Polisi Kinondoni wadaiwa kubomoa nyuma ya mwananchi

Nanu

JF-Expert Member
May 29, 2009
1,222
68
Polisi Kinondoni wadaiwa kubomoa nyuma ya mwananchi

Na Felix Mwagara
9/23/2009
Source: Majira

POLISI wa Kituo cha Wazo Hill, wilayani Kinondoni Dar es Salaam, bila ya kuwa na vielelezo vyovyote huku wakiwa na silaha kali, wamevamia nyumba ya mkazi mmoja wa Kitalu B huko Tegeta na kuibomoa na kusambaratisha mali zote zilizokuwa ndani ya nyumba hiyo.

Tukio hilo limetokea juzi saa 6:30 mchana baada ya kundi la askari hao kuanza kubomoa nyumba hiyo huku kukiwa hakuna wananchi wala taarifa kwa miliki wa nyumba hiyo, Hadija Boki.

Hata hivyo, wakiwa katika hatua za awali za uvunjaji, Boki na wananchi wa maeneo hayo waliwataka askari hao watoe vielelezo vinavyowaruhusu kubomoa na mtu aliyewatuma kufanya hivyo wakati viongozi wa serikali ya mitaa hawakuwa na taarifa.

Kwa mujibu wa wananchi hao, askari hawakujibu na badala yake waliondoka na ilipofika saa nane na dakika 45 walirudi tena wakiwa na nguvu mpya ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya askari wakiwa wakiwa na silaha mkononi na kuendelea na uvunjaji.

“Walikuja askari polisi wengi lakini, tulifanikiwa kuandika namba za askari wawili ambao ni Hoseyn D066 na Paulo D5159, waliokuwa na bunduki mikononi na kufanikiwa kuivunja nyumba yote na kutupa vyombo vya mama Boki,” alisema mmoja wa wananchi hao.

“Mapolisi wa Wazo wanatumiwa sana katika kutunyanyasa watu, nadhani wanapewa hongo na watu wenye fedha hili waje kutuvamia na kutuweka maabusu," alidai na kusisitiza mwananchi huyo ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe.

Kwa upande wake Boki ambaye mmiliki wa nyumba hiyo alifika katika ofisi za gazeti la Mwananchi akiwa anatokwa na machozi na hatimaye kuongozana na mwandishi wa habari hizi hadi katika eneo la tukio.

Akiwa katika eneo hilo mama huyo alisema nyumba na kiwanja hicho ni mali yake tangu mwaka 1982 na kwamba analipia kodi kama inavyotakiwa.

Alisema mwaka 2006 alitokea mtu mmoja na kudai kuwa kiwanja hicho ni mali yake na kuanza kukizungushia ukuta wakati nyumba yake (Boki) ikiwa ndani ya ukuta huo.

Boki alisema kufuatia uvamizi huo, mwaka 2007 alifungua kesi katika Mahakama ya Ardhi ya Wilaya ya Kinondoni na alikabidhi gazeti hili kithibitisho cha hukumu kutoka katika mahakama hiyo.

Kithibitisho hicho kilikuwa kinahusu kesi namba 35 ya mwaka 2007 kati yake na Noel Kazimoto na kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa Februari 15 mwaka jana, Boki alishinda kesi na mshitakiwa alitakiwa alipe uharibifu alioufanya katika ardhi ya Boki na kuacha kufanya shughuli yoyote katika kiwanja hicho.

“Hiki kiwanja ni changu tangu mwaka 1982 nipo hapa zaidi ya miaka 20 leo hii anatokea mtu ambaye anasema hiki kiwanja ni chake eti Manispaa ya Kinondoni ndiyo iliyommilikisha kiwanja, naomba haki itendeke kwa watu wenye fedha kuja kutuonea sisi maskini, mimi kw asasa sijui nitakaa wapi wameshanivunjia nyumba yangu,” alilalamika Boki na kuongeza;
“Mimi nataka wanionyeshe ruhusa kutoka manispaa ambayo inawaruhusu waje kubomoa nyumba yangu na kunifanya masikini kiasi hiki, nitaenda wapi jamani na umri huu mimi nitaweza kupanga kweli, serikali naomba munisaidie,” alisema Boki ambaye ana umri wa miaka 47.

Baadhi ya wananchi ambao walikuwepo katika eneo ilo waliliambia gazeti hili kuwa mambo yaliofanywa na askari hao ni ya unyanyasaji na kwamba tatizo hilo halipo kwa Boki pekee yake bali kwa wengi wao.

“Kwa kweli tunapata shida sana, wenye pesa wanakuja kutudhulumu mali zetu, manispaa hawajafanya tathimini ingawa tulishaandika barua na wakajibu kuwa eneo letu bado halijafanyiwa tathimni ,e lakini cha kushangaza kuna watu wanakuja wanasema hivi viwanja ni vyao wakati sisi ndiyo wamiliki halali," alisema mwananchi mwingine.

Mkuu wa kituo cha Polisi cha Wazo Hill Erick Kiponda alisema" unaingiaje ofisini kwangu bila kunisalimia, hakuna chochote kilichotokea hapa,".

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Noel Mahyenga, alisema, "siwezi kuzungumza chochote bila kufanya utafiti. Naomba ulete maswali niyafanyie kazi," alisema

Hata hivyo alishauri mama huyo kwenda mahakamani au vituo vya haki za binadamu kwa ajili ya kutafuta haki kama anaona ameonewa.
Swali: Kumekuwepo na malalamiko mengi kuhusu polisi wa kituo cha Wazo Hill lakini hatujawahi kusikia tamko la serikali kwamba wanasingiziwa au la? Kunanini hapa? Kama Jijini watu wanaweza kutopata majibu, kijijini je?
 
Back
Top Bottom