Polisi, TRA wahusishwa kupeleka mahindi Kenya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Polisi, TRA wahusishwa kupeleka mahindi Kenya

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mlachake, Jun 27, 2011.

 1. Mlachake

  Mlachake JF-Expert Member

  #1
  Jun 27, 2011
  Joined: Oct 13, 2009
  Messages: 2,920
  Likes Received: 619
  Trophy Points: 280
  WAKATI maeneo mengi nchini yakikabiliwa na uhaba wa chakula, maelfu ya tani za mahindi zinavushwa kupelekwa nchi jirani ya Kenya kupitia njia za panya, huku askari polisi wenye silaha wakidaiwa kuyasindikiza magari yanayotumika kusafirishia mahindi hayo.

  Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili kwa siku kadhaa katika Mji wa Himo, unaonyesha kuwa wafanyabiashara kutoka eneo la Lotima nchini Kenya, wanaingia katika mji huo kununua mahindi hayo ambayo Serikali imepiga marufuku uuzaji wake nje ya nchi.

  Uchunguzi huo umebainisha kuwa ili waweze kuyasafirisha mahindi hayo, wafanyabiashara hao hutoa rushwa kwa askari polisi na baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Ushuru wa Forodha, Kituo cha Holili.

  Imebainika kwamba, kwa kutumia mtindo huo, polisi na wafanyakazi wa Idara ya Ushuru wa Forodha Holili wanajipatia mamilioni fedha kila siku kutokana na wingi wa magari yanayotumika kuvusha mahindi kwenda Kenya.

  Mwananchi Jumapili limebaini kuwa watendaji hao wamerasimisha mchezo huo mchafu ambao pia umezoeleka kwa wafanyabiashara hao.

  Wastani wa malori 400 huegeshwa kila siku katika mitaa ya mji wa Himo yakipakua magunia ya mahindi na kupakiwa katika malori madogo aina ya Fusso ambayo hutumika kuyasafirishia kwenda Kenya usiku.

  Jumatano wiki hii, gazeti hili lilishuhudia Mtaa wa Mtenga pekee ukiwa na malori 68 (namba tunazo), yakipakia shehena ya mahindi kutoka katika stoo moja tayari kusafirishwa kwenda Kenya.

  Habari zaidi uhakika zinaonyesha kuwa, mamilioni ya fedha za rushwa zinazokusanywa kila siku kutoka kwa wafanyabiashara hao na askari polisi, huwafikia pia baadhi ya vigogo wa jeshi hilo Kituo cha Himo, Wilaya ya Moshi na ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, ili wafumbie macho uozo huo.

  Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani humo, zinaeleza kuwa biashara hiyo imewafanya polisi kugombania kupangwa kufanya doria za usiku katika mji wa Himo na barabara kati ya mji huo na mpaka wa Holili.

  Mwananchi Jumapili kwa siku kadhaa imeshuhudia gari ya doria ya polisi kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi wa mkoa, likiwa limeegeshwa gizani chini ya mti, kando ya barabara hiyo nje kidogo ya mji wa Himo, huku askari wakisimama kandokando ya barabara na kuyasimamisha malori ya mahindi na kukusanya fanikisha fedha za rushwa.

  Askari wa kikosi cha farasi Himo pia nao wamekuwa wakipiga doria mchana na jioni katika barabara za vumbi zinazotumiwa na wafanyabiasahara hao, kuhakikisha hakuna anayevusha mahindi bila kupata baraka zao.

  Mbali na gari la pilisi kutumika, gari la wafanyakazi wa ushuru wa forodha wa TRA pia hufanya doria katika barabara hiyo karibu na makutano ya barabara ya vumbi maarufu 'panya route' inayotumiwa na malori kwenda Kenya.

  Naibu Waziri
  Naibu Waziri Kilimo na Chakula, Christopher Chiza juzi aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa Serikali inafahamu kuwepo kwa biashara hiyo haramu na wanaofanya hivyo kutumia njia za panya kuvusha mahindi hayo.

  Alisema tayari amezungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu suala hilo na baada ya mazungumzo yao Pinda amemwagiza kuhakikisha uuzaji nje ya mahindi unakomeshwa ili kulinusuru taifa na njaa.

  “Nimezungumza na Waziri Mkuu ameniagiza kudhibiti biasahara hiyo mara moja ili kulinusuru taifa na njaa," alisema Chiza.

  Taarifa zinaonyesha kuwa mahindi yanayoingia katika mji wa Himo na baadaye kusafirishwa kwenda Kenya, yanatoka Kiteto mkoani Manyara, Handeni mkoani Tanga na Kibaigwa mkoani Dodoma .

  Njia za kuvushia

  Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa kuna njia kuu mbili zinazotumika kuvushia mahindi hayo. Ya kwanza ni barabara ya Himo - Marangu - Tarakea. Wanapokaribia mpakani huingia njia za panya na kuvuka mpaka na njia ya pili ni Himo-Hosein Uchaku-Marangu na kuingia nchini Kenya.

  Pia njia nyingine ndogo nyingi zinazotumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wanaojaribu kukwepa kutoa rushwa kwa maafisa wa polisi na TRA.

  Mgawo wa rushwa
  Uchunguzi umebaini umebaini kuwa maandalizi ya kusafirisha mahindi huanza saa 11:00 jioni baada ya wafanyabiashara kuwasiliana na askari polisi wa dori na wafanyakazi wa TRA kwa kuwapa rushwa ili wasikamatwe usiku wakianza safari.

  Wapo pia baadhi ya wafanyabiashara ambao hawafanyi maandalizi ya kusafisha njia nao huamua kutoa rushwa kwa polisi na TRA baada ya kusimamishwa njiani.

  Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili unaonyesha kuwa mfanyabiashara ili aweze kuvusha mahindi yake hulazimika kutoa rushwa mara nne.

  Kituo cha kwanza cha rushwa ni baada ya mahindi kufika Himo mjini na kupakiwa katika Fusso ambapo wafanyabiashara hao kutoka Kenya kwa kushirikiana na wenzao wa hapa nchini, hupeleka fedha kwa polisi wanaolinda kizuizi (road block) ambacho awali kilikuwa kikitumiwa na kikosi cha Chura katika barabara ya kutoka Himo-Holili.

  Askari wa kituo hiki wanadaiwa kupokea Sh50,000 kutoka kwa kila lori la mahindi linalopita eneo hilo.

  Kituo cha pili ni kwa askari polisi wanaofanya doria katika barabara ya Himo-Holili kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kilimanjaro ambao wanadaiwa kupokea Sh70,000 kwa kila gari.

  Kituo cha tatu ni kwa maafisa wa TRA ambao hufanya doria wakiwa na gari ambao wanadaiwa hupokea Sh 60,000 kwa kila lori linalolipita, huku kituo cha nne cha rushwa kikiwa kwa Kikosi cha Farasi kutoka Kituo cha Polisi Himo ambao pia hufanya doria.

  Askari wa kikosi hiki ambao huingia kwa zamu wanadaiwa kupokea Sh 50,000 kwa kila lori linalopita.

  Kwa wastani kila usiku mmoja malori 70 hadi 100 huvusha mahindi kwenda Kenya na askari wa doria wanadaiwa kukusanya rushwa inayokadiriwa kufikia Sh8 milioni ambazo ni sawa na Sh240 milioni kwa mwezi ambazo wanagawana maafisa wa polisi na TRA.

  “Aisee, we acha tu mahindi sasa ni dhahabu yanatajirisha watu, kuanzia askari polisi, TRA, mizani na hata wafanyabiashara wenyewe,” anasema askari polisi mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina na kuongeza: “Hata wakubwa wetu wanapata mgawo huo.”

  Bei ya mahindi

  Ingawa wafanyabiashara hao hutoa fedha nyingi kwa ajili ya kusafisha njia, lakini bado wanapata faida kutokana na kuuzwa bei ya juu katika soko la mahindi lililopo eneo la Lotima nchini Kenya .

  Kilo moja ya mahindi katika mji wa Himo huuzwa Sh400 na yakifikishwa kwenye soko hilo la wazi nchini Kenya huuza Sh760 kwa wafanyabiashara wakubwa wanaosafirisha kwenda Somalia, Ehiopia na Sudan ambako pia huuzwa kwa faida kubwa zaidi.

  Lotima Kenya

  Mwananchi Jumapili ambayo ilivuka mpaka na kuingia nchini Kenya katika Soko la Lotima ilishuhudia wafanyabiashara wengi wakinunua mahindi hayo huku wengine wakipakia kwenye malori makubwa kwa ajili ya kuyasafirisha kwenda Bandari ya Mombasa tayari kupakia melini kupelekwa nje ya nchi hiyo.

  “Watanzania wametupa utajiri mkubwa, tunaomba Serikali yao ishituke mapema, tuendelee kupata fedha, huku mahindi ni mali, sikutegemea kama ningeweza kupata faida kubwa kiasi hiki,” alisema mfanyabiashara wa soko hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Joshua.

  Kisha akamshwishi mwandishi akisema: “Hebu na wewe changamka, fanya biashara hii, uwe tajiri, au hutaki utajiri?”

  Mnunuzi mwingine wa mahindi mwenye asili ya Somalia alisema ananunua mahindi Sh740 kwa kilo kutoka Tanzania na husafirisha kwenda Somalia.

  “Una mahindi? Nitanuua kwa Sh740 kwa kilo, lakini lazima yawe makavu, unajua nyinyi Tanzania waongo sana, unaweza kuniletea juu makavu chini mabichi ambayo yatanifanya niingie gharama nyingine ya kuyaanika,”alisema Msomali huyo.

  RPC Mwakyoma

  Kamanda mpya wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema bado hajaripoti katika kituo chake cha kazi, lakini atakapoingia wiki ijayo litakuwa suala la kwanza kulishughulika.

  “Bado sijaripoti, nikiingia kazini wiki ijayo jambo la kwanza kulifanyia kazi ni suala la rushwa ya mahindi Himo,” alisema.

  Naye Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Yusuf Ilembo, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema Jeshi la Polisi mkoani humo limeanzisha operesheni maalumu ya kuzuia biashara ya mahindi Himo ambayo ipo chini ya RCO.

  Alishangaa kusikia biashara hiyo imeendelea licha ya operesheni hiyo kufanyika na kuahidi kulifuatilia sula hilo.

  Meneja TRA
  Meneja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Patience Minga, alisema kwa vile Serikali imepiga marufuku uuzaji wa mahindi nje ya nchi, maafisa wake nao hawana budi kushirikiana na polisi kuzuia biashara hiyo.

  Alisema hana taarifa kama baadhi ya maafisa wake wanashiriki katika mchezo huo mchafu na kwamba yeye kwa sasa yupo likizo, akirejea ofisini wiki ijayo atalifanyia kazi suala hilo .

  “Nipo likizo, nikingia ofisini Jumatatu (Kesho) nitalifanyia kazi suala hilo ,” alisema na kuongeza:
  “Suala la rushwa tulishalizungumza ofisini na kutoa onyo kwa wafanyakazi wote, sasa nashangaa kusikia wapo wanajihusisha.”

  Source: Mwananchi Tar 26 june 2011

  Kama hii serikali haijachukulia hatua Jambo hili basi ni serikali ya kisanii.
   
Loading...