Penzi la umauti

*PENZI LA UMAUTI-06*
Mtunzi: *Juma Hiza*


Baada ya miezi tisa kutimia Julieth alifanikiwa kujifungua mtoto wa kike ambaye niliamua kumuita jina la Glory. Nilimpongeza sana mke wangu kwa zawadi ile ambayo alikuwa amenipatia katika maisha yangu, nilimwambia kila aina ya maneno mazuri siku hiyo.

“Yani mke wangu siamini, hivi ni kweli leo naitwa baba?” nilimuuliza Mke wangu nilipokuwa nikizungumza naye kwenye simu, wakati huo alikuwa bado yupo hospitalini.

“Ndiyo mume wangu amini sasa hivi unaitwa baba,” alinijibu mke wangu kwa sauti iliyokuwa na furaha.

“Asante mke wangu ila pia pole najua umeumia kwa ajili yangu, nakupenda sana laazizi wangu,” nilimwambia.
“Asante mume wangu,” alinijibu kisha na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mazungumzo yetu.

Nilitawaliwa na furaha sana, sikutaka kuamini kama kweli nilikuwa naitwa baba kwa wakati ule. Huo ulikuwa ni ukweli ambao ulizidi kuniweka katika wakati wa furaha muda wote, sikutaka kuamini kwa kweli.

“Dominick, Dominick unaitwa baba,” nilijiambia kisha nikaanza kucheka kama mwendawazimu.

Japo ilikuwa imepita miezi mingi tangu Mama yangu aliponifukuza nyumbani kwake na kuniambia kuwa nisimtambue lakini sikuacha kumpigia simu na kumueleza tarifa zile, alionekana kuzipuuzia kisha hakutaka kubaki kimya akaniambia kuwa namba ile niione kuwa kama kituo cha polisi, nisiizoee.

Alifika mbali akaanza kumtukana mke wangu pamoja na mwanangu, malaika ambaye alikuwa hajui lolote kuhusu baba wala bibi katika hii dunia.

Nilizidi kushangazwa na matusi aliyokuwa akiyatoa Mama yangu dhidi ya mke wangu na mwanangu, nikajiuliza juu ya makosa ambayo walikuwa wameyafanya mpaka wakafikia hatua ya kutukanwa, hakukuwa na kosa lolote bali lilikuwa ni gubu la Mama yangu.

“Mama mbona unanitukania mke wangu na mwanangu kwani wamekukosea nini?” nilimuuliza Mama yangu baada ya matusi kumkoma.

Hakunijibu lolote mwisho akaamua kunikatia simu, kitendo kile kikaniweka katika hali ya sintofahamu, chuki alizokuwa nazo Mama yangu zikazidi kunishangaza. Nikajiuliza kama kweli yule alikuwa ni Mama yangu mzazi sasa kwanini anifanyie yale au hakuthamini uwepo wangu kama mtoto wake.

Inamaana hakutaka kujua lolote kuhusu mwanaye, ukimya wangu wa miezi yote niliyokaa kimya tangu pale aliponifukuza hakutaka kujua lolote, hakutaka kunisikiliza japo kwa sekunde kadhaa ambazo ningezitumia vyema kuzungumza naye.

Niliguna mara baada ya kukatiwa simu kwa wakati ule, nilihisi kukosea namba, akilini nikajiambia kuwa labda yule hakuwa Mama yangu mzazi hivyo nikarudia kuitazama ile namba vyema.

Naam! Ilikuwa ni namba ya Mama yangu Mzazi, sikutaka kuamini kama bado alikuwa na chuki na mke wangu tena chuki zake zilipitiliza kiasi kwamba akawa anamchukia na mwanangu ambaye hakuwa na hatia yoyote. Nilijaribu kumpigia simu kwa mara nyingine lakini haikupolewa mwisho akaamua kunizimia kabisa simu, ikawa haipatikani.

Sikutaka tena kuishughulisha akili yangu kuendelea kuwaza mambo ambayo yalikuwa yanaendelea kuniumiza kwa wakati ule ambao nilikuwa katika furaha, niliamua kuyaacha kama yalivyo na kama tatizo alikuwa ni Mama yangu nilipanga kutomsumbua tena kwa kumpigia simu wala kumtafuta kwa njia yoyote ile kama alivyokuwa akitaka nifanye. Nilifahamu fika kwa kuendelea kumsumbua ningezidi kujitafutia matatizo mengine.

****
Baada ya kupita miezi mitatu niliowaomba wazazi wa mke wangu niweze kumrudisha mke wangu na mwanangu kisha maisha yetu yaendelee kama kawaida.

Hawakuonekana kunipinga kwa lolote, walinikubalia ombi langu kisha wakaniruhusu nimchukue mke wangu.
Baada ya kufanikiwa kumrudisha mke wangu pamoja na mwanangu nyumbani maisha yaliendelea vizuri, nilikuwa nikifanya kazi yangu ya ufundi simu huku nikitegemea kipato nilichokuwa nikikipata kiniwezeshe kuilea familia yangu ambayo ilikuwa imeongezeka.

Nilimpenda sana mwanangu Glory ambaye kila nilipomtazama kwa mbali nilikuwa nikiiona taswira ya Mama yangu mzazi, alifanana sana Mama Dominick.
Maisha yaliendelea huku mwanangu naye akizidi kukua vyema.

Bado niliendelea kumficha mke wangu juu ya kile kilichokuwa kimetokea kwa Mama yangu lakini ni kama vile nilikuwa nikijaribu kuificha siri ambayo tayari ilikuwa ikifahamika na wengi, nilijidanganya.
Siku moja mke wangu aliniuliza swali ambalo liliniweka katika wakati mgumu sana wa kuweza kulijibu.

Aliniuliza juu ya ukimya aliyokuwa nao Mama yangu pamoja na tukio la kutokuja kumuona mjuu wake. Lilikuwa ni swali gumu ambalo liliniwia vigumu kutoa jibu kwa uharaka, nilibaki kimya huku nikiendelea kumtazama usoni kana kwamba sikuwa nimemsikia swali alilokuwa ameniuliza.
“Mume wangu,” aliniita.
“Naam,” nilimuitikia.

“Mbona Mama yako hataki kuja kumuona mjuu wake?” aliniuliza.
“Labda itakuwa ni ubize wake lakini atakuja kumuona usijali,” nilimjibu kwa kumdanganya uwongo ambao haukuwa na mashiko hata kidogo.

“Ubize inamaana ndiyo akose hata nafasi ya kuja kumuona halafu mbona nikimpigia simu hapokei kuna nini?” aliniuliza tena akinitazama kwa macho yaliyogubikwa na kila aina ya wasiwasi.
“Hapokei?” nikamuuliza huku nikijifanya kushangazwa.

“Vipi kwani wewe ulizungumza naye?”
“Ndiyo na tena aliniambia atakuja kumuona mtoto,” nilimwambia huku nikijitahidi kutomuonyesha tofauti yoyote ambayo ilikuwa imetokea na mwisho aliweza kuniamini, akaridhika na maneno yangu.

