Polisi wadaiwa kuchoma nyumba za wananchi kaya zaidi ya 500 kukosa makazi Muleba, Karagwe

R.B

JF-Expert Member
May 10, 2012
6,303
2,000


[h=2] Unyama wa kutisha [/h] Jumamosi, Novemba 17, 2012 08:34 Na Victor Bariety, Karagwe

*Polisi wadaiwa kuchoma nyumba za wananchi
*Wengi wakosa makazi, waishi maporini
*Mifugo, vyakula, fedha vyaporwa Muleba, Karagwe
VILIO, simanzi na huzuni vimetawala katika wilaya za Muleba na Karagwe, kutokana na kaya zaidi ya 500 kukosa makazi, baada ya kile kinachodaiwa makazi yao kuchomwa moto na askari polisi wanaoendesha operesheni Okoa Mazingira mkoani Kagera.

Mbali na uchomaji nyumba unaofanywa na askari polisi, wakishikirikiana na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kumeacha mamia ya wananchi ambao wamelazimika kuishi porini kama wanyama.

Operesheni hiyo, imejikita zaidi katika vijiji vya Bitunzi, Nyabilanda, Kasharara na Kyebitembe, Kata ya Kalambi Wilayani Muleba, ambako inadaiwa wafugaji wamekuwa wakiporwa maelfu ya mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na kila kitu kinachokutwa kwenye miji yao.

Vijiji vingine ambavyo vimeathirika ni Luhita na vitongoji vyake Kibati, Msasa, Chechebu, Kanelo na Kikoto vyote viko wilayani Karagwe.

Inadaiwa hadi sasa, takwimu zinaonyesha zaidi ya Sh milioni 40 zimeporwa na askari, huku magunia zaidi ya 40 ya udaga na 100 ya mpunga yamechomwa moto.

Lakini pia kumekuwa na wimbi kubwa la ubakaji wa watoto wa kike unaofanywa na baadhi ya askari polisi wanaoendesha operesheni hiyo.

Operesheni hiyo, iliyoanza Novemba Mosi mwaka huu inadaiwa kuwa ni ‘chaka’ kubwa la uporaji na kusababisha mamia ya familia kukimbilia kwenye nyumba za ibada kwa ajili ya kupata hifadhi.

MTANZANIA iliyotembelea maeneo yaliyoathiriwa na zoezi hilo, imeshuhudia uharibifu mkubwa ambao haujawahi kutokea katika wilaya hiyo.

“Nakwambia sijawahi kuona maishani mwangu unyama huu ambao unafanywa na vyombo vya dola, sijui Serikali iko wapi, tunakufa jamani.

“Tumeshuhudia kuwapo na askari polisi wengi wenye silaha za moto, tunaporwa mifugo yetu kama wakimbizi wakati tupo kwenye nchi yetu.

“Haiwezekani watu ambao tumeishi maeneo haya miaka yote leo tunaambiwa sisi ni wakimbizi, wavamizi, haiingii akilini hata kidogo, mazao yetu yanafyekwa vibaya,” alisema Mayunga Byabato.

Alisema kutokana na unyama huo, hivi sasa akina mama wajawazito wamelazimika kujifungulia porini na kulala na watoto wachanga huko.

Naye mkazi mwingine, Siyengo Sanane, alisema wamewaona viongozi wa wilaya ya Muleba kuwasilisha malalamiko yao, lakini wamekuwa wakitishiwa kuswekwa rumande.

“Unajua maeneo yetu yanataka kumilikishwa kwa Wanyarwanda, wala si kweli kwamba sisi tumevamia na kujenga hapa…tumeishi hapa zaidi ya miaka 15, iweje leo ndiyo tuonekane wavamizi,” alihoji Sanane.

“Sijawahi kuona Serikali isiyojali watu wake…hii ni danganyatoto..tuna taarifa kuwa hii ni njama ya wahamiaji haramu ambao wanataka tuondolewe hapa wamilikishwe,” alisema Sanane.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kyebitembe, Paschal Mnyangote, alikiri kutokea kwa tukio hilo.

Alisema kumekuwa na njama ya kutaka kutaifishwa kwa maeneo yao ili wakabidhiwe wawekezaji.

Alisema kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kupambana na wahamiaji hao na kuwataka wasikubali kuondoka kwenye maeneo yao, kwa sababu ni unyanyasaji mtupu.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kuna hatari ya kutokea magonjwa ya mlipuko kutokana na wananchi wengi kurundikwa sehemu moja na kukosa huduma za msingi kama vyoo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lembiris Kipuyo, alipohojiwa kwa njia ya simu alikiri nyumba za wananchi hao kuchomwa na kubomolewa, na kujitetea kuwa zoezi hilo linafanyika ili kulinda mazingira ya mkoa huo.

“Kuna Operesheni Okoa Mazingira Mkoa wa Kagera, inaendelea kwenye wilaya za Biharamlo, Kagera na Muleba…lengo ni kuwahamisha wahamiaji haramu wanaoingia na makundi makubwa ya ng’ombe katika misitu ya hifadhi.

“Ni operesheni ya wazi, maana inaendeshwa na polisi na inasimamiwa na maafisa Usalama wa Taifa, TAKUKURU na wanasheria..hivyo wanaolalamika hawajui kuishi maeneo ya hifadhi kama ni kosa,” alisema Kipuyo, ambaye alidai yuko mkoni Dodoma, akihudhuria kikao cha wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Mangu, aliiambia MTANZANIA, kuwa zoezi linaloendelea limefuata taratibu zote zinazotakiwa.

“Ni kweli tumekuwa na zoezi la kuhamisha watu kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi tangu Novemba Mosi mwaka huu. Hao wanaosema tumechoma nyumba ni waongo, sisi tulichofanya tumechoma vibanda tu ambavyo tumevikuta kwenye maeneo husika.

“Madai ya kuwa tumepora ng’ombe hayana ukweli, sisi tumekamata mifugo mingi tuko nayo hapa kituoni, mwananchi yeyote mwenye malalamiko aje ofisini kwetu tu, napenda kukwambia ikiwezekana tumeni waandishi wenu wakajionee wenyewe,” alisema Kamanda Mangu.
 

Ciril

JF-Expert Member
Jan 10, 2011
7,868
2,000
Ili haki ipatikane kwa wanadamu ni lazima anaengoza awe ni mtu mwenye busara/mcha Mungu/asiependa makuu na mwenye UPENDO kwa watu wake..
 

papason

JF-Expert Member
Sep 14, 2010
3,413
2,000
Wengi ya wanao chomewa nyumba na kunyang'anywa mifugo ni wahamiaji wa kitutsi, all in all wanachofanyiwa sio haki!
 
Top Bottom