Pendekezo la Maridhiano Juu ya Lowassa (A Proposal on Compromise): Kutoka Hapa Kwenda Kule...(2015)*

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,988
PENDEKEZO LA MARIDHIANO: KUTOKA HAPA MPAKA KULE (2015)+

Note: Hii nayo ni makala ndefu, unaweza kudownload nakala ya kuchapa hapa chini.

1.png



Na. M. M. Mwanakijiji

UTANGULIZI

Waziri Mkuu wa zamani Bw. Edward N. Lowassa ambaye anamaliza pia muhula wake wa Ubunge wa Monduli ana haki zote zakugombea nafasi yoyote ya uongozi anayoitaka katika Uchaguzi Mkuu unaokuja Oktoba 25, 2015. Hili halibishaniwi. Kwamba alitumia haki hiyo kutafuta kwa nguvu kubwa kama mafuriko nafasi hiyo ndani ya Chama cha Mapinduzi ikashindikana hili nalo halijibishaniwi. Kwamba, baada ya jina lake kukatwa (kama wengine tulivyopendekeza bila kuomba radhi) akaamua kutumia haki hiyo hiyo kutafuta mahali pengine pa kutokea na akapapata CHADEMA hili nalo halina mjadala. Kwamba, sasa amepata nafasi hiyo ya kutimiza ndoto yake kupitia CDM hili nalo siyo suala la kujadiliana sana.

Kwamba, sasa kwa vile yule tuliyempinga na kuonesha kuwa ni miongoni mwa viongozi wasiofaa Tanzania (rejea mada zangu kadhaa nyuma) sasa amebeba bendera ya mabadiliko ambayo tulidhani itabebwa na wale ambao tunajua ni viongozi bora zaidi hili limezua mjadala. Mimi yawezekana nikawa mtu ambaye nimempinga Lowassa na aina ya uongozi wake kiasi kwamba hata kufikiria kuwa naweza kutoa hoja ya mapendekezo ya maridhiano itakayomwacha Lowassa kugombea na kuungwa mkono na mtu kama mimi napata hisia siyo tu ya kula matapishi yangu bali kula vibaya zaidi ambavyo havijatokea mdomoni.

Mjadala ambao umetokea katika siku hizi chache kwenye mitandao ya jamii na kwa upande wangu mawasiliano yangu na viongozi mbalimbali ndani ya CDM – ambao wanajua msimamo wangu kuhusu Lowassa – umenifanya nifikirie mambo mengi na kuona kama kuna namna yoyote naweza kupatanisha (reconcile) ukweli ambao nimeufikia na matamanio ya kuona CCM iondolewa madarakani. Watu wengine wanafikiria – kwa makosa makubwa – kwamba sijui au wengine kama mimi hawajui ni kitu gani kinapiganiwa hapa.

Ni kwa sababu hiyo mapendekezo haya ya maridhiano yana lengo moja tu kujaribu kusogeza pande hizi mbili zinazotofautiana sana kuhusiana na suala la Lowassa kubeba bendera ya CDM badala ya mtu ambaye kwa muda wa miaka tuliaminishwa kuwa ameandaliwa kugombea tena – Dr. Wilbrod Slaa. Baadhi yetu hatukushtushwa na Lowassa kuondoka CCM na kujiunga na chama cha upinzani akijaribu kuendeleza safari yake ya matumaini; tulishtushwa kwa sababu chama alichochagua ni CDM. Hakukuwa na sababu yoyote ya kiakili ambayo ingetosha kuelezea kwanini Lowassa aliingia CDM na wao wakamkubalia kirahisi sana bila kufikiria matokeo yake mbalimbali.
Lengo langu basi ni kujaribu – kwa kadiri ya uwezo wangu – kuonesha kuwa wakati Lowassa ana haki ya kugombea nafasi yoyote na CDM ina haki ya kumpokea yeyote na kumtumia watakavyo wananchi, wanachama, mashabiki na wapenzi hawana ulazima wa kumkubali bila kuuliza, kumpokea bila kumhoji, au kukubali uamuzi wa viongozi bila kuwauliza na hata kuwakatalia.

HAKI YA KUPINGA

Demokrasia ya kweli haijengwi kwa kuona jinsi gani watu wanakubaliana na kuwa na misimamo ya aina moja au mawazo ya aina moja. Mojawapo ya hoja ambazo zimetolewa sana baada ya baadhi yetu kupinga ukaribisho wa vigelegele wa Lowassa ni kuwa ati tunawagawa watu wakati tunatakiwa wakati huu tuwe wamoja. Kwamba, tusitoe mawazo yetu yenye kupingana na mawazo ya viongozi au wanaojidhania wengi kwa sababu kwa kufanya hivyo tutawagawa watu. Hii mojawapo ya hoja muflisi kabisa kutolewa!

Mahali pekee ambapo watu wanatakiwa kuwa na imani, mawazo na fikra za aina moja ni kwenye masuala ya dini na imani ya Mungu na hata huko watu hawako na mawazo ya aina moja. Sehemu nyingine ambapo watu wamejaribu kujenga jamii yenye kukubali mawazo ya viongozi tu ni kwenye tawala za Kikomunisti na hata huko watu wamekufa, kufungwa na wengine kufanywa duni kabisa kwa sababu hawakukubali kujipanga mstari na kusema "ndiyo mzee". Sipendi, na tena sitaki kabisa kusikia ati watu wanaosema wanaamini katika demokrasia ndio wanakuwa wa kwanza kutaka watu wasiwapinge ati kwa vile wakiwapinga watu wanaweza kugawanyika! Haki ya kupinga (the right to dissent) ni haki ya msingi sana katika utawala wa kidemokrasia. Hili nimeshawahi kuliandika nyuma kwenye sakata la Zitto Kabwe na viongozi wa CDM.