Maisha yaliendelea huku kila siku swali likiwa ni lile lile kuhusu Mama yangu, kwa kweli kuna kipindi nilikwazika moyoni hasa baada ya mke wangu kuzidi kung’ang’ania ujio wa Mama yangu. Kuna kipindi tulikuwa tukiingia katika ugomvi na sababu kubwa ilikuwa ni Mama yangu.

Mke wangu alikuwa hajui ni kitu kilichokuwa kikiendelea, kuna wakati nikatamani nimueleze ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea lakini nafsi yangu ilisita nikahisi ningeweza kuzua ugomvi ambao kwa kweli ningeshindwa kuuamua.
Kuendelea kuwaza na kujiuliza maswali lukuki bila kupata majibu yake ni sawasawa na kuteka maji katika tenga.

Niliamua kumueleza Chrispine kuhusu janga lile lililokuwa limeikumba ndoa yangu kiasi kwamba kuna kipindi furaha ilikuwa ikitoweka kabisa.
“Unajua kuna kitu kimoja unakosea Dominick,” aliniambia Chrispine huku akionekana kunisikitikia.

“Nakosea nini sasa?” nilimuuliza.
“Julieth kwani ni nani yako?” aliniuliza swali ambalo jibu lake lilikuwa wazi kabisa, nilihisi kama alikuwa akinikejeli.
“Ni mke wangu inamaana hujui?” nilimjibu kwa kumuuliza swali.
“Nafahamu ila inawezekana ukawa umesahau kuwa Julieth ni mkeo ukahisi labda ni mpenzi wako,” aliniambia maneno yaliyoniacha njia panda.

“Una maana gani?” nilimuuliza.
“Kwa ninavyojua mimi mpaka mnaamua kuishi kama mke na mume katika ndoa basi maana nyie ni kitu kimoja sasa kutakuwa kuna maana gani ya ndoa wakati matatizo yako unayafanya kuwa siri usiyotaka hata mkeo kufahamu au unataka kuniambia unaamini katika ule msemo wa kipumbavu eti! Changu ni changu?” aliniuliza.

“Hapana sio kama naficha lakini,” nilimwambia lakini kabla sijamaliza akanikata kauli.
“Lakini nini?”
“Namjua vizuri mke wangu, sitaki kumuumiza.

“Kuna vitu vya kuficha lakini si kama hili, mueleze ukweli mkeo ili aweze kujua ni cha kufanya wakati mwingine unaweza ukaona upo sahihi kuficha lakini baadae itakuja kukugharimu maisha ohoo,” aliniambia Chrispine maneno yaliyokuwa na maana kubwa sana.

Nilijiona kuwa sahihi kwa kile nilichokuwa nikikifanya, kumficha mke wangu ukweli wa jambo lile, niliamua kuuvunja ukimya nikapanga kumueleza mke wangu ukweli wote uliyokuwa umetokea mpaka kufikia hatua Mama yangu kunitafutia mwanamke mwingine ambaye alinilazimisha nimuoe, kwa kweli sikujua nilitakiwa nianzie wapi kumuelezea mke wangu ambaye alikuwa hafahamu lolote.

Je, nini kitaendelea?
 
*PENZI LA UMAUTI-07*

Nilipanga kumueleza ukweli mke wangu wala sikutaka tena kumficha, maneno ya Chrispine yaliiingia vilivyo mpaka nikajiona kuwa nilikosea. Nilianza kwa kumuomba msamaha kwa kosa nililokuwa nimelifanya, akaonekana kushangazwa na msamaha wangu, alinitazama kama mtu aliyekuwa katika mshangao wa kuitazama sinema ya kutisha. Nilifahamu nilikuwa nimemuacha njia panda hasa baada ya kumuomba msamaha wa kosa ambalo sikulikiri mbele yake.

“Unaniomba msamaha kwani umenikosea nini mume wangu?” aliniuliza huku akiendelea kunishangaa, sikutaka kumuacha aendelee kuwa katika mshangao ule sajari na hali ya sintofahamu iliyokuwa imemkumba ghafla! nikaamua kumuelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Hakutaka kuamini hata kigogo kwa kile nilichokuwa nikimueleza kuhusu Mama yangu na mambo aliyokuwa akinifanyia, akabaki akiwa ameyatoa macho yake mithili ya mtu aliyekuwa katika kabali nzito baada ya kusikia kuwa nilitafutiwa mwanamke ambaye nililazimishwa nimuoe kipindi kile ambacho alikuwa nyumbani kwao akiilea mimba.

Kama ilivyokuwa kawaida yake machozi hayakuwa mbali, yalianza kumdondoka huku midomo yake ikionekana kumchezacheza, alikuwa na maneno ya kuniambia lakini yalikwamishwa na kilio kilichomkumba ghafla! Nikapata kazi ya kumbembeleza mpaka pale alipotulia ndipo alipoweza kuzungumza.

“Dominick kwanini mama yako ananichukia kiasi hiki nimemkosea nini mimi?” aliniuliza kwa sauti dhaifu iliyokaribisha kilio kingine, akaanza kulia tena, nikamsihi anyamaze huku nikimfuta machozi yake.

“Dominick hivi nimemkosea nini mimi mama yako?” aliniuliza huku machozi yakiendelea kumbubujika mashavuni mwake. Nilipomtazama alinisikitisha mno, nikajikuta maumivu yakianza kunichoma katika moyo wangu.

“Hapana mke wangu usiseme hivyo,” nilimwambia kwa kumkataza, sikujua hata nilikuwa namkataza nini wakati ukweli nilikuwa tayari nimeshamueleza.
“Dominick mama yako hanipendi, hampendi hata huyu mwanao hivi unafikiri tutaishi vipi?” aliniuliza huku machozi yakiwa yamemjaa katika macho yake.

“Julieth mke wangu najua Mama yangu hakupendi lakini mimi ndiye ninayekupenda hivyo naomba usijisikie kuwa mnyonge, umesikia mke wangu,” nilimwambia lakini hakunijibu lolote, alibaki kuwa kimya huku akiwa ameyaelekeza macho yake chini, machozi bado yalikuwa yanaendelea kumbubujika.

Haikuchukua sekunde chache akainua kichwa chake kisha akanitazama, maneno yangu yalionekana kumuumiza sana.
“Dominick najuta hata kumzaa huyu mtoto,” aliniambia huku akiyafuta machozi yake.

“Mke wangu ndiyo maneno gani hayo unanayoniambia kwanini hutaki kuwa mwelewa, nimekwambia usijali lolote,” nilimwambia.

“Hivi kwa haya yote uliyonieleza bado niendelee kuishi na wewe kweli au unasubiri mama yako aje aniue ndiyo ufurahi?”

“Julieth mke wangu.”
“Naomba uniache,” aliniambia huku akionekana kujawa na hasira, hakutaka hata nizungumze lolotr, hakuwa tayari kunisikiliza tena.

Nilianza kujilaumu kwa uamuzi ule niliyokuwa nimeuchukua wa kumueleza ukweli mke wangu, moyo wangu ukaanza kumchukia Chrispine, nilimuona kuwa kama adui mwingine wa ndoa yangu yani ushauri kwa wake badala uiokoe ndoa yangu ndiyo kwanza ulienda kuiharibu na kwa wakati ule nilikuwa katika ugomvi na mke wangu.

Nilijitahidi kuomba msamaha lakini hakukuwa na msamaha, nilichukiwa ghafla! na mke wangu hata ile furaha ambayo ilikuwa imetawala katika maisha yetu ikapotea, hakukuwa na aman tena.
“Kwanini hutaki kunielewa mke wangu?” nilimuuliza wakati huo nilikuwa nimepiga magoti.

“Nikuelewe nini Dominick we nenda kamuoe huyo mwanamke aliyekutafutia mama yako,” aliniambia huku hasira pamoja na wivu vikiwa vimemtawala.

“Nakupenda wewe mke wangu huyo mwanamke kama ningekuwa nina nia ya kumuoa ningemuoa tangu ulipokuwa nyumbani lakini sikuwa tayari kufanya hivyo, nakupenda mke wangu,” nilimwambia.
“Nimesema Dominick naomba uniachee,” aliniambia.

“Kumbuka tuna mtoto hivi kama tukianza kugombana wakati huu unafikiri mtoto atakuwa katika misingi ipi?”
“Dominick sitaki kukugombanishe na Mama yako nende ukamuoe huyo mwanamke ili umridhishe mimi niache na maisha yangu.”

“Hiyo ndoto isiyoweza kutimia, siwezi kukuacha wala siwezi kuruhusu ukapotea katika maisha yangu, wewe ni mke wangu tafadhali naomba unielewe.”
“Nikuelewe nini?”
“Nakupenda.”

“Na mama yako je?”
“Mama yangu asikuumize kichwa, sisi tuishi maisha yetu kama yeye hataki basi ila sisi ndiyo tumependana na tayari tupo katika ndoa hivyo hawezi kufanya lolote,” nilimwambia.

“Niahidi,” aliniambia hapa alikuwa tayari ameshaacha kulia.
“Sitokuacha kamwe katika maisha yangu mpaka mwishi wa pumzi zangu,” nilimwambia.

“Kweli?” aliniuliza.
“Namaanisha,” nilimwambia.
Tuliendelea na Maisha yetu huku huku mawazo ya mama yakiendelea kufutika, sikutaka Mama yangu aendelee kuwa kikwazo cha ndoa yangu, nilifanya kila niwezalo ilimradi ndoa yangu iendelee kuwa salama.

Baada ya kupita mwaka mmoja nilihisi kuwa na kila sababu ya kubadilisha kazi, majukumu yaliongezeka na kama unavyojua tena swala la kulea mtoto siyo kazi ya mzahamzaha. Pale Kariakoo nilipokuwa nikifanya kazi yangu ya ufundi simu haikuwa ikinilipa sana kama hapo awali, maisha yalibadilika na kila siku ilikuwa ni afadhali ya jana.

Kuna kipindi tulikuwa tukishindia uji siku nzima huku pesa niliyokuwa nikifanikiwa kuipata nilikuwa nikiichanga kwa ajili ya kulipa kodi ya chumba. Maisha yalikuwa magumu sana, ukichanganya na uwepo wa mtoto tuliyekuwa naye ndiyo kwanza kichwa kilizidi kuniuma.

Nilimueleza mke wangu juu ya mpango wangu wa kubadilisha kazi akaonekana kuniunga mkono lakini pia hakuacha kunishauri,

“Kwanini usiangalie kazi ambayo inalipa ndiyo uifanye?” aliniuliza.
“Ni kazi gani hiyo?” nilimuuliza.
“Kuna biashara nimeifikiria,”aliniambia.
“Biashara gani hiyo?”
“Kwanini usifanye biashara ya kuuza mitumba nasikia inalipa,” aliniambia mke wangu.

Kwa kweli biashara hiyo ya kuuza mitumba ilionekana kuniingia akilini, nilitabasamu baada ya kusikia hivyo, sikuacha kumshukuru mke wangu ambaye ndiye aliyenipa wazo lile, hakutaka kunishukuru zaidi aliniambia kuwa lile lilikuwa ni jukumu lake kama mke kuhakikisha nafanikiwa katika maisha.
“Hivi mtaji wake ni shilingi ngapi?” nilimuuliza.

“Inategemea na uwezo wetu ila kwa kuanza itabidi ukanunue mzigo pale Ilala sokoni kwa bei rahisi halafu utakuwa unaenda kuwauza wateja mitaani mpaka pale ambapo tutapata mtaji kisha na sisi tutakuwa tukinunua kwa jumla na kuziuza kwa upana,” aliniambia mke wangu maneno ambayo niliyapitisha katika serikali ya ubongo wangu.

****
Niliamua kufanya rasmi biashara ya kuuza nguo za mitumba mitaani, biashara ambayo ilifanya watu wengi wanishangae kipindi ambapo nilikuwa nikianza hata rafiki yangu Chrispine alinishangaa sana na kuniona kuwa nilifanya maamuzi ya kukurupuka bila kuhitaji ushauri.

Kama walivyosema wahenga kuwa katika wengi kuna mengi pia ndivyo ilivyonitokea kipindi ambapo naanza kufanya biashara yangu ya kuuza nguo za mitumba mitaani.

Nilianza kusikia maneno ya watu wakisema kuwa nilifilisika kiasi kwamba niliamua kuacha kazi yangu ya ufundi simu Kariakoo nikawa muuza mitumba. Kila mtu alikuwa na lake la kusema.

Miongoni mwa maneno ambayo siwezi kuyasahau katika maisha yangu nayakumbuka mpaka leo katika kumbukumbu zangu ni siku moja nilisikia watu wakinizungumzia vibaya, walikuwa wakisema kuwa nililogwa na mke wangu ambaye alikuwa hana kazi yoyote Ati! Limbwata la mke wangu ndiyo lilikuwa linaniongoza niende kufeli katika maisha yangu ili tuwe sawa.

Je, nini kitaendelea?
 
*PENZI LA UMAUTI-08*

Maneno hayo yaliniumiza sana moyoni, sijui ni kwanini ila nilishangaa nikikosa uvumilivu, machozi yakaanza kunidondoka mfululizo. Nilikuwa nikilia machozi yaliyochanganyika na maumivu yaliyo ndani ya moyo wangu.

Siku moja majira ya usiku niliamua kumueleza mke wangu juu ya maneno niliyoyasikia kwa watu wakitusema vibaya lakini mke wangu mimi aliyeumbwa na upole, roho yake iliyochanganyika na ustahimilivu hakuacha kunena japo maneno ya kishujaa akiniambia mimi mume wake ambaye uvumilivu ulikuwa tayari umeshanishinda, kama ni maji basi yalikuwa yamenifika kooni.

