Rev. Kishoka
JF-Expert Member
- Mar 7, 2006
- 4,526
- 1,529
Papa na Nyangumi: Nani atawavua tuwale?
Katika bahari, kuna samaki wakubwa wawili, Papa na Nyangumi. Samaki hawa wanaogopewa kwa kuwa ni wakubwa na wana uwezo wa kudhuru kila kilicho karibu yao.
Tumeshasikia simulizi nyingi za watu kuuawa na kuliwa na Papa Yule anayeitwa kwa Kiingereza Great White, tunajua kuwa Nyangumi ni mkubwa kama Lori la Scania na mlo wake ni mkubwa.
Lakini pamoja na sifa zote za hawa samaki, bado Mwanadamu ana uwezo wa kuwavua kama samaki wengine, kwa kutumia mitego mikubwa na maarifa kuwazidi akili. Kwa hiyo dhana ya kuwa Papa na Nyangumi hawawezi kuvuliwa ni batili! Wanavulika kirahisi tuu, na hivyo ubabe wao ndani ya Bahari hauna nguvu yeyote pale panapokuwa na dhamira ya kuwavua!
Kwa muda wa wiki mbili hivi, Taifa letu limekumbwa na malumbano kati ya Wafanyabiashara kadhaa, wakinyoosheana vidole vya nani kati yao ndie mhujumu au fisadi, nani kati yao ni Papa na Nyangumi amb aye hula kila kilichomo baharini.
Nasi kama Taifa, tumegeuka na kuyumbishwa na malumbano hayo, kama ushabiki wa Simba na Yanga.
Lakini katika haya yote yanayosemwa na kudaiwa kati ya wafanyabiashara hawa, Mchungaji anajiuliza, je wale wenye Mamlaka ya kulinda Sheria na Haki Tanzania wako wapi?
Je wamekaa mguu pande wakipagawa kutokana na mlipuko wa mabomu Mbagala? Au Wanatahayari kutokana na Rais wa Zanzibar Karume kushindwa kuhudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 45 ya Muungano?
Kinachonishangaza mimi ni jinsi kila mmoja wa hawa wafanyabiashara wakubwa nchini mwetu alivyo na habari kuhusu mwenzake. Kila mmoja wao anajua undani wa biashara za mwenzake mpaka nambari za akaunti za Benki au mkopo jambo ambalo kwa mujibu wa kanuni za Kibenki, ni kati ya Benki na Mteja au Serikali pindi inapokuwa inafanya upelelezi.
Bwana Mengi, alianzisha hii Sandakalawe, akatamka kuna Mafisadi Papa, akawataja majina, sikumbuki ni ushahidi wa namna gani aliutoa, lakini alitaja majina na watu wa Serikali na Chama Tawala, wakakasirika.
Si mara ya kwanza kwa Reginald Mengi kutoa tuhuma kubwa namna hiyo, ni jambo ambalo kalifanya miaka nenda rudi.
Waliotuhumiwa na Mengi, nao wakarudi mapigo, Maji kafungua kesi ya madai, somaiya anajiandaa kufungua kesi, lakini Rostam Aziz akaamua kumjibu Mengi kwa kutumia mkutano wa waandishi, ambapo alitoa vielelezo vingi kana kwamba yeye ndiye benki zilizotoa mkopo kwa Mengi au yeye ndiye Serikali mwenye mamlaka kumchunguza Mengi kama si mkusanyaji madeni aliyeombwa akamate mali za mengi zitaifishwe.
Kilichonishangaza sana ni katika orodha ya Rostam ya kuutaja Unyangumi wa Mengi, alitoa maelezo ya kina ya mambo ambayo Mengi alikumbana na ama wafanya biashara wenzake au waliomo Serikalini pale Mengi alipolalamika kuwa kadhulumiwa au hakutendewa haki.
Rostam kawataja Lowassa, Mramba, Masha, Manji, Somaiya, na Malima kati wengi aliodai wamefanyiwa visa na Mengi kama vile wameonewa, kinachoniudhi kwa hawa sita waliotajwa kuonewa, wao wenyewe hawana rekodi nzuri na wanatuhuma nyingi mno ambazo mpaka leo hazijatatuliwa.
Najiuiliza tena, inakuwaje leo Mtuhumiwa mkuu wa Ufisadi, ushahidi wake ni kuwataja watuhumiwa wenzake na si kujisafisha yeye kwanza?
Kitendo cha kuwepo kwa Masha katika orodha ya Rostam kujitetea au kumuumbua Nyangumi, kinanipa tatizo, Masha ambaye ni waziri wa Mambo ya Ndani, ana uwezo mkubwa sana kisheria kufanya alilofanya Rostam kwa kutamka wazi masuala binafsi ya Kibenki kama akaunti namba, na si Rostam.
Swali linakuja tena, Rostam alipata wapi namba za akaunti za Mengi? Je mabenki yote ambayo Mengi alikopa ni mali ya Rostam?
Nikigeuka kwa Mengi, naye katoa tuhuma nyingi, kana kwamba ana ushahidi tosha. Lakini hata pamoja na kuwa Rostam hana mamlaka yeyote (huenda anayo, ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM!), lakini madai ya Rostam kuhusu vitendo vya Mengi si ya kupuuziwa hata kidogo!
Je Mengi pamoja na kudai kalipa madeni , iweje kila siku yeye ndiye analia moto, samba na nyuki? Kwa nini Mengi anakuwa mzito kuwajibika inavyopaswa, kama kulipa madeni au kutojiingiza katika vitendo vichafu huku akijifanya ni mtakatifu?
Nashukuru hawaPapa na Nyangumi wanajitoa hadharani tuwaone, lakini lengo langu leo ni kuuliza, wale wenye mamlaka ya kuongoza nchi yetu wako wapi?
Mabenki yanafanyia usailiwa kihasibu, ni lini yamemfikisha Mengi mahakamani kwa kushindwa kulipa mikopo na kukimbilia kuuza habari za Mengi kwa Rostam?
Je Serikali yetu iko wapi? Tuhuma hizi kutoka kila upande ni kubwa sana na si za kupuuziwa, je Serikali yetu imefanya nini kupata ufumbuzi wa mambo haya ya uhujumu uchumi wan chi yetu yanaofanywa na Papa na Nyangumi?
Ni lini Serikali itakuwa mvuvi stadi iweze kuwavua hawa samaki wakubwa wanaosemekana ni hatari? Ili tuweze kula nyama zao na mafuta yao kututengenezea mishumaa na sabuni?
Tumechoka kusikia maigizo na ngonjera, tunataka Serikali inayofanya kazi, Serikali itakayohakikisha kuwa mazingira ya haki na sheria yanafuatwa na kuthaminiwa na kila mtu aliye ndani na nje ya nchi yetu.
Ni aibu sana kusikia malumbani kama haya, na cha kujiuliza ni hivi, ikiwa haya tunayoambiwa ni ya Mengi , Rostam, Somaiya, Manji na wachache, je Wafanyabiashara wengine wote nao ni mchezo huo huo?
Je leo tutashangaa Benki zetu kushindwa kufanya kazi kutokanana mikopo isiyolipwa kutokana na mianya iliyotengenezwa kukidhi mahitaji ya Wafanyabiashara mashuhuri? Leo hii pesa zinapohujumuwa Benki Kuu na kila mtu anakana, na mpaka Taifa linagundua tunaingia hasara, ni wajibu wa nani kuhakikisha kuwa tabia kama hizi haziiendelei?
Je tunamwambia nini Mtanzania mfanyakazi na Mkulima ambaye kila siku anavuja jasho na akitaka kuinua ubora wa maisha yake, hata kupata mkopo kulipia matibabu, elimu ya watoto, kujijengea nyumba, kununua gari, kununua zana za kilimo na pembejeo au kupata mtaji wa kujianzishia biashara, Mtanzania huyu anapigwa dana dana na kunyimwa mkopo, lakini tuna kundi la watu maarufu ambao wakiingia Benki au kupiga simu tu, mkopo unatolewa bila masharti na malipo ni mpaka siku watakapoamua kulipa?
Imekuaje tumefika hapa tulipo ambapo tuna taifa la wanaojifanyia kila wanalotaka kutokana na nguvu na umaarufu wao na si kufuata kanuni na maadili?
Serikali ambaye ni Mvuvi Mkuu, nasubiri kauli yako rasmi itakayoandamana na vitendo na si manung'uniko ya chini chini kama ya Sophia Simba!