Polisi wamshikilia Mjumbe wa CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Polisi wamshikilia Mjumbe wa CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, May 21, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  May 21, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,499
  Likes Received: 5,726
  Trophy Points: 280
  Polisi wamshikilia Mjumbe wa CCM

  Na Waandishi Wetu

  21st May 2009


  • [​IMG]Alikuwa anaandikisha shahada za kura Busanda
  • Mgombea wao aelezwa afya yake imetetereka
  • [​IMG]Malecela azushiwa kuondoka, atamba nimejaa tele

  Polisi katika mji mdogo wa Katoro, Wilaya ya Geita, mkoani Mwanza, wanamshikilia Mjumbe wa Nyumba Kumi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kijiji cha Katoro, Nathaniel Ezra, kwa tuhuma za kukutwa akiandika majina ya watu kwa ajili ya kuwagawia vyandarua ili wakipigie kura chama hicho.

  Balozi huyo alikamatwa jana saa 7:30 mchana na makamanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiendesha zoezi hilo.

  Baada ya kumkamata, makamanda hao wakiongozwa na Afisa wa Idara ya Utafiti ya Chadema, Mwita Mwikabe Waitara, walimpeleka katika kituo cha polisi cha Katoro, ambako hadi jioni alikuwa akiendelea kuhojiwa na polisi.

  Mjumbe huyo alidai kuwa waliitwa Jumapili na Mtendaji wa Kata ya Katoro na kupewa maelekezo ya kuandikisha majina ya watu katika vitongoji vyote vya kata hiyo kwa ajili ya kuwagawia vyandarua vilivyotiwa dawa.

  Mjumbe huyo alidai walielekezwa kuendesha zoezi hilo kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi wiki hii siku, ambayo kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Busanda zinatarajiwa kuhitimishwa.

  Habari zinadai kuwa Mjumbe huyo alikamatwa baada ya kuwatishia baadhi ya watu kwamba, iwapo hawataipigia kura CCM, watakiona cha moto.

  Aidha, katika maelezo yake, alikiri kwamba, katika kuendesha zoezi hilo kuna nyumba alizoziruka. Hata hivyo, hakueleza sababu ya kuziruka nyumba hizo.

  Polisi wa kituo hicho waliahidi kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.

  Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita (OCD), Shaban Kimea, alipoulizwa na Nipashe muda mfupi baada ya Mjumbe huyo kukamatwa, alisema wakati huo alikuwa bado hajaarifiwa tukio hilo.

  Katika tukio lingine, kampeni za kuwanadi wagombea katika uchaguzi mdogo wa ubunge yameibua mambo mapya baada ya wananchi wa kabila la Wasumbwa kuibua siasa za ubaguzi wa kijinsia wakipinga kuongozwa na mwanamke kwa madai kwamba kufanya hivyo ni kukiuka mila ya kabila lao inayopinga suala hilo.

  Wananchi hao wanaoishi kwa wingi katika Kata ya Nyarugusu, wamekuwa wakieleza msimamo wao huo tangu baadhi ya vyama vya siasa visimamishe wagombea wanawake katika uchaguzi mdogo wa kiti hicho unaotarajiwa kufanyika Jumapili.

  Vyama vilivyosimamisha wagombea wanawake katika uchaguzi huo, ni CCM na United Democratic (UDP). Wakati UDP imemsimamisha Beatrice Lubambe, CCM kwa upande wake, imemsimamisha Lolensia Bukwimba.

  Tofauti na CCM na UDP, vyama vya CUF na Chadema, vimewasimamisha wagombea wanaume. Wagombea hao, ni Primus Ndalahwa Oscar (CUF) na Finias Magessa (Chadema).

  “Kwetu mnajisumbua bure, ni mwiko kwa mila yetu kuongozwa na mwanamke,” mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Doto Manyilizu alisikika akisema.

  Manyilizu alisema hayo huku akiungwa mkono na kundi la wenzake katika kijiji cha Busolwa ‘B’, Kata ya Nyarugusu muda mfupi baada ya Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM Taifa, Richard Hiza Tambwe, kuhutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za kumnadi mgombea wao.

  Hata hivyo, Mratibu wa Kampeni za CCM, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, George Mkuchika, akizungumza na Nipashe mjini Katoro jana, alizishutumu siasa hizo kwa kuziita kuwa ni “mawazo ya kizamani.”

