Polisi wawapiga mabomu wanafunzi Chuo Kikuu Arusha

Mallaba

JF-Expert Member
Jan 30, 2008
2,554
47
Jeshi la Polisi wilayani Arumeru, mkoa wa Arusha jana lililazimika kufyatua mabomu ya machozi na kurusha risasi hewani kuwatawanya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Arusha, baada ya kufunga barabara kwa mawe na kusababisha baadhi ya watalii kushindwa kuendelea na safari kwenye mbuga ya wanyama ya Anapa.
Wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza zaidi ya 400 walifunga barabara hiyo kwa lengo la kushinikiza kulipwa fedha za kujikimu, kwa awamu ya pili, ambazo kila mmoja anadai Sh. 300,000 hali iliyosababisha kutoka nje ya geti la chuo hicho na kwenda umbali wa mita tano kuziba barabara, kwa mawe makubwa, huku wakiutuhumu uongozi wa huo hicho kushindwa kuwapa majibu sahihi kuhusu fedha zao.
Wakizungumza na waandishi wa habari Chuoni hapo, wanafunzi hao ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao, walisema waliamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuzungumza na uongozi wa chuo na kujibiwa kuwa hawana fedha kwa kuwa serikali bado haijatoa fedha hizo.
Baada ya uongozi kutoa majibu hayo na viongozi wa wanafunzi kuwaambia majibu waliyopewa na uongozi wa chuo wanafunzi hao, waliamua kufanya mgomo wa kutoingia madarasani na kuanza kuandamana hadi nje ya geti la chuo hicho na kuweka mawe barabarani.
Mawe hayo yalizuia baadhi ya watalii waliokuwa wakienda kuangalia wanyama, kwenye mbuga ya Anapa na wale waliokuwa wanatoka mbugani pamoja na daladala zinazochukua abiria kutoka eneo la mjini na kwenda Ngarananyuki. Hali hiyo ilisababisha usumbufu kwa saa zaidi ya tatu.
Wanafunzi hao walikuwa wakisema kuwa hawakubaliani na sababu zilizotolewa na uongozi wa chuo hicho na ndiyo maana wameamua kuziba barabara ili kufikisha ujumbe kwa serikali kwamba Bodi ya Mkopo ya Elimu ya Juu inashindwa kutatua kero za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini.
Mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaja jina, alisema wanamshangaa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Irvent Torres, kwa kuamua kuingia barabarani na kuondoa mawe hayo kwa nguvu kisha kuita polisi kuwapiga mabomu.
”Sisi tunadai haki zetu, lakini tunashangaa polisi kumsikiliza Mzungu na kuamua kupiga mabomu kwani sisi ni wahalifu, ni raia tena Watanzania kwanini polisi hivi sasa wanaamua kila mgomo suluhisho ni mabomu tutafika wapi?” Alihoji.
Spika wa Bunge la Chuo hicho, Jonson Kiravu, alisema amesikitishwa na kitendo cha polisi kupiga mabomu na risasi hali iliyosababisha baadhi ya wanachuo hao kukimbilia vichakani na wengine kukamatwa na kupelekwa kituo cha polisi Arumeru.
”Lengo la kufunga barabara ni kutoa ujumbe kwa serikali kuwa tunahitaji fedha zetu na si majibu ya leo, kesho tumechoka ndio maana tunaamua kuchukua uamuzi huu ili tupate haki zetu,” alisema Kiravu.
Hata hivyo, waandishi walipojaribu kumuona Torres ili kuzungumzia mgomo huo, alisema alikuwa na shughuli nyingi na hana muda wa kuzungumza nao kisha kuingia ndani na kujifungia.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, alisema kuwa hana taarifa za tukio hilo na akizipata atazungumza.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom