Pd Titus Amigu: Uanaume ni nguvumali si kubweteka

Ramark

JF-Expert Member
May 19, 2015
1,960
1,392
NGUVU NI MALI, USIPOSADIKI BWETEKEA AKILI YA KINJIKITILE

Waafrika wenzangu, nguvu ni mali, tusiposadiki tubwetekee akili ya Kinjikitile! Akikuambia mtu, “Akili mali” mwambie pia “Nguvu mali.” Jambo hili ni kweli na ndiyo maana wengine wakaja kusema, “Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe.” Laiti mwono huu ungekuwa wa dhati kuliko watu kujipa majina ya “NGUVUMALI” tu, Afrika tungejiponya wenyewe. Tungelijua kwa kuwa hatuna wajomba “tujijombaze.” Tungelijua kwamba “Mtegemea cha nduguye hufa hali maskini.” Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba wanaume Waafrika hatujamakinika na ukweli wa nguvu mali. Nitajieleza, usiwe na munkari.

Wanaume, eh!
Wanasayansi wanasema, kama mwanaume si mlemavu, basi ana chembe chembe hai nyekundu 10% zaidi ya mwanamke. Na kwa vile chembe chembe hai nyekundu ndizo zinazochukua hewa ya oksejeni, maana yake ni kwamba mwanaume akitafuna au akila chakula chochote cha wanga (wali, pilau, ubwabwa, ugali, chapati, mihogo, viazi vitamu, viazi mbatata), huo wanga unapochomwa na oksejeni anafumuka nguvu 10% zaidi ya mwanamke yeyote. Kwa kumweleza kifupi, mwanaume ni injili kubwa. Ni injili ya “silinda nane.” Mwanaume ana “horse power” nyingi na kadhalika.

Kwa maana hii, kila mwanaume, kama si mlemavu, anaweza kubadili maisha yake mwenyewe, maisha ya familia yake mwenyewe, maisha ya jamii yake mwenyewe, maisha ya nchi yake mwenyewe na hata maisha ya bara lake mwenyewe kwa mtaji wa nguvu zake, mtulinga!

Natoa mfano kushadidia ukweli huu. Ni mfano wa makazi bora. Wataalamu wanasema, mwanaume kwa nguvu zake, akitia nia na kujikalifu anaweza kutengeneza matofali ya kuchoma 300 kila siku. Maana yake kwa siku 30 anaweza kupata matofali 9,000 na kwa miezi miwili matofali 18,000 na kwa miezi mitatu matofali 27,000 na kwa miezi minne matofali 36,000 na kadhalika. Staajabu hapo! Matofali mengi namna hiyo atakaaje mtu tena kwenye nyumba ndogo kama kiberiti? Atakaaje tena ghetto? Atalalaje tena katika nyumba ya chumba kimoja akiwa na vitu vyake vyote humo humo kana kwamba ni stoo? Hii maana yake, kwa nguvu za mwili wake tu, mwanaume anaweza kuamua kujenga nyumba kubwa, jiko kubwa, choo kikubwa na kadhalika.
Hii maana yake wanaume, kwa nguvu zao wanaweza kulima mashamba makubwa.

Hii maana yake wanaume wanaweza kupasua mawe magumu ya kujengea nyumba imara za kudumu. Hii maana yake wanaume wanaweza kuchimba makorongo na kutengeneza barabara zao nzuri. Hii maana yake wanaweza kuchimba visima vikubwa wao, wake zao na watoto wao wakanywa maji maangavu. Hii maana yake wanaweza kukata miti mikubwa na kutengeneza wanachotaka duniani. Hii maana yake wanaweza kukata miti wakatengeneza vitanda watu wao wakalala juu na siyo kulalia ngozi chini au kulala ardhini kama hayawani. Hii maana yake wanaume wanaweza kuchana mbao na kutengeneza samani watu wakastarehe majumbani mwao kwa vitu vyenye kupendeza na si kukalia viti vya “mikao ya nyani” na kadhalika. Kifupi, hayo ndiyo majukumu ya mwanaume aliyejengeka kama “mwindaji” kiuhalisia.

Nachelea kuchoka kwako, basi acha nisitoe mifano mingi. Hebu sasa nijumlishe kunena. Tukilisoma jambo hili, ni lazima tuhitimishe kwamba Mungu hakumuumba mwanaume pasi kusudio. Mungu alitaka mwanaume akiwapo pahala alete mabadiliko kwa mtaji wa nguvu zake, afanye kazi kubwa kubwa na kupanga mipango mikubwa mikubwa, wakati akina mama wakifanya kazi nyingi ndogondogo na kusimamia kazi mbalimbali pamoja na kuwalea watoto wao kwa wororo wao wa kutunza viota.

Tukijumlisha tena kunena, ni hivi, Mungu alitaka wanadamu wagawane majukumu. Nikirudia kwa maneno mengine, kusudio la Mungu kwa kuwaumba wanaume halikuwa kula, kulala na kutungisha mimba basi. Badala yake alimpa nguvu nyingi awe mtaji wa maendeleo ya binafsi, ya familia yake, ya jamii yake, ya nchi yake na hata ya bara lake.

Hivi basi, hapa petu Afrika, ukiona mwanaume aliyeoa, tena mwenye ndevu zake, analala na mkewe kwenye nyumba ndogo, ambapo wakilala miguu yao inaonekana nje, ujue shida ni ya mwanaume pale, hajitambui. Hajatambua maana ya “nguvu mali.” Ukiona mwanaume aliyeoa, tena mwenye ndevu zake, yeye na watoto wake wanatumia choo kidogo ambacho mlango wake ni gunia la katani na ili kuingia mtu anaingia akiwa ameinama, ujue shida ni ya mwanaume pale, hajitambui. Hajatambua maana ya “nguvu mali.”Ukiona familia fulani nguo wanaanika kwenye nyasi au majani, yaani hawana hata kamba ya kuanikia nguo, ujue shida ni ya mwanaume pale, hajitambui. Hajatambua maana ya “nguvu mali.”

Ukiona umaskini umebamba mahali, wakati vijana wake wa kiume wanajazana vijiweni kucheza karata, kucheza drafti, kubeti na kucheza au kutazama mpira kwenye “vibanda umiza” tu, walaumu hao vijana usiwalaume akina dada na mama zao. Ukiona wanakijiji hawajali hata aibu ya kujengewa vyoo vya shule yao ya msingi, au ya sekondari na hata ya Chuo chao Kikuu na Umoja wa Ulaya au na USAID, ujue shida ni ya wanaume, hawajitambui. Hawajatambua maana ya “nguvu mali.”
Naongeza kusema kidogo. Ukiona watu katika mkoa au nchi fulani wana mashamba madogo madogo kama viwanja vya “chandimu”, ujue shida ni ya wanaume, hawajitambui. Hawajatambua maana ya “nguvu mali.” Ukiona kijiji kina kisima kidogo kama jicho la ng’ombe na wanawake wake wanachota maji kwa taabu, ujue shida ni ya wanaume, hawajitambui. Hawajatambua maana ya “nguvu mali.”