“Mume wangu najua sio wote watakao tupenda kuna wengine watatuchukia hata hivyo hutakiwi kukata tama kumbuka tuna mtoto na anatutegemea kwa kila kitu, mimi sina kazi yoyote mume wangu angalau wewe umepata nafasi hii ya kuuza mitumba basi ifanye kwa bidii ili baadae izae matunda,” aliniambia mke wangu wakati huo alikuwa akiandaa chakula mezani, alikuwa amepika ugali na mboga ya kisamvu.

“Miongoni mwa vitu ambavyo najivunia katika maisha yangu ni kuwa na wewe katika maisha yangu, sijuitii kukuita mke wangu kwani kila ninapolitamka neno hili linanipa picha halisi ya mwanamke sahihi aliyeumbwa kwa ajili ya maisha yangu,” nilimwambia huku nikimtazama alipokuwa akininawisha mikono tayari kwa kula chakula alichokiandaa usiku ule.

“Ni wajibu wangu kama mkeo kuhakikisha nakuwa mstari wa mbele kutetea hitaji la moyo wako, kutetea ndoto yako na kuhakikisha kila ulilolipanga nakuwa nyuma yako kwa kila hali mpaka litimie,” aliniambia alipomaliza kuninawasha mikono kisha na nikampokea jagi pamoja na lile beseni dogo aliloninawishika, nikamnawisha.

“Asante mume wangu,” aliniambia mara baada ya kumaliza kumnawisha mikono yake, akaketi chini kisha tukaanza kula kwa pamoja, nilianza kwa kumlisha tonge moja, akacheka wakati huo mtoto wetu alikuwa ameshalala.

“Glory ameshiba kweli?” nilimuuliza mke wangu nilipomkumbuka mwanangu.
“Ndiyo nilimnywesha uji, ameshiba sana,” alinijibu mke wangu kisha tukaendelea na zoezi letu la kula ugali na mboga ya kisamvu iliyopikwa ikapikika.

Kila nilipokuwa nikimtazama Julieth usoni nilizidi kuiona taswira ya mwanamke mvumilivu ambaye alivumilia mambo mengi sana japo kuna kipindi alionekana kuchoka na kukata tamaa lakini hiyo haikuwa sababu ya kufanya mapenzi yetu yafutike, ndoa yetu ivunjike, hilo lilikuwa ni jambo gumu mno kuweza kutokea.

Niliendelea na biashara yangu mpaka pale ambapo nilifanikiwa kupata mtaji uliyoniwezesha na mimi kununua mabeli nikawa nauza kwa jumla jumla. Ilikuwa ni hatua nzuri niliyoipiga katika biashara yangu hiyo ukilinganisha na mwanzo ambapo nilipoanza.

“Hivi umewezaje kufanya haya yote?” lilikuwa ni swali la Chrispine huku akionekana kutoamini kwa hatua niliyokuwa nimefikia katika biashara yangu ya kuuza mitumba. Alikuwa bado akiendelea kuuza Cd katika duka lake Kariakoo, kwa upande wake biashara ilionekana kuwa ngumu mno.

“Ni mipango ndugu yangu,” nilimwambia.
“Mipango ipi tena wakati naona sasa hivi mambo yako sio mabaya,” aliniambia Chrispine huku akicheka.

“Kwa kweli mimi sikuwahi kuamini kama nitafanikiwa kufika hadi huku ila yote haya shemeji yako ndiyo kafanya mpaka yametimia,” nilimwambia kisha akaonekana kama kutoelewa lolote, nikaamua kumuelewesha kwa kirefu, akaonekana kuvutiwa na biashara ile niliyokuwa nikiifanya.

“Itabidi na mimi nianze kuuza mitumba aisee kule biashara imekuwa ngumu,” aliniambia Chrispine maneno ambayo alionekana kuyamaanisha kwa kila kitu.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kufanya biashara ya kuuza mitumba na Chrispine, aliamua kuniongezea mtaji na sasa tukawa kitu kimoja, tukaamua kufungua duka la pamoja Kariakoo, tukawa tunauza na kununua kwa wingi.

Biashara ikaonekana kukuwa kila siku na tulikuwa tunapata faida kubwa sana.
Baada ya kupita miaka mitano biashara ya kuuza mitumba ilikuwa imetupa mafanikio makubwa sana.

Nilikuwa nimefanikiwa kufungua duka langu la nguo pia niliamua kumfungulia mke wangu saluni ya kike pamoja na mgahawa na biashara zote hizo nilimuweka yeye ndiyo aongeze. Julieth alifurahi sana hakutaka kuamini kama kweli na yeye alikuwa anaitwa boss.

Wakati huo Mtoto wetu Glory alikuwa na umri wa miaka saba na tayari alikuwa ameshaanza kusoma darasa la kwanza katika shule ya msingi ya Ali Hassan Mwinyi.

“Jamani Dominick mume wangu nakupenda sana,” aliniambia huku akiwa amenikumbatia kwa furaha nilipomueleza kuwa biashara zote alitakiwa aziongeze.
“Nakupenda pia mke wangu,” nilimwambia kisha nikambusu shingoni.

Nakumbuka mpaka kufikia wakati huo nilikuwa nimefanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Vikindu na nilikuwa katika mipango ya kuanza kujenga, sikutaka kumwambia mke wangu kwa haraka, nilipanga kumfanyia Surprise kama wazungu wanavyosema.

Baada ya miezi kadhaa kupita huku biashara zikiendelea kupamba moto mke wangu alianza kuonekana kuhitaji kitu katika maisha yake, kuna kitu alionekana kukisubiri kwa muda mrefu sana na hakikuweza kutimia, aliamini kwa wakati ule ndiyo ulikuwa muda muafaka wa yeye kunieleza ili niweze kumtimizia.
Alitamani sana kuwa mwandishi wa habari, ndoto yake kubwa ilikuwa ni siku moja kuwa mwandishi wa habari mkubwa sana hapa Tanzania.

Hakutaka kunificha lolote lile lililokuwa likiendelea kumuumiza moyoni mwake, alinieleza kitu kitu na mipango yake ya kurudi shule ili aweze kuitimiza ndoto yake hiyo ambayo aliishi nayo kwa muda mrefu sana.
“Una uhakika utaweza kufanya vizuri?” nlimuuliza mara baada ya kunielezea malengo yake kwa wakati ule.

“Ndiyo mume wangu natamani sana kuwa mwandishi wa habari wa kidunia,” alinijibu huku akionekana kuwa na munkari kupita kawaida.
“Umepanga uanzie wapi sasa?” nilimuuliza.

“Itabidi nirudi shuleni ili nitafute cheti cha form four halafu nikajiunge na chuo kinachofundisha masomo ya uandishi wa habari,” alinijibu huku akionekana kudhamiria kufanya kweli yale aliyokuwa akinieleza.

Kwa kweli nilishindwa kumkatalia mke wangu kwa yale aliyokuwa akinieleza, maneno yake niliyachukulia kuwa kama zaidi ya taarifa muhimu ambayo nilitakiwa kuisikiliza kwa umakini na kuizingatia.

Nilimkubalia kila kitu alichokuwa akikihitaji kwa wakati huo kisha nikaanza kupanga mipango ya kumrudisha shule mke wangu.

Nilimpeleka katika elimu ya watu wazima Qualify Test (QT) ambapo aliweza kusoma na baadae kufanikiwa kumaliza na kupata cheti cha kidato cha nne. Hiyo ilikuwa ni zaidi ya furaha kwa mke wangu, hakutaka kuamini kama alifanikiwa kusoma na kupata cheti cha kidato cha nne.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho mahali hapahapa.
 
*PENZI LA UMAUTI-09*
*Mtunzi:Juma Hiza*

Upendo ulizidi kuongezeka pale ambapo niliamua kumpeleka chuo cha uandishi wa habari kilichojulikana kwa jina la Daresalaam school of Journalisim kilichopo Ilala.

Akafanikiwa kusoma kozi ya uandishi wa habari na utangazaji kwa muda wa miaka mitatu akamaliza.
Furaha ikazidi kumtawala mke wangu ambaye alitamani sana siku moja kuonekana kwenye runinga akitangaza habari au kipindi chochote ambacho angeweza kupewa akiendeshe.

“Kuna siku utaniona kwenye runinga mkeo nikitangaza taarifa ya habari,” aliniambia Julieth tulipokuwa tukitazama taarifa ya habari.

“Usijali mke wangu tumuombe sana Mungu kwani kwa Mungu hakuna kinachoshindikana,” nilimwambia huku nikijaribu kumkumbusha uwepo wa Mungu katika maisha yetu.

“Namuomba sana Mungu azidi kutujaalia maisha mazuri pamoja na mtoto wetu aendelee kukua vyema ili siku moja ajivunie kuwa na wazazi kama sisi,” aliniambia Julieth.

“Hilo ndilo jambo la msingi mengine huwa yanakuja yenyewe,” nilimwambia.
“Ila kuna kitu nataka nikuombe mume wangu,” aliniambia Julieth huku akiwa ananitazama kwa macho ya kuniuliza nikwambie.

“Kitu gani gani hicho?” nilimuuliza huku nikijiweka tayari kusikia hicho kitu.
“Nataka unichagulie jina zuri ambalo ungependa nilitumie nitakapokuwa mtangazaji,” aliniambia.

“Mimi napenda utumie jina lako hilo hilo.”
“Hapana itabidi nibadilishe jina mume wangu ili liwavutie wengi hata nitakapokuwa natangaza wapende aina ya utangazaji wangu.”

“Unataka ujiite jina gani sasa?”
“Nataka unichagulie wewe,” aliniambia Julieth kisha nikapata kazi ya kuanza kufikiria jina ambalo ningeweza kumpa na likampendeza.

Kichwani yalianza kunijia majina ya watangazaji lukuki ambao walikuwa wakavuma sana kwa aina ya utangazaji wao hata katika majina yao yalivutia mno.

“Sasa nikuite nani?” nilimuuliza.
“Fikiria jina lolote bhana mume wangu,” aliniambia Julieth huku akiwa umeupindisha mdomo wake kuashiria kuwa alikuwa ameanza kukasirika
“Ok ngoja nikuchagulie,” nilimwambia kisha nikanyamza kidogo nikafikiria halafu nikaendelea kuzungumza.

“Jiite basi Julie Pretyy,” nilimwambia huku nikitabasamu, nilifahamu fika nilimpa jina ambalo halikumpendeza, nikaamini hatalipenda hata kidogo. Ajabu akaonekana kulipenda, alifurahi sana kusikia hivyo.

“Ooooh! My God jina zuri sana nimelipenda mume wangu,” aliniambia Julieth mke wangu huku furaha ikiwa imemtawala.

Maisha yalibadilika kwa kiasi fulani kutoka katika maisha ya kushindia mlo mmoja kwa siku mpaka kufikia wakati ule ambapo tulikuwa tunauwezo wa kubadilisha mboga.

Kila nililoamua kulifanya kwa mke wangu niliamua kulifanya kwa moyo mmoja wala sikutaka mtu wa kunishauri lolote katika hilo. Niliamini katika mapenzi ya dhati ambayo nilikuwa nayapata kwa mke wangu, mapenzi hayo ndiyo yaliyosababisha nikaamua kumsomesha mpaka kufikia wakati akamaliza na sasa alikuwa akisubiri kupata kazi.

Alianza kuhangaika kutafuta kazi ya utangazaji katika vituo mbalimbali vya runinga na redio, kila alipokuwa akipeleka barua kwa ajili ya maombi ya kazi alikuwa akikosa, hilo likazidi kumuweka katika wakati wa mawazo, kuna kipindi alianza kukata tamaa, nikamsihi hakutakiwa kufanya hivyo kwani kila kitu kilikuwa na wakati wake hivyo asichoke kusubiri.
“Siamini kama kweli ndoto yangu itatimia,” aliniambia.

“Kwanini isitimie mke wangu muamini Mungu kila kitu kinawezekana,” nilimwambia.

“Kila ninapoenda kuomba kazi nakataliwa halafu bado unaniambia kila kina wakati wake hivi ni wakati gani huo usiyoweza kutimia.”

“Mke wangu hutakiwi kusema hivyo bali unachotakiwa ni kuwa na subira, kila kitu kitatimia,” nilimwambia.

Julieth alizidi kuhangaika kutafuta kazi huku na kule, hakuchoka na kama Mungu siku moja aliweza kupigiawa simu na namba ya simu ya mezani. Ilikuwa ni simu iliyomtaarifu kuwa alikubaliwa kufanya kazi katika kituo kituo cha habari kilichojulikana kwa jina la HIZA TV.

Taarifa hiyo ilileta furaha nyingine ndani ya nyumba bila kujua kuwa baadae nilikuwa naenda kumwaga machozi.
Hatimaye mke wangu akafanikiwa kuanza kazi katika kituo hicho cha habari cha televisheni kilichokuwa maarufu sana.

Nilifurahi sana kuona nimefanikiwa kuzitimiza ndoto za mke wangu kipenzi ambazo alionekana kuishi nazo kwa muda mrefu bila kutimia, hilo likanifanya nizidi kujivunia sana wala sikuona sababu ya kuacha kumpongeza mke wangu, nikampongeza kwa kumuahidi kuwa shabiki yake namba moja hasa katika kazi yake ya utangazaji redioni pamoja kwenye televisheni.

Julieth alinishukuru sana, hakutaka kuamini kama kweli alifanikiwa kusoma na kwa wakati ule alikuwa ameanza kazi ya utangazaji. Kila alipokuwa karibu yangu alizidi kunishukuru sana.

“Hapana mke wangu hupaswi kunishukuru kiasi hicho,” nilimwambia mke wangu.
“Yani siamini mume wangu kama kweli nimekuwa mtangazaji, ndoto yangu imetimia,” aliniambia huku furaha ikionekana kutawala uso wake, alifurahi mno.

Kwa kipindi hicho mtoto wetu Glory alikuwa ameshafika darasa la tano na katika upande wa malezi bora hatukuwa nyuma, tulihakikisha tunamlea katika malezi bora, hilo naweza kujivunia kwa wakati ule, niliishi vizuri na familia yangu wala hakukuwa na tatizo lolote.

Tulikuwa bado tukiishi katika nyumba ya kupanga lakini maisha yetu yalikuwa mazuri, mahitaji yote muhimu tulikuwa tukiyapata tena kwa wakati.

Sikuacha biashara yangu ya kuuza nguo za mitumba, niliendelea kuifanya huku nikiamini kuwa ilikuwa ndiyo kazi yangu mama ambayo ilinizalishia biashara nyingine ndogo ndogo.
****
Mke wangu alikuwa ni mtangazaji wa redio na tv katika vipindi vyake pendwa alivyokuwa akiviendesha. Alipendwa sana hasa kutokana na aina ya utangazaji wake, hilo lilinifanya nijivunie sana na kujiona kuwa mtabiri ambaye nilitabiri ukweli uliyoweza kutokea katika maisha ya kweli.

Kazi yake utangazaji ikaanza kumuweka bize mke wangu mpaka akawa anakosa muda wa kusimamia biashara alizokuwa akiziongoza hapo awali. Ikabidi nisaidiane nae katika kuziongoza biashara hizo wala hakukuwa na tatizo lolote lile.

Niliamini majukumu ya kikazi aliyonayo ndiyo yaliyokuwa yakimsababisha mpaka akawa anakosa muda wa kufuatilia biashara.

“Mume wangu usione nakuwa mzembe kufuatilia biashara siku hizi nakuwa bize sana,” aliniambia Julieth huku akionekana kutingwa na majukumu ya kikazi.
“Mke wangu naelewa hali uliyokuwa nayo kwasasa wala usijali,” nilimwambia.
“Nafurahi mume wangu kwa kunielewa,” aliniambia.

Hakukuwa na mtu niliyekuwa namuamini kama mke wangu, nilimuamini kupita kawaida wala sikuwa tayari kuona anatokea mtu anakuja kuuvunja uaminifu huo niliyokuwa nao kwa mke wangu. Nilimpenda sana na pia nilimuheshimu kwa kila kitu.

Katika kumbukumbu zangu sikumbuki kama kuna siku niliwahi kumsaliti mke wangu wala kuwa na chembechembe zozote za kutaka kumsaliti, nilijiheshimu sana na ndoa yangu niliyokuwa naipenda kuliko kitu chochote kile.

Uaminifu niliyokuwa nao kwa mke wangu ulimshangaza mpaka Chrispine japo yeye ndiye aliyekuwa mtu wangu wa karibu wa kunishauri mambo mengi sana kuhusu ndoa yangu.

“Dominick kama ikitokea siku watu wakaamua kutoa tuzo za uaminifu basi katika wanaume kumi bora wewe huwezi kukosekana,” aliniambia Chrispine huku akionekana kutabasamu.

“Kwanini unasema hivyo?” nilimuuliza.
“Sijui nikwambie nini ili kiukweli wewe ni muaminifu sana na ndoa yako,” aliniambia.

“Ni kweli unajua unapoamua kuingia katika ndoa inabidi ukubali kuacha mambo yote ambayo hutakiwi kuyafanya wakati ukiwa ndani ya ndoa,” nilimwambia.

“Julieth kapata mume aisee,” aliniambia Chrispine maneno ambayo yakatufanya wote tukacheka.

Siku hiyo tulizungumza mambo mengi sana kuhusu maisha, ndoa, biashara ila lilipofikia suala la Chrispine kumsifia mke wangu juu ya kazi yake ya utangazaji aliyokuwa akiifanya pamoja na changamoto ambazo angeweza kukutana nazo kidogo nilianza kuingiwa na wasiwasi lakini baada ya dakika kadhaa kupita ule wasiwasi uliniondoka.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho tena mahali hapahapa.
 
*PENZI LA UMAUTI-10*
*JUMA HIZA*


“Mbona kama umesita kidogo?” aliniuliza Chrispine.
“Hapana,” nilimjibu.

“Ila inabidi uwe makini sana na mkeo unajua hawa viumbe hawakawi kubadilika sasa hivi ameshakuwa mtangazaji wa tv na redio, anakutana na watu wengi maarufu na wenye uwezo wa kifedha zaidi yako, inabidi uwe makini sana usipoangalia unaweza kuja kuyadondosha machozi baadae halafu ukakosa wa kukufuta,” aliniambia Chrispine.

Sikutaka kuyachukulia maneno ya Chrispine kuwa kama ya kufikirika na kwamba yasingeweza kutokea kwa mke wangu, kwa kipindi kile ambapo alikuwa akinieleza kuhusu changamoto ambazo angeweza kukutana nazo mke wangu pamoja na aina ya watu mashuhuri aliyokuwa akikutana nao nilianza kuingiwa na wasiwasi, niliamini kuna ukweli ambao ulikuwa ukiishi katika maisha ya mke wangu ambapo kwa muda mfupi tangu alipoianza kazi yake ya utangazaji nilianza kuyaona mabadiliko makubwa sana.

Alianza kuchelewa kurudi nyumbani na kila nilipokuwa nikimuuliza alinijibu kuwa alipangiwa ratiba ya kutangaza usiku redioni jibu ambalo likanifanya nikubali bila kipingamizi chochote.

Nakumbuka kuna kipindi nilikuwa nikimsikiliza mke wangu redioni alipokuwa akitangaza na hata wakati mwengine kwenye Tv, nilijikuta nikianza kuwa mpenzi wa kusikiliza redio na kufuatilia vipindi vilivyokuwa vikirushwa kwenye Tv na yote sababu alikuwa ni mke wangu.

Nilizidi kumuamini mke wangu hata ule wasiwasi wangu ambao ulikuwa umeanza kuniingia moyoni ukaanza kupotea, sikutaka kumuonyesha mke wangu tofauti yoyote, niliamua kuyapuuzia mawazo yote mabaya niliyokuwa nikimuwazia mke wangu.

“Dominick mume wangu ni nini hivyo embu punguza wivu,” nilijiambia kisha nikajipiga kofi kuashiria kuwa nilikuwa katika mawazo ya kijinga.

Nilimuamini mke wangu kwa kuwa hakukuwa na sinema iliyokuwa ikiendelea nyuma ya pazia ambayo sikuwa nikiifahamu, alikuwa akinieleza ukweli wa kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake.

Ukweli wake aliyokuwa akinieleza juu ya wanaume waliyokuwa wakimsumbua ofisini ukanifanya nizidi kumuamini kabisa.

Nikawa nakesha kumuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumlinda na pepo baya la ngono ambalo lingeweza kumuingia. Sikuwa tayari kupokea maumivu ya usaliti moyoni.
“Mume wangu niamini nakupenda sana na ndiyo maana nakueleza ukweli,” aliniambia Julieth.