Kwa hiyo, tusiogope watu wanapotupinga kwa hoja na tusijaribu kujibu hoja kwa vihoja au viroja! Wakati mwingine ni wale wenye kupinga – hata kama ni wa kundi dogo (minority) ndio hao hao wanaweza kuwa ndio wako sahihi hata kama hatuoni usahihi wao sasa.

HALI HALISI

Hali halisi ni kuwa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo imechukua uamuzi ambao haukuwa umefikiriwa miezi michache nyuma tu kama siyo wiki chache. Uamuzi wa kumchukua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Mbunge wa Monduli Mhe. Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa Urais kuelekea Uchaguzi Mkuu. Mazingira ya uamuzi huu ni vigumu kuweza kuyaelezea na kumridhisha kila mwanachama, mpenzi, shabiki au kila mtu Tanzania. Kwa wengine uamuzi huu ni jibu la matamanio ya kutaka kuiondoa CCM madarakani na kwa wengine ni uamuzi huu umeonesha jinsi gani katika kuridhisha matamanio hayo Chama kimekubali kuvunja na hata kuacha misingi yake kwa ajili tu ya kupata ushindi kwa gharama yoyote.

Hali halisi ni kuwa kumchukua na kumsimamisha Lowassa kama mgombea wa Urais inawezekana kuwa ni uamuzi wa kimkakati zaidi (the most strategic decision) kuweza kufanywa na chama cha upinzani Tanzania hasa kwa vile chama chetu ndicho kilichosimama na ajenda ya kupinga ufisadi ambao unahusisha siyo tu ubadhirifu bali pia matumizi mabaya ya madaraka, uvunjaji wa sheria n.k Lowassa kwa muda mrefu amekuwa sehemu ya mfumo ambao ndio umeliingiza Taifa kwenye kashfa mbalimbali, tangu Loliondo hadi Escrow. Kwa muda wote ambao tumepigia kelele kashfa hizi mbalimbali hakuna ushahidi wowote wa Mheshimiwa Lowassa kusimama upande wetu ama akiwa Waziri Mkuu au akiwa Mbunge wa kawaida au Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge. Katika dhamira safi ukweli huu hatuwezi kuupuzia au kuubadili kwa kisingizio cha "mbona hakupelekwa mahakamani".

Lipo lundo la viongozi wengi wa CCM ambao wamehusishwa na kashfa mbalimbali kuanzia Meremeta hadi Dowans ambao hadi leo wako huru na hawajahi kufikishwa mahakamani lakini hakuna utata wa kuhusika kwao katika kashfa hizi. Kutofikishwa mahakamani na utawala ambao umenufaika na kashfa hizo haiwezekani iwe kigizo cha kusema mtu hakuhusika au kunufaika na kashfa fulani.

MFUMO (SYSTEM) NI WATU

Hali halisi ni kuwa kitu kinachoitwa "mfumo" au maarufu kama "system" siyo mashine fulani au dubwasha fulani limejichimbia sehemu fulani isiyoonekana; mfumo ni watu, ni binadamu na ni Watanzania kama sisi ambao wananufaika na hali ilivyo sasa (benefit from the status quo). Hata watu wanaosema tunapambana na "mfumo" wanasahau kuwa mfumo huo umeundwa, unalindwa na kunufaisha watu siyo mashine au mizuka. Kupambana na mfumo ni kupambana na watu. Wanachama wetu walipopigwa mabomu hawakupigwa mabomu na mfumo, wanachama wetu walipouawa hawakuuawa na chombo fulani kinachoitwa "system"; tulipokataliwa vibali na kufikishwa mahakamani kwa visingizio uchwara vyote hivi vilifanywa na watu, na binadamu wenzetu, na raia wenzetu walio kwenye madaraka. Mfumo basi ni watu walioko madarakani. Kuuondoa mfumo huu ni kuwaondoa watu hawa madarakani. Sheria, kanuni, na maelekezo mbalimbali yanayotekelezwa yametungwa na watu na yanatolewa na watu. Huu ndio "mfumo" hasa; siyo kitu cha kufikirika (an abstract entity).

Hali halisi ni kuwa kuondoa mfumo huu ni kuwaondoa watu hawa. Kubadilisha mfumo ni kubadilisha watu, kutaka kuondoa sera au sheria mbalimbali mbovu inakuja kwa kubadilisha watu wanaotunga sheria na sera hizo. Huwezi kuziondoa kwa kuombea au kunuia ziondoke; utahitaji kutumia watu kubadilisha mifumo hii. Lakini pia ni vizuri kuwa wa kweli kama watu wote walioko ndani ya chama tawala wakaondoka na kuanzisha chama kingine uwezekano wa chama kingine kuwa kama kile chama tawala ni mkubwa sana na wakipewa nafasi ya kutawala wanaweza kutawala kama walivyotawala wakiwa ndani ya chama tawala.

LENGO LETU NI ZAIDI YA KUIONDOA CCM MADARAKANI

Kinyume na maono au maoni ya watu wengine, lengo letu kama watu tunaounga mkono chama cha upinzani (kama wanachama, mashabiki, wapenzi au wapiga kura tu _ kisiasa nchini siyo kuiondoa tu CCM madarakani.

Kumekuwepo na kauli nyingi zenye kuashiria kuwa lengo letu "kuu" ni kuiondoa CCM madarakani. Lengo letu pia siyo "kuvunja mfumo" uliopo sasa. Lengo letu ni zaidi ya haya; lengo letu ni kuipatia Tanzania uongozi bora zaidi na utawala utakaotimiza matarajio na matamanio yao. Kuiondoa CCM na kubadilisha au kuvunja mifumo iliyopo sasa ni hatua za lazima tu ili kufikia lengo hilo kuu. Kuiondoa CCM madarakani ni daraja tu ambalo ni lazima tulipitie lakini hatuwezi kutaka tu kupita daraja bila kujua tunakoenda kukoje au kutakuwa vipi. Kubadilisha tu utawala (regime change) haitoshi; hili limejaribiwa nchi kadha wa kadha na matokeo yake tumeyaona; watawala wapya hawakuweza kukidhi haja na matamanio ya watu wao.

Tunataka viongozi wetu, mgombea wetu na wagombea wetu wote nchini watambue jambo hili; lengo letu ni kubwa sana kuliko kuiong'oa CCM madarakani. Kama ingekuwa shamba, hatuwezi kusema lengo letu ni kung'oa visiki shambani halafu ikaishia tu. Ni lazima tujue tunataka kupanda nini, vipi na kwa sababu gani. Lengo letu ni zaidi ya kusafisha shamba; ni kupanda na hatimaye kuvuna na kufurahia mavuno hayo yakitunufaisha. Tunataka kuing'oa CCM madarakani kwa sababu sera zake zimeshindwa, uongozi wake umeshindwa kukidhi matumaini ya Watanzania.

Lengo letu basi ni kutaka kuipatia Tanzania nafasi ya kujenga utawala mpya na bora zaidi. Kusema tu tena kwa haraka haraka tu kuwa "lengo letu ni kuitoa CCM madarakani" ni kuzungumza bila kufikiri kwa kina; ni kuwa na tamanio lisilo na sababu hasa. Kuitoa tu ili kiwe nini? Kwamba tusijali kitakachokuwa kwamba tutajua mbele ya safari? Hivi bado watu hawajajifunza kuwa wapo watu wengi tu Tanzania wanataka mabadiliko ya kweli lakini kila wakifiria ni nini kitakuja baada ya CCM wanaona bora CCM iendelee? Kwamba, wanadai hawaoni chama au kiongozi wa upinzani ambaye kweli ataliongoza Taifa bora zaidi kuliko CCM.

Kushirikiana na Lowassa au mtu mwingine yeyote katika hili kunahitaji dhana hii ieleweke kwa kila mtu. Hatuwezi kuwapatia Watanzania uongozi ule ule; hata mgeni wetu Lowassa anapoingia hatutaki aje na uongozi wa aina ya CCM. Tunataka awe na alipatie taifa uongozi mpya, bora kuliko ambao umetolewa na waliowahi kuwa wenzake katika CCM. Huwezi kumchukua mtu wa dini moja ambayo ameitumikia dini ile kwa muda mrefu halafu akaamua kuongoka (convert) kwenda dini nyingine halafu huko akapewa uongozi wa dini hiyo lakini akaachwa atumie lugha, vitabu, na mafundisho ya dini yake ya zamani! Mtasema kweli huyo ‘amebadili' dini au atakuwa amebadili jina tu?

LENGO NI KULETA UTAWALA BORA SIYO BORA UTAWALA


Hoja kuu ya upinzani inahusiana na utawala uliopo kuwa umeshindwa. Harakati zote, kampeni zote na madai yote ambayo wapinzani wamekuwa wakitoa miaka yote hii inahusiana na utawala bora; kwamba chini ya utawala wa CCM Tanzania imepata ‘bora utawala' na wakati umefika kwa Taifa letu kupatiwa "utawala bora". Tunapozungumzia utawala bora tunazungumzia siyo tu kubadilisha watu bali sera, sheria, mwelekeo na maono ya taifa ili yaendane na changamoto za wakati huu na kuwa hazina kwa changamoto za vizazi vijavyo.

Wagombea wote watakaosimama nyuma ya Lowassa wajue kuwa tunachogombania na ambacho kimegombaniwa hadi hivi sasa siyo kubadilisha sura za watawala bali sera za watawala. Ni kwa sababu hiyo mgombea wa Urais ni lazima atambue kuwa ugomvi haupo kwenye jina "CCM" kwamba hili jina likiondolewa basi utawala bora utatokea. Tunachotaka kubadilisha ni utawala ulivyo sasa ili kujenga utawala siyo unaodai "kufuata sheria" bali "unaofuata sheria" unazodai. Katika kufikia hili kutakuwa na mapendekezo mengi na mazito ambayo Lowassa na wagombea wengine ambao wametoka upande ule kuja upande huu wajue ndio ajenda ya upinzani kwa muda wote huu.

Ni lazima tukubaliane mapema kabisa, lengo letu SIYO kuiondoa CCM madarakani tu. Lengo letu ni kuindoa CCM madarakani ILI kuipatia Tanzania uongozi mpya, bora na ambao utakidhi matarajio na matamanio ya Watanzania wa sasa na vizazi vinavyokuja. Nje ya hapa, ni bora CCM wabakie hadi tunaotaka kuwaondoa tujue tunataka kufanya nini tukiwaondoa! Mexico walikaa na chama cha Mapinduzi kwa miaka 70 kabla hawajawaondoa chini ya Vicente Fox; kwa miaka arobaini chama cha Demokrati kilishikilia Bunge la Marekani hadi Newt Gingrich alipoingia na kuvunja uhodhi huo; Chama cha Colorado Party cha Uruguay kilishikilia madaraka kwa miaka 61 lakini nacho kilikuja kung'olewa mwaka 2008 na mifano mingine ipo. Kwamba CCM itakuja kuondoka siyo suala la "kama" bali ni "lini" na ninaamini kama hoja zetu zikatosheleza (siyo kura tu) basi hiyo lini inaweza kuwa miezi mitatu hivi ijayo.

UJIO WA LOWASSA CHADEMA


CHADEMA ilikuwa imejipanga kuendesha kampeni yake na kuchukua hatamu za uongozi wa bila kutegemea watu kutoka CCM. Angalau hivyo ndivyo tulivyokuwa tumeaminishwa kwa kuangalia harakati zake na jinsi ilivyojieneza na kupeleka watu hadi "ngazi za chini". Tuliaminishwa kuwa safari hii CDM itasimamisha mgombea kila jimbo na kuwa ina watu wa kutosha kushindana na mtu yeyote wa CCM. Tulikuwa tumeaminishwa kuwa CDM imejipanga na kujiandaa kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu ikitegemea wanachama wetu ambao wameshirikiana na viongozi wao kukijenga chama kwa miaka hii mitano tangu Uchaguzi Mkuu wa 2010 na hata kabla. Ilipotokea nafasi ya kumpokea Mheshimiwa Lowassa mjadala mzito, mkali, wa kina na ambao ulitishia kukipasua chama ulifanyika. Hata ulipofikiwa uamuzi wa kufanya hivyo bado wapo baadhi ya viongozi na wanachama ambao hawakuelewa, kukubali au kushabikia uamuzi huu. Wengi wakiwa na sababu za msingi kabisa.

Kubwa ambalo tunajua kwa uhakika wa kutosha limetokea ni kuwa Lowassa aliombwa aingie kutoa nguvu kwa mgombea aliyeandaliwa wa chama na viongozi wapime faida na hasara ya kumchukua na kuona ni masharti au makubaliano gani watakuwa nayo naye. Hata hivyo baadhi ya viongozi wakaona (labda nay eye mwenyewe) kuwa mpiga filimbi ya pili haiwezekani hasa kwa mtu ambaye anakuja na uzito wa jina lake na nafasi yake ndani ya CCM wakaona ni bora abebe kabisa tarumbeta la CDM.

Hali halisi ni kuwa upande wa pili wa wale waliopendekeza na kushawishi kukubaliwa kwa Lowassa ili awe mgombea wetu wa Urais huku pia akibeba bendera ya ushirika wa UKAWA wamefanikiwa kufanya hivyo na sasa Lowassa atakuwa ndiye mgombea wa CDM na washirika wake. Siyo wote tumelipokea hili kwa furaha kama wengine, siyo wote tumelikubali hili na kusema tuna imani sana naye, na siyo wote tuko tayari kufanya kampeni ya kumuuza kwa wananchi hasa akiwa ametoka kwenye mfumo ule ule ambao yeye alikuwa katika sehemu ya watu walioujenga, kuulinda na kuutetea.

LOWASSA SIYO TENA MWANACHAMA WA CCM

Pamoja na ukweli huo, hali halisi ni kuwa Lowassa hayuko tena CCM, ameamua kutoka na kujiunga na CHADEMA, iwe ni kwa ajili ya kupata nafasi nyingine ya kugombea Urais au kwa vile anaamini kile ambacho CHADEMA na washiriki wake wanaamini – mabadiliko chanya ya utawala nchini – hakuwezi kupita bila kuangaliwa na kuchukuliwa kwa umakini wote unaostahili. Kwa kuamua kujiunga nasi Lowassa amefanya kitu ambacho hakikutarajiwa kufanyika katika siasa zetu hasa kwa mtu mwenye historian a wadhifa kama aliowahi kuwa nao. Anakuwa Waziri Mkuu wa zamani wa kwanza kuhamia katika upinzani akiwa bado katika kilele cha umaarufu wake. Wapo Mawaziri Wakuu wengine wa zamani ambao wamekuwa wakizungumza lugha ya kimabadiliko, wakikosoa mfumo wa utawala lakini wakiwa hawana uthubutu wa kutenda kwa kadiri ya maneno yao – kujiunga na watu wanaotaka mabadiliko ya kweli yaani wapinzani.

Ni hali halisi hii inayotulazimu kukubali na kumpokea – siyo kwa furaha kuu kama wengine - Lowassa kwenye chama tukitambua (siyo kupuuzia) historia yake ndani ya CCM, harakati zake za kuutaka Urais kupitia chama hicho na kuungwa kwake mkono na watu mbalimbali ndani na nje ya CCM. Binafsi kama nilivyoandika kwenye mada nyingine ni vizuri kwenda vitani na wapiganaji wetu wenyewe ambao tunawajua kuliko kutegemea wapiganaji tusiowajua wanaokuja baada ya kukataliwa kupigana upande ule mwingine.

HATUKUBALI KIRAHISI RAHISI

Mojawapo ya mambo ambayo labda yamesumbua wengi na hata kusababisha mgogoro ni hili la kuona kuwa Lowassa amekuja bila kuwa na makubaliano yoyote ya maana ambayo wanachama wameambiwa. Ni jambo moja mwanachama wa kawaida kutoka CCM kuja CDM lakini ni jambo jingine kumchukua kiongozi wa juu wa kutoka CCM na kumfanya kiongozi wenu wa juu tena wakati wa kuelekea Uchaguzi. Ndio maana basi baada ya tafakari kubwa sana na ya siku kadhaa na nikiamini naweza kuwa nawakilishi wengine wenye mawazo kama yangu kumkubali Lowassa na kugombea kwake kunahitaji kuwe na mambo ya kuaminiana; atufanye tumuamini kweli na yeye atuamini hatutampinga na kudhoofisha kampeni yake.

Kwa vile hana misingi katika harakati za mabadiliko wala katika upinzani basi kumpa nafasi hii kubwa ambayo inaweza kumfanya awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunatulazimisha kuweka makubaliano haya.

LENGO LA MAKUBALIANO YA MARIDHIANO


Lengo kuu la makubaliano ya maridhiano (agreement on compromise) haya ni kulinda maslahi ya chama kuelekea wakati wa Uchaguzi Mkuu na baadaye na kuhakikisha kuwa kama chama hakipotezi mwelekeo, dira, na sera zetu tunapomkaribisha mgeni huyu kuchukua bendera yetu. Pamoja na hili tunataka pia kuhakikisha kuwa kwa vile Lowassa anasimama kama mwanachama mwenzetu na pamoja na ugeni wake kupeperusha bendera ya chama chetu na kuwakilisha ndoto za washirika wenzetu wa UKAWA basi tuhakikishe anapata ushirikiano wote anaostahili kama mgombea wetu; ushirikiano kutoka ngazi zote za juu hadi ngazi za chili ili kuweza kupata ushindi usio na utata. Hatuwezi kumuunga mkono wakati kuna maswali bado yako yanasumbua fikra zetu na hadi hivi sasa hajayapewa majibu ya kuridhisha.

Haifai kukubali tu wakati hujui ukikubali wewe unafaidika vipi. CDM na wanamageuzi nchini ni lazima wanufaike – malengo yao yatimie – na uamuzi wa kumuunga mkono Lowassa. Kuwaambia watu ati wamuunge mkono tu kwa sababu ni kutaka kuiondoa CCM ni kutokuwa na umakini unaostahili mwanasiasa yeyote.

Naomba kupendekeza kuwa maridhiano au makubaliano haya yawe yanahusisha sehemu tatu – kwanza kwa Lowassa mwenyewe, kwa Ofisi ya Katibu Mkuu, na kwa viongozi wa chama, na viongozi wengine wa UKAWA.

Kwa Upande wa Mhe. Edward Lowassa


  1. Mheshima Edward Lowassa atambue na kukubali hadharani (publicly) kuwa katika muda wa uongozi wake kuna makossa ambayo aliyafanya kama kiongozi ambayo akiangalia leo kwa mwanga wa umbali wa historia hakupaswa kuyafanya na yalisababisha matatizo kwa taifa. Kwa makubaliano haya achukue nafasi ya kuliomba radhi taifa kwa sehemu yake na kuwa yuko tayari kujenga imani kwa wananchi na kuahidi makosa kama yale hayatotokea tena chini ya uongozi wake. Anataka kuwaongoza Watanzania ni lazima aoneshe unyenyekevu wa kukubali nafasi yake na makosa yoyote ambayo yalifanyika wakati wake kama kiongozi mkuu wa Serikali; haitoshi tena kutupa lawama kwa watu wengine. Itakuwa hatua ya kwanza kuanza kuaminiana;
  2. Alaani waziwazi na hadharani vitendo vya serikali kuminya upinzani na kuomba radhi kwa ukimya wake wakati haki za raia zikivunjwa. Kwa mtu mwenye sauti na nafasi kama yak wake hasa kile kinachoitwa ushawishi ukimya wake wakati wapinzani wananyanyaswa na vyombo vya dola umeacha doa kubwa sana la kuweza kumwamini;
  3. Mheshimiwa Edward Lowassa kama mwanachama mwenzetu na mbeba bendera ya Chama kwa niaba ya UKAWA vile vile ataunda timu ya kampeni itakayoongozwa na wanachama waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na vyama washirika katika UKAWA; kama kuna mtu yeyote ambaye anamhitaji kutoka nje ya chama mtu huyo au watu hao wataangaliwa na kupitishwa na Ofisi ya Katibu Mkuu kwa niaba ya chama;

Ahadi nyingine ambazo tungependa azitamke hadharani na tujue kuwa zitakuwa ni sehemu ya ahadi zake kama Mgombea wa Urais kupitia CDM. Mgombea wa Urais anayebeba matamanio na ahadi za vyama vya upinzani ni lazima asimamie mambo yale ambayo Upinzani Tanzania umesimamia miaka hii yote. Litakuwa ni kosa kubwa na usaliti wa harakati za upinzani nchini kwa mgombea wake wa Urais kutosimamia wazi, hadharani na bila utata hoja kuu za upinzani nchini. Kwa vile Lowassa ndiye ambaye CDM na vyama washirika wamekubaliana awe ndiyo mtu atakayepeperusha bendera ya upinzani ni muhimu na lazima kwa Lowassa kutangaza hadharani kuwa atasimamia mambo yafuatayo ambayo tayari yamepaziwa sauti na CDM na vyama vingine hasa ndani ya miaka hii mitano.
Atakaposhika Madaraka ya Rais;


  1. Lowassa alikuwa ni sehemu ya wajumbe wa Bunge la Katiba ambao walipitisha Katiba ile iliyotengenezwa na CCM. Tungependa aikane Katiba ile na kuahidi kuwa atakaposhinda kiti cha Urais basi atanzisha mchakato sahihi, bora, wa wazi, na utakaokidhi matarajio ya Watanzania kuhusiana na Katiba Mpya. Mchakato huu utaanzishwa kwa kuleta kwanza mabadiliko ya Katiba ya sasa ili kuruhusu uwezekano wa kuandikwa upya kwa Katiba yetu kwa kufanyia marekebisho Ibara ya 100 ya Katiba. Mchakato wowote ujao wa Katiba Mpya utaondoa wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa Wabunge wa Bunge la Katiba na utatengeneza namna bora ya kupata wawakilishi wengi zaidi wa Bunge la Katiba kuliko mchakato uliobuniwa na CCM. Mchakato huu ujao utahakikisha baadhi ya mambo yanaamuliwa kwanza kabisa kabla ya kura ya maoni juu ya Katiba Mpya;
  2. Aahidi hadharani na wakati wote wa kampeni kuanzisha ndani ya muda maalum – mapema iwezekanavyo – uchunguzi juu ya uvunjaji wa haki za binadamu na uhalifu dhidi ya waandamanaji katika matukio mbalimbali ambayo wanachama na mashabiki wa vyama vya upinzani walipoteza maisha yao. Ataanzisha uchunguzi wa Kimahakama (Judicial Inquiries) ya matukio ya mauaji ambayo yametokea katika mazingira ya kisiasa – wakati uliopita na wakati huu wa kampeni za Uchaguzi - ili kuhakikisha ukweli unajulikana na sheria inafuata mkondo wake kwa wahusika;
  3. Serikali yake italeta miswada ya mabadiliko ya Sheria mbalimbali au miswada ya sheria mpya ambazo zimekuwa ni tatizo kwa taifa kwa miaka hii yote. Miswada hii italetwa katika kikao cha mapema zaidi baada ya Bunge Jipya kuapishwa. Baadhi ya Sheria ambazo miswada yake itatakiwa kuletwa mara moja ili kuliondoa taifa na masalio ya sheria mbovu za utawala wa CCM na ambayo Lowassa ataahidi hadharani na wakati wa kampeni kuwa italetwa mapema hivyo ni ile inayohusu:
- Mabadiliko ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya 1996
- Mabadiliko ya Sheria ya Usalama wa Mitandao ya 2015
- Sheria ya Uhuru wa Habari na Ulinzi wa Wafichua Maovu (Whistleblower Protection ACT)
- Mabadiliko ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa ya 2007
- Mabadiliko ya Sheria ya Jeshi la Polisi ya 2007
- Kupitia Sheria zile au Vipengele 40 ambavyo vilioneshwa na Tume ya Jaji Kisanga kuwa vinahitaji mabadiliko. Ndani ya Mwaka mmoja hili liwe limetimizwa ili kuondoa Sheria zote zilizopitwa na wakati vitabuni
- Na sheria nyingine ambazo zinaonekana ni kikwazo katika kutengenza utawala bora
4. Lowassa aagize makundi yake ambayo yamekuwa yakimuunga mkono (hasa yale ya vijana) na ambao wamejiunga CDM kukubali kuwa chini ya uongozi wa CDM mara moja. Haiwezekani ndani ya chama kuwa na chama halafu chama kiwe kimoja. Walitoka CCM na wamejiunga CDM na waagizwe kujiunga kweli. Vinginevyo, kutakuwa na kampeni ya wana CCM ndani ya CDM kumpeleka Lowassa Ikulu.

