2008-03-03 20:09:21
Na Mwandishi Wetu, Mpanda
Wale waliodhani Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bwana Mizengo Pinda ni mtu laini laini, basi wameula wa chuya kwani mzee ni mchungu kuliko hata shubiri na tayari ameanza kufyatua makucha yake na kuwaonyesha watendaji wababaishaji kuwa, yeye ni kiboko na kamwe hawatapumua chini ya uongozi wake.
Bwana Pinda ambaye wanaomfahamu wanamuelezea kuwa ni mtu mpole na asiyependa kabisa kujihusisha na dili chafu za kifisadi, ameonyesha makucha yake hayo baada ya kuwanyaka mafisadi wapya kibao na kuamuru hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Akihutubia mkutano mmoja wa hadhara uliofanyika wilayani Mpanda jana, Bw. Pinda amewataja mafisadi hao kuwa ni pamoja na vigogo walio katika ngazi za manispaa, Serikali za vijiji na zile za mitaa.
Akasema katika maeneo hayo, kuna baadhi ya viongozi ambao hujilimbuikizia mali haramu, kwa kuchota mapesa yanayotolewa na Serikali na kuchangiwa na wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kama shule.
Aidha, Bwana Pinda akaagiza kuwa kuanzia sasa, wakaguzi wa mahesabu watue kwenye maeneo hayo na kukagua mapato na matumizi ili yeyote atakayebainika kutumia pesa hizo isivyo halali, achukuliwe hatua kali za kisheria.
Vilevile amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watendaji vijijini kuwakamata wananchi na kuwaweka ndani kwa madai ya kutotoa michango, akisema kuwa kamwe hakuna sheria inayoruhusu unyanyasaji huo kwa wanyonge.
``Pinda kiboko. Kwa kuvalia njuga ufisadi huu unaofanyika kila kukicha katika manispaa na vijiji vyetu, ni wazi kwamba sasa mafisadi watakiona,`` amesema Bw. Daud Elias, mkazi wa Mpanda ambaye naye alihudhuria mkutano huo wa hadhara.
``Kauli yake inaonyesha wazi kuwa walaji sasa hawana chao. Wengi wataswekwa ndani ama kufilisiwa mali walizojilimbikizia kwa njia za kifisadi,`` akaongeza mkazi mwingine wa Mpanda aliyejitambulisha kama Mama Adam.
Hivi karibuni, Serikali imekuwa katika zoezi kabambe la kupambana na vitendo vya kifisadi, ambavyo kila kukicha vinaigharimu mabilioni ya pesa.
Mikataba bomu inayoingiwa na baadhi ya vigogo Serikalini kama ule wa Richmond, manunuzi feki na ulipaji mapesa wa kitapeli kama uliofanyika katika akaunti ya madeni ya nje, EPA ni baadhi ya vitendo hivyo vya kifisadi ambavyo Waziri Mkuu Pinda alishaapa kupambana navyo.
SOURCE: Alasiri