..Haya jamani waziri wetu wa fedha katuletea changamoto hapa...
Mkulo: Ndullu kafanya maajabu BoT
na Salehe Mohamed na Kulwa Karedia
Mkulo: Ndullu kafanya maajabu BoT
na Salehe Mohamed na Kulwa Karedia
SERIKALI imesema kuimarika kwa shilingi dhidi ya dola na kushuka kwa mfumuko wa bei, vimetokana na uongozi mpya wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na sera zilizowekwa na Gavana mpya Profesa Beno Ndullu.
Uuzaji bidhaa za Tanzania nje ya nchi, umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa uchumi wa nchi na bidhaa za nje kuuzwa hapa kwa bei ya chini ndani ya soko letu.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mipango na Fedha, Mustafa Mkulo, alipokuwa akifunga semina ya wabunge kuhusu mwongozo wa kutayarisha mipango na bajeti ya serikali kwa kipindi cha mwaka 2008/2009.
Utoaji mikopo wa benki kwa watu mbalimbali, kutokukopa ndani kwa serikali na mfumuko wa bei kuwa asilimia sita kwa sasa, ni miongoni mwa chachu za ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema, hadi sasa mfumuko wa bei ni chini ya asilimia sita na benki mbalimbali zimeshusha riba ya mikopo yao na kubainisha kuwa mambo hayo yameimarisha uchumi.
Mkulo alisema, maajabu hayo katika uchumi wetu yametokana na mabadiliko yaliyofanyika BoT baada ya kuondolewa kwa Gavana wa zamani, Daudi Ballali.
Alisema miaka mitano hadi sita iliyopita, benki hazikukopesha watu kwa kasi kama ilivyo sasa na riba zimeshuka kulingana na taratibu walizojiwekea, lakini lengo likiwa ni kuimarisha uchumi na kuwawezesha wananchi.
"Mabadiliko yaliyofanywa na Ndullu pale BoT yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uchumi wa Tanzania, na hivi sasa shilingi ya Tanzania inapambana na dola," alisema Mkulo na kuongeza kuwa, uchumi wa nchi yeyote hauendelei bila wananchi hasa wa tabaka la chini kupata mikopo itakayowawezesha kufanya shughuli za kuwaongezea kipato.
Alisema, ni vigumu kwa wananchi kugundua ukuaji wa uchumi, lakini njia ya kuthibitisha hilo ni kukamilika kwa miradi mbalimbali huku akiainisha miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa shule, zahanati na maeneo mbalimbali ambayo yamesaidia kuboreka kwa uchumi wa Tanzania.