Pitio la kitabu cha Khamis Abdulla Ameir sehemu ya tatu na ya mwisho

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,906
30,248
PITIO LA KITABU CHA KHAMIS ABDULLA AMEIR: ‘’MAISHA YANGU MIAKA MINANE NDANI YA BARAZA LA MAPINDUZI KHAINI AU MHANGA WA MAPINDUZI?’’
SEHEMU YA TATU NA YA MWISHO

Kila msomaji atachokisoma katika kitabu hiki kinatoka kwa mtu wa kuaminika ingawa wakati mwingine unaweza kuona tofauti ya taarifa kupishana.

Mathalan Mzee Aboud Jumbe amepata kunieleza kuwa Saleh Saadallah aliuawa kwa kuwa alitaka kumuua Mzee Karume kwa kumchomolea Mzee Karume bastola ndani ya kikao cha Baraza la Mapinduzi.

Khamis Abdulla Ameir katika hili ameeleza kuwa Saleh Saadallah tayari alikuwa katika ‘’hit list,’’ yaani orodha ya wanamapinduzi 14 waliotakiwa wauliwe.

Sababu ya hukumu hii ikiwa ni msimamo wao katika kuyaelekeza mapinduzi katika haki ili Zanzibar iwe nchi yenye utulivu na amani.

Khamis Abdulla Ameir katika kitabu hiki kaorodhesha majina yote.
Mimi sitayaweka hapa msomaji atayakuta majina haya ndani ya kitabu.

Nitayataja majina matatu tu kwa kuwa majina haya ni sehemu muhimu ya historia ya mapinduzi – Abdullah Kassim Hanga, Othman Shariff na hili la Saleh Saadallah.

Katika kitabu Khamis Abdulla Ameir anawaeleza hawa watatu kuwa walikuwa wanasiasa wa mrengo wa kushoto ndani ya ASP Hanga akishirikiana na Oscar Kambona katika mipango ya kufanya mapinduzi ukipenda mavamizi ya Zanzibar.

Kitabu hiki kitamuhangaisha kila mwanafuzi wa historia ya Zanzibar.
Mathalan kwa nini viongozi wa mapinduzi waorodheshwe katika orodha ya maadui wa mapinduzi na kuuawa?

Msomaji atajiuliza kulikuwa na tofauti gani kati ya Khamis Abdulla Ameir na hawa watatu.

Kwa nini ‘’Weird Brothers,’’ Abdulrahman Babu na Ali Sultan wanusurike hawakuwa katika orodha ile ya kuuliwa?

Hapa msomaji anaweza akajiuliza maswali mengi sana.

Je, Khamis Abdulla Ameir katupa majibu katika simulizi hii ya kuwapoteza wanamapinduzi wenzake?

Naamini kwa takriban nusu karne baada ya kifo cha Hanga wengi wamejiuliza, ‘’Kipi kilichosababisha Hanga kuuliwa khasa ikizingatiwa kuwa Hanga amefanya makubwa mosi katika kufanikisha mapinduzi na pili kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika?

Julius Nyerere alimwita Hanga ‘’mpumbavu.’’ Nini ulikuwa upumbavu wa Hanga?
Upumbavu wa Hanga ni kule kuitoa Zanzibar akampa Nyerere?

Ukimsoma Khamis Abdulla Ameir utakutana na kisa cha Hanga, Ahmed Sekou Toure, Nyerere na Karume ambacho hakikupata kuelezwa kwa ithibati na yakini kama alivyoeleza yeye.

Hiki ni kisa sijapatapo kukisoma au kukisikia popote pale hadi Theoretician alipokieleza katika kitabu hiki.

Nitadokeza kidogo.

Hivi Hanga hakuwa na akili ya kutambua kuwa kupanga kumpindua Mzee Karume ni sawa na kupanga kumpindua Julius Nyerere na kuhatarisha muungano?

Kisa hiki kimehitimishwa kwa kuuliwa Hanga.

Mauaji ya hawa wanamapinduzi Khamis Abdulla Ameir ameyaeleza Waingereza wanasema, ‘’in graphic detail,’’ na anataja jina la muuaji.

Hiki ni kitabu cha kutisha.

Maneno aliyosema mhanga mwingine wa mauaji, Othman Shariff kumwambia muuaji wake wakati imemdhihirikia kuwa anauawa yanaliza.

Hiki ni kitabu cha kutisha.

Kisa hiki kingeelezwa na mwingine yeyote awaye yule ningekisikiliza Waingereza wanasema, ‘’with a pinch of salt,’’ yaani tabu kuaminika.

Lakini kisa hiki kinatoka kwa Memba wa Baraza la Mapinduzi na yeye kakipata kwa mpashaji habari wa kuaminika. Khamis Abdulla Ameir kalamu yake inajua kuchokonoa mambo ambayo yatatabisha akili ya msomaji.

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali kuwa hiki si kitabu rahisi kukipitia na hii ndiyo sababu mambo mengi nimeyagusia tu na kumwachia msomaji ayasome kitabuni.

Mwandishi kwa kutambua kuwa yeye mwenyewe alikuwa ndani ya Baraza la Mapinduzi anafichua ukweli kuwa mauaji yaliyotokea yaliidhinishwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi si kuwa ulikuwa uamuzi wa wajumbe wote.

Ukimsoma Khamis Abdulla Ameir anavyoyaeleza mauaji haya tena kwa utulivu mwili unaingia baridi.

Yapo mauaji ambayo hayakuwa na uhusiano wowote na siasa kwa hiyo katika hali ya kawaida yasingepashwa kutokea kabisa.

Khamis Abdulla Ameir anasema hii ndiyo historia ya Zanzibar.
Khamis Abdulla Ameir kama nilivyogusia hapo juu ana kalamu chokonozi.