Upande wa Chama, Hususan Ofisi ya Katibu Mkuu

Kwa vile CDM ndiyo chama ambacho Lowassa ameamua kujiunga nasi basi nacho kina maslahi makubwa zaidi katika kampeni ya Lowassa kuliko kikundi kingine chochote. Sasa hivi CDM ndiyo inatakiwa iwe kundi pekee na lenye nguvu zaidi kuhusiana na kampeni ya Lowassa kuliko kikundi kingine chochote.

1. Lowassa akitekeleza hilo la kwanza hapo juu basi Chama kitatambua rasmi kuwa Edward Lowassa amelipa gharama ya makosa yake kama kiongozi akiwa ndani ya Chama cha Mapinduzi. Alilazimika kujiuzulu uongozi katika Serikali na chama chake hakikumpa wadhifa mwingine wowote Serikalini. Na alipotaka kugombea Urais kupitia chama hicho na licha ya kuungwa kwake mkono na watu wengi Chama chake kilimkataa na hivyo kumwadhibu tena kwa kumnyima nafasi ya kugombea Urais. Adhabu hizi tunaamini zinatosha na amelipia vya kutosha siyo tu kwa kupoteza vyeo, bali fedheha, hisia kuumizwa na kuhusishwa kwake na kashfa mbalimbali;

2. Chama kinatambua na kukubali kuwa jukumu lake la kuwapatia Watanzania uongozi bora unaoongozwa na sera bora zaidi kuliko zinazopendekezwa na CCM linabakia pale pale. Kuelekea Uchaguzi huu Mkuu mgombea wetu wa Urais atabeba sera za chama chetu na ilani yetu kama ambavyo tulivyokuwa tumeipanga hata kabla ya yeye kujiunga. Kama ilivyo kawaida tutapokea mapendekezo ya maono yake na kuyaoanisha na vipaumbele ambavyo tayari tuliviweka ili Ilani yetu na ahadi zetu za Uchaguzi ziakisi misimamo na malengo ya chama; Lowassa hatogombea na ilani ya CCM au maono ya KiCCM;

3. Chama kinaendelea kutambua kuwa tatizo la ufisadi katika sura zake zote halikuanza leo ndani ya CCM na halijaisha kwa Lowassa kuondoka; mtu aliyeachia Uwaziri Mkuu miaka karibu nane iliyopita. Tatizo hili limejikita ndani ya CCM kiasi kwamba limeendelea bila kuzuiliwa miaka yote hii na ni uthibitisho tu kuwa mtu akiondoka kwenye taka na kujisafisha anaweza mwenyewe kuwa msafi lakini taka alizoziacha kule bado zikabakia takataka. CCM haijaweza kujisafisha kwa sababu haiwezi kujisafisha; Njia pekee ya kuisafisha CCM ni kuitoa madarakani ili ikajisafishe nje ya madaraka; CDM na washirika wake wanampokea Lowassa ili hatimaye kuipatia Tanzania uongozi bora, safi na utakaowajibika kweli kweli kwa wananchi;

4. Kutakuwa na uhusiano wa pekee katika kuelekea Kampeni kati ya Ofisi ya Katibu Mkuu na Kampeni ya Urais ya Mheshimiwa Lowassa ili kumpatia msaada wote unaohitajika kuweza kuendesha kampeni itakayoakisi na kukidhi matarajio ya wanachama wetu, washirika wenzetu katika UKAWA na wananchi wote;

5. Katibu Mkuu wa chama ambaye ndiye ana majukumu ya Mtendaji Mkuu wa Chama anawajibika kuhakikisha kuwa Chama kinasimamia kanuni zake, sera na itikadi yake lakini zaidi kinasimama kwenye ahadi zake kwa Watanzania. Kila mwanachama wetu anayetafuta nafasi ya uongozi – haijalishi ngazi gani – basi anapaswa kutambua kuwa anafuata na kusimama Katiba ya chama, sera zake, mipango yake na itikadi yake.

Kwa upande wa uongozi wa Chama


Viongozi wa CHADEMA ambao ndio wameaminisha wanachama kuwa uamuzi wa kumchukua Lowassa kama mgombea ni sahihi kwa sababu unakipatia nafasi ya kipekee ya kuing'oa CCM madarakani basi wao nao wawe tayari kuahidi hadharani kuwa wanaamini hicho wanachokisema. Haitoshi kutaka watu wengine waamini ukweli huu kiasi cha kumuweka pembeni mtu wao wenyewe waliyemuandaa au kumfanya aamini wanamuandaa na kwenda kumchukua mtu wa CCM. Kwa sababu hiyo, wao nao wana ulazima wa kuahidi haya hadharani;

1. Mheshimiwa Freeman Mbowe, na Tundu Lissu wajitoe kugombea Ubunge kwenye majimbo yao ya Hai na Singida Mashariki. Mbowe na Lissu wamekuwa mbele kutaka watu wakubali uamuzi wa Kamati Kuu kumchukua Lowassa. Naamini wanasema kweli kuwa hii ni nafasi ya pekee ya kuweza kuing'oa CCM. Kwa sababu hii waoneshe kwa vitendo imani yao hii kwa kutokugombea Ubunge na badala yake wawe ndio viongozi wa kampeni ya CDM ya Urais na Wabunge ili kuepushe yale yaliyotokea 2010 ambao viongozi hawa walijikuta wanabanwa kwenye majimbo yao wakati wa kampeni na siku ya Uchaguzi. Siamini kuwa hili litakuwa tatizo kwao kwani Lowassa atakaposhinda Urais atawateua kuwa wabunge katika zile nafasi kumi za Ubunge ambazo Rais anatoa;

2. Tumeambiwa kuwa uamuzi wa kumpokea Lowassa ni uamuzi uliofanywa kwa pamoja na kuridhiwa na Kamati Kuu. Kwa vile hili ni kweli (sina sababu ya kulibishia) Mwenyekiti Mbowe atamke hadharani wakati wa Mkutano Mkuu kuwa endapo CHADEMA mkakati wao huu ukiishindwa kukiletea chama ushindi (hasa kwa vile wamesema ni jambo lililotoka kwa Mungu) basi Kamati Kuu nzima ya CDM itajiuzulu ndani ya masaa 24 baada ya kushindwa kuleta matokeo wanayotuahidi ambayo yamesababisha wao kumchukua Lowassa na kundi kubwa ambalo tumeambia anakuja nalo; Kwa kuahidi hivyo mapema watafuata mifano ya viongozi wengine wa kisiasa duniani ambao walilazimika kujiuzulu nafasi zao mara tu baada ya kushindwa kutekeleza ahadi za ushindi kwa vyama vyao;

Ikumbukwe kuwa ahadi ambayo wametupa viongozi wa CDM ni "kuindoa CCM madarakani" kwa namna yoyote ile. Isipoondoka wao itabidi waondoke kwenye madaraka yao kwa namna yoyote ile ili kutoa nafasi kwa viongozi wengine kuponya majeraha na kukijenga chama upya.

3. Vile vile, Mkutano Mkuu wa CDM uazimie kuwa viongozi wa Taifa wa Chama ambao watakuwa wamegombea Ubunge na kushinda watajiuzulu nafasi zao za uongozi wa chama ili kutenganisha vyeo hivi na kutengeneza mfumo mzuri wa kusimamiana (checks and balances) kuliko ilivyo sasa ambapo viongozi wa Taifa wako Bungeni na wanasimamia chama kiasi kwamba hakuna mfumo mzuri wa kusimamiana;

4. Mkutano Mkuu umtake radhi Katibu Mkuu wake kwa yale yaliyotokea na kumwomba rasmi akubali kuunganika nao na kutekeleza majukumu yake hasa katika kusaidia kampeni za wabunge na madiwani wengi wao wakiwa ni watu ambao wameandaliwa na chama kwa muda mrefu. CDM isijivunie kumpoteza kiongozi wake hivi hivi kwa ajili ya faida ya muda tu. Ingawa kweli Lowassa anaweza kuwa amekuja na kura zake lakini kutokuwepo kwa Slaa hasa kwa mazingira haya kunaweza kufuta (cancel) faida yoyote ambayo CDM ilikuwa ipate kwa ujio wa Lowassa.

Kwa upande wa Washirika wa UKAWA


Kwa upande wa washirika wa UKAWA pendekezo moja kubwa linatosha. Kwa vile tumeona viongozi wa CUF na vyama vingine nao wakijitokeza kuonesha wao wameridhia Lowassa awe mgombea wa Urais na kubeba matamanio yao vile vile basi na wao pia waoneshe kwa vitendo kuwa wanaamini kuwa ushindi wa kishindo unanukia.

Hivyo basi, Maalim Seif Sharrif Ahmad aamue kujitoa kugombea urais wa Zanzibar – anaweza kumpisha Jussa – ili awe mgombea mwenza wa Lowassa kwenye tiketi ya Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano. Ana uzoefu wa kutosha wa siasa za upinzani na anazijua vizuri siasa za Tanzania. Naamini atakuwa ni mgombea mwenza mzuri kabisa na hakutakuwa na tatizo kubwa kwake kukaimu nafasi ya kiti cha Urais itakapobidi hivyo.

HITIMISHO


Endapo haya yote yatafanyika mapema kuelekea wakati wa kampeni, na tukaona kuwa kweli hawazungumzi tu bali wako tayari kutenda basi hata sisi wengine ambao tunasita kutoa mkono wetu wa pongezi au kudandia treni la Lowassa tutakuwa tayari kuwaunga mkono na kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa Lowassa anachaguliwa kuwa Rais kwani atakuwa ametujengea imani kidogo na viongozi wa CDM nao watakuwa wametupa mwanga kuwa kweli wanaamini katika hii "nafasi ya pekee". Kinyume cha hapo sisi wengine bado tuna mioyo ya kusita sita. Hatujaona sababu au vitendo vya kutuaminisha kuwa pande hizi mbili kwel zinaamini katika kuiondoa CCM madarakani mwaka huu. Kama kweli wanaamini basi ramani ya kuunganisha fikra za wapinzani ndiyo hii.

Umoja wa Kweli Ndio Ushindi wa Kweli
MMM

* Niliandika mwaka 2010 mada nyingine yenye sehemu ya kichwa cha habari kama hiki hapata JF wakati wa kuelekea kampeni za Rais na wabunge. Sikutegemea kama ningejikuta naandika tena mwaka huu.
 

Attachments

  • MARIDHIANONALOWASSA2015.docx
    32.3 KB · Views: 1,089
Vile vile najaribu kujiuliza; hivi unafikiri wanahitaji ushauri wako!? kama hawauhitaji, kuna haja gani ya wawe kuwalazimishia kuwashauri na mishipa ya ubongo kukutoka kwa kujifikirisha juu yao!? unafikiri wanakuthamini? kwa nini uvunjike mguu bongo kwa mpira wa ulaya?
 
Mbowe na mashabiki wake wanaweza wasielewe madhara ya hii hatua wanayoipigia debe sasa, ila ukweli unabaki palepale kwamba Chadema sasa hivi haijulikani inapigania nini.

Mimi kama mwananchi wa kawaida sijui misingi ya itikadi ya Chadema ni ipi kwa sasa. Je ni kuingia ikulu tu; na wakishindwa kuingia ikulu Chadema watatuambia nini, wakati tayari wameshakana "principles" zao; kwamba wao ni chama kinachopinga ufisadi nchini?

Najiuliza, next time Chadema watasafiri kwenda nchi tajiri kutafuta support ya kitu gani kama wameamua kwamba ufisadi siyo vita wanayopigana nayo?
 
Mwanakijiji katika ubora na utata wake,sikubaliani na wewe unaposema mbowe na lissu wasigombee ubunge kwenye majimbo yao,hapo ni sawa na kuzidi kuwaongezea viti ccm bungeni na kuendeleza ile mikelele ya ndiooooooo.

Kwa nini katibu mkuu aombwe radhi?(is this personal?)
Unaongea as if lowassa akiweza kuwa rais atatawala kwa ilani yake ya mfukoni na sio ya chadema!!!!
Woga ulionao kwa lowassa ndio nilionao na mimi,but sometimes we have to take risks.
 
Ni bandiko zuri na lenye weredi wakutosha ni lazima hii sintofahamu hii ituondolee utata je ,lengo ni kuiondoa ccm then what lazima watueleze wataondoa vp mfumo uliopo.pili naunga na wewe mzee mwanakijiji lowassa lazima atuweke wazi na kukana elements za kiccm ama za kifisad hili kufuata mlengo wa upinzan na ukawa kwa jumla lazma umma wa wa Tanzania nia ya mabadiliko toka kwake aeleze kwa kina shutuma za ufisad s juju tu namini hata dr slaa n miongon mwavtu vna mtatiza.naunga mkono hoja
 
at least naona some positive view, nashauri nyinyi kama watu wenye ushawishi ndani ya chama mjaribu kuangalia pia mood ya wa sisi wanachama wenu, ni wazi kua pamoja na mapungufu yote ya lowassa, bado ni kete muhimu sana kwetu kushinda uchaguzi. sisi mashabiki weenu tunataka kuona mkiwa timu moja na kusiwe na kutokuwezekana katiaka jitahada zenu za ndani kumaliza tofauti zenu ninyi kama viongozi wetu, tunawaombea kwa Mungu mfanikishe hil0
 
Mwanakijiji, mkuu umeandika na toa mapendekezo mazuri lakini hayatafuatwa. It's too late. Lowassa hatakubali masharti haya esp hiyo ya 1. Maana ndo sharti alilotoa Dr Slaa na matokeo yake ndo haya. Lakini pia Dr Slaa hajaenda likizo kama tulivyoaminishwa bali amejivua uanachama kabisa wa Chadema.
Labda ueleze kuwa unajaribu ku-salvage the impossible yaani Chadema the way you thought it was. Kiukweli Chadema will never be the same.
Lakini nakupongeza sana kwa sababu hii ni manifesto ya mwana mageuzi wa kweli ambaye ambayo imeweka wazi kuwa hawawezi Mbowe na Ukawa ku-justify eti any means necessary. .na umewavua nguo kuwa kiukweli hawana lengo lolote zaidi ya uchu wa madaraka.
 
Naamini uko sahihi kwa kutazama maudhui ya hoja.
Kwa vile ni maridhiano (compromise) sio lazima yote uliyopendekeza yatimizwe.

Kubwa nililolipenda kwenye hoja yako ni ofisi ya katibu mkuu wa CDM kuwa kitovu cha uongozi wa kampeni. Slaa (kwa sasa) ndiye pekee anaweza kutoa uongozi huo kwa sasa maana hatakuwa akigombea nafasi yoyote [wasaidizi wake Mwalimu na Mnyika wote wanagombea].
 
Lengo kuu ni kuuondoa mfumo wa ccm wa kinyonyaji kwa nchi yetu. Hapa wasioona hili ni wale wanaofaidika na mfumo wa sasa.
 
Mwanakijiji mengi uliyosema ya maana ila jua kwamba yatatimia si Muda timiza wajibu wako. Juu ya usafi wa Lowasaa nadhani alihojiwa na kamati kuu, kuomba Radhi hadhrani si lazima ili kuwa safi.
 
Hivi mwanakijiji unalipagwa na nani? Mbona unahangaika sana kaka?

Wewe ni mpiga debe tu na kupokea ujira wako kwa siku
Kama hujamwelewa Mwanakijiji una wazimu kabisa , nadhani kafanya kazi nzuri ya uchambuzi na ndo ukweli.
CDM kutwaa uongozi ni ndoto
 
Back
Top Bottom