Ukiona barabara ya mahali fulani ina makorongo makubwa, na wenyewe wanapita kwa taabu masika na kiangazi, ujue shida ni ya wanaume, hawajitambui. Hawajatambua maana ya “nguvu mali.”
Ukiona watu wamekusanyika, wanaume na wanawake pamoja na watoto wao, kwenye kongamano na wanamwomba Mungu kwa kelele awaondolee umaskini kwa AKILI YA KINJIKITILE eti kwa kusema tu, “UMASKINI ONDOKA! UMASKINI ONDOKA!, UMASKINI ONDOKA!” au “UMASKINI ACHILIA! UMASKINI ACHILIA! UMASKINI ACHILIA!” au wakisadikishwa kwamba umaskini wao utaondoka kwa kula matango ya upako, au keki za upako, au kukanyaga mafuta ya upako, au “kujambiwa” ushuzi wa upako, au kupata teke la upako, au kuvaa “chupi za upako”, au kwa kunywa maji ya upako, ujue shida ni ya wanaume waliojiunga na akina mama pale, hawajitambui. Hawajatambua maana ya “nguvu mali.” Wangelitambua wangekataa utoto huo. Hapo wasamehe akina mama lakini usiwaache bila hatia hao akina baba. Malofa hapo ni hao wanaume.
Kwa haya ninayosema, kama unanipata vizuri, wanaolofaza Waafrika kwenye Karismatiki ni wanaume, hawajitambui. Wasamehe akina dada na akina mama pamoja na watoto wao, maana watunza viota, hasa hapa Afrika, wanafuata fikra za wanaume kwa kumbakumba tu. Lakini ikusikitishe zaidi ikiwa kati ya wanaume hao eti wapo marais, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, maaskofu, au mapadre, au mashemasi, au mafrateri, au mabruda (mabradha). Asikudanganye mtu, wote hao ni “wale wale wasiojitambua katika uanaume wao.” Ha, wanaume wazima wanalialia wakisadiki matatizo ya watu wao: bara lao, nchi zao, mikoa yao, majimbo yao, parokia zao, vigango vyao, familia zao na kadhalika yatatulika kwa AKILI YA KINJIKITILE! Usistaajabu Babu wa Loliondo, akitembelea akili hii hii, aliwapata watu milioni 4.5 akawapiga pesa. Na bado akina Babu wa Loliondo wengine watajitokeza na kupiga pesa vile katika siku za usono! Sisi hatugutuki, hatuambiliki na wala hatuamshiki.

Vivyo hivyo, wanaolofaza watu kwenye makanisa ni wachungaji, manabii na mitume wanaume; akina mama wanadanganyika na kusombwa sombwa tu. Katika hili tusimung’unye maneno na wala tusimwogope mtu! Acha tuseme ukweli huenda Afrika tutapona!
Ndiposa, ulofa huu wa Waafrika wa kutojitambua, hususan wanaume, Waarabu na Wazungu wajanja na wasio na huruma, waliujua ndiyo maana wakasema yafaa watupeleke utumwani Bara Arabu, Marekani, Brazili, Haiti na kadhalika. Wakawasomba babu na bibi zetu kama wanavyosombwa ng’ombe na mbuzi kutoka Usukumani kupelekwa machinjioni Dar es salaam. Basi, ukiwaona Wamarekani weusi walivyo mapande ya watu, miraba minne, usiseme mengi ujue ni mapato ya mkasa wa Waafrika kutojitambua tangu zamani za kale.

Kwa vyo vyote iwavyo, tungeweza kusema hapo kale vichwa vya Waafrika vilikuwa havijapambuzuka vizuri. Kwa namna hiyo, tungeweza kuwasamehe wazee wetu waliopelekwa utumwani zama zile za kale. Kauli ya ajabu ya wahenga inasema, “Mavi ya kale hayanuki.” Kwa mantiki hiyo, hali ya sasa ndiyo itusikitishe zaidi. Utusikitishe ukweli kwamba leo hii duniani kulipokucha, bado wanaume wa Afrika hatujitambui vyema.

Sasa kwa kutojitambua sawasawa wanaume Waafrika tunashindwa kujiletea maendeleo katika bara letu wenyewe, badala yake tunapumzika zaidi, tunaacha rasilimali zetu ziibiwe, tunaenda wenyewe kuwaalika wezi wa mali zetu waje waziibe kwa jina la wawekezaji na kadhalika. Kisha wao kuchukua vyetu vyenye thamani nyingi tunawageukia kuwaomba misaada ya pesa, misaada ya mikopo, misaada ya vitu walivyotumia tayari (mitumba) na kadhalika. Mkasa huu unasikitikisha na unauma sana. Au wewe waonaje? Kwa mfano, tunalima pamba, tunawauzia na baada ya wao kutengeneza nguo na kuzivaa, pamba yetu inaturudia katika mfumo wa mitumba (“sekendihendi”). Halisikitishi hilo?

