Panga la Kikwete kwa mawaziri lamkalia vibaya Waziri Mkuu Pinda | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Panga la Kikwete kwa mawaziri lamkalia vibaya Waziri Mkuu Pinda

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Ng'wanza Madaso, Nov 17, 2009.

 1. Ng'wanza Madaso

  Ng'wanza Madaso JF-Expert Member

  #1
  Nov 17, 2009
  Joined: Oct 21, 2008
  Messages: 2,278
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Date::11/17/2009Panga la Kikwete kwa mawaziri lamkalia vibaya Waziri Mkuu Pinda[​IMG]Waziri Mkuu Pinda, panga la Kikwete linamkalia vibaya kutokana na umri wake.Leon Bahati na Salim Said

  KAMA Rais Jakaya Kikwete atakuwa ametoa kauli thabiti ya kuwaengua wazee iwapo atachaguliwa tena mwaka 2010, basi atawapa kisogo mawaziri wengi wazoefu walio kwenye serikali ya sasa, akiwemo mtendaji wake mkuu, Mizengo Pinda.

  Akizungumza katika mkutano wa vijana wa kulea viongozi wa Afrika juzi, Rais Kikwete aliahidi kufanya mabadiliko makubwa kwenye serikali yake ijayo iwapo atashinda uchaguzi wa mwaka 2010, akisema kuwa ataingiza vijana wengi.

  Alisema: “Wale viongozi wa rika langu, lazima waanze kuwaachia nafasi vijana. Tunahitaji wakuu wa wilaya vijana zaidi; wakuu wa mikoa vijana zaidi na hata mawaziri vijana zaidi. Ndivyo ilivyotokea kwetu sisi wakati tukiwa vijana.”

  Lakini kama atasimamia ahadi yake, Rais Kikwete, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 59, atalazimika kuachana na Pinda, 61, katika kipindi cha pili cha uongozi wake baada ya serikali ya sasa kuwa mchanganyiko wa wazee waliowahi kushika nyadhifa tangu serikali ya awamu ya kwanza na vijana ambao ndio kwanza wameingia kwenye siasa.

  Pinda hakuwa chaguo la kwanza la Kikwete kwa nafasi hiyo ya waziri mkuu wakati aliposhinda kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005.

  Lakini mbunge huyo wa Mpanda aliteuliwa na Kikwete mwaka 2008 baada ya Edward Lowassa, ambaye ni rafiki mkubwa wa rais, kujiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu kutokana na kashfa ya utoaji zabuni kwa kampuni ambayo ilibainika kuwa haikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond Development LLC.

  Pinda, ambaye ni muhitimu wa shahada ya Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Dar es salaam, alikuwa msaidizi wa katibu wa Rais kati ya mwaka 1982 na 1992 na baadaye kuwa karani wa Baraza la Mawaziri kuanzia mwaka 1996 hadi 2000.

  Alichaguliwa kuwa mbunge wa Mpanda mwaka 2000 na baadaye kuwa naibu waziri wa Tamisemi na baadaye kuwa waziri kamili mwaka 2006 kabla ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu Februari 8, 2008.

  Tangu aanze kuwa waziri, Pinda hajawahi kuhusishwa na makundi na wakati wote amekuwa akichukuliwa kama mchapakazi na uteuzi wake ulipitishwa na wabunge 279, huku kura mbili zikimpinga na moja ikiharibika.

  Wakati ahadi hiyo ya Kikwete ikionekana kuwa kiashirio kibaya kwa watendaji wake wa sasa, baadhi ya wanasiasa na mawaziri wameiambia Mwananchi kuwa uamuzi huo utachangia maendeleo, huku wengine wakipinga.

  Baadhi ambao walihojiwa na Mwananchi kutaka maoni yao walisema ahadi hiyo itasaidia kuisafisha serikali yake kutokana na viongozi kadhaa wenye umri mkubwa wana uzoefu wa kutuhumiwa kwa ufisadi.

  “Mambo mengi yameonekana kuwashinda baadhi ya mawaziri wake na kumfanya yeye binafsi kuingilia kati kwa mawazo na hata wakati mwingine kutoa amri,” alisema mmoja wa wabunge wa CCM ambaye hakupenda jina lake litajwe kutokana na nafasi yake ndani ya chama.

  Alielezea baadhi ya mawaziri upeo wao umefikia mwisho na kwamba kuendelea kuwaweka kwenye nafasi zao kutawafanya waendeshe mambo kwa mazoea badala ya kwenda na wakati.

  “Kwanza ingetakiwa mawaziri na hata wabunge nao wawekewe ukomo. Hii ingesaidia sana... na tusingewasikia waking’ang’ania majimbo kama mbwa anavyong’ang’ania mfupa. Imefika mahali ukionekana unataka kugombea jimbo fulani ndani ya CCM, unaonekana kama mtovu wa nidhamu,” alilalamika.

  Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Itikadi na Uenezi), John Chiligati alionyesha kuwa na mawazo tofauti kidogo, akieleza alichosema rais ni utekelezaji wa sera za chama hicho.

  Alisema ni katika utekelezaji huo kanuni zinaelekeza wazee kupisha vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi.

  “Hii ni kanuni ya maisha na ndio sera ya CCM. Kama umri umeenda lazima tupishe tu,” alisema Chiligati ambaye pia ni Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

  “CCM imetenga nafasi maalumu kwa vijana kuingia Halmashauri Kuu ya chama na hata katika nafasi za ubunge... ukiachia wabunge wa majimbo, tumetenga nafasi 10 maalumu kwa ajili ya vijana,” aliongeza Chiligati ambaye ana umri wa miaka 59.

  Chiligati, ambaye ni mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), alisema: “Sisi tunajiandaa kwenda kupumzika, tunataka vijana wapate nafasi hata kama wazee watakuwamo, lazima vijana waonekane kwa wingi”.

  Alisema hiyo ni kwa sababu busara ya wazee katika uongozi ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba taifa linaongozwa vizuri kwa kuwa na maamuzi ya busara na hekima ya hali ya juu.

  Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa CCM na mbunge wa Newala, George Mkuchika, 61, aliunga mkono mtazamo wa Rais Kikwete akisema “hiyo ni sawasawa kabisa”.

  Mkuchika alisema huo ndio utaratibu walionao CCM na hata katika utamaduni wa jamii ya Tanzania.

  “Sio tu kwa Baraza la Mawaziri, bali hata katika nafasi zote za uongozi serikalini na katika chama chetu,” alisema Mkuchika.

  “Mawaziri, manaibu, makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara mbalimbali wanazeeka, hivyo lazima vijana washike nafasi hizo kwa maslahi ya maendeleo ya taifa, kwa sababu wao ndio chachu ya maendeleo.”

  Alisisitiza kuwa aliyosema rais Kikwete ni sawasawa kabisa, lakini ni kwa vijana ambao wameandaliwa na kupikwa vizuri, ili kupata uzoefu wa kuongoza katika nyadhifa mbalimbali za kitaifa.

  “Unajua kuna msemo usemao ‘uzee dawa’ hivyo pamoja na kwamba vijana watakuwa wengi, wazee wachache watakuwamo ili kutoa busara na miongozo yao katika kutoa maamuzi,” alisema Mkuchika.

  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye ni waziri kijana zaidi kwenye serikali ya awamu ya nne, aliunga mkono kauli ya rais akisema: “Haya ni mambo ambayo nimekuwa nikiyasema mara nyingi. Vijana wana nafasi na changamoto nyingi za maendeleo katika taifa.”

  Mbunge huyo alimsifu Rais Kikwete akisema kwamba hata katika uongozi wake wa sasa amejitahidi kuweka vijana kadhaa kwenye serikali yake.

  Hata hivyo, baadhi ya mawaziri ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini, walisema wapo tayari kuwaachia vijana madaraka bila ya wasiwasi wowote. Mara baada ya Kikwete kushinda kiti cha urais mwaka 2005 aliteua baadhi ya mawaziri ambao walitumikia serikali za awamu zilizomtangulia, wakiwemo Bakari Mwapachu, Basil Mramba, Joseph Mungai na Kingunge Ngombare Mwiru ambaye hata hivyo alimteua kuwa mbunge. Hata hivyo, baada ya kuvunja Baraza la Mawaziri Kikwete hakuwarejesha tena.

  Source:Mwananchi
   
Loading...