Pasaka Ya Tanzania Haijawadia Bado

George Kahangwa

JF-Expert Member
Oct 18, 2007
547
144
Watanzania kwa mara nyingine, kipindi hiki tunajiunga na watu wa mataifa mengine (hususan wakristo) kuadhimisha sikukuu ya pasaka yenye asili yake katika tukio la kuwekwa hur kwa taifa la Israel , na tukio la kiimani la kuuawa kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya yanahitimisha kipindi cha mfungo wa kwaresima amabacho mwaka huu nchini mwetu kiligubikwa na matukio ya kisiasa yaliyofananishwa kiutani na simulizi za mateso ya Kristo Yesu yapata miaka zaidi ya miaka 2000 iliyopita. kufananishwa huko ndiko kumepelekea nije na tafakuri hii, kwamba pasaka ya nchi yetu haijawadia bado.

Mjadala kuhusu Pasaka ya Tanzania miongoni mwa watanzania ulianza kwa utani, kwa watu kutumiana ujumbe mfupi wa simu wakilinganisha yaliyoyokea enzi za Yesu nyakati za mateso yake na yale yaliyojiri hivi karibuni nchini kwetu. Lakini kadri siku zinavyopita, niliona mjadala huo ukichukua sura ya hoja za kimantiki zaidi. Katika mazingira hayo nilijiuliza kama pasaka yetu kama taifa la watanzania imekwisha kuwadia au la. Ninaikita tafakuri yangu katika hilo kwa kurejea matukio ya kuanzia Mwezi Februari 2008 ya kuvunjwa kwa baraza la mawaziri na kuundwa kwa jingine tulilonalo sasa.

Moja ya mambo yaliyotaniwa katika dhana hii ya pasaka ya Tanzania ni Kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu baada ya kutolewa kwa ripoti ya Richmond. Binafsi naamini tukio hilo halikuwa ishara halisi ya pasaka yetu kwa kuwa kujiuzulu kwake hakukuwa kwa maslahi ya taifa ila kwa kiasi kidogo sana. Yamkini ni kwa maslahi ya chama chake kwa mujibu wa maneno yake mwenyewe, na kwa kuwa hasira ya Tanzania ilikuwa inazidi kuwaka, chama tawala (na serikali yake) kilikuwa hatarini. Kwa maneno yake mwenyewe Mheshimiwa alisema;
Mheshimiwa Spika, nimetafakari kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya Serikali yangu nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumwomba niachie ngazi

Kadhalika kuundwa kwa baraza ‘jipya’ hakukuwa upya wa maaana. Yamkini ni kwa maslahi ya chama kilichounda serikali hiyo. Uthibitisho mmojawapo wa hili ni hitimisho alilolitoa mwenyekiti wa chama hicho baada ya kutusomea watanzania baraza aliloliteua aliposema;
Ahsanteni sana, kidumu chama cha mapinduzi

Niliendelea kuona mwandelezo wa kurithishana madaraka katika baraza la sasa kama vile tuna utawala wa koo za kifalme, Msuya ndani, Mwinyi twende, na Malima haya. Bado wanaendelea kuteuana. Ni yale yaleee ya
Wasikilizaji mpira sasa anao Kenyatta, Kenyatta anatoa pasi kwake Moi, Moi, Moi, anatumia mbinu za uprofesa wa kisiasa anatoa pasi ndefu kule kumtafuta Uhuru Kenyatta, lakini anatokea pale nambari moja wa timu ya NARC na kuunyaka mpira ule.

Hapa nakumbuka pia mojawapo ya hotuba za mwisho mwisho za mzee Ruksa wakati wa utawala wake.
Aliwahi kusema kwamba katika utawala wake alijitahidi kuwashirikisha vijana, akatoa mfano wa JK na EL (asomaye na afahamu, kwa nini leo hii Mwinyi ni waziri)
Baraza jipya bado si serikali ya timu ya ushindi, si timu ya Taifa, ni timu ya klabu iliyoongoza ligi kuu.

Kimsingi pasaka ya Tanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii haijaja bado. Swali kuu la kujiuliza: Pasaka ya Tanzania itakuja lini na itakujaje? Hapo ndipo wasomi mliobobea, wajuvi wa nadharia na wenye exposure pana ya mambo, uzoefu na maono ya mbali mchanganue na kutafuta majibu

Kama nilivyodokeza awali,Neno pasaka lina asili katika utamaduni wa wana wa Israel wa kumchinja kondoo kwa ajili ya kuwekwa huru na kwa wengine ni ondoleo la dhambi.
Utaratibu huo waliutumia pia wakati wakiwa utumwani Misri, ikabidi wamchinje mnyama na kupaka damu yake mlangoni ili malaika wa Bwana atakapopita awatambue na hivyo kuwaepusha adhabu iliyolengwa kwa mabwana wa watumwa.
Katika kipindi hicho basi, pasaka ikamanisha kuondolewa katika utumwa wa Misri na kuwekwa huru kabisa, tena kwa kuhamishwa na kupelekwa katika nchi inayotirirka maziwa na asali, aliyoahidiwa baba yao Ibrahim.

