Ambiente Guru
JF-Expert Member
- May 21, 2012
- 2,597
- 1,072
Jina lake jipya ni Hope au Matumaini. Akiwa na miaka 2 alidhaniwa na wazazi wake kuwa ni mchawi, Wakamtupa na kumtelekeza mitaani, akadhoofika vibaya kabla ya kuokotwa na mwanamama Anja Ringgren Loven kutoka Denmark . Sasa amepata mabadiliko chanya katika afya yake baada ya kupewa lishe na matunzo kwa wiki 8 toka wasamaria wemahuko Nigeria.
Chanzo: Daily Mail
Chanzo: Daily Mail
NI asubuhi ya Januari 31, 2016, mitaa ya kijiji fulani nchini Nigeria imetulia, watu wanaendelea na shughuli zao za kila siku, lakini kandokando ya barabara, jirani na rundo kubwa la taka, mtoto mdogo, ambaye mwili wake umedhoofika sana, amekonda na kubaki mifupa, nywele zimenyonyoka na mwilini ana vidonda vikubwa, anapigania pumzi zake.
Ameshapigania sana maisha yake kwa takribani miezi nane tangu alipotupwa hapo, kwa kuokota uchafu na kuula, lakini sasa ni kama anaelekea mwisho, hana nguvu tena, malaika mtoa roho hachezi mbali naye! Si kwamba watu hawamuoni, la hasha! Watu wengi wanapita jirani kabisa na hapo alipolala lakini hakuna anayethubutu kumsaidia kwa chochote.
Kila mtu anamuogopa, jamii imembatiza jina la mchawi, anaonekana kuwa laana kubwa kwa watu wanaoishi kwenye kijiji hicho, anaonekana kuwa mkosi mkubwa kwa wazazi wake, ndiyo maana ameachwa afe! Inasikitisha sana.
Akiwa katika hatua za mwisho kabisa za uhai wake, muujiza unatokea. Mwanamke wa Kizungu kutoka nchini Denmark, Anja Ringgren Loven akiwa na wenzake kutoka kituo cha kusaidia watoto waliotengwa kwa tuhuma za uchawi cha DINNødhjælp, A Land of Hope wanazunguka mitaani kuwatafuta watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Macho ya mwanamama huyo, yanatua kwa mtoto huyo aliyejilaza kando la rundo la taka, akiwa katika hatua za mwisho za uhai wake. Moyo unamuuma mno, anamsogelea mtoto huyo akiwa na wenzake, wanapojaribu kumsemesha, wanagundua kwamba bado yupo hai.
Harakaharaka wanamuinua kutoka hapo alipokuwa amelala, kitu cha kwanza anapewa maji ya kunywa, mwili wake hauna nguvu kabisa kiasi kwamba hata kunywa maji, analazimika kushikiliwa. Akiwa ananywesha maji, anapigwa picha ambayo baadaye inasambaa kwenye mitandao ya kijamii na kugusa mno hisia za mamilioni ya watu.
Huo unakuwa mwanzo wa safari ya kuokoa maisha ya mtoto huyo na mwanzo wa safari ya matumaini. Loven na wenzake, wanamchukua mtoto huyo mpaka Lagos, kwenye ofisi za kituo chao, wakaanza kumpa huduma ya kwanza ikiwa ni pamoja na kumsafisha mwili wake uliokuwa hautamaniki kisha akakimbizwa hospitali ambako alianza kupatiwa matibabu ya maradhi mbalimbali yaliyokuwa yanamsibu, kubwa ikiwa ni utapiamlo.
Taratibu mtoto huyo alianza kurejea kwenye hali yake ya kawaida, tabasamu lililokuwa limepotea kabisa kwenye uso wake, likaanza kuchanua upya taratibu huku afya yake ikizidi kuimarika, na hatimaye nuru ya uhai ikarejea kwenye uso wake. Baadaye, mwanamama Loven alimbatiza mtoto huyo jina la Hope ambalo ndilo analolitumia hadi leo hii.
Hiyo ndiyo simulizi ya kuhuzunisha ya mtoto Hope. Mwaka mmoja baadaye, Hope alikuwa amerejea kwenye hali ya kawaida, akiwa na afya njema na furaha kama watoto wengine, lakini kubwa zaidi akiwa ameshaanza masomo. Ukimtazama, huwezi kuamini kama ndiyo yule aliyeokotwa kando ya rundo la taka akiwa katika hatua za mwisho za uhai wake.
Hope siyo mtoto pekee aliyewahi kukumbwa na mkasa kama huo, bahati yake ni kwamba alipata bahati ya ngamia kupenya kwenye tundu la sindano, lakini kila mwaka, idadi ya watoto wengine kama Hope, wanapoteza maisha yao kwa imani za kishirikina. Katika baadhi ya maeneo nchini Nigeria, watoto wadogo wanapozaliwa, wazazi wao huwa makini sana kuwachunguza hatua moja baada ya nyingine kwa makini.
Inapotokea tu mtoto akawa na dalili zinazotia shaka, kama kulia sana usiku, kuanza kuota meno ya juu kabla ya chini na dalili nyingine zisizo na mantiki, huamini kama mtoto huyo anatumiwa na wachawi na uamuzi wanaoufikia, huwa ni kwenda kumtupa mbali, kisha kuachwa afe. Wengine huamua kuwaua kabisa kwa kile wanachoamini kwamba ni kuzuia wasipatwe na madhara ya uchawi kama mabalaa, mikosi na nuksi kwenye familia zao.
“Maelfu ya watoto wanaotuhumiwa kwa uchawi, wanateswa, kunyanyaswa, kutupwa na wengine kuuawa. Kazi kubwa iliyonileta Nigeria ni kuwasaidia watoto wa aina hiyo na mpaka sasa tumeshawasaidia wengine kama Hope na tunamshukuru Mungu kwamba jamii imeanza kutuelewa,” anakaririwa mwanamama Love.
Anaendelea kueleza kwamba ugumu wanaokutana nao, ni kwa jamii zilizowatupa watoto hao kuwaona kama maadui zao pindi wanapowachukua, kwa sababu huwasaidia wasife kama jamii hivyo zilivyotaka itokee.
“Wanatuona kama maadui kwao, wanaona tunaingilia mila zao kwa kuwaokoa watoto waliotakiwa kufa. Pia kwa mujibu wa sheria za hapa, unapomkuta mtoto akiwa katika mazingira kama aliyokuwa nayo Hope, ukimchukua na kuanza kumsaidia bila kupata vibali serikalini, unahesabika kama umemteka. “Kwa kawaida vibali huchukua muda kutoka na hii ni changamoto kubwa kwetu, tunashukuru serikali nayo hivi sasa inatupa ushirikiano mzuri.”
Tukio la mwanamama Loven kuokoa maisha ya Hope, lilisambaa sana mitandaoni na kumpa heshima kubwa mwanamama huyo ambapo kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alishinda tuzo ya World’s Most Inspiring Person 2016 ambayo alikuwa akiiwania sambamba na Barack Obama na Papa Francis wa Vatican. Pia amekuwa akipata mialiko kutoka kwa watu wengi mashuhuri duniani, akiwemo Obama, Dalai Lama na wengine.