Pamoja na ukimya wa sasa wa RC wa DSM, lakini...

mbenge

JF-Expert Member
May 15, 2019
4,572
9,808
Katika wakuu wa mkoa waliowahi kuongoza jiji la DSM, kijana wetu ndiye ambaye miongoni mwao anayeongoza kwa kuthibitisha na hata kuja mara kwa mara na mipango mingi ya muda mfupi katika kujaribu kutafuta suluhisho na ufumbuzi wa kero zinazowakabili wananchi anaowaongoza kwa uwazi kabisa.

Nimegusia hapo juu, kwa kutumia maneno "mipango mingi ya muda mfupi" ili niweze kuelezea nini hasa kinachokwamisha juhudi zake hizo. Katika hali ya kawaida ya utendaji na uwajibikaji, suala la uwazi pamoja na dhamira ya dhati katika kutafuta njia mbadala kutafuta suluhisho za muda mrefu juu ya kero za wale ambao unaowaongoza ni jambo jema sana.

Na pia uthubutu wa kujaribu kutekeleza ubunifu wako ni suala muhimu mno, kwa kuwa ili maono ya kiongozi yeyote yule yakapate kutimia hilo suala muhimu sana kuzingatia. Kitu ambacho kiongozi huyu kijana anaonekana akijaribu kukifanya

Mkwamo kubwa kwake tena uliokuwa dhairi hutokea pale mipango yake mingi ya muda mfupi inapokosa "correlation" na ile mipango ya kati na pia ya muda mrefu (na tena pengine wala haipo kabisa), na hapo ndipo hasa hata ule ubunifu na uthubutu wake unabakia kuathirika na hata kujikuta umefunikwa na sura ya kutokufanikiwa.

Sisi sote tu mashahidi na hata kumuona kijana wetu mara kwa mara akija na mikakati tofauti ktk kutaka kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wale anaowaongoza. Mathalani, tumewahi kumshudia akija na mikakati ya usafi ndani jiji, kuwaondoa ombaomba, kupambana na madawa ya kulevya, kuwaondoa madada na makaka poa, kutambua viongozi ambao wametelekeza watoto wa nje ya ndoa zao, kutatua kero za umiliki wa viwanja na hata kutaka kutoa msaada wa kisheria kwa wale waliozurumiwa, kusajili ndoa ili matapeli na wenye kuwahadaa binti na dada zetu wakapate kubainika n.k.

Tatizo la msingi lipo na linajidhihirisha, hasa kwa kuzingatia kwamba licha ya ubunifu na uthubutu wake, anakwamishwa na jinsi anavyopata ushauri ktk kutaka kuyashughulikia mambo mtambuka kwa mipango ya muda mfupi. Ni ukweli uliyokuwa wazi kabisa, kuna mambo ambayo amewahi kuyafanyia kazi, tena kwa kasi ya ajabu na hata kupata msaada wa kipekee toka ktk mamlaka ya juu kabisa na hata vyombo vya ulinzi na usalama vilionyesha vikimpa tafu ya nguvu.

Lakini masuala mengi aliyojaribu kujikita nayo yanaonyesha kuwa yameainishwa na kuonekana yanaingiliana na wahusika wengine wenye dhamana kwayo moja kwa moja. Kitu ambacho washauri wake wanapaswa kumjulisha ili aepuke kuingia ktk anga za wateule wengine.

Mkuu wetu wa mkoa, bado ni kijana na ana hamu ya kuweza kufikia matarajio yake makubwa ili apate kutimiza ndoto zake nyingi chanya ndani ya jiji la DSM ili pengine likapate kufanana na mengine yenye hadhi Afrika na duniani kwa ujumla. Nashauri tuzidi kumpongeza pale tupoona amekuja na mikakati mizuri, lkn endapo tunaona anakosa "consistence" tumsahihishe kwa hoja mbadala. Na pia endapo tunaona anguko dhahiri llikimjia ama pale anapoingilia majukumu ya wenzake pia tumsaidie ktk kumkosoa ili apate kujisahihisha, tusiishie tu kimshambulia kwa tuhuma zinazohusu historia ya taaluma yake.

Naam! Yeye ndiye kakabidhiwa na kuaminika kushikilia ofisi hiyo nyeti. Lakini pia nimalizie kwa kumshauri tu, endapo naye pia ni mmoja wetu hapa katika hili jukwaa, ama inawezekana pia kupitia watu walio karibu yake, apate ujumbe maridhawa kwa nahau hizi;

Shime, shime - "Ukubwa ni jalala (ikijumuisha hata cheo chako pia)" na "Sikio lisikilizalo haliwezi kamwe kukatwa katika kichwa"

Jenga tabia ya kukubali kushindwa na kukosolewa kwa kuwa bado kuna mengi ya kujifunza kutokana na umri wako wa ujana, haijalishi iwe ni kwako wewe binafsi ama hata kwa wale ambao unawajibika kwao ama mnawajibika wote kwa pamoja. Tega sikio kwa maneno yote yaliyomo ndani ya jukwaa hili lenye madini, tena sana siku zote unapaswa kupunguza maadui bali uongeze mtandao wa marafiki wa uhakika.
 
Back
Top Bottom