Donatila
JF-Expert Member
- Oct 23, 2014
- 7,557
- 21,497
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema taarifa nyingi za mjadala wa akaunti ya Escrow iliyofunguliwa kutokana na mgogoro wa malipo ya gharama za umeme kati ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) ambao unaendelea bungeni, umeongezwa chumvi na wakati ukifika Watanzania watatolewa taarifa kamili.
Kauli hiyo ya Pinda aliitoa kanisa kuu la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika wakati wa kumsimika Dk Jackson Chilongani kuwa Askofu wa Sita wa dayosisi hiyo.
Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Jacob Chimeledya aliitaka Serikali kutoa taarifa juu ya akaunti ya Escrow ili wananchi wajue kilichotokea ili ijulikane ukweli upi na uvumi upi kwani iko hatari ya kutengeneza taifa lenye kuamini uvumi.
Dk Chimeledya alisema Watanzania sasa wanaishi kwenye hali ya sintofahamu kwani hawajui yupi anasema ukweli na yupi ni `mzushi. Alisema ni lazima Serikali itoe maelezo kwa wananchi juu ya kashfa hiyo ili wajue kilichotokea kwani ipo hatari ya kutengeneza taifa linaloishi kwa kuamini uvumi.
Hatutakiwi kuishi kwenye taifa linaloamini uvumi taifa halitapiga hatua kwa taarifa za kusikia tu bila kujua ukweli uko wapi, nini kimetokea na hatua gani imechukuliwa, alisema.
Pia Askofu Chimeledya alitumia fursa hizo kuuzungumzia mchakato wa Katiba iliyopendekezwa na Bunge, akiitaka Serikali kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kupiga kura ya maoni Aprili mwaka kesho.
Alisema wananchi waachiwe waamue baada ya kuisoma katiba hiyo na si kuwafuata wanasiasa ambao wamekuwa na milengo tofauti kutokana na wengine kushawishi wananchi kupiga kura ya ndio huku kundi lingine likitaka Katiba hiyo kupigiwa kura ya hapana.
Alisema kama Serikali haitasimama imara kusimamia mchakato huo, basi utatekwa na watu wenye nia mbaya.
Makundi yote yakae kimya Katiba hii ni ya wananchi, waachiwe waamue na si kuwasemea watu wapige kura ya ndio au hapana.
Askofu huyo aliwataka viongozi wa kanisa hilo kuongoza vizuri kwani ni aibu kwa Mkristo au kiongozi wa kanisa kuharibu kanisa, kinachotakiwa kila mmoja kuchukua nafasi yake kuongoza kanisa vyema.
Akitoa salamu za Serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kuhusiana na kashfa ya Escrow na IPTL alisema taarifa nyingi zimeongezwa chumvi. Hata hivyo hakutaka kuingia kwa undani kuzungumzia suala hilo, huku akisisitiza kuwa, wakati ukifika Serikali itatoa maelezo ya kina na kuwafanya Watanzania wapate ukweli.
Sakata la madai ya kuchotwa kwa fedha katika akaunti ya Escrow ndilo linalotawala kwa sasa nchini, hasa baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Swerikali (CAG) kuwasilishwa bungeni, na sasa ikitarajiwa kujadiliwa bungeni kwa siku mbili kuanzia keshokutwa. Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, alisema Serikali itatoa nakala za kutosha za katiba hiyo ili wananchi wengi wasome na kupata fursa ya kutoa maoni yao.
Aidha, alisema Kanisa la Anglikana nchini limetoa mchango mkubwa katika kuendeleza huduma za jamii kwa kujenga shule, hospitali, vituo vya afya na miradi mingine ya kijamii. Pia aliutaka uongozi wa kanisa hilo kuibua fursa za miradi ya maendeleo ili kusaidia familia masikini kuwa na miradi midogo ikiwemo ya ufugaji kuku.
Kwa upande wake, Dk Chilongani aliahidi kuboresha elimu na huduma za jamii na kusimamia kikamilifu vitenga uchumi vya kanisa hilo.
Sikuota kuwa askofu ni neema ya Mungu, alisema.
Chanzo :Habari leo