Polisi yakamata magari 6, ofisa usalama ‘feki’

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,000
9,861
JESHI la Polisi mkoa wa Dodoma linamshikilia Shaban Wisandala (32), mkazi wa Medeli jijini Dodoma, kwa kujifanya ofisa usalama wa taifa, pamoja na magari sita yaliyokamatwa kutokana na kusadikiwa kuwa ni ya wizi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema Mei 13, mwaka huu, Mtaa wa Medeli, Kata ya Tambukareli alikamatwa mtuhumiwa huyo akijifanya ofisa usalama wa taifa.

Alisema mtuhumiwa huyo amekuwa akijitambulisha kwa watu mbalimbali, kuwatishia maisha na kudai fedha kwa vitisho akitishia kuwakamata, kuwaharibia kazi na kutumia vibaya majina ya viongozi wa serikali wakati akidai fedha.

“Huyu mtuhumiwa tunamshikilia na bado tunamuhoji kwa kina na baadaye tutampeleka mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” alisema Kamanda Muroto.

Akizungumzia magari yaliyokamatwa alisema, Mei 10, mwaka huu majira ya 10:00, Kijiji cha Mbande, Kata ya Sejeli, Wilaya ya Kongwa, barabara kuu ya Morogoro na Dodoma, lilikamatwa gari namba T936 Toyota Land Cruiser VX, rangi nyeupe.

Muroto, alisema kuwa katika uchunguzi wa gari hilo limegundulika kutofautiana namba na taarifa zilizopo kwenye kadi.

Alisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Ramadhani Sekiondo (31), mkazi wa Magomeni Mikumi Dar es Saalam baada ya kukabidhiwa na mtu asiye mfahamu.

“Huu ni mtandao wa wizi wa magari tutaufutilia kwa kina na kuushughulikia bila huruma na sheria itachukua mkondo wake,” alisema Kamanda Muruto.

Pia alisema kuwa magari mengine mawili yalikamatwa Mei 11, mwaka huu mtaa wa Area ‘A’ Kata ya Kizota jijini Dodoma, yakiwa yamefungiwa ndani ya nyumba yasiyo na namba za usajili yakitumia namba za chassis ambayo ni Toyota Harrier Chassis namba MCU310001691, injini namba 1MZ1589700 na Toyota IST chassis namba NCP600209833, injini namba 2MZ3578179.

“Katika uchunguzi wa awali imegundulika kuwa hayana kumbukumbu zozote na yaliingia nchini bila kibali, uchunguzi zaidi unaendelea kwa kushirikiana na Interpol kubaini taarifa za kina za magari hayo na mtuhumiwa Omari Chilipachi (29), mkazi wa Sinza, Dar es Saalam, anahojiwa na polisi kuhusu tukio hilo,” alisema Kamanda Muroto.

Pia, Muroto alisema Mei 11, mwaka huu huko Area A, Kata ya Kizota, lilikamatwa gari aina ya Land Rover Discovery lenye namba za usajili wa nchi ya Afrika Kusini SJV576 GP.

Alifafanua kuwa kadi ya gari hilo inasomeka chassis SALLAAA135A339616, ambayo zinatofautiana na zilizopo katika gari ni 049053121030305071757 na hazipo katika mfumo wa usajili wa magari.

“Uchunguzi zaidi unafanyika ili kubaini ukweli wa uhalali wa gari hilo na mtuhumiwa Jamal Rashid (28), mkazi wa Area A, anahojiwa na jeshi hilo juu ya uhalali wa gari hilo,” alisema.

Katika tukio jingine Mei 12, mwaka huu huko Nzuguni, polisi ilikamata gari aina ya Toyota Alphard lenye kadi namba za usajili T384 DMU lenye chassis namba ANH100038956, injini namba 2AZ1184313 rangi ya Silver.

“Katika uchunguzi wa awali imebainika kuwa shassis ANH100030547 na ingini ZNZ 0860988 halisi kwenye gari zinatofautiana na kadi ya gari hilo aidha rangi ya gari hiyo ni nyeusi siyo Silver kama linavyoonekana,” alieleza Muroto.

NIPASHE
 
Uongo mbaya kuna jamaa lilikuwa linadanganya eti lenyewe ni mwanajeshi kumbe ni litapeli tuu.....

121.
 
4 Reactions
Reply
Back
Top Bottom