Pinda Ankwepa Nkapa

mwanaizaya

Senior Member
Apr 26, 2008
133
1
Pinda amkwepa Mkapa

Habari Zinazoshabihiana
• Nikichukua rushwa Mungu anichukue - Pinda 04.03.2008 [Soma]
• Mkapa sasa achunguzwa kwa ufisadi 25.04.2008 [Soma]
• Chukueni michango wakati wa msimu-Pinda 02.03.2008 [Soma]

Na Mwandishi Wetu

WAKATI Watanzania wakitarajia kusikia kauli yoyote ya serikali kuhusu utetezi uliotolewa hivi karibuni na Rais mstaafu Benjamini Mkapa kujibu kashfa za ufisadi zinazomwandama, jana Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alikwepa kuzungumzia jambo hilo, badala yake aliwataka Watanzania kutopakaziana rushwa kwa chuki binafsi.

Akizungumza na wananchi kijijini kwake Lupaso, Masasi, hivi karibuni, Bw. Mkapa aliwashambulia wanaomtuhumu kwa ufisadi na kueleza kwamba watu hao wana chuki binafsi na kwamba yeye si tajiri kama wanavyodai.

Bw. Mkapa, alisema wote wanaomwita fisadi, ni watu wa kupuuzwa kwa kuwa wana chuki binafsi naye kwani walikuwa na matumaini ya kupata upendeleo wakati wa utawala wake kitu alichosema, hakikufanyika.

Rais huyo mstaafu wa Awamu ya Pili alitoa kauli hiyo wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya tiba kwa uongozi wa Kituo cha Afya kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki kijijini hapo.

Aliwaambia wananchi hao kuwa yeye si tajiri na kwamba tuhuma zinazotolewa dhidi yake kuwa sasa ni tajiri wa kutupwa, ni za uongo na kuwataka kuzipuuza kwa kile alichosisitiza kwamba hazina msingi wowote.

"Sina uwezo wa, ingawa najua mnasikia na kusoma mengi ...naishi kwa pensheni yangu kutoka serikalini kutokana na kuwa kiongozi kwa miaka 10 ambayo hata Mzee Mwinyi ( Rais mstaafu wa Awamu ya Pili) anaishi hivyo maana sisi sote ni wastaafu," alikaririwa akisema Bw. Mkapa.

Bw. Mkapa amekuwa akihusiwa na kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kile kilichoelezwa, kufanya biashara akiwa Ikulu kufuatia usajili wa kampuni yake ya Tanpower Resources inayomiliki mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya .

Katika kile kilichodhaniwa kingefanyika, wananchi wengi walitarajia serikali kupitia Waziri Mkuu Bw. Pinda, jana ingetumia nafasi kuanzishwa Mbio za Mwenge wa Uhuru, kuzungumzia kwa kutolea ufafanuzi zaidi kauli hizo za Rais mstaafu Bw. Mkapa jambo ambalo halikufanyika.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa waliamini kwamba nafasi hiyo ilikuwa muafaka kwa serikali kuungana na kauli ya Rais huyo mstaafu, kukemea tuhuma hizo zinazomwandamana.

Bw. Pinda amekuwa kiongozi wa kwanza wa kitaifa kushiriki na kuhutubia katika shughuli ya kitaifa, siku chache baada ya Bw. Mkapa kutoa utetezi wake jambo ambalo wengi waliamini angezungumzia au kutolea ufafanuzi wa utetezi huo wa Bw. Mkapa kwa kina ili kuweka msisitizo.

Katika hutuba yake ya kuwasha Mwenge huo wa Uhuru katika kijiji cha Msoga, Kata Chalinze, mkoani Pwani alikozaliwa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, alisema mapambano dhidi ya rushwa siyo ya serikali pekee bali ni ya kila mwananchi na kuwataka wananchi kutooneana kwenye harakati hizo kwa sababu ya chuki binafsi.

Katika hotuba hiyo iliyotangazwa moja kwa moja na Televisheni na Redio ya Taifa, Bw. Pinda, alisema bila ya kushirikisha jamii nzima lengo la kuondoa rushwa nchini halitatimia.

"Serikali imetoa kipaumbele katika kukabiliana na rushwa nchini. Hata hivyo mapambano dhidi ya rushwa siyo ya serikali peke yake, mtu mmoja au taasisi moja bali ni ya kila mwananchi," alisema na kuongeza;

"Lakini katika kufanya haya yote, tusimwonee mtu kutokana na chuki binafsi. Tumesema Mbio za Mwenge zinatukumbusha kuondoa chuki miongoni mwetu. Hata hivyo mapambano haya yasiingize chuki binafsi kwa wenzetu."

Alisema miongoni mwa njia za kufuata ili kuepuka rushwa ni kuzingatia sheria na taratibu kwa kuepuka njia za mkato kupata huduma na kutowaonea aibu viongozi au watumishi wa umma na sekta binafsi wanaoomba au kupokea rushwa.

Mapambano dhidi ya Rushwa ni moja ya ujumbe wa Mbio za Mwenge mwaka huu. Ujumbe mwingine ni Hifadhi ya Vyanzo vya Maji, Mapambano dhidi ya UKIMWI na Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya.

Tangu ulipotangazwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992 mbio za Mwenge wa Uhuru, zimekuwa zikisimamiwa na Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana tofauti na miaka nyuma ambapo zilizimamiwa na kuratibiwa na umoja wa vijana wa CCM.

Katika siku za hivi karibuni viongozi kadhaa serikalini na taasisi zingine za umma, wakiwemo wastaafu, wamekuwa wakihusishwa na vitendo vya ufisadi hali inayowafanya wananchi wengi wa kawaida kutaka kujua hatma ya tuhuma hizo zikiwemo zile kuchota mabilioni ya pesa katika Akaunti ya Madeni ya Nje ( EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 
Back
Top Bottom