Pendekezo la Wastani: Tuwapige wabunge makonzi! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Pendekezo la Wastani: Tuwapige wabunge makonzi!

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Mzee Mwanakijiji, Apr 29, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Apr 29, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Na. Lula wa Ndali Mwananzela (Raia Mwema)

  WAKATI umefika wananchi wapewe uwezo wa kuwakusanya wabunge wote na kuanza kuwapiga makonzi mmoja mmoja hadi pale wananchi watakaporidhika kuwa wabunge wanaelewa kwanini wanapigwa makonzi.

  Yawezekana unadhani umenisoma vibaya au nasema kitu ambacho hakina mantiki hata chembe. Ukweli ni kwamba baada ya kufikiria sana hasa baada ya kuzingatia utendaji wa wabunge wetu na mlolongo wa matukio kadhaa nimejihakikishia kuwa wabunge wetu wana ukosefu mkubwa wa maono, hawajifunzi kutokana makosa ya zamani, na wako tayari kuendelea kufanya mambo yale yale na kwa namna ile ile wakitegemea matokeo tofauti. Kwa vile hatuna njia nzuri ya kuwaadhibu wabunge nimeonelea makonzi ndiyo njia pekee ya kibinadamu ambayo inaweza kutumiwa na wananchi wote pasipo kusababisha malalamiko makubwa.


  Kwa wale wasiojua makonzi naweza kuelezea ni namna ya kumpiga mtu kichwani kwa kutumia ngoko za vidole vilivyokunjwa kama ngumi. Kuelewa konzi lilivyo inabidi uelewe jinsi ambavyo vidole vinakunjwa wakati wa kugonga mlango.


  Sasa namna ile inagongwa kwenye kichwa cha mtu kwa haraka na kumuacha asikilizie maumivu. Zipo aina kubwa mbili za makonzi (watu wengine wanadai zipo nyingine nyingi kutegemeana na utaalamu na uzoefu wa mpiga konzi!). Namna ya kwanza ni konzi linalopigwa kwa kukigonga kichwa kwa nyuzi 90, hili ni konzi la adhabu tu. Konzi moja la namna hii linatosha kumshtua mtu na kumkumbusha kitu alichosahau.


  Namna nyingine ambayo inahitaji utaalamu (usijaribu namna hii kwa watu wasio wabunge!) ni pale ambapo konzi linateremshwa kichwani kama kipanga anavyojaribu kukinyakua kifaranga cha kuku. Linateremshwa halafu linavutwa kidogo na kuwa kama kukwaruza. Konzi hili linadaiwa kuacha hisia ya maumivu kwenye ulimi!. Binafsi ningependa hili la pili ndilo litumike.

  Bila ya shaka bado huamini pendekezo hili. Tukishakukubaliana haki hii ya wananchi kuwapiga wabunge wetu makonzi (kwa vile tuliwachagua sisi nadhani tuna haki ya kuwawajibisha tunavyopenda hata kwa makonzi) ni lazima tufatute mahali muafaka pa kutekeleza wajibu huu badala ya kuwaachia wananchi majimboni wajifanyie wenyewe pasipo utaalamu na usimamizi wa kutosha.


  Napendekeza tufanyie kama kwenye Viwanja vya Jangwani Dar es Salaam ambako tungeweza kuwapanga wabunge wote hawa (wakuchaguliwa, wa kuteuliwa na wa viti maalumu) kwenye mstari mmoja (nadhani mistari miwili itafaa kuharakisha “shughuli” yetu) na wakaanza kupita mmoja mmoja na kupokea “chai” yao hiyo ambayo naamini (kama utakavyoona hapa chini) wanaistahili kabisa.


  Sasa tumekwishakujua adhabu na tumekwishakujua mahali pa kuwapa adhabu hiyo, hatuna budi kujua ni kiasi gani cha makonzi wanastahili. Kwa maoni yangu (sidhani kama unaweza kuyabishia) tuamue kupiga konzi moja kwa kila kipindi cha ubunge ambacho mtu amekaa bungeni. Hivyo, mbunge aliyekaa mhula mmoja anapata konzi moja na yule aliyekaa vipindi zaidi naye anapata makonzi kufuatana na idadi ya mihula yake. Hii ni kwa sababu waliokaa bungeni zaidi wanastahili adhabu zaidi na wale wanaoanza wanastahili kidogo! Naamini hili ni haki kabisa tusiwaadhibu wageni sawa sawa na wazoefu.

  Baada ya kupata adhabu, mahali na idadi ya makonzi bila ya shaka ungependa kujua kwanini nimependekeza adhabu hizi kwa wabunge na kama ni adhabu zinazofaa. Kwanza niseme kwamba adhabu hii ya makonzi kwa wabunge haitalalamikiwa na taasisi za haki za binadamu wala hakuna chombo ambacho kitasema adhabu hizi ni za kiudhalilishaji hasa ukizingatia kuwa tutahakikisha watoto wote chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kukaribia Jangwani.


  Kama hapo itaonekana ni “upenuni mno” tunaweza kuhamishia zoezi letu hili kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam au kama ni kule Dodoma tunaweza kufanyia kwenye Ukumbi wa Msekwa! Tutawapa uchaguzi wao waamue ni wapi wangependa tuliendeshe zoezi hili. Kwa vile hii adhabu ni haki yao na kwa vile wao ni binadamu basi tutawaambia watakaotuuliza kuwa tunawapatia tu “haki zao za binadamu”.


  Sasa twende kwenye sababu. Pendekezo hili kama nilivyosema awali linatokana na kufikia hitimisho kuwa wabunge wetu ni watu wasio na maono ya mbali, wenye uwezo mdogo wa kutatua matatizo ya Taifa, na kwa kiasi kikubwa ndio wamekuwa walezi wa matatizo yetu kwa muda mrefu. Kwa vile wao ndio wawakilishi wetu katika kuisimamia Serikali dalili zote za miaka hii iliyopita zinaonyesha kuwa kwa ujumla wao, wabunge wetu wameshindwa kushughulikia hata mambo ambayo yanawahusu wao wenyewe na ambayo kama wangekuwa na dakika chache za kufikiria wangeweza kuyatatua.

  Mfano mzuri ni tukio la hivi majuzi la Mbunge wa Vunjo Aloyce Kimaro kupata kiharusi na kukimbizwa hospitali Dodoma na baadaye Muhimbili. Kwa wengine jambo hilo linaonekana ni utaratibu wa kawaida, kwangu mimi naona ni dalili ya uzembe unaoweza kupewa tuzo ya Nobel!

  Ili nilisemalo lieleweke niwakumbushe juu ya ajali ya Mbunge Juma Akukweti aliyoipata kule Mbeya na baadaye kukimbizwa Muhimbili na baadaye Afrika ya Kusini, kwa mtu mwingine hilo ni jambo la “kawaida”; au nikumbushe ajali ya Profeasa Juma Kapuya ambaye naye alikimbizwa Muhimbili na baadaye kupelekwa India? Kwa wengine hilo nalo ni kawaida. Au hata nikumbushe juu ya ajali ya mwandishi Athumani Khamisi ambaye naye baada ya kupata ajali alipelekwa Muhimbili na baadaye akapelekwa Afrika ya Kusini? Naweza kutoa mifano mingine mingi.

  Kwa kiongozi mwenye fikra butu au mtu ambaye kwake mazingaombwe yanafurahisha zaidi kuliko kitu halisi haya yote ni mambo ya “kawaida”. Hawaoni tatizo. Hii ndio sababu ya kuwapanga mstari wapigwe makonzi ili kuamsha katika vichwa vyao uwezo wa kufikiria.

  Inawezekana vipi mahali ambapo wabunge na viongozi wa kitaifa wanakutana mahali pamoja hospitali yake haina uwezo wa kushughulikia mgonjwa wa kiharusi kwa huduma zote? Inawezekana vipi Makao Makuu ya nchi hayana uwezo wa kutoa vipimo vyote ambavyo vinaweza kupatikana mahali pengine duniani ukizingatia kuwa kuna wakati Rais, Makamu, Waziri Mkuu na viongozi karibu wote wa kitaifa na mabalozi wanakuwa Dodoma kwa wakati mmoja?

  Wabunge wetu wenye kupanga bajeti ya taasisi zote za umma, wenye kutunga sheria zetu na wenye uwezo wa kusimamia Serikali wameshindwa kufikiria kuipa uwezo hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kuhakikisha kuwa ina uwezo wa kushughulikia na kutoa vipimo vya aina zote hasa vya magonjwa ambayo yanafahamika sana, moyo, kiharusi, shinikizo la moyo, ajali n.k! Kwanini tusiwapige makonzi kuwakumbusha?

  Au nitoe mfano mwingine ambao kwa wabunge wetu na Watanzania wengine wanaona ni mambo ya kawaida! Mara kwa mara utasikia wagonjwa wamepelekwa nje kwa matibabu kwa magonjwa mbalimbali hasa watoto huko India.


  Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Profesa David Mwakyusa (msisahau na yeye ni mbunge) tumetumia karibu shilingi bilioni 19 kwa miaka mitano iliyopita (kuishia Februari mwaka huu) kupeleka wagonjwa nje ya nchi kutibiwa. Tunaambiwa kuwa matibabu ambayo yanafanya tupeleke wagonjwa wetu huko ni pamoja na mishipa ya fahamu, saratani, uti wa mgongo, figo n.k


  Sasa haya yote ni mema. Lakini kwa miaka karibu 50 wabunge wetu wameshindwa kuweka kipaumbele cha kutatua matatizo haya! Hivi bilioni 19 miaka minne kwa miaka 50 hii wametumia kiasi gani? Halafu wapo watu wamekaa bungeni miaka 40!! Kwanini tusiwapige makonzi kuwaamsha?

  Au nitoe mfano wa jambo jingine linalohusiana na haya haya ya afya. Kwanini Tanzania haina Hospitali ya Taifa ya Watoto? Sijasema “wodi ya watoto!” vinginevyo ntaanza kupiga makonzi na wasomaji vile vile. Kwa taifa la watu milioni 40 ambalo linakutwa na majanga ya kila namna, na mahali ambapo kuna magonjwa ya kila namna ya watoto au yanayowasumbua watoto kwanini kwa miaka karibu 50 hatujajenga hospitali ya rufaa ya watoto!?

  Kwamba kati ya wagonjwa wote1380 waliopelekwa nje miaka hii mitano iliyopita 996 walikuwa ni watoto. Tukienda kwenye hospitali zetu mbalimbali tutawakuta watoto wenye matatizo mengi ya kiafya na wengine ambao wangehitaji uangalizi maalumu wa wataalamu wa magonjwa ya watoto lakini karibu wote wanahudumiwa na madaktari wa kawaida. Hivi tukiwauliza wabunge wetu mahitaji yetu ya madaktari ya watoto ni kiasi gani wanaweza kutuambia? Kwanini tusiwapige makonzi?


  Niulize nini tena? Bila ya shaka wengi mmekwishakusikia juu ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ambayo kwa mwaka mwingine imerudia baadhi ya mapendekezo yale yale ya miaka karibu minne iliyopita. Fikiria ati wanapendekeza wabunge wasiwe wajumbe wa bodi! Pendekezo lililotolewa na kurudiwa sijui mara ngapi na Rais Jakaya Kikwete mwenyewe kukubali ukweli wake.

  Lakini mawaziri hao hao (ambao nao ni wabunge) wameendelea kuwateua wabunge kuwa kwenye bodi mbalimbali za mashirika ya umma! Ni kana kwamba kuna kamdudu kausahaulifu kamewashikilia. Kwanini lisitolewe tu agizo moja kuwa wabunge wote walio kwenye bodi mbalimbali wamepoteza nafasi zao na mawaziri wazijaze kwa kuteua watu nje ya wabunge? Hilo haliwezekani hadi tuwagonge kwenye vichwa vyao kwanza!