Khamis Abdulla Ameir anasema Zanzibar haiko huru na sababu ni muungano na Tanganyika; na anaeleza kuwa Karume alijuta kuungana na Tanganyika.

Maneno mazito na maneno fikirishi yenye kuumiza kichwa.

Zanzibar inajigamba kuwa huru baada ya mapinduzi. Khamis Abdulla Ameir anasema Zanzibar ni koloni la Tanganyika baada ya muungano.

Khamis Abdulla Amer anasema Wazanzibari katika Bunge la Muungano waliamrishwa kuwa kimya wasichangie chochote.

Khamis Abdulla Ameir anasema kuwa Zanzibar ilikuwa huru kuanzia siku ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza tarehe 10 December, 1963 hadi tarehe 26 Apil, 1964.

Baada ya hapo Zanzibar ilipoungana na Tanganyika Zanzibar ikawa koloni la Tanganyika na kupoteza utambulisho wake kama nchi huru.

Khamis Abdulla Ameir anaongeza kuwa kama hili lilikuwa halitoshi mwaka wa 1977 ASP ikaunganishwa na TANU.

Hapa ndipo Zanzibar ikapoteza uwezo wa kuchagua viongozi wake ndani ya nchi yao bila ya kuingiliwa na Tanganyika.

Khamis Abdulla Ameir anasema mapinduzi ni janga kwa Zanzibar kwa kuwa yamesababisha maafa makubwa kinyume na mategemeo waliyokuwanayo baadhi ya wanamapinduzi na Wazanzibari kwa ujumla.

Huu ndiyo uandishi ambao ulioko hivi sasa na msimamo huu inaelekea ndiyo msimamo wa makomredi wote wanaojitambulisha kwa wao ni wapenda maendeleo wanaopinga kila aina ya ubaguzi.

Katika fikra hii Khamis Abdulla Ameir ameibua jambo zito sana la uhalali wa madaraka yanayotawala Zanzibar kutoka mwaka wa 1964 hadi hii leo.

Hapa Khamis Abdulla Ameir anaeleza bila ya kupepesa matatizo ya kushindwa kuheshimu matokeo ya uchaguzi.

Swali kubwa ambalo bila shaka litataabisha vichwa vya wengi viongozi na wanaoongozwa.

Khamis Abdulla Ameir ametoa changamoto ya kuiangalia hali ya baadae ya Zanzibar na mapinduzi yenyewe katika kujenga demokrasia ya kweli ili Zanzibar isitawaliwe na viongozi ambao sanduku la kura limewakataa.

Ikiwa Zanzibar imepoteza uhuru wake na haiwezi kuchagua viongozi wake kwa kuingiliwa na Tanganyika nini maana ya hili?

Ikiwa serikali zote za Zanzibar zimeingia madarakani kwa kusaidiwa na Tanganyika nini pia maana ya hili?

Khamis Abdulla Ameir anahitimisha kitabu chake kwa kueleza kurejea upya kwa enzi nyingine mpya ya watu kupotea, kuteswa na kuuliwa baada ya Zanzibar kuingia katika siasa za vyama vingi.

Mwandishi anaeleza kuzuka upya watesaji raia wanaojulikana kama ‘’Mazombie.’’

Khamis Abdulla Ameir anaunganisha tatizo hili na hali ya baadae ya Zanzibar kama nchi yenye, ‘’Muslim majority,’’ yaani nchi yenye Waislam ni wengi.

Khamis Abdulla Ameir anasema kuwa Nyerere alifanya jitihada kubwa kuupa nguvu Ukatoliki Tanganyika ili uvunje nguvu ya Uislam na Waislam Tanganyika.

Anaendelea kwa kusema kuwa Nyerere alitaka muungano na Zanzibar kwa maslahi ya Ukristo.

Hapa swali linalojitokeza ni kuwa leo Wazanzibar kama Waislam wanasimama wapi na vipi katika hali kama hii?

Ukimsoma Khamis Abdulla Ameir katika fikra zake hizi swali linakuja ni hili kuwa inawezekana maadiliko ya upigaji kura yaliyojitokeza Zanzibar ya wananchi kuunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na upinzani kupata nguvu kila uchao ni katika mikakati ya kuirudishia Zanzibar heshima yake kupitia sanduku la kura?

Haya ndiyo yaliyomo ndani ya kitabu hiki, ‘’Maisha Yangu Miaka Minane Ndani ya Baraza la Mapinduzi Khaini au Mhanga wa Mapinduzi?’’

Hiki ni kitabu ambacho kinatakiwa kisomwe na kila Mzanzibari na Watanzania wote kwa ujumla wa na wasomaji wasiishie kusoma peke yake bali wakijadili kitabu na maudhui yaliyomo.

Mohamed Said
25 May 2022

Hapo chini ni picha ya pamoja ya Makomredi waliohudhuria uzinduzi wa kitabu:

1655662424510.png
 
SHUKURANI SANA mtaalamu wetu hazina kama wewe ni MUHIMU kwa history.Naomba soft copy ya nakala za baadhi ya vitabu
 
SHUKURANI SANA mtaalamu wetu hazina kama wewe ni MUHIMU kwa history.Naomba soft copy ya nakala za baadhi ya vitabu
Babluu...
Mimi mimi ni mwandishi tu.
Vitabu ni mali ya publisher yeye ndiye anaweza kujua mambo hayo.
Ninachofahamu vitabu vinauzwa madukani.
 
Abdullah Kassim Hanga. Oscar Kambona, Abdulrahman Babu, Captein Ali Sultan...and et al
Hawa walikuwa Autistic Genius with Asperger Syndrome...but the nation saw them differently and punish them.....Sad..☹️
 
Back
Top Bottom