Pendekezo la 1: Tanga, Bagamoyo, Mafia na Pangani ziwe sehemu ya Zanzibar!



Majibu ya Zitto kwa MwanaKijiji

PENDEKEZO LA 1:TANGA, MAFIA, BAGAMOYO NA PANGANI ZIWE SEHEMU YA ZANZIBAR!

Na. M. M. Mwanakijiji

Hili ni pendekezo la kwanza kati ya mapendekezo kadhaa ambayo nitayatoa katika kusaidia kuleta fikra mpya katika mijadala mbalimbali ya kitaifa ambayo lengo lake ni kutupa uwanja mkubwa zaidi wa kuweza kufanyia maamuzi. Miaka 46 imepita tangu Muungano pekee wa nchi mbili za Kiafrika uasisiwe na hivyo kujenga katika bara la Afrika nchi pekee ambayo mipaka yake haikurithishwa na wakoloni! Tanzania tunayoishi leo hii ni tunda na zao la Watanzania wenyewe.

Pamoja na matatizo yote yaliyopo Muungano wetu unapaswa kutetewa, kulindwa na kudumishwa si kwa sababu ya woga, si kwa sababu hauwezi kuvunjika, na si kwa sababu hautakuwa na matatizo huko mbeleni. Tunapaswa kuulinda, kuudumisha na kuuboresha kwa sababu moja tunaupenda kwani ndio nchi pekee tuliyoijenga kwa ajili yetu sisi na watoto wetu.

Ninaamini kabisa kuwa siku watawala wetu watatoka kwenye ufinyu wa fikra wanaouonesha siku kwa siku wataweza hatimaye kuja na mapendekezo ya kuuboresha Muungano wetu na kuufanya uwe kwa faida ya kila Mtanzania na kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima na ambayo utatuzi wake unahitaji dakika chache tu za fikara. Pendekezo hili, halijawahi kutolewa na mtawala yeyote, hawawezi kulitoa kwani hawana uwezo wa kifalsafa kulitetea! Hawawezi kulikumbatia kwa uharaka kwa sababu wamefungwa na siasa zao za utengano hadi wanatia aibu. Hili hata hivyo, haliwezi kuwazuia Watanzania wengine kutoa mawazo yao na kuyasogeza mbele kama pendekezo ili kila Mtanzania ajue kuwa hatuhitaji wazungu watuletee mapendekezo yao ili tuyakumbatie kama yameletwa na wajumbe wa Mungu! Hili ni pendekezo la kuthubutu, la nguvu, la mkakati, la kisiasa, la kiutu, na la kiumoja kuliko mapendekezo mengine yote yaliyowahi kutolewa kuhusu kudumisha Muungano au kuondoa “kero za Muungano”.

Ninaamini ukifuatana nami, utaweza kuona mantiki ya pendekezo hili na utakosa sababu yoyote ya kiakili au ya kiutendaji ya kulipinga. Pendekezo hili likikubaliwa litaanza kutatua matatizo mbalimbali ya kiutendaji na litarejesha roho ya Muungano kama Mkataba wa Muungano unavyosema.

Jibu – Utangulizi mzuri uliojaa hamasa za kizalendo. Mpaka sasa sijaamini kama upo serious katka pendekezo lako hapa chini maana licha ya kwamba ni wazo ‘jipya’ lakini bado lina masuala kadhaa ambayo kifalsafa nina tatizo nayo kama nitakavyoeleza hapa chini.

Pendekezo lenyewe:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aigawe sehemu ya mkoa wa Tanga (Tanga mjini na Pangani), pamoja na sehemu ya Mkoa wa Pwani (Mafia na Bagamoyo) na kuziweka sehemu hizo chini ya utawala wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kimsingi kufanya sehemu hizo nne kiutawala kuwa sehemu ya Zanzibar. Hili tifanywa kwa mujibu wa Ibara ya ya 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema:

2.-(1) Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania
inapakana nayo.
(2) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu
uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge:

Isipokuwa kwamba Rais atashauriana kwanza na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika Mikoa, Wilaya au maeneo mengineyo.

Kugawanywa huku kutafanywa na Rais kwa nguvu hiyo ya Kikatiba kama ambavyo tayari amekuwa akifanya katika kugawa sehemu mbalimbali za nchi yetu kwa ajili ya sababu za kiutawala. Huko nyuma maeneo mbalimbali yaligawanywa kuunda mikoa tuliyonayo leo hii. Kwa mfano, mwaka 1967 Mkoa wa Shambani huko Zanzibar uligawanywa kuwa Kusini na Kaskazini baadaye kubakia mkoa wa Kaskazini na Kusini, na mwaka 1971 mikoa ya Mbeya na Tabora ilimegwa kuunda mkoa wa Rukwa. Hivi karibuni zaidi Mkoa wa Arusha uligawanywa na kuunda pia Mkoa wa Manyara. Hivyo, Rais anazo nguvu na uwezo wa kisheria kufanya hili.

Jibu – Tanzania ni Muungano wa Dola mbili huru. Dola ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Dola ya Jamhuri ya Tanganyika. Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua sehemu mbili za Muungano kama zilivyokuwa wakati tunaungana na sio vinginevyo. Rais wa Jamhuri ya Muungano hana mamlaka yeyote ya Kikatiba ya kugawa sehemu ya mungano na kuwapa wengine (kama kugawa ardhi ya Tanganyika na kuweka chini ya himaya ya Zanzibar). Anaweza kufanya hivyo kwa Mikoa na Wilaya za Bara tu na kama ulivyosema kikatiba kwa mikoa na wilaya za Zanzibar tu. Katiba inatambua maeneo haya mawili ya Muungano kama maeneo mawili tofauti na imeweka mipaka. Ndio maana sheria zinazotungwa Bungeni husema wazi zinatumika wapi katika eneo la Muungano.
Hivyo Ingawa Rais anayo mamlaka ya kugawa mikoa na Wilaya, hana mamlaka ya kumega sehemu ya Muungano na kuifanya kuwa sehemu nyingine ya Muungano. Katiba pia inampa Rais mamlaka na wakati huo huo kumnyima mamlaka hayo na ndio maana waandishi wa Katiba walitumia maneno ‘kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria’
Zaidi ya hapo, hata siku moja haijawahi kuwa kilio cha Wazanzibari kuwa wanahitaji eneo kubwa zaidi kijiografia. Tutaona huko mbele jinsi Zanzibar ilivyokuwa kubwa na waliachia maeneno yao na wala hawalalamiki. Tatizo kubwa kwa Zanzibar ni autonomy yao kama Taifa!


Nini kitatokea baada ya kugawanywa huku?
Endapo pendekezo hili litafanyiwa kazi basi kuna mambo kadhaa ambayo yatatokea katika Tanzania kiutendaji na kiutawala lakini kikubwa ni kuwa hatimaye Muungano wetu utakuwa umesogezwa zaidi kati ya bara na visiwani na hivyo kuendeleza umoja na utaifa wa Watanzania. Ni sawa na kuongezea misumari kwenye mbao ambayo tayari ilishawekwa gundi. Muungano utaimarishwa zaidi. Lakini kuna matokeo yake mara moja ya kimuundo, kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Jibu – Muungano utasogezwa mbele kwa kujenga heshima miongoni mwa mataifa haya mawili, kuheshimu makubaliano ya muungano ya mwaka 1964 na kuepuka kuingiliana. Muungano utaimarika iwapo sehemu moja ya muungano haitaona sehemu nyingine kama ni ndogo na kuidharau bali kuona kuwa dola mbili huru ziliungana kwa makubaliano maalumu. Kwa kuwa Zanzibar haijawahi kudai eneo kubwa la Ardhi, bado pendekezo hili halitakuwa limetatua matatizo ya msingi ya Muungano yanayolalamikiwa na Wazanzibari ikiwemo kuongeza kiholela bila ridhaa yao masuala ya muungano kutoka 11 mpaka 22. Katika hali hii hii ya sasa bado muungano unaweza kuwa imara zaidi iwapo tutajibu changamoto za sasa badala ya kuongeza vurugu nyingine za watu wa Tanga, Bagamoyo na huko kwingine kulalamika kwa nini wapelekwe chini ya himaya nyingine. Kwa misingi ipi?

Zanzibar mara moja itajikuta inaongezewa eneo kubwa la kiutawala. Sasa hivi Zanzibar ina jumla ya kilometa za Mraba zipatazo 2460 hivi. Wilaya ninazozipendekeza kuwa chini ya Zanzibar ziko hivi kwa sasa: Tanga mjini ina kilometa za Mraba 474, Pangani ina 1019 , Bagamoyo ina 9842 na Mafia ina 518. Hivyo utaona kuwa mara moja eneo la kiutawala na kijiografia la Zanzibar linaongezeka mara 4.8 na kuwa kilometa za Mraba 11853. Hili litafanya eneo la ardhi la Zanzibar kuongezeka kama nilivyoonesha na idadi ya watu wa Zanzibar kuongezeka. Katika Zanzibar hii mpya idadi ya wananchi itaongezeka kutoka milioni 1.07 na kuwa karbu 1.6. Wilaya hizi nne zitaongea eneo kubwa karibu mara tano, lakini litaongeza idadi ya watu kama kwa theluthi moja tu ya idadi ya watu wa Zanzibar.

Jibu – Zanzibar haijawahi kudai eneo kubwa zaidi katika madai yake ya kero za muungano. Ikumbukwe kuwa kabla ya ukoloni wa kijerumani na kabla ya makubaliano kati ya Wajerumani na Waingereza kuhusu Zanzibar na Heligoland, Sehemu ya Dar es Salaam mpaka mbele ya Ubungo (16 miles) zilikuwa ni sehemu ya himaya ya Sultan wa Zanzibar. Central Government District ya Dar na Bandari na Kigamboni zote zilikuwa sehemu ya Sultan wa Zanzibar. Kilwa ilikuwa sehemu ya Sultan wa Zanzibar lakini Mafia haikuwa sehemu ya Sultani wa Zanzibar (alishindwa vita na sultan local wa pale Mafia). Haya yote waliyaachia miaka takribani 150 iliyopita na wala hawajawahi kuyataka tena (sehemu hizi ziliitwa Mrima). Tanganyika ikachukua maeneo hayo na Zanzibar ikabaki na Zanzibar ya sasa pamoja na Mombasa. Pangani haijawahi kuwa sehemu ya Sultani wa Zanzibar. Pangani ilikuwa ni Dola inayojitegemea chini ya Abushiri Bin Salim na alinyongwa na Wajerumani na kuwa sehemu ya Deutsche Ostafrika.

Mpaka Disemba 10, 1963 saa tano na dk 59 usiku Mombasa ya sasa (Mkoa wa Pwani wa Kenya) ulikuwa ni sehemu ya Zanzibar. Ilikuwa ikitawalia kutokea Nairobi na Waingereza kwa niaba ya Sultani wa Zanzibar na hata kodi zilizokuwa zikikusanywa Momabasa Port zilikuwa zinakwenda Zanzibar kama makao makuu. Wakati wa Juhudi za Uhuru wanasiasa wa Kenya walilumbana juu ya nafasi ya Mombasa ambapo baadhi walitaka Pwani iwe nchi huru (Coast Peoples Party cha Katana Ngala badae ikawa KADU alipoungana na Moi), wengine walitaka iendelee kuwa sehemu ya Zanzibar (Mazrui family) na wengine walitaka iwe sehemu ya Kenya (Oginga Odinga na Kenyatta chini ya KANU). Katika mazungumzo yaliyofanyika Lancaster kuhusu Uhuru wa Kenya na Zanzibar, Mohamed Shamte aliyekuwa Waziri Mkuu (designate) wa Zanzibar baadae alikubaliana na kina Oginga makubaliano maalumu na hivyo kuiachia Mombasa kuwa Kenya. Kuna makubaliano maalumu ambayo mpaka leo Kenya haijayatekeleza ikiwemo Zanzibaris kuingia Kenya kama kwao bila ya Passport wala visa na hata sehemu ya mapato ya Mombasa Port yaende Zanzibar. Kutokana na Historia hii ndio maana mpaka leo Mombasa hupiga kura kwa chama chochote chenye Odinga kwa heshima ya Jaramogi katika mazungumzo ya Lancaster.

Hivyo eneo la Ardhi halijawahi kuwa sehemu ya madai ya Zanzibar katika Muungano na hivyo pendekezo hili halitatatua tatizo lolote la muungano uliopo sasa.

Matokeo ya mgawanyo huu.
Ninaamini baada ya kugawa sehemu hizo na kuziweka chini ya serikali ya Zanzibar basi matokeo mbalimbali hayana budi kufuatana na mgawanyiko huo. Haifai kugawa sehemu hizo bila kuendana na matokeo yafuatayo au hata yanayofanana kwa ukaribu. Matokeo yote ninaamini kabisa yatakuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili za Muungano. Hata hivyo, ni lazima tutambue vile vile kuwa katika kufanya hivyo sehemu zote mbili ni lazima ziwe tayari kupoteza kitu na wakati huo huo kupata kitu. Hii ndiyo maana ya kuungana. Matokeo yafuatayo ni muhimu kuyaangalia.

RAIS WA ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar anakuwa ni Waziri Mkuu wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nchi itakuwa na Rais mmoja tu wa Muungano lakini kwa kuendeleza makubaliano ya Muungano Zanzibar itaendelea kuchagua Mtendaji wake Mkuu ambaye atakuwa ni Waziri Mkuu atakayechaguliwa kwa kura kama ulivyoutaratibu wa sasa. Waziri Mkuu atakayechaguliwa ataunda serikali kama ilivyo sasa na kuwa na Waziri Kiongozi wake (nitawaachia wengine kufikiria mengine hapa). Hata hivyo itoshe kusema tu kuwa Waziri Mkuu wa Zanzibar atakuwa ni makamu wa pili wa Rais wa Muungano akiwa na majukumu mawili makubwa: kwanza, atakuwa anakaimu nafasi ya Urais wa Muungano endapo Rais wa Muungano na Makamu wake hawapo nchini na kuondoa utaratibu wa sasa (sijui nani aliufikiria) ambapo Waziri Mkuu aliyechaguliwa katika jimbo moja tu anaweza kukaimu Urais wa Muungano!

Na pili, endapo kwa sababu yoyote Rais wa Muungano na Makamu wake hawawezi kuendelea na uongozi basi Waziri Mkuu wa Zanzibar atakaimu uongozi wa Taifa aidha kuelekea uchaguzi mpya wa Rais au ataitisha Uchaguzi mpya wa Rais wa Muungano ndani ya kipindi maalum. Yeye mwenyewe hatokuwa Mgombea wa kiti hicho.

Hii itaondoa mojawapo ya migongano ya kikatiba iliyopo sasa ambapo Rais wa Zanzibar hana nafasi ya kazi za Kimuungano na hata inaleta mgogoro linapokuja suala la Baraza la Mawaziri. Kutokana na pendekezohili, Waziri Mkuu wa Zanzibar ataingia kikao cha Baraza la Mawaziri akiwa ni nafasi ya tatu baada ya Rais wa Muungano na Makamu wake na atakuwa na uwezo wa kuendesha kikao hicho kama hao wawili awapo.

Japo nina mawazo kadhaa ya muundo mpya wa kikatiba nitayaacha hata hivyo masuala mengine ya kikatiba kwa watu wengine kufikiria na matokeo yake ya kiutawala endapo wataamua kuliangalia pendekezo hili.

Jibu – Muundo wa sasa wa Muungano kuwa na Marais wawili na hata baadhi ya watu kutaka kuwepo na Rais wa Tanganyika ni mawazo mgando yanayotokana na mazoea tu. Pendekezo langu siku zote ni kuwa ni kuwa na Serikali ya Muungano yenye nguvu na Rais Mmoja na Amiri jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na usalama. Zanzibar kama ilivyo sasa iwe na Waziri Mkuu atakayetokana na Chama chenye wabunge wengi katika Bunge la Zanzibar . Tanganyika iwe na Waziri Mkuu atakayetokana na chama chenye wabunge ndani ya Bunge la Tanganyika. Kuwe na Bunge la Juu (call it senate etc) ambalo Mkuu wa shughuli za Serikali ya Muungano Bungeni atakuwa Makamu wa Rais. Rais wa Muungano atateua viongozi wa vyama vyenye wabunge wengi Bungeni kama Mawaziri Wakuu kuongoza serikali zao nay eye Rais atateua Mtanganyika au Mzanzibari yeyote ambaye ataona anafaa kuwa katika Wizara za Muungano kama Mambo ya Nje, Ulinzi, Fedha, Immigration, International Trade, Higher Education, Union Affairs etc.

Mawaziri Wakuu hawa watahudhuria vikao vya Cabinet za Muungano kama wajumbe kamili na wataongoza vikao vyao vya mawaziri (Vikao vya kazi) katika Serikali zao. Hawataitwa Waziri Mkuu wa Zanzibar au Tanganyika bali Waziri Mkuu wa Serikali ya Zanzibar au wa serikali ya Tanganyika ! Makamu wa Rais wa Muungano na Mkuu wa Shughuli za Serikali ya Muungano ndani ya Bunge la Juu ndio atakaimu wakati Rais wa Muungano hayupo na kama wote hawapo Rais wa Senate atafanya hivyo na kama wote hawapo Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Huko Tanganyika na Zanzibar kama Waziri Mkuu hayupo, Naibu Waziri Mkuu atafanya hivyo na kama wote hawapo mmoja wa Mawaziri.

Viongozi wa Kitaifa watakuwa Rais wa Muungano, Makamu wa Rais, Rais wa Bunge la Juu na Jaji Mkuu. Hawa wengine watakuwa viongozi wa Serikali zao tu na protocol itafuata huko chini. Isipokuwa pale ambapo Mawaziri Wakuu hawa wapo, watakuwa na hadhi sawa sawa. Rais wa Muungano atakuwa na Vikao kila Wiki Jumatatu na Makamu wake, Mawaziri wakuu, Rais wa Senate na Maspika wa Mabunge (Baraza la Uongozi la Taifa) kujadili masuala nyeti ya nchi. Vikao hivi vitahudhuriwa pia Na Mkuu WA Usalama WA Taifa, Mkuu WA Majeshi, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Uhamiaji.

KISIASA NA KIUTAWALA
Pendekezo hili linazingatia vile vile ukweli wa kihistoria kuwa maeneo yote haya manne tayari yamewahi kuwa sehemu ya utawala wa Zanzibar. Tanga, Pangani, Mafia na Bagamoyo (kama ilivyo Dar) vimewahi kuwa sehemu ya utawala wa Sultani. Na hata leo hii katika maeneo hayo hayo familia zenye damu ya bara na visiwani zimetapakaa. Hivyo, kuweka maeneo hayo mikononi mwa utawala wa Zanzibar halitakuwa kwa mara ya kwanza, ila sasa hivi itakuwa inafanywa na watu huru wenyewe siyo zao la utawala wa kikoloni au wa kisultani.

Jibu - Kama nilivyosema huko juu hii haiwezi kuwa sababu ya kugawa sehemu ya Tanganyika kwenda Zanzibar. Lakini pia huku ni kurudi nyuma kihistoria. Kama tunataka hili na Dar es Salaam irudi Zanzibar. Pia turudishe Rwanda na Burundi kama sehemu za Tanganyika au tukubaliane na Anglo-Belgiam Agreement na kurudisha Kigoma kama Nchi huru (Kigoma ilikuwa dola inayojitegemea kutokea 1918 – 1926) na kutawaliwa na wabeligiji kama Rwanda na Burundi. Kigoma hiyo ilikuwa inafika mpaka Lolangulu Tabora na mpaka Kahama).

KIUCHUMI
Mojawapo ya matokeo mazuri ya mpango huu ni kuwa tutakuwa tumetatua baadhi ya matatizo ya sasa ya kiuchumi ya karibu maeneo yote hayo manne pamoja na Unguja na Pemba. Tutakuwa tumeongoza eneo la uzalishaji mali kwani ilivyo sasa Zanzibar baada ya muda si mrefu itajikuta haina ardhi ya kutosha kwa ajili ya watu wake, lakini kwa kuongeza eneo la sasa kwa pendekezo hili Zanzibar inaweza kutulia na kuondoa msukumizo wa masuala ya ardhi ambao utaweza kutokea huko mbeleni.

Lakini, kwa wakati huu na mara moja msingi wa mapato wa Zanzibar utaongezwa mara moja. Kuanzia kodi mbalimbali na uzalishaji wa bidhaa na huduma vitaongezeka mara moja. Fikiria viwanda vilivyoko Tanga, bwawa la kuzalishia umeme la Pangani, n.k Nenda kwenye maeneo ya kihistoria ya Bagamoyo, Mafia na Pangani, yote haya yanaweza kabisa kuwa maeneo ambayo yatavutia watalii wengi zaidi ambao wakisikia wanaenda Zanzibar ina maana ni hadi Bagamoyo, Tanga (ambako kuna maeneo mengi ya kihistoria ambao hata Watanzania wengi hawajui kuwa yapo!) na Mafia vile vile. Hivyo, Zanzibar itaongeza wigo wake wa vyanzo vya mapato na wakati ule ule maeneo haya yatanufaika sana kiuchumi kwani na yenyewe yatakuwa chini ya mfumo na usimamizi tofauti. Naamini itakuwa ni bora zaidi kiutawala kuliko ilivyo sasa.

Ukiongeza na uwanja mpya wa ndege wa kimataifa wa Bagamoyo, mabadiliko yatakuwa ni ya manufaa kwa watu, uchumi, na maisha ya Watanzania bara na visiwani.

Jibu – Sijaona hoja ya msingi katika hili la kiuchumi. Syschelles inapata watalii wengi zaidi na ni sehemu ndogo kuliko Zanzibar na ina watu 80,000 tu.

KIJAMII
Mabadiliko haya ninayoyapendekeza hayatabadili sana au kabisa taswira ya kijamii ya Zanzibar. Kama nilivyoonesha hapo juu kuwa maeneo haya manne tayari yamewahi kuwa chini ya utawala wa Zanzibar na kwa kiasi kikubwa kimila na desturi, lugha na dini yanakaribiana zaidi na maisha ya watu wa Unguja na Pemba na hivyo kuyaweka chini ya Zanzibar siyo tu ni suala la kisiasa lakini ni sehemu ya kuunganisha na kuendeleza historia ya pwani yetu ya Afrika ya Mashariki.

Kwa ujumla pendekezo hili la kwanza linazingatia ukweli kwamba Muungano wetu ni lazima uboreshwe na kuangaliwa katika mtazamo wa kizazi cha mbeleni na siyo cha sasa. Mojawapo ya matatizo makubwa ya muungano sasa hivi ni fikra za leo na jana; watawala wetu hawataki (au hawana uwezo wa) kuona mbali kwani fikra na mawazo yao yamezungukwa na manufaa ya sasa na matatizo ya sasa. Pasipo kuangalia Tanzania huko mbeleni ni wazi kuwa maamuzi mengi ya sasa yanabakia kuwa yasiyo na kina yenye mapungufu mengi tu.

Ninafahamu bila ya shaka wapinzani wa muungano (wa bara na visiwani) watakuwa wa kwanza kuhofia pendekezo hili; tatizo ni kuwa hawana sababu hata moja ya kimantiki na kiakili kupinga pendekezo hilo isipokuwa woga wa kufanya jambo jipya! Hakuna mtu yeyote Zanzibar au bara ambaye anaweza kutoa sababu ya msingi kwanini pendekezo hili lisiwezekane. Labda mjadala unaweza kuwa kwenye nafasi za kiutawala n.k lakini hayo yanajadilika na watu wenye uwezo wa kufikiri na wanaolitakia taifa lao mema.

Wiki ijayo nitakuja na pendekezo jingine ambalo kama hili nina uhakika hakuna mtu ambaye anaweza kulikisia. Kizazi kipya kinahitaji fikra mpya katika ujenzi wa Taifa jipya.

Jibu - Hapatakuwa na sura tofauti kwani kimsingi hapa utakuwa umeamua kuwaweka Waislamu wa Tanzania pamoja kwa kuwaundia nchi yao na kuwaunganisha na Zanzibar. Hii itakuwa ni hatari kwa kuondoa mchanganyiko wa kidini uliopo nchini hivi sasa na pendekezo lako laweza kuleta umwagaji damu na chuki kubwa za kidini. Waislamu waliopo Bara zaidi kama kule kwetu Kigoma wataona umepunguza idadi ya waislamu Tanzania Bara. Kimsingi kama umesoma historia ya India na Pakistani unacofanya ni kuanzisha Pakitastan from India. Hii imeleta vita kubwa sana kati ya Hindus and Muslims kwani mataifa yaliundwa kutokana na hilo. Fanatics katika hili watakwambia unataka kupunguza idadi ya waislamu katika Tanzania Bara na kuwarundika katika Taifa lao ‘Zanzibar’… after all walikuwa chini ya Sultan! Same old stories. Religious harmony iliyopo sasa inatokana na muundo wa sasa wan chi kijiografia.

Nitafute: Facebook “mzee Mwanakijiji”




 
Shukurani Mzee Mwanakijiji kwa makala hii.Sema bado imeniacha hoi kwamba mapendekezo haya yanapewa nguvu na katiba ya muungano, ambayo ndio mzizi wa matatizo yote ya muungano.

Mawazo yangu mimi kurekebisha muungano suluhisho ni 2 tuu.

1.Kuvunja muungano wenyewe, hii ni kutokana na uwezo wetu wa kiuchumi ni duni hatuna uwezo wa kushughulikia complexity za muungano.Hii ni fact kabisa, nchi zote zilizoungana zimeungana baada ya kumaliza masuala muhimu katika jamii.

2.Njia ya pili ni kuujadili muungano wote upya, ikiwezekana kuwapatia wananchi referendum watoe maoni yao kama wanataka muungano au hawataki.Tukubali muungano sio maamuzi ya viongozi, bali wananchi wenyewe wana maamuzi na haki kamili ya kujiamulia kama wanapendelea muungano.

Hayo ndio maoni yangu, mimi binafsi yangu ni mzanzibari mwenye kupinga kwa nguvu zote kuwepo kwa muungano huu.Naamini kabisa, kuwa muungano huu umezaliwa kwa sababu potofu.Aidha kwa mawazo yako ya kuunganisha Zanzibar na hizo sehemu ulizozitaja pia sioni kama ni wazo lenye manufaa yoyote.Labda kama litapigiwa referendum, vyenginevyo naliona kama ni sawa na wazo la Nyerere akishinikizwa na mataifa makubwa kuimeza Zanzibar.

Let Zanzibar be a free country, thats my advice!
 
Mkuu wazo lako sikubaliani nalo kabisa! Unabembeleza nini Zanzibar mpaka udiriki ku-suggest kuimega Tanganyika?
 
Mzee Mkjj, mawazo ya kiuchokozi haya, kwa nini usifikirie kugawa vile vile Tabora na Kigoma kwa waZenj ili kudumisha zile "caravan routes" za bisahara ya utumwa?
 
Mzee Mwanakijiji,

Nimesoma pendekezo zima leo hii na naomba nipingane na wewe kwa jambo moja tuu.

Mfumo wa Urais na Makamu wake. Kwa namna ulivyojenga hoja, inaelekea Urais wa Muungano daima utatoka kwa mtu wa Bara! Hili sikubaliani nalo hasa kama ni CCM ndio itakuwa kwenye usukani wa kubadilisha hili.

Kwa nini basi Urais wa Muungano uwe kama ule wa Banana na pande zote Tanganyika na Zanzibari ziwe na Mawaziri wakuu ambao ndio watakuwa wakuu na kuchaguliwa na Wananchi? Nao Mawaziri hawa Wakuu, ndio wawe Makamu wa Kwanza na wa Pili kutegemeana na Rais katokea upande gani wa Muungano?
 
Mheshimiwa nakubaliana na mawazo yako ukiyatazama katika mtazamo mwepesi.Tuna mengi ya kujifunza yaliyotokea kwa muungano uliofuata mtazamo huo,kwa bahati nzuri naishi katika nchi ambayo ilitumia mfumo huo kulete muungano ambayo ilifanikiwa kabla ya imaya hiyo kuanguka kilichozuka baada ya imaya hiyo kuanguka ni vita na umwagaji damu.Hapa namaanisha USSR au Urusi au Russia ilitumia utaratibu huo USSR ilikua ikiundwa na nchi 15.Katika kujaribu kudumisha muungano kulikua na utaratibu wa kuyaungani majibu kadha kutoka nchi (Mshiriki)Kutoka sehemu ya nchi nyingine kwenda nchi nyingine Mfano sifelpol(Krim) kutoka Russia kwenda Ukraine,Georgia kuunganishwa na Abhasia na asetia ya kusini.Azerbajania na Armenia( Gorn karabah Chechenya na Ingusheti n.k baaada ya kuanguka maeneo hayo yakakubwa na vita na na umwanaji wa damu na migogoro ambayo inaendelea mpaka leo kwa baadhi ya majimbo kudai kurudi kama ilivyokua awali kabla ya kuhamishia katika uongozi wa nchi nyingine na baadhi ya majimbo kujitangazia uhuru.Hii inaweza kutokea kwa wazo ulilopendeke baadae sio Pangani,Mafia au Bagamoyo tunaweza kuirudisha.Tuanaweza kutunga sheria ya kua pale Muungano utakapovunjika majimbo hayo yarudishwe,lakini mchango wa majimbo hayo kiuchumi yatarushwa vipi?Kama yanazuka mlumbano kuhusu mafuta ambayo hata haijulikani kama yaopo au hayapo yakishaanza kuchimbwa itakuaje?Kuna watu watalitazama wazo hilo kama HONGO kwa Zanzibar kwa ajiri ya mafuta.Mh. Mwanakiji naheshimu ushauri wako katika kutafuta ufumbuzi wa swala la muungano ambapo sasa limegeuka kua wimbo lakini wazo ulilolitoa ni sawa na kutumia SINDANO YA GANZI kutibu jino.MUNGU IBARIKI TANZANIA
PENDEKEZO LA 1:TANGA, MAFIA, BAGAMOYO NA PANGANI ZIWE SEHEMU YA ZANZIBAR!

Na. M. M. Mwanakijiji

Hili ni pendekezo la kwanza kati ya mapendekezo kadhaa ambayo nitayatoa katika kusaidia kuleta fikra mpya katika mijadala mbalimbali ya kitaifa ambayo lengo lake ni kutupa uwanja mkubwa zaidi wa kuweza kufanyia maamuzi. Miaka 46 imepita tangu Muungano pekee wa nchi mbili za Kiafrika uasisiwe na hivyo kujenga katika bara la Afrika nchi pekee ambayo mipaka yake haikurithishwa na wakoloni! Tanzania tunayoishi leo hii ni tunda na zao la Watanzania wenyewe.

Pamoja na matatizo yote yaliyopo Muungano wetu unapaswa kutetewa, kulindwa na kudumishwa si kwa sababu ya woga, si kwa sababu hauwezi kuvunjika, na si kwa sababu hautakuwa na matatizo huko mbeleni. Tunapaswa kuulinda, kuudumisha na kuuboresha kwa sababu moja tunaupenda kwani ndio nchi pekee tuliyoijenga kwa ajili yetu sisi na watoto wetu.

Ninaamini kabisa kuwa siku watawala wetu watatoka kwenye ufinyu wa fikra wanaouonesha siku kwa siku wataweza hatimaye kuja na mapendekezo ya kuuboresha Muungano wetu na kuufanya uwe kwa faida ya kila Mtanzania na kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima na ambayo utatuzi wake unahitaji dakika chache tu za fikara. Pendekezo hili, halijawahi kutolewa na mtawala yeyote, hawawezi kulitoa kwani hawana uwezo wa kifalsafa kulitetea! Hawawezi kulikumbatia kwa uharaka kwa sababu wamefungwa na siasa zao za utengano hadi wanatia aibu. Hili hata hivyo, haliwezi kuwazuia Watanzania wengine kutoa mawazo yao na kuyasogeza mbele kama pendekezo ili kila Mtanzania ajue kuwa hatuhitaji wazungu watuletee mapendekezo yao ili tuyakumbatie kama yameletwa na wajumbe wa Mungu! Hili ni pendekezo la kuthubutu, la nguvu, la mkakati, la kisiasa, la kiutu, na la kiumoja kuliko mapendekezo mengine yote yaliyowahi kutolewa kuhusu kudumisha Muungano au kuondoa “kero za Muungano”.

READ AT YOUR OWN INTELLECTUAL PERIL!
View attachment 9855
 
Mheshimiwa nakubaliana na mawazo yako ukiyatazama katika mtazamo mwepesi.Tuna mengi ya kujifunza yaliyotokea kwa muungano uliofuata mtazamo huo,kwa bahati nzuri naishi katika nchi ambayo ilitumia mfumo huo kulete muungano ambayo ilifanikiwa kabla ya imaya hiyo kuanguka kilichozuka baada ya imaya hiyo kuanguka ni vita na umwagaji damu.Hapa namaanisha USSR au Urusi au Russia ilitumia utaratibu huo USSR ilikua ikiundwa na nchi 15.Katika kujaribu kudumisha muungano kulikua na utaratibu wa kuyaungani majibu kadha kutoka nchi (Mshiriki)Kutoka sehemu ya nchi nyingine kwenda nchi nyingine Mfano sifelpol(Krim) kutoka Russia kwenda Ukraine,Georgia kuunganishwa na Abhasia na asetia ya kusini.Azerbajania na Armenia( Gorn karabah Chechenya na Ingusheti n.k baaada ya kuanguka maeneo hayo yakakubwa na vita na na umwanaji wa damu na migogoro ambayo inaendelea mpaka leo kwa baadhi ya majimbo kudai kurudi kama ilivyokua awali kabla ya kuhamishia katika uongozi wa nchi nyingine na baadhi ya majimbo kujitangazia uhuru.Hii inaweza kutokea kwa wazo ulilopendeke baadae sio Pangani,Mafia au Bagamoyo tunaweza kuirudisha.Tuanaweza kutunga sheria ya kua pale Muungano utakapovunjika majimbo hayo yarudishwe,lakini mchango wa majimbo hayo kiuchumi yatarushwa vipi?Kama yanazuka mlumbano kuhusu mafuta ambayo hata haijulikani kama yaopo au hayapo yakishaanza kuchimbwa itakuaje?Kuna watu watalitazama wazo hilo kama HONGO kwa Zanzibar kwa ajiri ya mafuta.Mh. Mwanakiji naheshimu ushauri wako katika kutafuta ufumbuzi wa swala la muungano ambapo sasa limegeuka kua wimbo lakini wazo ulilolitoa ni sawa na kutumia SINDANO YA GANZI kutibu jino.MUNGU IBARIKI TANZANIA

Advocate.. mfano wa Urusi hauzingatii uhalisia wa historia yetu. Mapendekezo yangu yanaangalia zaidi kwanza kabisakukubalika kwa principle ya Umoja wa TAifa letu. Tukikubali hiyo principle na kuilinda, basi yote yanawezekana. Sasa hivi nikiangalia watu bado wanaangalia muungano kwa macho ya Uzanzibari na Utanganyika kitu ambacho kinasikitisha sana! Watu wakianza kuangalia kwa macho ya "Utanzania" utaona mambo mengi ni rahisi mno kuyashughulikia.
 
viko visiwa viwili tu Unguja na Pemba lakini hapakaliki wanatoana mijicho sasa tuwape na tnda nk?
 
Unamaanisha hivi?:
attachment.php
 
well... ni kuamua tu.. haya ni mapendekezo kama hayafai mnatakiwa kusema kwanini hayafai.. kuseema "why not dar or pwani" sijui kama kunaunga mkono haya au kunapinga..

Kwa mtazamo wangu geographically haijakaa vizuri.Zejni na Tanga hivyo kuwa nchi maoja naona kama ni kushoto bora Dar na Pwani ni karibu zaidi kuliko Tanga.
 
Kwa kweli nakuunga Mkono kwamba Mikoa hiyo iwe sehemu ya Zanzibar ili kuimarisha Muungano na kuimarisha uhusiano wa miaka nenda miaka rudi.

Lakini hivi sasa Dunia inazizima na kitu kinachoitwa "Regionalisation" muungano wa mataifa yaliyokaribu na kuwa pamoja kiuchumi, kijamii na kiasia na hata kiulinzi.

Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa 21 ya Tanzania Bara, Mkoa huu una historia kubwa sana. Umetoa Viongozi wakubwa kama Marehemu Mzee Saadan Kandoro n.k.

Tangu UHURU ( yaani utawala wa Nyerere) Mkoa huu umeendelea kusahahuliwa kwa kila nyanja, ukianzia Elimu, Afya, Mawasiliano n.k

Mkoa wa Kigoma ni Mkoa unaoitegemea Nchi za Rwanda, Burundi na DRC pamoja na mapigano yake.

Wenyeji wa Mkoa huu wa Kigoma wengi (zaidi ya 90%) wanasikilizana kwa lugha na wenzao wa Burundi na Rwanda na kuna wakati imekuwa vigumu kumtambua Muha wa Kigoma ni yupi na Muhutu wa Rwanda au Burundi ni yupi.

Sasa kwa kuwa tuna Jumuiya ya Afrika Mashariki NASHAURI MKOA HUU WA KIGOMA UGAWANYWE, NUSU yaani kuanzia Wilaya ya Kibondo iende Nchini Rwanda yaani iwe sehemu ya Nchi ya Rwanda, Wilaya ya Kasulu iende Burundi yaani iwe sehemu ya Nchi ya Burundi na Kigoma Mjini iwe sehemu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mpaka uwe eneo la Uvinza, yaana Uvinza ibakie Tanzania. Maeneo ya mwambao wa Ziwa yaende DRC.

Kwa kufanya hivi Mkoa ule utandelea sana maana utakuwa ni sehemu mpya ya Nchi hizo na kutokana na rasilimali zilizopo najua Kagame ataifanya Wilaya ya Kibondo kuwa eneo la Biashara kama kiunganishi cha Nchi ya Rwanda na Nchi ya Tanzania, Na Mhe. Nkurunzinza ataibadilisha Kasulu na kuwa eneo la Bandari ya Nchi kavu kwa kupitia eneo la Manyovu na itakuwa na maendeleo.
Na Generali Kabila ataifanya Kigoma kuwa ni mlango bahari wa mawasiliana na Nchi za Maziwa Makuu.

HILI ni wazi lenye kuona namna ya kuusaidia Mkoa wa Kigoma na kukuga Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama vile tunavyotaka kuihamishia Tanga, Pangani na Bagamoyo iwe sehemu ya Zanzibar.
 
Tawire Mzee, ndivyo tutakavyoimarisha Muungano wetu!

I solute you Mwanakijiji kwa kufikiria mbali na fikra za kawaida tulizozoea. Ni kwa jinsi hii tu ndio tunaweza kupata mawazo mapya ya kuimarisha muungano badala ya kulumbana kila siku. HONGERA
 
Hofu ya kuipenda zanzibari kinafiki inakufanya ufikirie nadharia ya kujidai unagawa sehemu ya Tanganyika kwao...wazanzibar hawahitaji eneo zaidi ila "Justice"

Uchumi hauongezeki kwa kuongeza eneo la ki-utawala...ila kwa mipango thabiti na watu thabiti ..somo la uchumi limekupita pembeni

Nikitafakiri pendekezo lako limekaa kidini dini zaidi hivyo huna jipya...
 
Back
Top Bottom