  Mkuchika alisema mawazo hayo yamepitwa na wakati na hayapo Busanda kwani katika Mkoa wa Mwanza, ambao wananchi wenye msimamo huo wanatoka, kuna viongozi wanawake wanaotoka CCM. Aliwataja kuwa ni pamoja na Mbunge wa Ukerewe, Getrude Mongella na Diwani wa Kata ya Katoro, Maimuna Mingisi.

  Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema suala la jinsia si kigezo cha msingi cha mtu kupewa uongozi katika jamii na ndio maana katika chama chake kuna viongozi wanawake, wakiwamo wabunge wa viti maalum.

  Naye Afisa Habari wa Chadema, David Kafulila, alisema hawawezi kumhukumu mgombea yeyote kwa sababu tu ya jinsia yake, bali wanamhukumu kutokana na rekodi yake ya kuwatumikia wananchi kupata maendeleo.

  Wakati huo huo, wananchi wa Kata ya Nyarugusu, jana walijitokeza kwa wingi katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyarugusu kushuhudia helikopta ya Chadema.

  Walianza kujitokeza majira ya saa 8.00 mchana, lakini ilipofika saa 10.00 walianza kukata tamaa na kusema kuwa huenda wamedanganywa kutokana na kutoiona.

  Baadhi ya wafanyabiashara walifunga maduka na kusogelea uwanja huo kushuhudia helikopta hiyo ikitua. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akifuatana na mgombea wa Chadema,Finias Magessa, waliwasili kijijini hapo saa 11.35 jioni.

  Akimnadi Magessa, Mbowe aliwaambia polisi waliokuwepo kuwa umati uliokuwa katika uwanja huo haukwenda kucheza ngoma bali walikwenda kwa mapenzi yao kuishuhudia Chadema na kuwataka ikifika saa 12 wasimfuate jukwaani kumtisha.

  Alisema jimbo hilo lina wapiga kura 130,000 hivyo ifikapo Jumapili wananchi waionyeshe serikali kuwa wanauchukia umaskini kwa kumpigia kura mgombea wa Chadema.

  Alisema Tanzania ina msiba na kilio kikubwa na kwamba jimbo la Busanda lina kilio cha ziada kwa kuwa lina wananchi 280,000 ambao hawana shule hata moja yenye kidato cha tano na cha sita.

  Aliwaomba radhi kwa kuchelewa mkutanoni kwa maelezo kuwa huo ulikuwa mkutano wake wa 12 kwa siku ya jana.

  Katika tukio lingine, jana zilizuka taarifa za uvumi kuwa Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Tanzania Bara, John Malecela, ameondoka Busanda kurejea Dar es Salaam.

  Hata hivyo, Malecela mwenyewe alipoulizwa na Nipashe kwa njia ya simu jana jioni, alikanusha uvumi huo kwa kusema amekuwepo jimboni humo tangu mwanzo na kwamba ataendelea kuwepo hadi mwisho.

  Mgombe wa CCM mgonjwa
  Katika hatua nyingine mgombea wa CCM Bukwimba alivumishiwa kuwa amejitoa katika kinyang’anyiro hicho, baada ya kutokuonekana kwenye mikutano ya kampeni jana.

  Taarifa hizo ziliwaletea kiwewe baadhi ya wakereketwa wa CCM, ambao walikusanyika kwenye ofisi za Chama hicho wakitaka kujua ukweli juu ya suala hilo.

  Hata hivyo Afisa wa Propaganda wa Chama hicho makao Makuu, Hiza Tambwe, aliwatoa hofu wanachama hao na kusisitiza kwamba mgombea wao hajajitoa.

  Hiza akiwa eneo la Katoro aliwaambia wakereketwa hao kuwa mgombea wao hajajitoa ila afya yake imedhoofu kidogo.

  Kutokana na udhaifu huo, Tambwe alisema wameamua kumpangia mgombea mikutano ambayo ipo karibu na nyumbani kwake kijiji cha Nyabulolo ili wasimchoshe.

  “Unajua tena mikiki mikiki ya kampeni mgombea ameamka vibaya na sasa ameamua kujipumzisha na anafanya mikutano ambayo ipo karibu na nyumbani kwake,” alisema.

  Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha jana alipata wakati mgumu wa kuzomewa, baada ya msafara wake kukatisha sehemu ambapo ilishuka helkopta ya Chadema.

  Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Nyakakombe, ambapo Masha alikuwa akielekea kwenye harakati za kampeni za kumnadi mgombea wao.

  Katika tukio jingine, jana kulizuka mtafaruku baina ya CCM na UDP, ambapo wapiga debe wa vyama hivyo walikuwa wakigombea uwanja wa kufanyia kampeni.

  Mtafaruku huo ulitokea katika kijiji cha Bugogo, ambapo mgombea wa UDP Beatrice Lubambe aliwahi eneo hilo na kutengeneza jukwaa kwa lengo la kumwaga sera.

  Hata hivyo baadaye lilikuja fuso la CCM na lenye sauti kubwa na kuegeshwa eneo hilo na kuanza kupiga nyimbo za kuisifu CCM.

  Kutokana na mabishano ya hapa na pale mgombea wa UDP aliamua kunyoosha mikono juu na kuwaachia CCM waendelee na mkutano japo ratiba haikuwaruhusu kuwepo eneo hilo.

  Imeandikwa na Muhibu Said, Grace Chilongola na Simon Mhima.

  CHANZO: NIPASHE
   
 2. Teamo

  Teamo JF-Expert Member

  #2
  May 21, 2009
  Joined: Jan 9, 2009
  Messages: 12,286
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  kweli nimekubali!HII NI ISHARA KUTOKA MAGHARIBI
   
 3. R

  Rwabugiri JF-Expert Member

  #3
  May 21, 2009
  Joined: Jul 10, 2007
  Messages: 2,777
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 135

  Kinacho nisikitisha, kwanini polisi hawawachukulii hatua hao wanao kamatwa wakinunua shahada? unajua wange wasweka ndani kidogo ingekuwa funzo kwa wengine, ili next time wakifatwa na majambazi kwamba wafanye uhuni huo wajue cha moto kinawasubili!
   
 4. Ibrah

  Ibrah JF-Expert Member

  #4
  May 21, 2009
  Joined: Mar 22, 2007
  Messages: 2,721
  Likes Received: 36
  Trophy Points: 145

  Hao Polisi wetu wamezoea kupambana na wapinzani wa CCM tu. Tangu mwaka juzi wanamtafuta John Komba wa TOT kwa vurugu alizofanya Kiteto na hawajampata!
   
 5. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #5
  May 21, 2009
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Sio kuswekwa ndani tu, waburuzwe mahakamani kabisa ili sheria ichukue mkondo wake
   
 6. Fidel80

  Fidel80 JF-Expert Member

  #6
  May 21, 2009
  Joined: May 3, 2008
  Messages: 21,976
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 145
  Angekuwa wa upinzani mngeona kelele zake mbona Mkuchika kafyata?
   
 7. Masanilo

  Masanilo JF-Expert Member

  #7
  May 21, 2009
  Joined: Oct 2, 2007
  Messages: 22,303
  Likes Received: 168
  Trophy Points: 160
  Ama kweli bado tuna kazi kubwa...hivyo vyandarua inabidi wapewe bure bila kuuza uhuru wa kura zao! CCM bwana wakati mwingine hawawezi kufikiria hvyo vyandarua wanatakiwa kugawa bure nadhani ni vile vilivyotolewa na Global Health Initiative katika kampeni ya kupunguza malaria....jamaa wameisha fanya mtaji kisiasa!
   
 8. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #8
  May 21, 2009
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Hapo ndipo tunapoweza kuona jinsi ujinga unavyoiumiza jamii yetu. Hivi vyandarua vinapaswa kugawiwa bure, lakini wajanja mbuzi kama hawa wanaanza kuleta za kuleta!!!
   
 9. m

  mmaroroi JF-Expert Member

  #9
  May 21, 2009
  Joined: May 8, 2008
  Messages: 2,536
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  Busanda mfanye kweli Jumapili 24/05/2009 mpembue vizuri mchele,muwaonyeshe CCM kuwe wakitaka ushindi 2010 wawafukuze mafisadi wanaolindwa na MKUCHIKA na MAKAMBA.
   
 10. MwanaHaki

  MwanaHaki R I P

  #10
  May 21, 2009
  Joined: Oct 17, 2006
  Messages: 2,403
  Likes Received: 122
  Trophy Points: 145
  Ama kweli CCM sasa maji yamewafika shingoni. Mpaka wanatoa hongo ya waziwazi? Du! 2010 mbona itakuwa rahaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa?
   
Loading...