Pinda: Serikali haikuwajibika ipasavyo

Mitomingi

Senior Member
Jan 15, 2008
130
0
Shadrack Sagati, Dodoma
Daily News; Friday,February 15, 2008 @07:10


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amekiri kuwa Serikali haikuwajibika ipasavyo ndiyo maana ikaundiwa kamati teule na Bunge kuichunguza juu ya mkataba wa kampuni ya Richmond iliyopewa jukumu la kuzalisha umeme wa dharura.

Akiahirisha Bunge mapema leo, Pinda alisema utaratibu huo unapata mwanya wa kutumika inapobainika kuwa sheria, taratibu na kanuni mbalimbali zilipuuzwa na serikali katika utendaji wake wa kazi.

Kitendo hicho kinaonyesha kuwa kuna mahali viongozi hawakutimiza wajibu wao na ndio maana Bunge halikuridhika na hali hiyo. “Kwa nini Serikali ifikishwe katika hatua ya kuundiwa kamati teule wakati inao uwezo mkubwa wenye utaalamu wa kutosha?” alisema.

Pinda alisema serikali imejifunza mengi kwani utaratibu huo wa kuunda kamati teule upo kwa lengo la kuwezesha tu uwapo kwa "checks and balances" ndani ya nchi.

Alisema jibu sahihi kwa serikali ni kufanya kazi kwa umakini na uadilifu mkubwa. “Kwa hiyo ahadi yangu kwa Bunge hili ni kuhakikisha timu hii mpya ya mawaziri inatimiza wajibu wake ipasavyo,” alisema.

Alisema mawaziri wasiile nchi ama kwa makusudi ama kwa uzembe kwani kufanya hivyo ni kuwasaliti Watanzania. Aliongeza kuwa dawa ya kweli kwa serikali kuepuka kuundwa kamati teule za Bunge ni serikali kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kutanguliza mbele uzalendo na
maslahi ya taifa.

“Vinginevyo kamati hizi zitaendelea kuundwa…serikali tujipange upya,” alisema Pinda ambaye hiki ni kikao chake cha kwanza kuahirisha Bunge akiwa Waziri Mkuu. Aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete baada ya Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na
kashfa ya Richmond.

Katika hotuba yake Pinda alizungumzia suala la chakula nchini na kueleza kuwa uzalishaji wa mazao ya nafaka kufikia tani milioni 5.5 badala ya tani milioni 6.2 hali ambayo imesababisha kuwapo kwa pengo la tani 828,093.

Alisema uzalishaji wa mazao yasiyo nafaka uliofikia tani milioni 5.2 wakati mahitaji ni tani milioni 3.7 umesababisha kuwa na ziada ya tani milioni 1.4 za mazao hayo hali ambayo inaondoa pengo la uhaba wa nafaka na kuwa na zida ya tani 626,817 za chakula nchini.

Pinda alisema kupungua kwa nafaka hususan katika maeneo yanayozalisha mahindi kwa wingi kumesababisha kupanda kwa bei ya mahindi. Alisema kupanda kwa bei ya nafaka kwa kasi kumesababishwa na kuongezeka kwa matumizi ya nafaka duniani katika uzalishaji wa
nishati.

Alisema hali hiyo imesababisha uhaba wa mahindi yanayoweza kuagizwa kutoka nje ya nchi. Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo haitegemewi kushuka kwa bei ya nafaka katika soko la dunia.

Waziri Mkuu alisema serikali imechukua hatua za kusimamisha kwa muda uuzaji wa nafaka hasa mahindi na mchele kwenda nchi za nje hadi Mei mwaka huu. Alisema hatua hiyo itasaidia chakula kilichopo nchini kuendelea kupatikana na pia kupunguza kasi ya kupanda kwa bei.

Pinda alisema umeondolewa ushuru kwa waagizaji wa mahindi kutoka nje ya nchi. Lengo ni kupunguza uhaba wa nafaka kwa kipindi hiki hadi Mei mwaka huu ambapo mazao mapya yataanza kuingia sokoni. Alisema tani 300,000 za mahindi zimeruhusiwa kuingizwa nchini bila kodi kati ya kipindi cha mwezi Januari hadi Mei 2008.

Kuhusu elimu aliitaka mikoa ambayo wanafunzi wake wamefeli zaidi katika mtihani wa kidato cha nne waongeze juhudi ili kuondokana na tatizo hilo.

Akizungumzia tatizo la kupanda kwa nishati ya mafuta, alisema serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuzalisha nishati mbadala kutokana na mimea. Aliongeza kuwa serikali ina matumaini kuwa jitihada hizo zitawezesha kupunguza kwa kasi fulani makali na athari za ongezeko la bei ya mafuta duniani.
 
Back
Top Bottom