  Sasa kwa vile nina uhakika pendekezo hili haliwezi kukumbatiwa hasa ukizingatia kuwa wabunge wenyewe ndio vigogo wenyewe wa nchi hii, na kwa vile pendekezo hili linaweza kuonekana ni la msimamo mkali nimefikiria labda tunaweza kubadilisha makonzi haya na kuyaweka katika mtindo ambao wananchi wataweza kuutumia bila kushtakiwa kwa kufanya mashambulio au kuwaabisha watu wazima kwa kuwakwangua vichwa vyao kwa makonzi!


  Pendekezo hili linaweza kuwa kali lakini nadhani tukiliangalia kwa namna tofauti linaweza kuwa linafaa. Kwa hiyo napendekeza haya makonzi ambayo tungeweza kuwagonga kwenye vichwa vyao tuyabadilishe na yawe ni kura. Kila konzi moja liwe sawa na kura moja ambayo tutamnyima mgombea ambaye hatumtaki. Kuna wabunge ambao hawastahili kupata kura hata za kwao wenyewe. Kwanini wabunge hao tuwape nafasi hata ya kupita kujiuza tena?


  Naamini Watanzania wanaweza kuamua kuwapiga makonzi wabunge hawa wote kwa kutowapigia kura, kwani hakuna kitu kinachowauma vichwani kama kukosa kura! Ndiyo maana wanajipitisha pitisha na kujibaraguza na wengine kuanza hata kuonyesha heshima kwa wananchi.


  Makonzi ambayo hawatasahau uchungu wake ni yale ya kukosa kura. Tusiende kwenye mikutano yao, tusipokee rushwa yao ya uchaguzi a.k.a misaada ya nyakati za majeruhi, na wakati ukifika tuwanyime kura.

  Nimeanza kufikiria orodha ya wabunge hao ambayo nikiamka vizuri wiki chache zijazo nitawawekea hadharani ili tujue kabisa kwanini wabunge hao hawastahili kurudi tena bungeni. Kama hatuwezi kuwashika vichwa na kuwakwangua kwa makonzi ya vidole vyetu, nina uhakika tunaweza kuwasumbua vichwa tukiwatimua kwa kutowapigia kura!!


  Kama unaushauri mwingine niandikie: lulawanzela (kwenye) yahoo.co.uk
   
 2. Felixonfellix

  Felixonfellix JF-Expert Member

  #2
  Apr 30, 2010
  Joined: Feb 16, 2010
  Messages: 1,680
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Hii niliisoma kwenye Raia Mwema
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  May 3, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Ndiyo ilitoka kwenye raia mwema!
   
 4. Kisoda2

  Kisoda2 JF-Expert Member

  #4
  May 4, 2010
  Joined: May 30, 2008
  Messages: 1,240
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Kwenzi la kura lina uma sana.
  Ila wasiwasi wangu wanaweza kuja na helmet yao waliyoizoe kila mwaka "CHAGUA CCM" hii mara nyingi wanawapata waliowengi kwa ubwege wa kuto fikiria ni nani mwakilishi wa hii CCM ninayoichagu.
  Na hapa ndipo inatufikisha kuwapata wabunge vihiyo wasoamka wenyewe mpaka tuwaamshe.

  Tutafika tu,siku si nyingi.
   
 5. m

  mageuzi1992 JF-Expert Member

  #5
  May 13, 2010
  Joined: Apr 9, 2010
  Messages: 2,512
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  Makonzi tu! Tuwazabe vibao pia!
   
 6. Kite Munganga

  Kite Munganga JF-Expert Member

  #6
  May 13, 2010
  Joined: Nov 19, 2006
  Messages: 1,298
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 145
  Helmet? kama ni hivyo basi wanatakiwa wapigwe Konzi kwa kutumia kitako cha Shoka
   
 7. Ringo Edmund

  Ringo Edmund JF-Expert Member

  #7
  May 13, 2010
  Joined: May 10, 2010
  Messages: 4,895
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 0
  mimi napendekeza mitama a.k.a ngwara ili walambe na vumbi
   
Loading...