“Nakuamini sana mke wangu kuhusu hilo ondoa shaka kabisa,” nilimwambia huku nikiwa msisitizo wa maneno yangu.
“Mkeo ni mzuri sana eti na ndiyo maana nasumbuliwa na wengi ila mimi najiheshimu na kujilinda mume wangu,” aliniambia Julieth. Maneno yake ya upole yaliyoandamana na maana ya kile alichokuwa akinieleza yalizidi kuniteka vilivyo.

Alipoanza kubadilisha mavazi yake ya heshima na kuvaa nguo fupi nilimuuliza lakini hakukuwa na jibu lingine alilonijibu zaidi ya kuniambia kuwa kazi yake ilimuhitaji awe katika mavazi yale ili azidi kuwavutia mashabiki wakipende kipindi chake.

Sikutaka kujifanya mjuaji sana, niliamua kumuacha kama alivyo maadam aliniambia kuwa ananipenda na kuniheshimu basi hiyo ndiyo ilikuwa ngao niliyoishikilia siku zote.

Sasa kama alikuwa akinipenda kulikuwa kuna sababu gani za kutomuamini? Hilo ndiyo swali kubwa lililonijia katika kichwa changu, sikuwa na jibu kamili zaidi ndiyo kwanza nilizidisha mapenzi kwa mke wangu.

Baada ya kupita miezi kadhaa siku moja majira ya usiku mke wangu alirudi nyumbani akiwa na gari aina ya Land cruiser Prado lenye rangi nyeusi. Nilibaki katika mshangao mara baada ya kumuona mke wangu.

Sikushangazwa na uzuri wa mke wangu ambao kila siku ulizidi kuongezeka bali kitu kilichonishangaza ni aina ya gari alilokuja nalo. Nikakadiria hesabu ya miezi aliyokuwa nayo tangu alipoanza kazi yake ya utangazaji, alikuwa na miezi mitatu tu.

“Yaani ndani ya miezi mitatu ndiyo anunue gari lenye thamani kubwa kiasi hiki?” nilijiuliza swali ambalo jibu lake alikuwa nalo mtu mmoja tu! alikuwa ni mke wangu. Sikutaka kupoteza muda niliamua kumuuliza.

“Hili gari umetoa wapi?” nilimuuliza mara baada ya kushuka kwenye gari, nikashangazwa na kioja kingine. Ilikuwa ni udereva wake.

“Unajua kuendesha gari siku hizi?” nilimuuliza tena na sasa yalikuwa ni maswali mawili aliyotakiwa kuyajibu.
“Hee! Mume wangu hata salamu,” aliniambia huku akionekana kujiamini.
“Nimekuuliza hili gari umetoa wapi?” nilimuuliza.

“Nimehongwa,” alinijibu kwa dharau.
“Unasemaje?” nilimuuliza kwa ghadhabu.
“Unataka nikujibu nini wewe mwanaume,” aliniambia maneno ambayo yalinishangaza sana.

Kwa sinema aliyonionyesha Julieth ni dhahiri alikuwa amebadilika, sikutaka kuamini kile nilichokuwa nikikishuhudia, nilimtazama mara mbilimbili huku nisijue ni nini nilitakiwa nifanye.

Aliponiambia maneno yale hakutaka kuendelea kuzungumza na mimi, aliongoza moja kwa moja mpaka ndani.

Niliendelea kushangazwa na sinema niliyokuwa nikiendelea kuishuhudia, nikalitazama lile gari hakika lilinifanya nibaki katika wakati wa maswali yaliyokosa majibu.

“Ni nini hiki kinachotokea katika maisha yangu?” nilijiuliza kimoyomoyo kisha sikupata jibu lolote zaidi nilizidi kupandwa na hasira na nilijiapiza kuwa liwalo na liwe.

Niliingia ndani huku hasira zikiwa zimenitawala kichwani mwangu, nikamkumbuka mwanangu Glory ambaye alikuwa tayari ameshalala, sikutaka kufanya vituko vyovyote mbele yake hata vya kuigiza, niliamua kufanya hivyo ni kutokana na malezi bora ambayo nilipanga kumpa, sikutaka niwe chanzo cha kuyaharibi maisha yake kwa kumuathiri kisaikolojia.

Licha ya kuwa hasira zilikuwa zimenitawala lakini sikuwa na budi ya kuzipunguza, nakumbuka nilipanga kumpiga Julieth lakini nilishindwa kufanya hivyo.

Nilipoingia chumbani nilimkuta tayari ameshalala tena usingizi haswaa! nikajiuliza iliwezekanaje huo usingizi ukampata kwa dakika chache ambazo alikuwa ameingia ndani tena sidhani kama hata kuoga alikuwa ameoga. Tukio hilo likazidi kuniudhi.

Je, nini kitaendelea?
 
*PENZI LA UMAUTI-11*
*JUMA HIZA*

“Mke wangu,” nilimuita lakini hakuitika, nikanyamaza kama muda wa sekunde tano halafu nikamuita tena ndipo hapo alipoweza kuitika.

“Unasemaje mimi nataka kulala nimechoka,” aliniambia maneno ambayo yalinizidi kunikwaza sana moyoni.
“Unasemaje?” nilimuuliza.
“Sitaki usumbufu nataka kulala nimechoka,” aliniambia kwa sauti ya dharau maneno ambayo yalizidi kunichoma moyoni mwangu.

Siwezi kusema ni maumivu kiasi gani ambayo nilikuwa nikiyapata kwa wakati huo ni kama vile kulikuwa na msomaji ambaye alikuwa akinisimulia simulizi nzuri ya kimapenzi na kwa wakati ule alikuwa ameufikia ukurasa uliyobeba maumivu makali mno.

Nilivumilia mambo mengi sana na bado niliendelea kuyavumilia, naweza kusema kati ya wanaume waliyokuwa na mapenzi ya dhati kwa wake zao basi nilikuwa miongoni mwao. Licha ya mateso yote niliyokuwa nikipitia bado niliendelea kuvumilia huku nikijipa moyo yalikuwa na mwisho wake. Siku hiyo ikapita.
****

Siku iliyofuata majira ya asubuhi mara baada ya Glory kwenda shuleni niliamua kumuuliza mke wangu kwa kile kilichokuwa kimetokea siku iliyopita.
“Bado siamini kama umeninunia mke wangu hivi ni nini kimetokea?” nilimuuliza.

“Huamini nini sasa?” aliniuliza.
“Mbona jana nakuuliza kuhusu gari ulilokuja nalo hujanijibu lolote?”

“Unajua wewe ni mwanaume wa ajabu sana yani nakushangaa Dominick badala ya kunipa pole mkeo narudi kutoka kazini wewe una kazi ya kuulizia gari nimetoa wapi hivi umesahau kuwa mkeo sasa hivi nafanya kazi?” aliniuliza.

“Julieth mke wangu mbona mapema sana yani miezi mitati tu! umeshanunua gari?”
“Ni kitu gani ambacho unashindwa kukiamini hapo au unataka nizungumze lugha ipi ili uweze kunielewa.”

