Paul Makonda kufikishwa Mahakamani Februari 3, 2022 katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka

telegram

JF-Expert Member
Mar 10, 2021
297
330
ALIYEKUWA Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Christian Makonda, sasa ameamriwa kufika mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni, Dar es Salaam, tarehe 3 Februari 2022, kujibu mashitaka ya jinai yanayomkabili.l

Taarifa kutoka Mahakama hapo na ambazo zimethibitishwa na mwandishi wa habari mwandamizi, Saed Kubenea, ambaye ndiye aliyefungua shauri hilo zinasema, tayari mhimili huo umetamtaka Makonda kufika siku hiyo.

Katika kesi hiyo ambayo imevuta hisia za wengi na kuibua mjadala mzito kila kona ya nchi hususani katika mitandao ya kijamii, Kubenea anamtuhumu Makonda kwa makosa mbalimbali.

Miongoni mwa makosa hayo, ni matumizi mabaya ya madaraka ya umma, wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kesi dhidi ya Makonda, imesajiliwa mahakamani kama Miscellaneous Criminal Application Na. 1 ya mwaka 2022 na imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Aron Lyamuya.

“Ni kweli kwamba kesi tayari imesajiliwa na kupangiwa hakimu wa kuisikiliza na kwamba, Mahakama imetoa amri (summons), inayomtaka Bwana Makonda kufika mahakamani, Februari 3 mwaka huu,” ameeleza Kubenea

Katika kesi hiyo, Kubenea anawakilishwa jopo la mawakili wakiongozwa na Nyaronyo Mwita Kicheere na Hekima Mwasipu.

Kupatikana kwa taarifa hizi kunakuja siku tatu, baada ya gazeti hili kuripoti kuwa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imeziagiza Mahakama za Kinondoni na Kisutu, kufungua shauri la jinai dhidi ya Makonda.

Mahakama ilitoa maelekezo hayo, baada ya Kubenea kuandika barua ya malalamiko kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, akisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Kinondoni, zimegoma kufungua kesi yake.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Joseph Luambano, Januari 14 mwaka huu, ni kwamba Kubenea “anayo haki ya kufungua shauri hilo la jinai, iwapo anataka kufanya hivyo.”

Kabla ya hatua hiyo, Kubenea alikuwa amefungua shauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni na kusajiliwa kama – Miscellaneous Criminal Application No. 7/2021 – akiomba kuruhusiwa kumshitaki Makonda.

Aidha, Desemba 3 mwaka jana, akawasilisha maombi Mahakamani ili kuondoa shauri lake, kwa ajili ya kufanyia marekebisho baadhi ya maeneo, jambo ambalo Mahakama ililikubali; lakini katika mazingira ya kutatanisha, baadaye Mahakama hiyo hiyo, ikagoma kupokea kesi hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Makonda anadaiwa kuwa siku ya tarehe 17 Machi 2017, akiwa na watu waliobeba silaha za moto, alivamia Clouds TV na kumuagiza mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu kurusha video inayomwonesha mwanamke aliyejulikana kwa jina la Grace Athuman.

Katika video hiyo, ambayo haijulikani nani ameiandaa, mwanamke huyo alidaiwa kuonekana akifanya tendo la ndoa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Kwa mujibu wa ushahidi wa video za CCTV, Makonda anaonekana kuvamia kituo cha Clouds saa nne usiku, akiwa anaendesha mwenyewe gari namba T553BFM.

Vilevile, Camera za CCTV pamoja na kitabu cha kumbukumbu za walinzi, vinamuonesha Makonda aliingia Clouds akiwa na askari wanne waliokuwa na sare tofauti za majeshi ya ulinzi na usalama, kati yao watatu wakiwa na silaha za moto.

Askari hao waliingia hadi chumba cha utangazaji, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji, huku Makonda akitumia vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Clouds kwa kutumia silaha za moto.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo ya Kubenea, kitendo cha Makonda cha kuvamia televisheni ya Clouds, tena akiwa ameongozana na askari waliobeba silaha za moto, ni kinyume cha sheria ya Kieletroniki na Posta ya mwaka 2010.

Maombi ya kutaka kumshitaki Makonda yamewasilishwa mahakamani, chini ya kifungu cha 99 (1) cha Sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai, Sura ya 20.

Kubenea ambaye amewahi kuwa mbunge wa Ubungo (Chadema), katika Bunge lililopita anasema, hatua ya Makonda kuvamia Clouds, ni matumizi mabaya ya madaraka, chini ya kifungu cha 96 ya Kanuni ya adhabu (Penal Code), Sura ya 20 na kuingilia moja kwa moja, mawasiliano ya Kieletroniki.

Mbali na Makonda, wengine walioitwa mahakamani siku hiyo, ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Wawili hawa wanadaiwa wameshindwa kuchukua za kumfungulia mashitaka ya jinai mtuhumiwa huyo.

Maombi ya kumshitaki Makonda yameambatanishwa na wito maalum (Chamber Summons) na hati ya kiapo (Charge Sheet).

Katika kujenga hoja yake mahakamani, wakili wa Kubenea ameambatanisha ripoti ya uchunguzi ya Kamati Maalum iliyoundwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.

Ripoti ya Nape iliyochunguza tukio la kuvamiwa Clouds, ilimtia hatiani Makonda na kupendekeza kwa mamlaka yake ya uteuzi, kumchukulia hatua za kinidhamu; Makonda mwenyewe kuwajibika binafsi na kuwaomba radhi Clouds na wananchi kwa ujumla.

Hata hivyo, mapendekezo yote ya Kamati ya Serikali hayakutekelezwa. Muda mfupi baada ya Nape kumaliza kusoma ripoti yake kwa waandishi wa habari, Rais John Magufuli alitangaza kumfuta kazi.

Nape alirejea kwenye baraza la mawaziri wiki iliyopita, kufuatia Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alishika madaraka ya urais baada ya kifo cha Magufuli, kuamua kumrejesha katika wizara hiyo.

Kamati ya Nape ilithibitisha kuwa Makonda alivamia kituo hicho cha televisheni akiwa anaendesha mwenyewe gari lenye namba T553 BFM na kuingia hadi chumba cha utangaji, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za utangazaji.

Tangu kuripotiwa kufunguliwa kwa shauri dhidi ya Makonda, kumekuwa na matukio mbalimbali yanayojitokeza. Katika gazeti la Jumatano iliyopita, wakili mwingine wa kujitegemea, Peter Madeleka, alinukuliwa akisema, yuko tayari kujiunga na mawakili wengine watakaoteuliwa na Kubenea, kuendesha kesi hiyo.

Madeleka ambaye alikuwa ofisa wa Jeshi la Polisi alisema, anataka kutumia ujuzi wake wa kisheria na kiuchunguzi, kuendesha kesi hiyo aliyoita, “imebeba maslahi ya taifa.”

“Lengo siyo kushinda tu. Kesi hii, inalenga kuzionyesha mamlaka za kuendesha mashitaka ya Jinai (DPP), kwamba kuna mtuhumiwa mmoja anastahili kuburuzwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili. Lakini hawajaweza kufanya hivyo na kunyamaza kwao, ni kuvunja Ibara ya 59 (B) Ibara ndogo ya (4) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” ameeleza Madeleka.

Alisema, “ikumbukwe kuwa hata mataifa makubwa kama Marekani, yamewahi kumuwekea vikwazo vya kwenda nchini humo Makonda na familia yake, kutokana na tuhuma za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

“Pamoja na Marekani kuwa taifa mshirika na Tanzania kwenye mambo kadhaa kihistoria, pamoja na uwezo wa Marekani kuweza kutambua mambo mbalimbali yanayotokea duniani, lakini serikali imeshindwa kufanyia kazi taarifa ya Marekani kuhusiana na matendo ya Makonda.”

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, 31 Januari 2020, ilieleza kuwa serikali ya nchi hiyo, imempiga marufuku Makonda na mke wake, Mary Massenge, kufuatia tuhuma za ukandamizaji wa haki za wananchi; kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wa watu.

“Wizara ina taarifa za uhakika kuwa Makonda amehusika katika uvunjifu huo wa haki kupitia nafasi yake kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Katika nafasi yake hiyo, pia amelaumiwa kwa kukandamiza upinzani wa kisiasa, kukandamiza haki ya kujieleza, na kushambulia makundi yasiyo na sauti,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo alitumia mtandao wake wa Twitter kutangaza marufuku hiyo.

Alisema, “…leo tumetangaza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Christian Makonda, hataruhusiwa kuingia Marekani, kutokana na kushiriki kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.”
 
Pia tunaomba ajibu haya

1. Nani alimuua Ben, Azory, Mawazo Lwajabe.

2. Nani alimteka, Roma, Nondo, Mo,

3. Waliookotwa kwenye viroba ufukweni walikuwa akina nani

Kumbukeni huyu ndiye aliyekuwa anatoa taarifa kuwa Fulani atapatikana siku Fulani.
 
😁😁😁
D4M.jpg
 
Pia tunaomba ajibu haya

1. Nani alimuua Ben, Azory, Mawazo Lwajabe.

2. Nani alimteka, Roma, Nondo, Mo,

3. Waliookotwa kwenye viroba ufukweni walikuwa akina nani

Kumbukeni huyu ndiye aliyekuwa anatoa taarifa kuwa Fulani atapatikana siku Fulani.
Kiongozi mkuu wa kikosi cha utekaji na mauaji akisaidiwa kwenye top list na Kinga, Jumane, Mahit na Badluck.
 
Makonda atajua kuwa alikuwa hajui.
Kwa kushitakiwa na kubenea?

Ingekua jamhuri, hapo mtu unaweza kuwaza!

Vipi clouds wakigoma kutoa ushirikiano! mutawalazimisha?

Maana huo ndio ushahidi pekee kila mjinga anashabikia!

Kuhusu mauaji hata USA wameshindwa kutoa ushahidi!
 
Back
Top Bottom