Enzi za Bwana Yesu (Issa bin Mariam?), aligeuzwa yeye kuwa kondoo wa pasaka kwa kuuawa msalabani ili Taifa la Israel pamoja na mataifa mengine (of course wale wanaoamini hivyo) wakombolewe kutoka utumwa wa dhambi ambamo bwana wa watumwa ni Ibilisi mwenyewe, waingie katika uhuru wa Yesu na hatimaye katika uzima wa milele, katika nchi mpya, miji mipya (Yerusalem mpya) na mbingu mpya. Heri ni kwa wale waliojitakasa. Kuwepo huko kwa nchi mpya kutamaanisha uwepo wa mifumo sahihi ya maisha miongoni mwa wateule, ilihali mbingu mpya maana yake ni uwepo wa utawala bora kabisa (tafsiri ni yangu, na si ya kitheologia)

Basi pasaka ya Tanzania itakapowadia, itavaa sura zinazofanana na hayo. Tutaondolewa (tutapasaka- Passover) kutoka katika utumwa na mizigo ya ufukara na ufisadi inayolielemea Taifa kwa sasa na tutaingia katika enzi ya uhuru wa kimaisha sote! Wakati huo tutaiona faida halisi ya kuzaliwa katika nchi nzuri ya Tanzania inayofuka maziwa na asali (maliasili) mengi pengine kuliko hata Israel yenyewe ya huko mashariki ya kati. Tutakuwa na miji mipya na vijiji vipya ( hata kule kunakoitwa madongo poromoka patakuwa papya na penye hadi ya kuishi watu)

Wakati huo uchumi utarejeshwa mikononi mwa watanzania wenyewe na si kushikiliwa na wageni kama ilivyo sasa.
Wakati huo akina mama wajawazito hawatalala tena mzungu wa nne kule Amana (na kwingine). Tunaowauguza hawatakufa kwa kukosa dawa, watoto hawatazaliwa tena pembeni mwa njia eti kwa sababu baikeli iliyombeba mama imeharibika.

Wakati huo kilio hakitasikika kusini, kaskazini, Mashariki wala magharibi mwa nchi yetu cha watoto wa kitanzania wanaoshindwa kwenda shule kwa sababu wazazi wao hawana pesa au serikali yao inatoa mikopo kwa wachache (chini ya 1% ya rika lengwa!). wala hatutasoma tena katika magazeti na blogi habari ya shule moja wanafunzi 400 mwalimu mmoja, ilhali kwingine walimu wapo hadi wa ziada.

Mr. Ebbo (mwimbaji wa Bongo flava) hatamwogopa tena traffic police, eti hata akimwona kwenye TV ya nyumbani anastuka, kwa maana tutakuwa tumazipasaka enzi za rushwa barabarani, rushwa maofisini, rushwa mahakamani na kwingineko. Kwa maana licha ya mfumo tutakaokuwa tumeuanzisha kuwatiisha na kuwaogofya kabisa watoa na wapokea wa rushwa, watakuwa hawalazimiki kuichukua kwani mioyo yao imejengewa uadilifu sasa na wale wanaopokea rushwa ili waweze kumudu maisha hawatakuwepo tena maana maslahi ya kazi zao yanawatosheleza.

Wakati huo kutofautiana kwetu kiufuasi wa vyama vya siasa hakutakuwa sababu tena ya kubaguana, bali kutageuka kuwa kichocheo cha maendeleo ya hali ya juu ya nchi yetu.
Enzi hizo wenye dhamana ya uongozi watawaheshimu sana waliowapa dhamana hiyo (waongozwa) kwa maaana ndio waajiri wao.

Lo! Pasaka ya hivyo itakuja kweli? Ni swali ambao mtu aweza kujiuliza.

Pasaka hiyo itakuja siku ile tutakapokubali kubadilisha kabisa mifumo tuliyonayo kwa sasa na kuanza kufuata mifumo yenye maslahi dhahiri kwa Taifa letu.
Katika suala la kubadilisha mifumo, wapo wanaoona hilo lianze kwa kubadilisha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba tuliyonayo sasa, imepigiwa kelele sana kwamba inaendekeza uwepo wa mfumo wa chama dola badala ya kukifanya chama kilichoko madarakani kiwe chama cha siasa na si vinginevyo. Watawala wa sasa hawataki hilo libadilike maana linawahakikishia kuendelea kutawala ( ndio maana mara kadhaa wamejitapa wakisema kuwa watatawala milele). Kiburi chote hicho kinatoka kwenye katiba yetu wenyewe.

Hakika pasaka yetu haiji hadi hapo katiba itakapoondokana na mfumo huo. Itakaporuhusu, matharani uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa badala ya serikali ya chama tawala. Itakapotenganisha waziwazi mihimili mikuu ya dola, mfano wabunge wakabaki kuwa wabunge na mawaziri wakawa ni wateule wa mkuu wa dola kwa mujibu wa wasifu wa kila mmoja wao na wakatibitika hivyo mbele ya bunge.
Katiba yetu pia haina budi kachana na kutuadaa kwamba tuko katika mfumo wa kijamaa( kumbe yale mazishi yaliyofanyika Zanzibar, ulizikwa mfumo gani wa uchumi, kumbe hizi sera za ubinafsshaji na uwewkezaji wa kigeni ni za mfumo gani wa uchumi?)
Lakini hapa nachelea kumpigia mbuzi ngoma ya kihaya. Nakumbuka katika miaka ya tisini wasomi wa chuo kikuu mlimani (sio wote) walianzisha jitihada iliyojulikana kama National Committee for Constitutional Reform (NCCR), iliyolenga kuhakikisha kwamba ama tunakuwa na katiba mpya au iliyopo inafanyiwa marekebisho ya haja, lakini watu walipoanza kuonjeshwa ‘atamu’ za ujumbe wa halmashauri kubwa na uanakamati katika kamati ya wenye shingo nene (NEC) waka declare the co- mission futile na wakai- abandon.

Mfumo mwingine ambao hatuna budi kuubadili ili kuruhusu pasaka yetu ije ni Mfumo wa kiutendaji/ kiutawala kutoka ngazi moja hadi nyingine. Mawakili wetu katika eneo hili wanapenda kusisitiza haja ya Genuine Decentralization. Ingawa Tanzania tunadai tumepeleka madaraka ngazi za chini, kwa kuwa tuna halmashauri za wilaya na serikali za vijiji, tena eti tunatumia mikakati shirikishi katika uandaaji na usimamizi wa mipango ya maendeleo, mambo hayajakaa sawa. Utawala wa juu licha ya kwamba bado unazinyima autonomy mamlaka hizo za chini, bado mahusiano ya serikali kuu na serikali za mitaa yanaendekeza urasimu usiokuwa wa lazima.
Nitoe mfano, alipotutangazia baraza jipya Mheshimiwa Rais alisema anaunganisha masuala ya Elimu yashughulikiwe na Wizara moja. Lakini ki muundo bado sio hivyo. Hiyo TAMISEMI (ambayo binafsi sipendi iwepo) bado ina mkono wake wa kirasimu katika masuala ya elimu huko ngazi za chini. Tena nadhani kwa sasa hali itakuwa mbaya zaidi, maana Halmashauri zimepewa hata elimu ya sekondari ( kwa maana hiyo TAMISEMI imejitanua sasa kutoka elimu ya msingi hadi hata ya sekondari, si ajabu pasaka yetu ikichelewa zaidi utasikia na vyuo vya ualimu navyo)
Hili linanikumbusha enzi zile za ualimu wangu wa katika shule za msingi, tulimlilia Rais wa chama chetu wakati huo Mhe. Mama Margareth Sita, tukiomba masuala yetu yashughulikiwe na chombo kimoja, maana tulikuwa tukishindwa kuelewa, unapata tatizo unaambiwa nenda wilayani, mara hili ni la Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), mara hapa ukawaone watu wa mkoani, nako uaambiwa labda uende TAMISEMI Dodoma, unafika huko nako wanakusukuma wizarani Dar es Salaam, ili mradi ni mgongano tu wa majukumu na hiyo kero kubwa kwa mwenye kuhitaji kuhudumiwa ili naye akawahudumie wengine.
Tulilia sana walimu wa wa shule za msingi, wengine waliolewa, wakashindwa kuhama kutoka katika Halmashauri zinazowaajiri kuwafata wenzi wao waishio katika wilaya tofauti. Basi hayo yakawapata walimu wa msingi, sasa wameingizwa huko huko walimu wa sekondari.
Yamkini, kuzungumzia walimu ni mtazamo wa upande mmoja. Upande mwingine ni suala zima la ubora wa elimu chini ya mamlaka ya TAMISEMI kwa mgongo wa halmashauri. Tunasema tena tunaamini, kwamba kila mtoto wa taifa hili ana haki ya kupata elimu bora, kwa maana hiyo asome katika shule bora, zenye walimu bora, mitaala bora na vifaa bora vya kufundishia. Nasikitika chini ya mamlaka na muundo wa sasa hilo halitawezekana (pasaka bado) . kitakachotokea halmashauri/ manispaa za miji zitaendelea kuwa na umiliki wa walimu wa kutosha katika sekondari na praimari, ilhali kule vijijini taabu na mashaka makubwa yataendelea. Kwa maana itakuwa sasa kwamba si rahisi tena mwalimu aliyeajiriwa na manispaa ya Kinondoni akahamishiwe (wapi kule ambako hakuna barabara na hivyo Rais hajawahi kufika?)

Mfumo mingine wa kubadili ni CCM, ni ama chama hicho kioge kwa damu ya mwana kondoo ili kiwe safi kama theruji ya Finland, au kitoke madarakani sasa (kwani kitafia madarakani?) Hapa natahadhari kidogo ugomvi wa kisiasa maana najua katika nchi yetu kuna wana CCM si haba. Jamani, Baba wa Taifa, mhasisisi wa chama hicho si alisema kiko kama kokoro, sasa kwa nini tusione haja ya chama hicho kuoga? Jamani, mmoja wa waliowahi kuwa makatibu wake wakuu (Marehemu Kolimba) si alisema hakina dira, sasa haja ya kuitafuta dira sahihi itakosaje? Mnh, Wapinzani nao (sijui wanampinga nani – wamepewa jina baya!) si walisema wakati fulani kwamba kashfa ya BOT ni ya CCM moja kwa zote, kwa kuwa mafwedha yaliyochotwa huko yalimwagwa kwenye kampeni za kisunami za chama hicho mwaka 2005. We ngoja Dr. Balali arudi, huenda akatufungulia njia ya pasaka yetu kwa kusema ukweli wote ( hivi na yeye alitolewa kafara kama mwana kondoo wakati huenda maskini dhambi si yake?)

Mfumo mwingine wa kubadili ni utaratibu wetu wa kuwalea na kuwaibua viongozi. Nashawishika kusema kwa sasa utaratibu huo kama upo hauna tija wala ufanisi, na si ajabu haupo kabisa. Tunapolia leo kwa kukosa viongozi waadilifu, tumlaumu mama mlezi na tumlazimishe basi arekebishe staili yake ya ufundaji. Katika hilo vyuo vyetu vinaguswa. Hey, Universities and other higher learning institutions, how do you nurture the future leaders of the nation?
( Niliwahi kumsikia Prof. Mmoja akijivunia utendaji wa Mhe. Zitto, akaongeza kusifia kwamba ni zao halisi la Mlimani. Na sasa nimesikia hapo mlimani kuna wanaojivunia umwenzetu wa Dr. Mwakyembe) Binafsi namkumbuka Zitto akiwa mwanafunzi mwenzangu UDSM, tulifahamiana kwa karibu kwenye mambo ya uongozi wa wanafunzi. Nasikitika ukweli ni kwamba malezi ya kiuongozi aliyopewa na mlimani yalilenga kumdumaza. Mara kadhaa alisimamishwa masomo. Nakumbuka siku moja nikiwa nazungumza naye chumbani kwake, walikuja watu wa ofisi ya Mwadili wa wanafunzi, wakamtaka aondoke chuoni mara moja kwa kuwa wanamtuhumu kupanga njama za mapinduzi ya serikali ya DARUSO (chama cha wanafunzi).
Nasikitika kwamba wakati huo badala ya chuo kulea kipaji chake cha uongozi na uthabiti katika misimamo, kilim- intimidate mara nyingi. Well, hayo yalimpata Zitto, waliopo sasa chuoni hapo wanalelewaje, au wanafundwa kuukubali mfumo wa kifisadi tena kwa namna ya kitiifu ya yours faithfully.

Ipo pia mifumo mingine ya kubadili, wakati ukiruhusu tutaijadili pia.

Pasaka yetu itakapowadia,Mwanakondoo wa pasaka ya Tanzania, hatutamchinja physically, ila itamlazimu kuitoa kafara nafsi yake (maslahi yake binafsi, ya familia na ukoo wake) ili ayatumikie tu maslahi ya Taifa. Jukumu letu la pamoja ni kumtambua mwanakondoo huyo ili tuchinje kula pasaka yetu mapema zaidi.

Pasaka ya Tanzania itakuja,haijaja, itakuja lini? Watanzania tutafakari na kuamua sasa.

By the way, waliokaangiza vya sikukuu tukaribishane jamani
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom