za kigeni za kuagizia mashine, vipuri na malighafi kutoka nje ya nchi.

Utafiti katika nchi nyingi zinazoendelea unaonesha kuwa kasi ya kukua kwa tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo kunapunguza umaskini kwa kasi kubwa kuliko ukuaji wa sekta nyingine yeyote.

IMG_20201005_210258_946.jpg
 
Back
Top Bottom