Mzungukomshenzi wa Umaskini
Matokeo ya haya yote ni mzungukomshenzi (Waingereza wanaita vicious circle). Kwa mzungukomshenzi umaskini wetu unazidi kukita mizizi barani mwetu. Matokeo yake bara la Afrika linageuka bara la dhiki na adha, bara lisilokalika, bara la kukimbiwa na watoto wake.

Katika hali hiyo hata HISA YA AKILI (IQ) ya jamii inashuka. Matokeo yake baadhi yetu wanadhani tumelaaniwa na mababu zetu au tumerogwa au tumefanywa hivyo na ukoloni. Matokeo ya fikra hizo ni maamuzi ya kitoto: kuingia makanisani kumwomba Mungu miujiza, kuamka manane na kusali, kufanya ibada za kung’oa miti ya laana, kufanya ibada za kufunguliwa pamoja na kuuziana vitu vinavyoitwa vyenye upako. Matokeo mengine ni baadhi yetu kufanya “maamuzi ya kipaka”, ndiyo kwenda Ulaya na Marekani wakiridhia hata kufanywa watumwa mamboleo.

Ukibisha habari ya mchanyato huu wa matokeo ya ovyo, nijibu kwa nini makongamano ya kuombeana ututoke umaskini na magonjwa yanastawi zaidi Afrika tena kati ya watu wa rangi nyeusi? Nijibu kwa nini ukienda kwenye makongamano hayo huwakuti Wahindi wala Wazungu wa kweli? Hapa nijibu hata kwa mapovu! Potelea mbali!

Kwa nini Wahindi na Wazungu Hawako kwenye Makongamano Yetu?
Nalichomoa mwangani swali hili. Narudia. Hivi kwa nini Wahindi na Wazungu wa kweli hawako kwenye makongamano yetu? Niambie kama umewaona. Kama umewaona niambie walikuwa wangapi. Utake usitake, jibu halisi la maswali hayo ni moja, kwamba wanaume wa Kihindi au Wazungu wamewaimarisha akina dada na akina mama zao. Wameshaagana na akili za kitoto. Hawabwetekei AKILI YA KINJIKITILE kama sisi. Tangu zamani kabisa walishatambua maana ya “nguvu mali.” Kinyume chao ni wanaume sisi weusi, ashakum si matusi, “tuliomwanamkika”, yaani tulio na tabia za kuelekea tabia za wanawake.

“Kumwanamkika” na “Kumwanaumika”
Niache nikuelimishe kidogo maana nakusudia uerevuke. Tafadhali elewa vizuri jambo lifuatalo, kwamba kisaisokolojia na kihisia, wanawake ni watunza viota (nestkeepers) na wanaume ni wawindaji (hunters). Mgawanyo huu ni mtakatifu; haifai mwanaume “kumwanamkika” na mwanamke “kumwanaumika”, yaani mwanaume kujizoesha tabia za mwanamke na mwanamke kujizoesha tabia za mwanaume. (Samahani, BAKITA, nimewaongezea maneno mapya, mkiyapenda yachukueni, kama sivyo niachieni mwenyewe). Ukinibisha habari za utakatifu wa mgawanyo wa jinsi alioupanga Mungu, niambie kwa nini wanawake “waliomwanaumika” hawaolewi kirahisi na wanaume “waliomwanamkika” hawamudu kujenga familia imara.

Hasara ya Kutojitambua Wanaume Weusi
Hasara za wanaume Waafrika kutojitambua ni nyingi mno: kuchukuliwa watumwa, kutawaliwa na wakoloni, kunyonywa na wakoloni, kuharibu kazi ya wazalendo, kuzidi kudidimia kwa bara hili na Waafrika kugeuka ombaomba. Sikiliza. Kuna tofauti kubwa kati ya wanaume weusi na wanaume weupe. Wazungu walitambua maana ya “nguvu mali.” Kifupi, walijitambua na tena walipitiliza sana kujitambua kwao, wakaona wanaweza kuliibia bara hili au tuseme wakatambua wakijifanya wezi au majambazi na kutunyang’anya vitu sisi mazoba wangeweza kujiletea maendeleo kwao. Na kweli ikawa hivyo.

Samahani, ni kama walisema badala ya wanaume wazima na wake zao na watoto wao eti wamlilie Mungu makanisani katika mambo ya kidunia, aheri wawe wezi au majambazi kwani walikuwapo watu “mazoba” barani Afrika. Nakuhabarisha. Wazungu wakipata tatizo kwao husema mara moja, “Afrika must be part of the solution” yaani kwamba “Afrika lazima iwe sehemu ya suluhisho.”

Ndiyo kisa wakaja Afrika kutuchukua tusiotambua hilo. Ukinibisha jiulize Wazungu walifauluje kutuchukua watumwa wanaume wenzao? Pamoja na Waarabu, kwa miaka 246, yaani rasmi tangu 1619 hadi tarehe 1.2.1865, wakatuuza kama mbuzi. Kweli, pasi masihara, baadaye walipogundua kwamba sisi “mazoba,” wakaamua kugawana bara letu kama keki, kule Berlin kwenye mkutano uliofanyika tangu tarehe 15.11.1884 hadi 26.2.1885. Kabla kidogo ya kufika kwao wakawatuma watu wa kutuchungulia jinsi tulivyozubaa, akina David Livingstone, akina Henry Stanley na wenzao. Jina zuri wanalopewa watu haeo eti huwa “wavumbuzi! Wakavumbua machoni petu, mito, maziwa na mabonde ambayo tulikuwa tunakaa nayo kizoba. Ndipo hao, waliripoti kwamba sisi tulikuwa na minyama mikubwa tu lakini si lolote, hivyo tusiogopwe.

Ndipo kweli wakaja wakagawana bara letu, kwa mabavu na wakati mwingine kwa vizawadi vya kitoto kabisa kwa wafalme na machifu wetu: shuka, vioo vya kujitazamia usoni, sufuria, sahani, vikombe na hata vijiko. Katika uzoba wetu, sisi tukawapa ardhi, dhahabu, almasi, chuma na kadhalika. Je, wanaume babu zetu hawakuzubaa?

Tuendelee kusimulia. Wanaume weupe wakatutawala walivyotaka, tangu mwishoni mwa karne ya 19 hadi katikati ya karne ya 20. Waliogoma wakawalipua kwa baruti na bunduki. Lakini baadaye wanaume wenzetu wazalendo wakagutuka. Wakapigana vita vya ukombozi. Akina Bushiri, akina Mkwawa, akina Munyigumba, akina akina Patrice Lumumba, akina Kwame Nkurumah, akina Samora Machel, akina Nelson Mandela wakapigania ukombozi, wakafaulu.
Lakini sasa tunaharibu mafanikio ya wazalendo wetu, nasi tunarudi kule kule kwenye kuzubaa. Tunawaachia wanaume weupe na Wachina watuibe vyetu na watutawale watakavyo. Hii ni aibu sana na katika hali hii, akina Bushiri, akina Mkwawa, akina Munyigumba, akina akina Patrice Lumumba, akina Kwame Nkurumah, akina Samora Machel, akina Nelson Mandela hawawezi kuibuka tena. Tumekwisha!

Lakini kwa nini wanaume wa Afrika “tunamwanamkika?” Jibu ninalo. Hatujitambui na wala hatujatambua maana ya “nguvu mali.” Tumezubaa na tunaleana tuzubae. Kifupi, hapa Afrika sasa malezi yanaenda kombo kiasi kwamba wanaume wazima tunakulia tabia za watunza viota. Napigia msumari na ashakum si matusi, wanaume wa Afrika “tunamwanamkika” zaidi na zaidi. Yaani, tunazidi kutoka kwenye sifa yetu ya kuwa wawindaji tunazidi kufanana na watunza viota. Lakini nani atatusaidia kufunga breki mserereko huu?

Inauma sana. Mserereko huu ni mkubwa siku hizi. Ndio maana ukienda kwenye kongamano unashangaa mwanaume mzima (aliyeoa) au kaka mzima amefika pale pengine na mkewe na watoto wake analia eti kumwomba Mungu msaada apate ajira, apone magonjwa kwa kukemea, apate nyumba ya kulala, apate chakula alishe familia yake, apate visa kwenda Marekani na kadhalika wakati musuli anao. Maskini, amemwanamkika! Hatambui “nguvu mali.”

Mwishoni mwishoni hapa acha nikufikirishe kwa sauti! Kama mwanaume analia na mkewe na watoto wake, hapo pataendelea nini kama si udumavu wa akili na ustawi wa AKILI YA KINJIKITILE tu? Unapata picha? Basi, usistaajabu, Afrika itabaki omba omba milele maana hakuna wanaume wenye kutumia nguvu na akili.

Hatujatambua “nguvu mali.” Ndiyo kisa watu hawatuogopi Waafrika maana tunafanana na familia ya paka au ya mbwa tu: “baba kulishwa, mama kulishwa, watoto kulishwa!” Mbwa wanaposubiri ugali kutoka kwa mfuga mbwa wote wanakuwapo. Ha! Yaani baba mbwa naye hajijui kwamba ameoa!

Lakini ebu nirejee pointi moja ya hapo nyuma. Ni hivi, kutokana na umaskini kutamalaki Afrika, wengine wetu, wanaume hasa, badala ya kutumia nguvu kuliweka bara hili katika chati ya maendeleo wanaamua, “maamuzi ya kipaka,” kwenda kuhemea maendeleo Ulaya, Marekani, China na Japani au hata kama ni kufanywa watumwa wafanywe tu. Wamefubaika vichwani na mioyoni. Wanaoamua hivi huamua kuvuka maji kwenda Ulaya hata kama watu wanakufa kwa mamia kila mwaka baharini.

Ukinibisha, nenda kwenye pwani za Tunisia na Libya, ukawaone vijana Waafrika weusi, wenye nguvu zao na mizuzu yao, wanavyogombea kuvuka Bahari ya Mediteraniani wakahemee maisha mazuri ughaibuni na hata Wazungu wakitaka kuwafanya watumwa wawafanye tu.

Lakini si hao tu, vivyo hivyo tafiti katika nchi zetu uone ni wanaume wangapi ambao ndoto zao ni kuvuka Bahari ya Atlantiki kwenda Marekani au kukwea “pipa” kwenda China au Japani na kadhalika. Nakwambia hawajali aibu wala mauti. Hata watu wafe kiasi gani katika safari hizo, hakuna anayeogopa. Hata watu weusi wabaguliwe sana huko ughaibuni hawajali.

Lakini usugu huo ukakujaje? Kwa sababu mioyoni mwao wanasema, “Heri kuwa mbwa Ulaya au Marekani kuliko kuwa mtu Afrika.” Lakini wanachosahau ni ule mzungukomshenzi kwamba umaskini wanaoukimbia wanaosababisha leo hii ni Waafrika wenyewe hao hao, maana hawajajitambua na wala hawajatambua “nguvu mali” na kwamba “Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe.” AIBU! AIBU! AIBU! Serikali zetu Afrika, TAFAKARINI pamoja nasi juu ya aibu hii! Tulifanyeni Afrika bara la kukalika!
Mzee wenu Pd. Titus Amigu
 

Mkalapa boy

Member
Aug 19, 2021
86
170
Baba padre nyumba za ibada zinachezewa Sana kwa nn wasanii waislamu hawafanyi Sanaa yao misikiti I? Wenzetu wanaheshimu Sana nyumba zao za ibada kwa wasimamizi wa hayo makanisani wanaruhusu upumbavu ufanyike kanisani tena na wasanii Waislam ipo siku wataigiza porn kanisani.Kemeeni jamani
 

Championship

JF-Expert Member
Aug 7, 2019
5,222
9,512
Padre Amigu nilikuwa namsikiliza zamani akijibu maswali redio maria na nikagundua kweli katoliki haihusiani kabisa na kanisa la Yesu Kristo. Ni dini nyingine kabisa
 

Fall Army Worm

JF-Expert Member
Jan 8, 2015
17,568
11,833
Padre Amigu nilikuwa namsikiliza zamani akijibu maswali redio maria na nikagundua kweli katoliki haihusiani kabisa na kanisa la Yesu Kristo. Ni dini nyingine kabisa
Hebu acha chuki zako mbwa wewe,Majitu mengine kazi kuleta chuki za kidini tu,sasa km kweli Wewe unakielewa unachokipinga si ueleze hapa kinagaubaga!!,Lkn kwasababu wewe una chuki tu na Kanisa Katoliki ndio maana huwezi kuelezea.Na mtakoma sana na chuki zenu tunaendelea kujizatiti kiimani,Redio Maria Sasa inazidi kuenea Nchi nzima ili watu wapate Injili,Wavimba macho mtakoma.
 

Fall Army Worm

JF-Expert Member
Jan 8, 2015
17,568
11,833
Baba padre nyumba za ibada zinachezewa Sana kwa nn wasanii waislamu hawafanyi Sanaa yao misikiti I? Wenzetu wanaheshimu Sana nyumba zao za ibada kwa wasimamizi wa hayo makanisani wanaruhusu upumbavu ufanyike kanisani tena na wasanii Waislam ipo siku wataigiza porn kanisani.Kemeeni jamani
Kweli kabisa.
 

Inside10

JF-Expert Member
May 20, 2011
25,036
21,829
"Ukibisha habari ya mchanyato huu wa matokeo ya ovyo, nijibu kwa nini makongamano ya kuombeana ututoke umaskini na magonjwa yanastawi zaidi Afrika tena kati ya watu wa rangi nyeusi? Nijibu kwa nini ukienda kwenye makongamano hayo huwakuti Wahindi wala Wazungu wa kweli? Hapa nijibu hata kwa mapovu! Potelea mbali!

Kwa nini Wahindi na Wazungu Hawako kwenye Makongamano Yetu?"
Padri Amigu
 

Ramark

JF-Expert Member
May 19, 2015
1,960
1,392
Baba padre nyumba za ibada zinachezewa Sana kwa nn wasanii waislamu hawafanyi Sanaa yao misikiti I? Wenzetu wanaheshimu Sana nyumba zao za ibada kwa wasimamizi wa hayo makanisani wanaruhusu upumbavu ufanyike kanisani tena na wasanii Waislam ipo siku wataigiza porn kanisani.Kemeeni jamani
Sanaa ina mawanda yake na ni lazima yatekelezwe na kazi ya kanisa ni kuendeleza sanaa hiyo na si kupingana.

Tazama kuna movie nyingi zimeekti kuhusu maisha ya mapadri , maaskofu na hata papa pia IPO movie POPE MUST DIE ni vituko lkn ipo duniani.

Tuaiche sanaa itambae inawezekana ina ujumbe kwetu tujifunze kama inapotosha unaiacha lkn ukweli upo.
 

Gulwa

JF-Expert Member
Jun 16, 2008
7,885
11,232
Padre Amigu nilikuwa namsikiliza zamani akijibu maswali redio maria na nikagundua kweli katoliki haihusiani kabisa na kanisa la Yesu Kristo. Ni dini nyingine kabisa
Wewe utakuwa ni msabato unayeongozwa na uzushi wa malaya mmoja mzungu hellen white
 

Championship

JF-Expert Member
Aug 7, 2019
5,222
9,512
Hebu acha chuki zako mbwa wewe,Majitu mengine kazi kuleta chuki za kidini tu,sasa km kweli Wewe unakielewa unachokipinga si ueleze hapa kinagaubaga!!,Lkn kwasababu wewe una chuki tu na Kanisa Katoliki ndio maana huwezi kuelezea.Na mtakoma sana na chuki zenu tunaendelea kujizatiti kiimani,Redio Maria Sasa inazidi kuenea Nchi nzima ili watu wapate Injili,Wavimba macho mtakoma.
Hili andiko lako hapa linathibitisha pasipo shaka yoyote hoja yangu. Yesu Kristo ninayemfahamu mimi hayupo kabisa sawa na lugha yako inayoonesha kilichopo moyoni mwako.
 
12 Reactions
Reply
Top Bottom