“Jana unakumbuka nilipokuuliza ulinijibuje?”
“Ndiyo nakumbuka.”
“Kwanini ulinijibu vile?”
“Unajua uliniudhi sana wewe hujui tu!” aliniambia Julieth kisha nikashindwa kuelewa ni kitu gani ambacho nilimuudhi.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuchanganywa na mapenzi, mapenzi yalikuwa yakinipeleka puta, nilishindwa kuamua lolote kwa mke wangu, alikuwa ameiteka nafasi kubwa sana.

Nilimkumbuka Mama yangu ambaye mpaka kufikia kipindi hicho sikuwa nafahamu lolote kuhusu yeye.

Tangu alipoweza kunifukuza nyumbani kwake na kuniambia kuwa nisimtafute kwa namna yoyote huku sababu kubwa ikiwa ni mke wangu kwa kweli sikuweza kumtafuta.

Nilikaa miaka mingi sana bila kuwasiliana na Mama yangu, nilifanya yote hayo nikiamini Mama yangu alikuwa na makosa. Kitendo cha kumchukia Mke wangu na kudai kuwa hakuwa mwanamke sahihi katika maisha yangu hakika kilinifanya nimchukie sana.

Nilimchukia mara baada ya kupata ushauri wa rafiki yangu Chrispine. Maneno yake yalinifanya nijione kuwa bora zaidi ya kila kitu na sikutakiwa kumsikiliza Mama yangu kwa lolote lile ambalo alikuwa akiniambia.

“Hivi nimefanya ujinga gani mimi?” yalikuwa ni majuto kwangu, nilianza kuona thamani ya maneno ya Mama yangu, Mama Dominick ambaye alikuwa ni mjane.

Kwa kipindi cha miaka yote hiyo sikufahamu ni nini kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake, nilimsusa kwa kiasi kikubwa sana na kwa kile kilichokuwa kimetokea katika ndoa yangu nilianza kuukumbuka uwepo wake, niliamini alikuwa na maneno mengi sana ya kunieleza mimi mwanaye.

“Nataka nijiandae niende zangu kazini,” aliniambia Julieth kisha akafanya kama alivyoniambia.

Bado nilizidi kuwa katika kiza kinene na sikujua ni nini kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.

“Julieth embu naomba tuzungumze kuhusu hili suala kabla hujaondoka,” nilimwambia alipomaliza kujiandaa na kwa wakati huo alikuwa anataka kuondoka.

“Nina haraka zangu please naomba tutazungumza nikirudi,” aliniambia huku akiitazama saa yake ya mkononi kuashiria alikuwa amechelewa.

“Dakika chache nipe ili niweze kuzungumza na wewe,” nilimwambia.
“Kwa sasa sina muda huo nina haraka labda tufanye kesho,” aliniambia.


“Kwanini hutaki kunisikiliza.”
“Sio sitaki tatizo lako sio muelewa,” aliniambia kisha akaondoka bila hata kuniaga.

****
Mateso ambayo nilikuwa nikiyapata kwa kweli siwezi kuyasimulia, nilianza kuwa mvivu katika kufanya kazi zangu hata katika biashara ya kuuza mitumba nilianza kuwa mtu wa kupata hasara kila kukicha, hilo lilimshangaza Chrispine ambaye yeye kwa wakati huo mambo yake yalikuwa mazuri tu.

“Una nini wewe?” aliniuliza siku moja alipoanza kuona tofauti.
“Mbona nipo kawaida hakuna kitu,” nilimjibu.

“Hapana kuna kitu sio bure unajua siku hizi sikuelewi kabisa maana hata katika biashara umekuwa ni mtu wa kuambulia hasara kuna nini?”

“Chrispine.”
“Niambie.”
“Kuna vitu sivielewi kwa mke wangu.”
“Vitu gani hivyo.”
“Unajua mpaka sasa nahisi nipo njia panda.”

“Kwanini?” aliniuliza.
Nilianza kumsimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea mpaka kufikia hatua mke wangu kumiliki gari ambalo hakuniambia lolote zaidi ya ugomvi na kunionyesha dharau.

“Ndugu yangu pole sana,” aliniambia.
“Bado sijapoa.”
“Piga moyo konde ndugu yangu.”
“Nashindwa kufanya hivyo Chris kiukweli nashindwa yani mpaka sasa sijui ni nini kinachoendelea.”

“Vipi kuhusu mwanao?”
“Hafahamu lolote na sitaki kwanza hafahamu.”

“Ndugu yangu ukisikia kua uyaone ndiyo haya, sasa hapa itabidi uanze kumchunguza mkeo ili ujue ni nini kinachomchanganya maana ukiendelea kuwaza mwisho wa siku utavuruga kila kitu.”

“Nitaanzia wapi?”
“Jifanye mjinga muache akutawale ila inabidi uishi kiakili ukiendelea kumsoma naimani mwisho wa siku utafahamu kila kitu.”

“Sijui kama nitaweza Chrispine unajua mpaka nimemkumbuka sana Mama yangu.”

“Ni lazima umkumbuke hasa kwa hili lililotokea lakini unajua wanawake ni viumbe wa ajabu sana,” aliniambia Chrispine huku akionekana kusikitishwa na kile kilichonitokea.

Nilishindwa kuelewa ni kitu gani nilitakiwa kufanya kwa mke wangu, alibadilika ghafla! na sikufahamu ni nini kilisababisha mpaka akawa katika hali ile.

Mwanzoni nilionekana kuipenda kazi ya mke wangu kwasababu nilishikiri kwa kiasi kikubwa katika kumsomesha mpaka kufikia hatua akapata kazi na miezi mitatu kupita baada ya kupata kazi ndipo mabadiliko yalipoanza.

Niliporudi nyumbani sikuweza kupata usingizi kabisa muda wote nilikuwa nikiifikiria ndoa yangu ambayo ilikuwa imeshaingia doa. Nilimtazama mwanangu Glory kama mboni yangu muda wote yeye ndiye alikuwa mfariji wangu kwa wakati ule.

Kuna kipindi kilifika Mke wangu akaanza tabia ya kutorudi nyumbani, hilo lilizidi kuniumiza sana na nilipomuuliza siku iliyofuata aliporudi nyumbani alidai kuwa amechoka na kazi yake ya utangazaji hivyo nimuache apumzike.

Wimbi la mawazo lililoambatana na upepo wa upweke ukanipitia, nilikuwa mnyonge mithili ya mkiwa. Sikuweza kufanya kazi, sikuweza kula, sikuweza kupata usingizi muda wote nilikuwa nikimuwaza mke wangu. Ama kwa hakika ndoa iikuwa imeniweka mahali pabaya sana. Nilishindwa kuwaza na kuwazua lolote.

Je, nini kitaendelea?
 
Julieth baada ya kupata, matako hulia mbwata sasa...

Anasahau kama Dominick ndiyo kamfikisha hapo alipo... inatia sana hasira...

Hiyo inaitwa fadhila mfadhili mbuzi... kashaona mume wake siyo level zake tena, yeye ni matawi...



Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom