Paul Makonda ni sawa na Usain Bolt asiyemaliza mbio

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,604
2,000
Habari wanaJF,

Muandishi wa habari za michezo na mchambuzi wa masuala mbalimbali ndugu Eddo Kumwembe ameibuka na makala ya kuelezea juhudi za Paul Makonda kuwa ni sawa na Usain Bolt asiyemaliza mbio.
===========
Mmoja kati ya watu wanaotoa mvuto katika taarifa za habari za siku hizi ni ‘bosi wetu wa mkoa’, Paul Makonda. Jiji lake hili anahakikisha kila baada ya saa 24 anatoa tamko au angalizo au amri. Inaweka tabasamu usoni unapoanza kutafakari.

Makonda anajaribu kushika kila sehemu. Inawezekana ni hulka yake binafsi na labda nafsi inavyomtuma kuwa huo ni mwendo mdundo wa kuendana na kasi ya Rais John Magufuli au inawezekana kabisa ujana na hamu ya kazi vinasababisha awe kama alivyo.

Mmarekani aliyewahi kuwa bosi katika katika kampuni ya magari ya Ford Mustang, Lee Iacocca aliwahi kusema ‘Ili upate mafanikio, unahitaji kuweka vipaumbele na kuvisimamia’.

Viongozi bora huwa wanaacha kumbukumbu nzuri kama wakiweka misimamo katika vitu vichache na kuvisimamia.

Kufikia 2020 wakati bosi mkuu wa nchi, Rais Magufuli atakapokwenda katika uchaguzi mwingine, huenda Makonda asiwe amefanikiwa katika chochote cha msingi kama ataendelea kushika jambo moja na kuliacha ndani ya saa 24 kabla ya kushika jambo jingine.

Unapopewa jiji kama la Dar es Salaam, yapi ni mambo ya msingi ya kuyafanya? Moyoni unapaswa kupata simanzi na umaskini uliopo, ukosefu wa ajira, uchafu, foleni na machache mengineyo.

Makonda ana kipaji cha kuamka na jambo jipya kutegemea tu na habari ambayo imevuma katika kituo fulani cha TV au redio. Lazima ajaribu kusimama juu ya habari hiyo. Hana moyo wa kusita na kuiacha ipite kama ilivyo ili aendelee na vipaumbele vikuu vya jiji hili ambavyo ni matatizo ya walio wengi.

Kwa mfano, kuna watu walioamua ‘kujiua’ wenyewe kwa kuvuta shisha katika maeneo machache ya Jiji la Dar es Salaam. Hili siyo tatizo la wengi. Hivi tatizo la uvutaji shisha na tatizo la uchafu katika masoko yetu ya Tandale, Kariakoo, Temeke, Mwananyamala, Vingunguti Machinjioni na kwengineko, kipi kinapaswa kupewa kipaumbele?

Katika shisha watu wanajaribu ‘kujiua’ wenyewe na afya zao, lakini kikitokea kipindupindu wanakufa na wasiohusika. Kiongozi anapaswa kuweka kipaumbele chake wapi katika maeneo haya?

Kiongozi wa jiji atakumbukwa kwa kusimamia miundombinu ya jiji inayoleta mafuriko kila kukicha kuliko kujaribu kushughulikia watu ambao wanafuatilia akaunti binafsi za watu wenye tabia za ushoga mitandaoni.

Suala hapa ni kipaumbele. Au kwa sababu mvua hazinyeshi kwa sasa kwa hiyo, tunasubiri mafuriko yatokee ndipo tujiweke mbele ya kamera za televisheni mbalimbali nchini?

Karibu kila kitu ambacho Makonda anakishika anajikuta akikiacha njiani na haraka haraka kujaribu kuwa sehemu ya taarifa mpya iliyotinga jijini. Suala la vijana waliojikusanya pale Leaders Kinondoni kusaka ajira zake sijui liliishia wapi?

Vipi walimu wanapanda bure daladala? Vipi suala la madawati, kila mwanafunzi anakaa katika madawati? Vipi ombaomba wameondolewa katika Jiji la Dar es Salaam? Yote yanaguswa na kisha yanaachwa kama yalivyo. Tunasubiri habari mpya na kuitolea tamko hata kama haina madhara kuliko matatizo ya wakazi wa jiji.

Ajifunze kwa Mwaibula

Akiwa kiongozi wa masuala ya usafiri ndani ya Jiji la Dar es Salaam, David Mwaibula anakumbukwa na kila mmoja kwa ubunifu wake wa kuzindua njia mbalimbali za daladala kupita. Mpaka leo tulio wengi tunamkumbuka kwa jambo hilo. Hiki kitu ndiyo kinaitwa Legacy.

Kuna asilimia kubwa Makonda akaondoka katika Jiji la Dar es salaam bila ya kuacha ‘Legacy’ kama ataendelea kushika jambo moja na kuliacha ndani ya saa 24 kisha anaibuka na jingine. Kitu cha muhimu ni kujaribu kufa na matatizo fulani ya msingi ambayo inaonekana yaliwashinda wakuu wa mikoa waliopita.

Washauri wake wafanyake kazi

Muda si mrefu Makonda ataanza kutoeleweka kwa watazamaji wengi wa taarifa ya habari. Washauri wake, kama anao, wasichelewe kumshauri katika hili. Matatizo mengi makubwa ambayo yatamwachia kumbukumbu nzuri ni yale ambayo yanahitaji ushauri, mkakati, malengo na utekelezaji.

Yote haya yanahitaji ushirikiano kati ya Makonda na watu wa idara nyingine. Ofisi yake siyo kila kitu katika kufuta matatizo ya Jiji la Dar es Salaam. Kuna watu wapo kando ndio watoa fedha, au waidhinisha mipango. Anashiririkiana nao?

Ukiamka na kusema ‘Ni marufuku watu kuvuta sigara hadharani’, watu watajiuliza, kuna chemba za kuvutia zinakuja? Kabla haujasema hakikisha kauli yako kuna sehemu inamalizia kwa kuelezea mkakati pendwa kwa watumiao.

Nina kila sababu ya kuamini kuwa Makonda ana dhamira nzuri. Huo ndiyo msingi wa kila anachojaribu kufanya. Lakini kitu cha muhimu katika nyakati hizi ni kutokuwa na haraka na badala yake ajikite katika mambo magumu machache ‘alale nayo mbele’ na yawe ajenda zake kuu.

Hotuba yake ya kujitambulisha kama Mkuu wa Mkoa pale Diamond Jubilee ungeweza kudhani ilikuwa ni hotuba ya Rais. Iligusa matatizo ya nchi nzima badala ya ya jiji la Dar es salaam pekee, hasa yale ya msingi ambayo ni kero za wananchi.

Asijiviringishe katika mambo mengi ambayo baadaye wapinzani wake kisiasa watatumia kama kitanzi chake siku za usoni. Umri wake bado mdogo na nyakati zinamruhusu kufanya mambo makubwa sasa kwa matokeo ya baadaye.

Utatuzi wa kero moja tu ya msingi unaweza kumgeuza Makonda kuwa Mwaibula mwingine, kuliko kugusa mambo arobaini na kuyashughulikia kwa asilimia moja moja. Itakuwa hadithi ya kuwa na kasi kama mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt lakini hamalizi mbio.
 

MsemajiUkweli

JF-Expert Member
Jul 5, 2012
13,025
2,000
Makonda ana raslimali watu kama Meya wa Jiji, Isaya Mwita ambaye ni mzalendo kweli kweli asiyetaka siasa katika utendaji lakini ninachokiona hamtumii vizuri katika kazi zake.

Matamko aviachie vyama vya siasa kwa sababu hizo ni kazi za vyama vya siasa. Kazi ya serikali ni utekelezaji.

Bila team work, atajikuta hana legacy baada ya miaka minne kama ataendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Team work na vipaumbele ndiyo nguzo ya mafanikio katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na kwamba ana idea nzuri.
 

MTK

JF-Expert Member
Apr 19, 2012
8,610
2,000
Hii ni sindano ya moto kwa Makonda, katika siku za karibuni hoja kama hii imekuwa ikijirudiarudia mara kwa mara kutoka kwa watu mbalimbali, Makonda shituka, jitathmini upya kiutendaji, umeanza kuwa kichekesho, vinginevyo usije lalamika kwamba hukushauriwa!? Kalagabaho!
 

PSPA Pure'12 udsm

JF-Expert Member
Jan 11, 2013
818
500
Nimepapenda hapa!

Ukiamka na kusema ‘Ni marufuku
watu kuvuta sigara hadharani’,
watu watajiuliza, kuna chemba za
kuvutia zinakuja?
Z cf Zszxcxx,Zzz czx
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom